Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Virusi Ambavyo Wanawake Wanapaswa Kujua

Virusi Ambavyo Wanawake Wanapaswa Kujua

Virusi Ambavyo Wanawake Wanapaswa Kujua

BAADA ya kuolewa kwa mwaka moja na nusu, Cristina * alienda kufanyiwa uchunguzi wake wa kwanza na daktari wa magonjwa ya wanawake kutia ndani uchunguzi wa chembe za mlango wa tumbo la uzazi, yaani, Pap smear. Daktari huyo aligundua jambo lililomtia wasiwasi, hivyo akadokeza kwamba Cristina afanyiwe uchunguzi mwingine kwa kutumia kifaa maalumu chenye kamera ili kuona vizuri mlango wa tumbo la uzazi. Daktari aligundua kidonda katika mlango wa tumbo la uzazi, naye akatoa sehemu ya tishu zilizoathiriwa ili zichunguzwe.

Cristina anasema hivi: “Majuma mawili baadaye, daktari alituomba twende kuchukua matokeo ya uchunguzi. Alituambia kwamba kidonda hicho kilisababishwa na virusi viitwavyo human papillomavirus (HPV) na kilikuwa kibaya sana. Alinieleza kwamba kidonda hicho kinaweza kusababisha kansa ya mlango wa tumbo la uzazi na kwamba nilihitaji kutibiwa mara moja.

“Baada ya kuelezwa matokeo ya uchunguzi huo, nilianza kulia. Mimi na mume wangu tulishtuka. Upasuaji mdogo ulipangwa kufanywa siku iliyofuata. Alasiri hiyo nilikuwa mwenye wasiwasi na huzuni. Nilijiuliza, ‘Kwa nini jambo hili limenipata mimi tu?’”

Kwa kuwa alikuwa amesoma kwamba virusi hivyo huambukizwa kupitia ngono, Cristina alishangaa kwa sababu hakujua jinsi alivyoambukizwa. Sikuzote yeye na mume wake walifuata viwango vya juu vya maadili vya Biblia.

Ugonjwa Unaowapata Wanawake Wengi

Ukweli ni kwamba, mamilioni ya wanawake ulimwenguni pote huambukizwa virusi hivyo ambavyo inasemekana ndio ugonjwa wa zinaa ambao huwapata watu wengi zaidi. Kulingana na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), virusi hivyo ndivyo kisababishi kikuu cha kansa ya mlango wa tumbo la uzazi. *

Kila mwaka, mamia ya maelfu ya wanawake huchunguzwa na kupatikana na virusi vya HPV na kila mwaka maelfu hufa kwa sababu ya kansa ya mlango wa tumbo la uzazi ambayo husababishwa na virusi hivyo. Virusi hivyo ndivyo kisababishi kikuu cha kansa inayowaua wanawake wengi katika nchi maskini. Ulimwenguni pote, kansa ya mlango wa tumbo la uzazi ndiyo aina ya pili ya kansa inayoathiri sehemu za tumbo la uzazi ambayo huwapata wanawake wengi. Haishangazi kwamba, shirika la WHO husema kwamba virusi vya HPV ni “tatizo kubwa la afya ulimwenguni pote”! Ni mambo gani unayopaswa kujua kuhusu virusi hivyo?

Virusi vya HPV hufanya wanaume na wanawake wapatwe na vipele vigumu, kutia ndani vipele vinavyotokea kwenye viungo vya uzazi. Kwa kawaida, vipele hivyo havina kansa. Ingawa kuna aina za virusi vya HPV zaidi ya 100, ni chache sana kati yazo ambazo husababisha kansa. Mtu hupata kansa ya mlango wa tumbo la uzazi ikiwa tu aina fulani ya virusi hivyo vinakaa mwilini kwa muda mrefu. Kwa upande mwingine, maambukizo mengi ya virusi hivyo hupona yenyewe baada ya kushindwa nguvu na mfumo wa kinga wa mwili.

Wanaoweza Kuambukizwa

Wale hasa wanaoweza kuambukizwa ni wanawake wanaoanza kufanya ngono wakiwa na umri mdogo, wale walio na wapenzi wengi wanaume, au wale wanaofanya ngono na mwanamume ambaye ana wapenzi wengi wanawake. Mara nyingi, mwanamume asiye na dalili zozote zinazoonekana za ugonjwa huo ndiye humwambukiza mwenzi wake.

