Divai, Mbao, na Utengenezaji wa Mapipa
Divai, Mbao, na Utengenezaji wa Mapipa
CHOKOLETI, kungumanga, vanila, au mkate uliounguzwa. Hayo ni baadhi ya maneno ambayo hutumiwa na watengenezaji wa divai ili kuelezea ladha ya divai. Ni vitu gani ambavyo hutokeza ladha hizo tofauti-tofauti? Aina ya zabibu, ubora wa udongo, na hali ya hewa huchangia. Hata hivyo, tangu karne ya kwanza, watengenezaji wa divai wameongeza kitu kingine mbali na vitu zaidi ya 400 ambavyo hutokeza ladha na harufu ya divai. Kitu hicho chenye ladha kali ni mbao, lakini si mbao yoyote tu, bali mbao ya pekee inayoitwa mwaloni mweupe.
Mbao ilianzaje kutumiwa katika kutengeneza divai? Na kwa nini watengenezaji wa divai bora hupendelea kutumia mbao za mwaloni?
Mbao Zatumiwa Badala ya Ngozi na Udongo
Mapema katika historia, mwanadamu aligundua mbinu ya kutengeneza divai. (Mwanzo 9:20, 21) Watengenezaji wa divai walitia maji ya zabibu ndani ya vyombo vya udongo au chupa zilizotengenezwa kwa ngozi za wanyama, na kuyaacha yachache. Vyombo vya ngozi na udongo vilitumiwa kuhifadhi na kusafirisha divai hadi wakati wa Kristo. (Mathayo 9:17) Hata hivyo, karibu na wakati huo, mbinu nyingine ya kuhifadhi na kusafirisha divai ilianza kuwa maarufu.
Mwanahistoria wa karne ya kwanza Plini Mkubwa aliandika kwamba mafundi walioishi Gaul, sasa ni Ufaransa, walibuni njia ya kuchonga na kuunganisha mbao ili kutengeneza mapipa. Watengenezaji wa mapipa walipitisha ustadi uliohitajiwa wa kutengeneza mapipa hayo muhimu kutoka kizazi hadi kizazi. Mbali na kutengeneza mapipa yasiyoweza kuvuja, ambayo yangeweza kubeba divai na mafuta, mafundi hao walitengeneza mapipa ambayo yangeweza kuvuja. Lakini yalifaa kwa kubeba bidhaa kavu kama vile unga au misumari. Katika kipindi ambacho kusafirisha bidhaa kulitegemea nguvu za mwanadamu na mnyama, kuvumbuliwa kwa mapipa kulikuwa maendeleo makubwa. Kwa nini?
Maendeleo ya Kiteknolojia
Mapipa hayo yalikuwa yenye nguvu sana na pia yangeweza kubingirishwa kwa sababu ya umbo lao lililovimba. Sanduku lililojazwa bidhaa nzito lingehitaji kubebwa na watu kadhaa au mnyama, lakini pipa lenye kiasi kilekile cha bidhaa lingeweza kubingirishwa na mtu mmoja tu. Kwa kuwa mapipa yalikuwa yenye nguvu kuliko vyombo vya udongo na rahisi kusafirisha kuliko masanduku, yalichangia kuongezeka kwa biashara ya bidhaa mbalimbali kwa karne nyingi.
Leo, vyombo vya chuma, plastiki, na kadibodi vinatumiwa sana badala ya mapipa hayo ya zamani. Hata hivyo, bado mafundi wa kutengeneza mapipa wanahitajiwa sana. Huko California, Marekani pekee, watu wapatao 12,000 wameajiriwa katika viwanda vya kutengeneza mapipa ambavyo huleta faida ya zaidi ya dola milioni 211 kila mwaka. Kiwanda kimoja tu huko Napa Valley, California, ambalo ni eneo maarufu la kutengenezea divai hutengeneza mapipa zaidi ya 100,000 kila mwaka. Mapipa hayo hutengenezwaje?
