Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Jantar Mantar—Kituo cha Kutazama Angani Kisichokuwa na Darubini

Jantar Mantar—Kituo cha Kutazama Angani Kisichokuwa na Darubini

Jantar Mantar—Kituo cha Kutazama Angani Kisichokuwa na Darubini

Na mwandishi wa Amkeni! nchini India

HUENDA wageni wanaotembelea Jantar Mantar huko New Delhi, India, wakatazama majengo hayo kwa mshangao na kujiuliza, ‘Je, kweli hiki kinaweza kuwa kituo cha kutazama angani?’ Wale ambao wamezoea majengo ya kisasa yaliyo na vifaa vya hali ya juu vya kuchunguza mambo ya nyota hawawezi kuamini kwamba vifaa vilivyojengwa kwa mawe vilivyo katika bustani kubwa vinaweza kutumiwa kutazama mambo ya angani. Lakini, hivyo ndivyo kituo cha Jantar Mantar kilivyokuwa kilipojengwa mwanzoni mwa karne ya 18. Inashangaza kwamba hata ingawa kituo hicho hakikuwa na darubini na vifaa vingine vilivyokuwa vikitengenezewa Ulaya, kilitoa habari nyingi na zilizo sahihi kwa kadiri kubwa kuhusu vitu vya angani.

Vituo vitatu kati ya vitano ambavyo vilijengwa na mtawala wa Rajput, Maharaja Sawai Jai Singh wa Pili vinaitwa Jantar Mantar. “Jantar” linatokana na neno la Kisanskriti “yantra,” linalomaanisha “kifaa,” na “Mantar” linatokana na neno “mantra,” linalomaanisha “fomula.” Jina Jantar Mantar lilitokana na zoea la kupatanisha maneno yanayokaribia kufanana ili kuyakazia.

Bamba lililobandikwa kwenye kifaa kimoja katika kituo cha Jantar Mantar huko New Delhi mwaka wa 1910 linaonyesha kwamba kituo hicho kilijengwa mwaka wa 1710. Hata hivyo, utafiti uliofanywa baadaye unaonyesha kwamba kilimalizwa kujengwa mwaka wa 1724. Kama tutakavyoona, masimulizi ya maisha ya Jai Singh yanaunga mkono dai hilo. Lakini kwanza acheni tuchunguze kifupi vifaa vya kituo hicho cha pekee kinachosemekana kuwa cha kale zaidi ulimwenguni.

Vifaa Vilivyojengwa kwa Mawe

Kituo hicho kina vifaa vinne vya mawe. Kifaa chenye kutokeza zaidi ni kile kinachoitwa Samrat yantra, au kifaa Kikuu ambacho ni “saa ya kivuli.” Hicho ndicho kifaa muhimu zaidi ambacho Jai Singh alibuni. Kina pembetatu kubwa ya mawe, yenye urefu wa meta 21.3, sehemu ya chini meta 34.6, na upana wa meta 3.2. Upande mrefu wa pembetatu hiyo wenye urefu wa meta 39 uko sambamba na mhimili wa dunia nao umeelekezwa kwenye Ncha ya Kaskazini. Pembe tatu hiyo au saa hiyo imegawanywa katika sehemu nne na kila sehemu ina vipimo vya saa, dakika, na sekunde. Ingawa saa za kivuli zilikuwepo kwa karne nyingi, Jai Singh alitumia kifaa hicho sahili cha kupima wakati ili kupima kwa usahihi umbali wa nyota kutoka kwenye ikweta iliyo angani na kutoka kwenye sayari nyingine zilizo angani.

Vifaa vingine vitatu vilivyo kwenye kituo hicho ni Ram, Jayaprakash, na Mishra yantra. Vilitengenezwa kwa ustadi ili kupima umbali wa nyota na jua kutoka kwenye ikweta iliyo angani, ziko juu kadiri gani angani, na umbali wake kutoka kaskazini kuelekea mashariki. Kifaa cha Mishra hata kilionyesha saa sita mchana zilipofika katika majiji mbalimbali ulimwenguni pote.