Hata hivyo, katika visa fulani, wanawake walio safi kiadili au wale ambao labda hawajawahi kufanya ngono huambukizwa virusi hivyo. Kwa mfano, uchunguzi wa hivi karibuni unaonyesha kwamba mtoto anaweza kuambukizwa virusi hivyo mama anapojifungua, au mtu anaweza kuambukizwa kwa njia nyingine. Ugonjwa huo unaweza kujitokeza miaka mingi baada ya mtu kuambukizwa.

Jinsi ya Kujua Ikiwa Umeambukizwa

Ikiwa wewe ni mwanamke, huenda ukajiuliza, ‘Nitajuaje kwamba nimeambukizwa virusi vya HPV?’ Hilo ni swali muhimu kwa kuwa dalili za ugonjwa huo hazijitokezi waziwazi. Kwa hiyo, kama alivyofanya Cristina aliyetajwa mwanzoni mwa makala hii, hatua muhimu ni kufanyiwa uchunguzi wa chembe za mlango wa tumbo la uzazi, yaani, Pap smear, au Papanicolaou smear. *

Ili kufanya uchunguzi huo, daktari hutoa chembe chache za mlango wa tumbo la uzazi na kuzipeleka kwenye maabara ili zichunguzwe. Uchunguzi huo unaweza kuonyesha ikiwa mtu ameambukizwa, ana uvimbe, au ana chembe zisizo za kawaida. Inaripotiwa kwamba uchunguzi wa Pap smear umepunguza idadi ya watu wanaopatwa na kansa ya mlango wa tumbo la uzazi na vifo vinavyosababishwa na kansa hiyo.

Shirika la WHO linasema: “Kutumia uchunguzi wa Pap smear ili kugundua mapema kidonda kinachoweza kusababisha kansa kumekuwa, na huenda kwa muda mrefu kukaendelea kuwa njia kuu ya kudhibiti ugonjwa huo ulimwenguni pote.” Ikiwa matokeo ya uchunguzi huo hayaridhishi, kifaa maalumu chenye kamera hutumiwa kuchunguza sehemu iliyoathiriwa. Kwa kutumia kifaa hicho, daktari anaweza kuona ikiwa kuna kidonda. Sehemu za tishu zilizoathiriwa hukatwa na kufanyiwa uchunguzi, kisha matibabu huanza.

Siku hizi, uchunguzi wa hali ya juu sana unaweza kufanywa kwenye maabara. Uchunguzi huo unaweza kuonyesha vizuri zaidi ikiwa mtu ameambukizwa.

Matibabu na Kinga

Kuna matibabu kadhaa yanayoweza kudhibiti maambukizo ya HPV. Wataalamu hutumia dawa za kupaka. Baadhi ya dawa hizo huharibu chembe zenye virusi hivyo, na nyingine husaidia mfumo wa kinga kupambana na virusi hivyo. Matibabu mengine hutia ndani kuondoa sehemu iliyoathiriwa kwa kutumia umeme, leza, au kwa kuigandisha. Hata hivyo, badala ya kufanyiwa upasuaji, ingefaa mtu aepuke kuambukizwa. Mtu anawezaje kuepuka kuambukizwa?

Miaka kadhaa iliyopita, kongamano lenye kichwa, “Kansa ya Mlango wa Tumbo la Uzazi na HPV Katika Milenia Mpya” lilifanywa huko Mexico City. Msemaji mkuu, Dakt. V. Cecil Wright, ambaye ni mwalimu wa chuo kikuu na mtaalamu wa HPV kutoka Kanada, alishauri hivi: “Usifanye ngono kabla hujaolewa.” Pia, Dakt. Alex Ferenczy, profesa wa magonjwa katika Chuo Kikuu cha McGill huko Montreal, Kanada, alisema hivi: “Ili kuzuia kansa ya mlango wa tumbo la uzazi . . . , ni lazima wenzi wawe waaminifu.”