Utengenezaji wa Mapipa ya Mbao
Mapipa bora zaidi hutengenezwa kwa mialoni inayotoka Ufaransa. Kwa sababu ya ubora na wingi wa mbao hizo, asilimia 45 hivi ya mapipa yote ya divai hutengenezwa nchini humo. Baada ya wakataji-miti kukata miti ya kati ya miaka 100 na 200, kiwanda cha mbao huikata kuwa magogo na kuipasua kwa uangalifu kulingana na mwelekeo wa nyuzi na kutokeza vipande vya mbao. Vipande hivyo vya mbao visipokatwa vizuri, vitavunjika vinapopindwa au vitavuja pipa linapojazwa divai. Vipande hivyo huwekwa nje ambako jua, upepo, na mvua huondoa kemikali chungu kutoka kwenye mbao hizo na kuboresha harufu nzuri ya mialoni. Lazima mbao hizo ziwekwe nje kwa mwaka mmoja hadi minne kabla ya mtengenezaji wa mapipa kuzitumia.
Unapotembelea kiwanda cha kutengeneza mapipa utaona jinsi kazi hiyo ilivyofanywa zamani. Hewa imejaa harufu ya mialoni na kelele za misumeno, randa, na nyundo. Kwa kufuata mbinu ambayo imetumiwa kwa muda mrefu, fundi huchonga mbao hizo hivi kwamba ni pana katikati na nyembamba kwenye miisho. Yeye huchonga pande za mbao hizo ili ziweze kufanyiza umbo la pipa zinaposimamishwa pamoja. Kisha yeye hupigilia mkanda wa chuma kwenye mwisho mmoja wa duara ya vipande hivyo vya mbao, na kufanya pipa hilo ambalo halijakamilika lifanane na sketi iliyopanuka upande wa chini.
Yeye huinua pipa hilo zito juu ya moto ili kupasha mbao hizo joto. Baadaye, yeye hutia maji upande wa ndani wa pipa hilo ambalo halijakamilika ili kuvukiza na kulainisha mbao hizo. Kisha, fundi huyo huzungusha kamba au waya kuzunguka upande ule mwingine wa pipa hilo na kuikaza, na hivyo kupinda mbao hizo ili zitokeze umbo la pipa. Kisha yeye hupigilia mikanda ya chuma isiyo ya kudumu kwenye mwisho ule mwingine; ile ya kudumu hupigiliwa baadaye. Kufikia hapa, pipa hilo halijazibwa juu na chini.
“Kuchoma” Pipa
Baada ya kutengeneza pipa, fundi huchonga sehemu fulani ya ndani ya kila upande ili aweze kuingiza mbao za mviringo zitakazofunika pipa hilo. Vifuniko hivyo vya mviringo hutengenezwa kwa mabamba ya mialoni na kutiwa matete membamba katikati. Matete hayo huziba mianya yoyote ili pipa lisivuje vifuniko hivyo vinapofura au kubonyea.
Kabla ya vifuniko kuwekwa, huenda fundi akaweka pipa juu ya moto, ili kuchoma kidogo upande wa ndani kwa miale. Mtengenezaji wa divai aliyeagiza pipa hilo ndiye huamua ikiwa pipa hilo litachomwa kidogo au litaunguzwa. Kuchoma mbao kwa njia hii huongeza ladha ambazo mwaloni utatokeza kwenye divai. Pia huenda vifuniko vikachomwa vikiwa peke yake. Kisha fundi hufunika pipa na kutoboa tundu kando ya pipa litakalotumiwa kujaza au kutoa divai. Hatimaye, yeye hupiga msasa na kusafisha upande wa nje wa pipa na kulisafirisha hadi kwenye kiwanda cha kutengeneza divai.
“Vikolezo vya Mtengenezaji wa Divai”
Bob, meneja wa kiwanda kimoja cha kutengeneza divai cha California anasema, “mwaloni ndio mti unaofaa zaidi kukoleza divai yetu.” Akitembeza wageni katika kiwanda hicho, anaeleza hivi: “Mwaloni ndio mti pekee unaoweza kutengeneza mapipa yenye nguvu na wenye uwezo wa kuboresha ladha ya divai.” Bob anasema hivi huku akielekezea kidole safu za mapipa: “Divai inapokolea ndani ya pipa, pipa hilo huwa kama pafu. Oksijeni hupenya polepole ndani ya mbao na kuingia kwenye pipa, na hivyo kufanya divai ichangamane na oksijeni. Jambo hilo hufanya divai idumishe rangi yake na iwe na ladha laini. Wakati huohuo, pipa hutoa alkoholi na maji, ambayo huvukizwa hewani. Chachu hutulia chini ya pipa, nayo sukari na kemikali chungu za mwaloni hujichuja ndani ya divai, na kufanya iwe na ladha yake ya pekee. Ikitegemea aina ya divai, huenda divai iliyo kwenye pipa ikakolezwa kwa miezi 18 au zaidi kabla ya kutiwa ndani ya chupa na kupakiwa.”
