Kutembelea Kisiwa cha Man
Kutembelea Kisiwa cha Man
NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI UINGEREZA
UNAWEZA kwenda wapi ili kuwaona papakiotajua? Mahali pazuri zaidi pa kuwaona ni karibu na Kisiwa cha Man kwenye Bahari ya Ireland. Watalii husafiri kwa meli kutoka Kisiwa cha Man ambacho kiko umbali sawa kutoka Uingereza, Ireland, Scotland, na Wales, ili kutazama samaki hao wapole wenye uzito wa tani tano ambao hula tu majani ya baharini. Bill Dale, mwanamazingira wa kisiwa hicho alisema, hapa ndipo “mahali pazuri zaidi pa kutalii bila kuharibu mazingira.”
Kisiwa cha Man kikoje? Kisiwa hicho chenye ukubwa wa kilometa 570 za mraba, kina wakazi 70,000, mabonde yenye mimea, nyika zisizo na miti, maziwa na vijito, ghuba maridadi, miamba, na pwani yenye mawemawe. Njoo tutembelee baadhi ya sehemu zenye kupendeza za kisiwa hiki ambacho ni mojawapo ya visiwa vya Uingereza vyenye mambo mengi ya historia.
Mambo Yanayowavutia Watalii
Mara nyingi, watalii wanaozuru Kisiwa cha Man hutaka sana kumwona paka anayeitwa Manx. Mnyama huyo wa pekee ana uso wa paka lakini miguu yake ya nyuma ni mirefu kuliko ya mbele, kwa hiyo yeye husimama kama sungura. Isitoshe, paka huyo hana mkia. Ingawa haijulikani paka huyo alitoka wapi, imedokezwa kwamba karne nyingi zilizopita mabaharia walileta watoto wa paka huyo kutoka Asia, ambako kuna paka wasio na mkia, na hivyo kukawa na paka wa aina hii katika Kisiwa cha Man.
Mashindano ya pikipiki yanayoitwa Isle of Man Tourist Trophy, ambayo hufanywa kila mwaka, pia huwavutia watu wengi. Barabara kuu ambazo hutumiwa zina urefu wa zaidi ya kilometa 60. Katika mashindano ya kwanza yaliyofanywa mwaka wa 1907, mwendo wa kasi zaidi ulikuwa kilometa 65 hivi kwa saa. Siku hizi mwendo ambao mshindi husafiri huwa angalau kilometa 190 kwa saa. Bila shaka, mchezo huo ni hatari, na kwa miaka mingi waendeshaji kadhaa wameuawa. *
Magari yaliyokokotwa na farasi katika kijia huko Douglas, mji mkuu wa kisiwa hicho, ni mojawapo ya vikumbusho vya nyakati zilizopita, na ndivyo na Reli ya Magari-Moshi ya Mvuke ya Kisiwa cha Man yenye urefu wa kilometa 24, ambayo ndiyo sehemu inayobaki tu ya reli iliyozunguka kisiwa chote wakati mmoja. Miaka 100 hivi iliyopita, Shirika la Reli ya Umeme la Manx lilifunguliwa, na baadhi ya magari yake bado hukwea meta 600 hadi kwenye kilele cha juu zaidi cha Manx kinachoitwa Snaefell.
Gurudumu Kuu la Laxey
Risasi, fedha, na zinki zilichangia kusitawi kwa kisiwa hicho, hasa katika Mgodi Mkuu wa Laxey. Gurudumu Kuu la Laxey huonyesha ustadi wa mainjinia wa zama za Victoria waliolijenga mwaka wa 1854 na ustadi wa msanii wake Robert Casement, aliyekuwa mwana wa mtengenezaji magurudumu. Lina kipenyo cha zaidi ya meta 20 na lilizungushwa kwa maji yaliyotiririka kutoka kwenye tangi juu ya bonde. Gurudumu hilo lilipozunguka mara mbili na nusu kwa dakika moja, lilitokeza nguvu za kutosha kupiga lita 950 za maji kutoka kina cha meta 360, na hivyo kuondoa maji katika mashimo ya migodi. Sehemu iliyokombo ya ekiseli hiyo ambayo imeunganishwa na fito kadhaa zenye urefu wa meta 180 hivi, ilitumiwa kuendesha mfumo wa kupiga maji kwenye mgodi. Ekiseli pekee ya gurudumu hilo kubwa ina uzito wa tani kumi.
