Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Watoto Wenye Matatizo Wanaweza Kurekebika

Gazeti The Sydney Morning Herald linasema: “Watoto wengi wa shule za msingi wenye matatizo hurekebika kadiri wanavyokua. Wanaweza kuwa vijana waliokomaa na wenye adabu.” Utafiti uliofanywa na Taasisi ya Australia ya Uchunguzi wa Familia ulichunguza maendeleo ya watoto 178 wenye umri wa miaka 11 au 12 ambao walionyesha sifa hizi tatu au zaidi, yaani, “kuwa wachokozi sana, kutotaka kushirikiana na wengine, kutojidhibiti, kutoweza kukazia fikira jambo kwa muda mrefu, kuwa watendaji kupita kiasi, na kukasirika haraka.” Miaka sita baadaye, vijana 100 kati yao walionyesha tabia “zinazokaribiana sana na za kikundi cha vijana wenye tabia nzuri.” Ni nini kilichowasaidia kubadilika? Ripoti hiyo inasema: “Watoto waliobadilika na kuwa vijana wenye furaha hawakushirikiana na marika wasio na urafiki [na] pia kuna uwezekano kwamba wazazi wao waliwasimamia vizuri.”

Dubu-jike Hawazuiwi na Watalii

Gazeti la Uingereza, New Scientist linaripoti kwamba “huenda kuwepo kwa watalii wenye kelele wasioharibu mazingira, kukanufaisha dubu wa kahawia walio porini.” Mara nyingi watu wanaotembelea mazingira ya asili yaliyojificha huvuruga tabia ya wanyama, na nyakati nyingine husababisha madhara. Hata hivyo, ripoti hiyo inasema kwamba watafiti wa Uingereza na Marekani wanaochunguza dubu wa kahawia katika mahali ambapo samoni huzalisha huko magharibi mwa Kanada “waligundua kwamba ingawa dubu wa kiume huepuka watalii, . . . dubu-jike na watoto wao hawaogopi watu, bali wao huona kelele za mabasi kuwa ishara ya kwamba dubu wa kiume walio hatari wameondoka mtoni. Hata wakati dubu wa kiume walipoondoka kabisa kwenye eneo hilo, dubu-jike hawakujitokeza hadi watalii walipofika.” Inaonekana kwamba dubu-jike hutumia nafasi hiyo nzuri kula katika maeneo bora zaidi bila kuwa na wasiwasi kwamba watoto wao watashambuliwa na dubu wa kiume.

Kufanya Kazi Ukiwa Mgonjwa

Gazeti Telegraph la Uingereza lililo katika Intaneti linaripoti kwamba “watu wanaojilazimisha kwenda kazini licha ya kuwa wagonjwa,” huenda wakawa wanazidisha uwezekano wa kupata ugonjwa wa moyo. Wanasayansi katika University College huko London walichunguza afya na rekodi za kufika kazini za wafanyakazi wa umma zaidi ya 10,000 huko London kwa kipindi cha miaka zaidi ya kumi. Bwana Michael Marmot, mkurugenzi wa utafiti huo alisema kwamba kati ya asilimia 30 na 40 ya wafanyakazi ambao hawakupumzika nyumbani walipokuwa wagonjwa, hata walipokuwa tu na homa, “walipatwa na ugonjwa wa moyo mara mbili katika miaka iliyofuata.”

Neno Gumu Zaidi Kutafsiri Ulimwenguni

Shirika la Utangazaji la Uingereza linasema: “Neno gumu zaidi kutafsiri ulimwenguni ni ‘ilunga’ la lugha ya Tshiluba,” inayozungumzwa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Neno hilo ndilo lililopigiwa kura nyingi zaidi katika kura iliyopigwa na wataalamu elfu moja wa lugha. Ilunga linamaanisha “mtu aliye tayari kusamehe kosa lolote analotendewa mara ya kwanza, kulivumilia mara ya pili, lakini si mara ya tatu kamwe.” Neno lingine lililopigiwa kura nyingi ni neno la Kijapani naa linalotumiwa tu “katika eneo la Kansai la Japani kutilia mkazo taarifa au kukubaliana na mtu.” Jurga Zilinskiene, mkurugenzi mkuu wa shirika la kutafsiri na kufasiri ambalo lilisimamia utafiti huo anasema kwamba “nyakati nyingine watu husahau kwamba lazima . . . mtafsiri atafsiri si kutoka tu lugha moja hadi nyingine bali kutoka utamaduni mmoja hadi mwingine, [na] nyakati nyingine, wazo lile halipo katika tamaduni zote mbili.”

