Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kubaki Hai Kunapotegemea Kujificha

Kubaki Hai Kunapotegemea Kujificha

Kubaki Hai Kunapotegemea Kujificha

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI HISPANIA

KILA siku wadudu hukabili matatizo mawili makubwa: jinsi ya kupata chakula cha kutosha na jinsi ya kuepuka kuliwa. Wadudu ni chakula kinachopendwa na ndege, vyura, na mijusi. Ili waendelee kuwa hai, wadudu wengi hujipatanisha na mazingira yao.

Ili wasionekane, wadudu mbalimbali hujificha kwa njia ya ajabu. Uwezo wa hali ya juu wa kufanya hivyo unazidi uwezo wowote wa kubuni wa wanadamu. Fikiria mifano mitatu ya pekee.

Vipepeo wanaoitwa dead-leaf. Sehemu ya chini ya mabawa yao yenye rangi ya kahawia hufanana sana na jani lililokauka. Mbali tu na rangi ya mabawa yao, mabawa hayo yana muundo unayoyafanya yaonekane kana kwamba yana mishipa na mashina kama ya majani. Hila hiyo hufanikiwa sana hivi kwamba vipepeo hao wanapotua kwenye majani mabichi, wao hufanana kabisa na jani kavu lililoanguka kutoka mtini.

Nyenje wa kichakani, au katididi. Nyenje wengi wa kichakani huendelea kuwa hai si kwa kuiga majani makavu, bali kwa kuiga majani mabichi. Kitabu kimoja kinaeleza hivi: “Ufanani huo hautii ndani umbo na rangi pekee: unahusisha pia miundo ya mishipa na madoadoa yenye maumbo tofauti-tofauti ya jani lililoliwa na kuvu.” Ukiangalia kwa makini picha iliyo kwenye ukurasa unaofuata, utaona madoadoa hayo madogo kwenye bawa la mdudu huyo, ambayo humfanya afanane kabisa na majani mabichi yaliyoliwa na kuvu.

Panzi-mti. Si rahisi kuwaona wadudu hao wadogo. Na hiyo ndiyo siri yao ya kuendelea kuwa hai, wao hujipatanisha na mazingira kwa kuiga miiba. Katika kisa hiki, kila mdudu huonekana kama mwiba, na kikundi kikubwa cha wadudu hao hujipanga juu ya tawi na kulifanya lionekane kana kwamba lina miiba. Mtu anapoangalia kwa makini ndipo tu atatambua kwamba “miiba” hiyo ni panzi-mti wadogo.

Inashangaza kuona hila mbalimbali ambazo wadudu hutumia kujificha kikamili. Kiwavi wa Kosta Rika huonekana tu kama kinyesi cha ndege, hali si rahisi kuwatofautisha wadudu wanaoitwa ukunikianzi na ukuni. Kuna nzige wa Afrika Kusini anayefanana sana na jiwe, na mdudu anayepatikana nchini Israel huiga kikamili mmea unaotoa maua ambayo mdudu huyo hula.

Iwe mdudu atatumia hila gani, hiyo humlinda na kutuonyesha kwa njia ya ajabu unamna-namna wenye kupendeza wa uumbaji.

[Picha katika ukurasa wa 22]

Ukunikianzi akitembea

[Picha katika ukurasa wa 23]

Kipepeo anayeitwa “dead-leaf”

[Hisani]

Zoo, Santillana del Mar, Cantabria, España

[Picha katika ukurasa wa 23]

Panzi-mti

[Picha katika ukurasa wa 23]

Nyenje wa kichakani

[Picha katika ukurasa wa 23]

Kiwavi anayefanana na kinyesi cha ndege

[Hisani]

© Gregory G. Dimijian/Photo Reasearchers