Vifaa vyote ambavyo vimetajwa isipokuwa Mishra yantra vilibuniwa na Jai Singh. Vilikuwa vya hali ya juu na sahihi zaidi kuliko vifaa vilivyokuwako wakati huo nchini India, navyo vilichangia kutokezwa kwa chati zenye habari za nyota na matukio na takwimu. Vilikuwa maridadi na vyenye umbo la kupendeza navyo vilitoa habari muhimu hadi darubini na vifaa vingine vilipoanza kutumiwa. Hata hivyo, kwa nini msomi huyo mwenye akili hakutumia vifaa vilivyokuwako Ulaya kutia ndani darubini-upeo katika utafiti wake kuhusu mambo ya nyota? Tutapata jibu kwa kuchunguza ukoo wa maharaja na historia ya nyakati hizo.

“Alijitoa Kusomea Sayansi ya Hisabati”

Jai Singh alizaliwa mwaka wa 1688 katika jimbo la Rajasthan huko India. Baba yake aliyekuwa mfalme huko Amber, mji mkuu wa ukoo wa Kachavaha wa Warajput, alikuwa chini ya mamlaka ya Mogul huko Delhi. Mwana huyo wa mfalme alifunzwa lugha mbalimbali kama vile Kihindi, Kisanskriti, Kiajemi, na Kiarabu. Pia alifunzwa hisabati, elimu ya nyota, na mafunzo ya kujihami. Lakini alipenda sana somo moja. Maandishi ya wakati huo yanasema hivi: “Tangu aanze kutumia nguvu zake za kufikiri hadi zilipokomaa, Sawai Jai Singh alijitoa hasa kusomea sayansi ya hisabati (elimu ya nyota).”

Mnamo 1700, akiwa na umri wa miaka 11, Jai Singh alikuwa mfalme wa Amber baada ya kifo cha baba yake. Muda mfupi baadaye, mfalme huyo mchanga alialikwa na maliki wa Mogul kwenye jumba lake kusini mwa India, ambako Jai Singh alikutana na Jagannātha, mwanamume aliyejua sana hisabati na elimu ya nyota. Baadaye mtu huyo akawa msaidizi mkuu wa mfalme. Maisha ya kisiasa ya mfalme huyo kijana yalibadilika-badilika hadi 1719 Muḥammad Shāh alipoanza kutawala. Wakati huo Jai Singh aliombwa aende Delhi, mji mkuu ili kukutana na mtawala mpya wa Mogul. Yaonekana Jai Singh alipendekeza kujengwa kwa kituo cha kutazama angani kwenye mkutano huo uliofanywa Novemba 1720. Labda pendekezo lake lilitekelezwa mwaka wa 1724.

Ni nini kilichomchochea mfalme huyo kujenga kituo hicho? Jai Singh alitambua kwamba chati zenye habari za nyota na matukio na takwimu za India hazikuwa sahihi hata kidogo na kwamba kulikuwa na maendeleo madogo katika elimu ya nyota. Hivyo akaamua kutengeneza chati mpya ambazo zingeonyesha kwa usahihi nyota na sayari zilizo angani. Pia alitaka kutengeneza vifaa vya kuchunguza nyota ambavyo mtu yeyote ambaye alisomea elimu ya nyota angeweza kutumia. Kwa hiyo, Jai Singh alipata vitabu vingi sana kutoka Ufaransa, Uingereza, Ureno, na Ujerumani. Aliwakaribisha wasomi kutoka shule za elimu ya nyota za Kihindi, Kiislamu, na Ulaya. Hata alituma wajumbe wa kwanza kutoka Mashariki kwenda Ulaya ili kukusanya habari kuhusu elimu ya nyota, na akawaagiza walete vitabu na vifaa.

Wasomi wa India Hawangewasiliana na Wasomi wa Ulaya

Kwa nini Jai Singh alijenga vifaa vya mawe hata ingawa darubini, maikrometa, na venia zilikuwa zikitumiwa Ulaya? Na kwa nini inaonekana kwamba hakuwa na habari kuhusu uvumbuzi uliofanywa na Kopeniko na Galileo kuwa dunia huzunguka jua?