Kwa hiyo ni vigumu sana kwa watu wanaofuata viwango vya maadili vya Biblia kupata kansa inayosababishwa na HPV. Hii ni kwa sababu Biblia hukataza kufanya ngono nje ya ndoa, huwatia moyo wenzi wa ndoa wawe waaminifu, na kuwashauri Wakristo wafunge ndoa tu na mtu anayefuata viwango hivyo.—1 Wakorintho 7:39; Waebrania 13:4.

Hata hivyo, ni muhimu kujua kuhusu HPV kwa kuwa unaweza kuzuia usiambukizwe virusi hivyo. Isitoshe, hata kama maambukizo hayo yanajitokeza na kuenea, bado unaweza kutibiwa. Shirika la WHO linasema: “Mara nyingi kansa ya mlango wa tumbo la uzazi inaweza kutibiwa ikigunduliwa mapema.”

Mbali na kujifunza kuhusu maadili, wanawake wanapaswa kujua kuhusu ugonjwa huo na kuelewa umuhimu wa kufanyiwa uchunguzi mbalimbali kwa ukawaida kama vile Pap smear. * Kasoro yoyote ikigunduliwa, mwanamke anaweza kutibiwa. Dakt. Montserrat Flores, ambaye ni mtaalamu wa kuchunguza mlango wa tumbo la uzazi kwa kutumia kifaa chenye kamera, anasema hivi: “Mwanamke akijua hatari za ugonjwa huo, anaweza kuepuka mambo mawili hatari: kwanza, kupuuza ugonjwa huo na kukosa kutafuta matibabu, jambo ambalo linaweza kusababisha kansa. Pili, ataepuka kuogopa sana kansa hivi kwamba atakubali kufanyiwa upasuaji asiohitaji.”

Bado wanasayansi wanaendelea kutafuta njia rahisi na zenye matokeo zaidi za kuchunguza virusi vya HPV. Pia, chanjo za kuzuia na kutibu ugonjwa huo zinaendelea kutengenezwa.

Ingawa uchunguzi wa mwisho aliofanyiwa Cristina ulionyesha kwamba hana virusi hivyo, bado yeye huenda kufanyiwa uchunguzi wa mlango wa tumbo la uzazi kila baada ya miezi sita. Baada ya kujifunza mengi kuhusu ugonjwa wake, anasema hivi: “Hata kama tuna virusi vya HPV, kuna mambo mengi tunayoweza kufanya ili kuwa na afya nzuri.”

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 2 Jina limebadilishwa.

^ fu. 7 Mlango wa tumbo la uzazi ni sehemu nyembamba iliyo katikati ya uke na tumbo la uzazi la mwanamke.

^ fu. 14 Uchunguzi huo ulipewa jina la daktari Mgiriki, George N. Papanicolaou, ambaye alivumbua mbinu ya kutia chembe rangi ili kuzichunguza.

^ fu. 23 Kulingana na Taasisi ya Kitaifa ya Kansa ya Marekani, uchunguzi huo unapaswa kufanyiwa mtu anapofikia umri wa miaka 18 au anapoanza kufanya ngono.

[Sanduku katika ukurasa wa 22]

Hatua Ambazo Wanawake Wanapaswa Kuchukua

Wanawake wanapaswa kufanyiwa uchunguzi wa Pap smear kwa ukawaida, hawapaswi kutumia tumbaku, na wanapaswa kula vyakula bora. Vyakula hivyo vinatia ndani mboga, matunda, na nafaka. Utafiti fulani unaonyesha kwamba kula vyakula vyenye karotini, vitamini A, C, na E, na aina fulani ya vitamini B kunaweza kupunguza hatari za kupata kansa ya mlango wa tumbo la uzazi.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 23]

Virusi Hatari

Virusi vya human papillomavirus (HPV) vinasemekana kuwa ugonjwa wa zinaa ambao huwapata watu wengi zaidi ulimwenguni na ndio kisababishi kikuu cha kansa ya mlango wa tumbo la uzazi katika nchi maskini. Kansa ya mlango wa tumbo la uzazi ndiyo aina ya pili ya kansa inayoathiri sehemu za tumbo la uzazi ambayo huwapata wanawake wengi ulimwenguni.

[Hisani]

© Science VU/NCI/Visuals Unlimited

[Picha katika ukurasa wa 23]

Dakt. George Papanicolaou, aliyevumbua “Pap smear”