Bob anaendelea kusema: “Mapipa yanayowekwa divai hudumu kwa muda mfupi tu. Sisi hukoleza baadhi ya divai yetu bora ndani ya mapipa mapya ya mwaloni kwa sababu baada ya kutumiwa mara moja vikolezo vingi vya mbao zake huisha. Mapipa yanaweza kutumiwa zaidi ya mara moja, lakini baada ya kutumiwa mara kadhaa yanaweza kuanza kufanya divai ziwe na ladha zisizopendeza.”
Akieleza kwa nini ni muhimu kuchagua mwaloni uliokuzwa mahali fulani, Bob anasema: “Mwaloni mweupe uliokuzwa huko Limousin, Ufaransa, utatokeza ladha tofauti na wa jamii ileile iliyopandwa huko Missouri, Marekani.” Kwa nini itofautiane? “Aina ya udongo, hali ya hewa, na muda ambao miti imedumu, ni baadhi ya mambo ambayo hutokeza tofauti hizo. Namna ambavyo mbao hukaushwa, iwe ni kwenye tanuri au kuanikwa nje, pia huathiri ladha ya divai. Mapipa bora zaidi ya divai hutengenezwa kwa mbao zilizokaushwa nje. Mengi ya mapipa yetu yametengenezwa kwa mialoni ya Marekani au ya Ufaransa au kutoka nchi zote mbili, lakini pia mialoni inayofaa kutengeneza mapipa hukuzwa huko China na Ulaya Mashariki.”
Mwishoni mwa matembezi, Bob anasema: “Mambo hayo mbalimbali, yaani, aina ya mwaloni uliotumiwa, kadiri ambavyo pipa litachomwa, na muda ambao divai itakaa ndani ya pipa, ni kama vikolezo vya mtengenezaji wa divai, ambavyo humwezesha kubadili ladha ya divai. Hivyo unapokunywa divai nyekundu bora, usifikirie tu wakati na jitihada iliyofanywa kutengeneza divai hiyo bali pia ustadi wa kutengeneza pipa ambalo lilitumiwa kufanya divai hiyo ikolee.”
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 26]
Ni Mapipa ya Mwaloni au Ni Unga wa Mwaloni?
Divai fulani nyeupe, kama vile chardonnay hukolezwa kwenye mapipa ya mwaloni. Hata hivyo, si divai zote nyeupe hukolezwa kwenye mapipa ya mwaloni. Watengenezaji fulani wa divai hutokeza ladha ya mwaloni kwa kutumbukiza vipande vya mwaloni ndani ya mapipa ya divai ya chuma isiyoshika kutu au kwa kuongeza unga wa mwaloni kwenye divai inapokolea ndani ya mapipa ya chuma au ya saruji.
[Picha katika ukurasa wa 24]
Mialoni bora kabisa ndiyo hutumiwa kutengeneza mapipa ya divai
[Picha katika ukurasa wa 24]
Magogo hukatwa kwa kutumia mashini ya haidroli
[Picha katika ukurasa wa 24]
Lazima mbao zikatwe kulingana na nyuzi zake, la sivyo vipande vya mbao vitapenya maji
[Picha katika ukurasa wa 25]
Mbao zilizo tayari kutumiwa kutengeneza pipa
[Picha katika ukurasa wa 25]
Baada ya kuchoma mapipa juu ya moto, mbao hufungwa pamoja kwa mkanda wa chuma
[Hisani]
Seguin-Moreau, France
[Picha katika ukurasa wa 25]
Divai hukolezwa ndani ya mapipa ya mwaloni ili kuboresha ladha yake
[Picha katika ukurasa wa 26]
Watengenezaji wa mapipa huko Paris, mapema katika karne ya 20
[Hisani]
© Cliché Bibliothèque nationale de France, Paris
[Picha katika ukurasa wa 27]
Kuonja divai iliyokomaa ndani ya mapipa, karibu mwaka wa 1900
[Hisani]
© Cliché Bibliothèque nationale de France, Paris
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 24]
© Sandro Vannini/CORBIS