Kusoma ili Kujifurahisha Huchangia Maksi za Juu

Gazeti Milenio la Mexico City linaripoti kwamba kusoma ili kujifurahisha huchangia maksi bora kuliko “kutumia saa nyingi kujifunza, kufundishwa na wazazi, kusoma maandishi waliyoandika darasani, au kutumia kompyuta.” Uchunguzi kuhusu mitihani zaidi ya nusu milioni iliyofanywa na wanafunzi waliotaka kuingia shule za upili ulionyesha kwamba wanafunzi ambao hutumia wakati kujifunza masomo ya shuleni na kusoma ili kujifurahisha wanaelekea kufanikiwa zaidi shuleni. Vitabu ambavyo wanafunzi wanachagua si lazima vihusu masomo ya shule tu bali vinaweza kutia ndani vitabu vinavyosomwa ili kujifurahisha, kama vile wasifu, vitabu vya mashairi, na vyenye habari za kisayansi. Kwa upande mwingine, ripoti hiyo inasema kwamba vijana ambao hutazama televisheni kwa vipindi virefu kwa siku badala ya kusoma hupata maksi za chini.

Udanganyifu wa Habari Kuhusu Elimu na Ujuzi

Ingawa kwa ujumla watu wanaotafuta kazi hutaka kuwaonyesha watu ambao huenda wakawaajiri kuwa wanastahili, wengine wao hudanganya kabisa. Gazeti The Sydney Morning Herald linaripoti kwamba uchunguzi uliofanywa na kampuni ya Australian Background kuchunguza watu waliotaka kuajiriwa uligundua kwamba kati ya watu 1,000 wanaotafuta kazi, asilimia 21 walidanganya wale waliotazamiwa kuwa waajiri wao kuhusu kustahili kwao. Isitoshe, gazeti hilo linasema kwamba “asilimia 60 ya watu wenye rekodi ya uhalifu hawakutaja jambo hilo hata walipoulizwa.” Gary Brack, mkurugenzi wa kampuni inayowasaidia watu kupata kazi anasema: “Huenda mtu anayeomba kazi akadai kwamba amewahi kutawala ulimwengu. Lakini unapochunguza kidogo kazi aliyokuwa akifanya, huenda ikawa alitawala sehemu ndogo tu ya ofisi.”

Kutofanya Mazoezi Ni Hatari Zaidi Kuliko Kuvuta Sigara

Uchunguzi wa zoea la kufanya mazoezi la wakaaji 24,000 wa Hong Kong waliokufa mwaka wa 1998 ulionyesha kwamba “kuishi bila kufanya mazoezi ni hatari zaidi kuliko kuvuta sigara.” Gazeti South China Morning Post linaripoti kwamba uchunguzi huo ulionyesha kuwa kutofanya mazoezi kulizidisha hatari za kufa mapema kwa asilimia 59 kwa wanaume na asilimia 33 kwa wanawake. Lam Tai-hing, msimamizi wa idara ya matibabu ya kijamii ya Chuo Kikuu cha Hong Kong alisema: “Inanufaisha ikiwa huvuti sigara. Lakini ikiwa hufanyi mazoezi, [bado] unakabili hatari kubwa sana.” Kulingana na Profesa Lam, hata kufanya mazoezi kidogo ni afadhali kuliko kutofanya hata kidogo. Anapendekeza kwamba badala ya kuketi kwa nusu saa, tembea au fanya kazi za nyumbani.

Kaswende Inaongezeka

Gazeti la kila juma la Italia Panorama linasema kwamba nchini humo, visa vya ugonjwa wa zinaa wa kaswende “vimeongezeka zaidi ya maradufu katika miaka miwili iliyopita.” Kulingana na Giampiero Carosi, mkurugenzi wa uchunguzi wa magonjwa ya kuambukiza na ya kitropiki katika Chuo Kikuu cha Brescia, visa vingi vinahusu hasa vijana ambao hawajawahi kuhudhuria mafunzo ya kuzuia UKIMWI na ambao huenda hospitalini baada ya kufanya ngono mara ya kwanza. Gazeti Panorama linasema kwamba asilimia 40 ya wale walioambukizwa kaswende hufikia hatua ya tatu ya ugonjwa huo, ambapo “madhara yaliyotukia katika viungo vya ndani huenea kwenye ubongo, moyo, mifupa, maungo, macho, na ini.”