Kwa kadiri fulani, hali hiyo ilichangiwa na mawasiliano mabaya kati ya Mashariki na Magharibi. Lakini kulikuwa na tatizo lingine. Hali ya kidini wakati huo pia ilichangia. Wasomi Wahindi walikataa kusafiri Ulaya kwa sababu wangepoteza tabaka lao ikiwa wangevuka bahari. Wengi wa watu kutoka Ulaya waliomsaidia Jai Singh kukusanya habari walikuwa wasomi Wayahudi. Kulingana na V. N. Sharma, ambaye aliandika simulizi la maisha la Jai Singh, waumini Wayahudi na Wakatoliki walikatazwa kukubali maoni ya Galileo na wanasayansi wengine kwamba dunia huzunguka jua, la sivyo wangeadhibiwa. Kanisa liliona maoni hayo kuwa uzushi na imani ya kwamba hakuna Mungu. Hivyo haishangazi kwamba wajumbe waliotumwa Ulaya na Jai Singh hawakununua vitabu vya Kopeniko na Galileo au vifaa vipya vilivyokuwa vikitumiwa kuunga mkono nadharia ya kwamba dunia huzunguka jua.

Jitihada ya Kutafuta Habari Kuhusu Nyota Yaendelea

Jai Singh aliishi katika kipindi ambacho watu walikuwa na ubaguzi wa kidini. Licha ya kutumia akili na jitihada nyingi kutoa habari za karibuni kuhusu vitu vya angani, kwa miaka mingi, kulikuwa na maendeleo machache katika nyanja hii nchini India. Hata hivyo, kituo cha kutazama angani cha Jantar Mantar kinaonyesha jitihada za mtu aliyetamani sana kupata ujuzi.

Kwa karne nyingi kabla Jai Singh hajaanza kupendezwa na jinsi nyota zinavyosonga, watu wengine wenye akili walikuwa wakitazama anga na kujaribu kuelewa maajabu ya ulimwengu. Bila shaka, wanadamu wataendelea ‘kuinua macho yao juu’ mbinguni katika jitihada ya kuongeza ujuzi wao kuhusu kazi za Mungu.—Isaya 40:26; Zaburi 19:1.

[Mchoro/Picha katika ukurasa wa 18]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Samrat yantra ilikuwa saa sahihi ya kivuli. Kivuli cha pembetatu kubwa kilianguka kwenye sehemu ya robo iliyojipinda (ona duara nyeupe kwenye picha) yenye vipimo

[Mchoro/Picha katika ukurasa wa 18]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Jayaprakash yantra ina nusu-duara zilizobonyea zenye alama juu ya sehemu iliyobonyea. Nyaya mbili zinazopitana zilivutwa kati ya sehemu za nje za nusu-duara hizo.

Akiwa ndani ya Ram yantra, mtazamaji angeweza kujua mahali nyota fulani ilipo kwa kutumia alama mbalimbali au ukingo wa dirisha

[Mchoro/Picha katika ukurasa wa 18]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Kifaa cha Mishra yantra kilionyesha saa sita mchana zilipofika katika majiji mbalimbali

[Picha katika ukurasa wa 19]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Mstari wa kutazama nyota, uliotumiwa tangu zamani, ulisahihishwa kabisa na Jai Singh

Ili kutafuta nyota, unahitaji kujua iko juu kadiri gani angani na umbali wake kutoka kaskazini kuelekea mashariki

Katika Samrat yantra, ilichukua watu wawili kutafuta nyota na kurekodi mahali ilipokuwa

[Hisani]

Bottom: Reproduced from the book SAWAI JAI SINGH AND HIS ASTRONOMY, published by Motilal Banarsidass Publishers (P) Ltd., Jawahar Nagar Delhi, India

[Ramani katika ukurasa wa 19]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

INDIA

New Delhi

Mathura

Jaipur

Varanasi

Ujjain

Jai Singh alijenga vituo vitano vya kutazama vitu angani huko India, kutia ndani kimoja jijini New Delhi

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 18]

Portrait: Courtesy Roop Kishore Goyal