Upande wa kusini wa nyumba ya gurudumu hilo, kuna sanamu ya chuma ya Three Legs of Man, ambayo ina kipenyo cha meta mbili. Nembo hii ambayo sasa inatumiwa kuwakilisha Kisiwa cha Man ilitoka wapi na ina maana gani?
Baada ya mwaka wa 1246, sanamu hiyo ilikuwa katika mihuri iliyopigwa kwenye hati za serikali kama ishara rasmi ya kisiwa hicho. Mchoro wake umepatikana katika chombo cha kuwekea maua cha Ugiriki cha karne ya sita K.W.K. na unahusiana na msalaba wa Ugiriki. Inakubaliwa kwamba nembo hiyo inawakilisha miale ya jua na inahusiana na ibada ya jua. Nembo hiyo ilifikaje kwenye Kisiwa cha Man? Huenda ilipelekwa huko na wafanyabiashara waliopitia Bahari ya Mediterania kutoka Sisili, kisiwa ambacho kilitumia ishara hiyo au ililetwa na maharamia Waskandinavia walioitumia katika sarafu zao. Sanamu ya miguu hiyo mitatu
iliyovishwa viatu vya vita kama inavyoonekana leo ilianza kutumiwa na wafalme wa baadaye wa Man.Pindi Nzuri na Mbaya za Kisiwa Hicho
Waroma walishinda Uingereza mwaka wa 43 W.K. na kukaa huko kwa miaka 400 hivi, lakini ni kana kwamba walipuuza kisiwa cha Man, ambacho Yulio Kaisari alikiita Mona. Maharamia Waskandinavia walivamia kisiwa hicho katika karne ya 9 na kukaa huko hadi katikati ya karne ya 13. Wavumbuzi hao jasiri kutoka Skandinavia waliona kisiwa hicho kuwa kinafaa kwa ajili ya biashara na kuvamia maeneo jirani. Wakati huo ndipo bunge la Manx linaloitwa Tynwald, lilianzishwa. Inasemekana kwamba bunge hilo ndilo bunge la kitaifa lililodumu kwa muda mrefu zaidi ulimwenguni bila kukatizwa. *
Baadaye, Kisiwa cha Man kilitawaliwa nyakati tofauti-tofauti na Scotland, Wales, Ireland, Uingereza, na Norway. Kisha, mnamo 1765, Bunge la Uingereza likanunua kisiwa hicho. Leo, gavana luteni wa kisiwa hicho ni mwakilishi wa kibinafsi wa Malkia wa Uingereza, na kisiwa hicho hujitawala ingawa bado kiko chini ya usimamizi wa Uingereza huku kikiwa na uhuru wa kadiri fulani wa kufanya biashara bila kulipa kodi za Uingereza. Pia kisiwa hicho kina stempu, sarafu, na noti zake ambazo zina thamani sawa na pesa za Uingereza.
Uhusiano Kati ya Kimanx na Kiselti
Lugha ya kale ya Kisiwa cha Man ni Manx, ambayo imetokana na lugha za Kiselti ambazo ni kati ya lugha nyingi zilizozungumzwa India na Ulaya. Manx imetokana na Kiselti cha Ireland na inahusiana na Kiselti cha Scotland. Zaidi ya miaka 100 iliyopita, ilisemekana kwamba Kimanx “ni lugha ambayo itatoweka, sawa na jiwe la barafu linaloelea kuelekea kusini.” Na ndivyo ilivyotukia. Mwenyeji wa mwisho aliyezungumza Kimanx alikufa mwaka wa 1974, akiwa na umri wa miaka 97; lakini ili kuhifadhi utamaduni wa kisiwa hicho, sasa Kimanx kinafunzwa tena shuleni.
Tofauti na Kiselti cha Ireland au Kiselti cha Scotland, Kimanx hakikuandikwa hadi mwishoni mwa mwaka wa 1610. Mnamo 1707, kitabu The Principles and Duties of Christianity, kilikuwa kitabu cha kwanza kuchapishwa katika Kimanx. Baada ya muda, vitabu vingine vilichapishwa katika Kimanx.
