Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Je, Misiba ya Asili Inaongezeka?

Je, Misiba ya Asili Inaongezeka?

Je, Misiba ya Asili Inaongezeka?

“Inatazamiwa kwamba matukio yasiyo ya kawaida yanayosababishwa na kubadilika kwa hali ya hewa yatatokeza madhara makubwa zaidi wakati ujao. Kwa hiyo tunapaswa kuwa tayari kukabiliana na hatari mpya zinazosababishwa na hali ya hewa na uwezekano wa kupata hasara kubwa zaidi. . . . Kupatana na kanuni ya kujikinga mapema, ni muhimu kujitayarisha mapema kwa ajili ya mabadiliko makubwa.”—“Topics Geo—annual Review: Natural Catastrophes 2003.”

KATIKA kiangazi cha 2003, sehemu fulani za Ulaya zilikumbwa na joto jingi sana. Joto hilo jingi lilisababisha vifo vya watu wapatao 30,000 huko Hispania, Italia, Ubelgiji, Ufaransa, Uholanzi, Uingereza, na Ureno. Joto kali la kabla ya mvua za msimu huko Bangladesh, India, na Pakistan lilisababisha vifo 1,500, na ukame na joto jingi sana huko Australia zikasababisha mioto ya msituni ambayo iliteketeza zaidi ya ekari milioni saba.

Kulingana na Shirika la Utabiri wa Hali ya Hewa Ulimwenguni, “msimu wa tufani wa Atlantiki wa 2003 ulitokeza dhoruba 16 zilizopewa majina. Idadi hiyo ilizidi wastani wa dhoruba 9.8 zilizotokea kila mwaka kuanzia 1944 hadi 1996, lakini zinapatana na ongezeko la kila mwaka linaloonekana wazi la dhoruba na tufani zinazotokea katika maeneo ya tropiki tangu miaka ya katikati ya 1990.” Ongezeko hilo liliendelea mnamo 2004, kulipotokea tufani zilizosababisha madhara makubwa huko Karibea na Ghuba ya Mexico, ambako watu 2,000 hivi walikufa na uharibifu mkubwa ukatokea.

Mnamo 2003, Sri Lanka ilikumbwa na kimbunga kilichosababisha mafuriko makubwa yaliyowaua watu 250 hivi. Mnamo 2004, angalau tufani 23 zilitokea magharibi mwa Pasifiki. Kumi kati yake zilikumba Japani, ambako zilisababisha madhara makubwa na vifo zaidi ya 170. Mafuriko yaliyosababishwa na mvua nyingi za msimu yaliathiri watu wapatao milioni 30 huko Asia Kusini, hasa Bangladesh. Mamilioni waliachwa bila makao, karibu watu milioni tatu wakalazimika kutoroka makwao na zaidi ya 1,300 wakafa.

Matetemeko makubwa kadhaa ya nchi yalitokea mwaka wa 2003. Katika Mei 21, tetemeko la nchi lilijeruhi watu 10,000 na kuacha 200,000 bila makao huko Algiers, Algeria. Desemba 26, saa 11:26 alfajiri, tetemeko kubwa la nchi lilitokea kilometa nane kusini ya jiji la Bam huko Iran. Tetemeko hilo la kipimo cha 6.5 liliharibu asilimia 70 ya jiji hilo, likaua watu 40,000, na kuacha watu zaidi ya 100,000 bila makao. Huo ndio msiba mbaya zaidi wa asili uliotukia mwaka huo. Pia liliharibu sehemu kubwa ya ngome ya Arg-e-Bam iliyokuwa imedumu kwa miaka 2,000, na kufanya jiji la Bam lipoteze pesa zinazoletwa na watalii ambao huja kuiona.

Mwaka mmoja kamili baadaye, tetemeko lenye kipimo cha 9.0 lilitokea karibu na pwani ya magharibi ya kaskazini mwa Sumatra, Indonesia, na kutokeza mojawapo ya tsunami mbaya zaidi katika historia. Mawimbi hayo yalisababisha vifo zaidi ya 200,000, yakajeruhi na kuacha watu wengi zaidi bila makao. Madhara ya tetemeko hilo yalifika pwani ya mashariki mwa Afrika, iliyoko umbali wa kilometa 4,500 au zaidi magharibi ya mahali tetemeko hilo lilipotokea.

Je, Tutazamie Misiba Mingi Zaidi?

Je, matukio hayo yanaonyesha mambo yatakayotukia wakati ujao? Kuhusiana na misiba inayotokana na hali ya hewa, wanasayansi wengi wanaamini kuwa mabadiliko ya hewa yanayosababishwa na wanadamu yanabadili hali ya hewa ulimwenguni na kufanya iwe mbaya zaidi. Ikiwa hilo ni kweli, hali itakuwa mbaya zaidi wakati ujao. Kuongezea hatari hiyo, watu wengi zaidi huishi katika maeneo yanayoweza kuathiriwa na misiba kwa sababu ya hali au kwa kutaka.

Takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 95 ya misiba yote inayosababisha vifo hutukia katika nchi zinazositawi. Kwa upande mwingine, watu wachache zaidi hufa katika nchi tajiri lakini hizo hupata asilimia 75 ya hasara ya kiuchumi. Mashirika fulani ya bima hujiuliza ikiwa yataweza kulipia hasara zinazozidi kuongezeka.

Katika makala inayofuata, tutachunguza baadhi ya mambo ya asili yanayosababisha misiba na njia ambazo huenda wanadamu wanachangia na kuifanya iwe mibaya zaidi. Tutachunguza pia iwapo mwanadamu ana uwezo na nia ya kufanya mabadiliko yanayohitajiwa ili dunia iwe salama zaidi kwa vizazi vijavyo.

[Picha katika ukurasa wa 3]

UFARANSA 2003, Joto jingi wakati wa kiangazi huko Ulaya lawaua watu 30,000; Hispania yafikisha nyuzi 44.8 Selsiasi

[Hisani]

Alfred/EPA/Sipa Press

[Picha katika ukurasa wa 4, 5]

IRAN 2003, Tetemeko la nchi huko Bam lawaua watu 40,000; wanawake waombolezea jamaa zao katika kaburi la jumla

[Hisani]

Background and women: © Tim Dirven/Panos Pictures