Kufikia 1763, maombi ya hima yalitolewa ili Biblia ya Kimanx itafsiriwe kwa sababu wakati huo thuluthi mbili ya wakazi wa kisiwa hicho walizungumza Kimanx peke yake. Kwa sababu hakukuwa na vifaa vingi na wasomi wengi wa kufanya kazi hiyo, vitabu mbalimbali vya Biblia vilianza kutafsiriwa tangu mwaka wa 1748. Mnamo 1775, nakala 40 za Biblia nzima zilichapishwa ili kutumiwa na makasisi, na mnamo 1819, nakala 5,000 zikachapishwa kwa ajili ya umma. Watu waliitikiaje? Mwanamke mmoja alisema hivi kwa hisia nyingi baada ya mwana wake kumsomea Biblia ya Kimanx: “Tumekuwa gizani kwa muda mrefu hadi sasa.”
Watu 25 walitafsiri Biblia hiyo kutoka katika Biblia ya Kiingereza ya King James Version ya mwaka wa 1611, na wachache kati yao waliweza kuchunguza tafsiri ya Kigiriki ya Maandiko ya Kiebrania, ya Septuajinti. Jina la Mungu limebaki vilevile kama katika Kiingereza, yaani, Jehovah. * Kwa kweli, kama vile W. T. Radcliffe alivyoandika katika mwaka wa 1895, Biblia hiyo ni “uandishi wa pekee na hakuna mwenyeji wa Manx mwenye elimu anayeweza kuidharau.”
Ukristo Leo
Wakazi wa kisiwa hicho bado wanaiheshimu Biblia, nao Mashahidi wa Yehova wanajulikana kwa kuwafundisha watu Biblia. Jumba lao la Ufalme la karibuni zaidi lilijengwa Mei 1999 katika eneo lenye kuvutia chini ya Mlima Belmont, huko Douglas. Likiripoti kuhusu jengo hilo lililojengwa kwa siku sita na wajitoleaji ambao wote walikuwa Mashahidi wa Yehova, gazeti Isle of Man Examiner lilisema hivi: “Kazi hiyo inaweza kuonwa kuwa muujiza mdogo.”
Ikiwa unaweza kutembelea kisiwa hiki chenye kupendeza, uwe na hakika kwamba wakazi wapole wa kisiwa hiki watafanya ufurahie sana matembezi yako. Lakini uwe mwangalifu unapozungumza na mwenyeji wa Manx. Kwa maoni yake, Kisiwa cha Man ndicho “kisiwa kikuu;” Uingereza ni “kisiwa kile kingine.”
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 7 Ona simulizi la Fred Stevens aliyekuwa mwendeshaji wa pikipiki katika mashindano ya Tourist Trophy, lililochapishwa katika makala “The Greater Challenge, the Greater Thrill!” katika gazeti la Amkeni!, Septemba 22, 1988 la Kiingereza.
^ fu. 14 Mabunge mawili, baraza la watunga-sheria la Wafaroese na bunge la Waiceland, yalianzishwa mapema zaidi, lakini hayakudumu.
^ fu. 20 Jina la Mungu katika Kiselti cha Ireland na Kiselti cha Scotland ni Yehobhah, na katika lugha ya watu wa Wales ni Jehofah.
[Ramani katika ukurasa wa 14]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
IRELAND
SCOTLAND
UINGEREZA
WALES
Bahari ya Ireland
KISIWA CHA MAN
[Picha katika ukurasa wa 15]
Gari la Shirika la Reli ya Umeme la Manx
[Picha katika ukurasa wa 15]
Gurudumu Kuu la Laxey
[Picha katika ukurasa wa 14, 15]
Reli ya Magari-Moshi ya Mvuke ya Kisiwa cha Man
[Picha katika ukurasa wa 15]
Paka asiye na mkia anayeitwa “Manx”
[Picha katika ukurasa wa 16]
Papakiotajua
[Picha katika ukurasa wa 16]
Mandhari ya pwani kutoka Mlima Peel
[Picha katika ukurasa wa 16, 17]
Bandari ya Peel, kasri ya Peel ikiwa nyuma yake
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 15]
All photos except center emblem: Copyright Bill Dale, IsleOfManPhotos.com
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 16]
Shark: The Basking Shark Society; right inset and background: Copyright Bill Dale, IsleOfManPhotos.com