Kwa Nini Watu Wengi Sana Huishi kwa Woga?
Kwa Nini Watu Wengi Sana Huishi kwa Woga?
WANADAMU wanakumbwa na woga mwingi. Woga ni hisia isiyoweza kuonekana ambayo humpata kila mtu, ingawa mara nyingi haitambuliwi. Hali hiyo imesababishwa na nini? Ni nini huwafanya watu fulani waogope wanapotoka nyumbani? Kwa nini watu wengi hawajihisi wakiwa salama kazini? Kwa nini watu wengi huwa na wasiwasi kuhusu usalama wa watoto wao? Ni hatari gani huwafanya watu wawe na woga wakiwa ndani ya nyumba zao?
Bila shaka, kuna sababu nyingi ambazo huwafanya watu wawe na woga lakini tutazungumzia hatari nne zinazoweza kuwapata watu daima, yaani, jeuri katika majiji, kusumbuliwa kingono, kulalwa kinguvu, na jeuri nyumbani. Kwanza na tuchunguze jeuri katika majiji. Habari hiyo inafaa sasa kwa sababu karibu nusu ya watu ulimwenguni huishi katika majiji.
Hatari Katika Majiji
Huenda ikawa majiji ya kwanza yalijengwa kwa ajili ya ulinzi, lakini watu wengi leo huona majiji kuwa maeneo hatari. Mahali ambapo wakati mmoja palionwa kuwa penye ulinzi sasa panaogopesha. Majiji yenye watu wengi ni mahali panapopendwa na majambazi, na katika majiji fulani, maeneo ya maskini yaliyo na taa chache barabarani na polisi wachache ni hatari.
Nyakati nyingine, watu huwa na sababu nzuri ya kuogopa kwani watu wengi sana hufa kikatili. Kulingana na ripoti moja ya Shirika la Afya Ulimwenguni, kila mwaka, watu milioni 1.6 huuawa kikatili ulimwenguni pote. Barani Afrika, kati ya kila watu 100,000, wastani wa watu 60.9 huuawa kikatili kila mwaka.
Watu, maeneo, na mashirika mengi yaliyoonwa kuwa mahali salama sasa yanaonwa kuwa tisho kwa usalama. Kwa mfano, viwanja vingi vya michezo, shule, na maduka sasa yanaonwa kuwa maeneo yenye uhalifu mwingi sana. Katika visa fulani, viongozi wa kidini, wafanyakazi wa jamii, na walimu, ambao wanapaswa kuandaa ulinzi, wamewakatisha watu tamaa. Ripoti kwamba baadhi ya watu hao huwatendea vibaya watoto huwafanya wazazi wasite kuwaacha watoto wao chini ya ulinzi wa wengine. Polisi wanapaswa kuwalinda watu, lakini katika majiji fulani ni jambo la kawaida kwa polisi kuwa wafisadi na kutumia mamlaka vibaya. Kuhusu walinda “usalama,” katika nchi fulani bado watu hukumbuka vita vya wenyewe kwa wenyewe ambavyo wapendwa wao walitoweka baada ya kuchukuliwa na wanajeshi. Kwa hiyo, katika sehemu mbalimbali za ulimwengu, badala ya kupunguza woga, polisi na wanajeshi wamefanya watu wawe na woga mwingi hata zaidi.
Kitabu Citizens of Fear—Urban Violence in Latin America kinasema: “Wakazi wa majiji makuu ya Amerika Kusini huishi kwa woga daima, chini ya hali hatari zaidi duniani. Katika eneo hilo kubwa, watu wapatao 140,000 hufa kikatili kila mwaka, na raia mmoja kati ya watatu ameathiriwa na jeuri moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja.” Pia katika sehemu nyingine za dunia, maandamano ya kisiasa hutukia mara nyingi katika miji mikuu. Maandamano hayo yanapokuwa na jeuri, watu wengi hutumia nafasi hiyo kupora vitu madukani, huku ghasia zikizuka. Wanaofanya biashara jijini wanaweza kujipata katikati ya umati wenye hasira.
Katika nchi nyingi, kumekuwa na pengo kubwa kati ya hali ya maisha ya matajiri na maskini na hilo limetokeza chuki isiyo ya wazi. Vikundi vikubwa vya watu wenye vurugu ambao huhisi wamenyimwa mahitaji ya msingi wamepora maeneo ambako matajiri huishi. Hilo bado halijatendeka katika majiji fulani, lakini inaonekana kwamba hali hiyo italipuka, ni kwamba tu hakuna ajuaye ni lini.
Huenda tisho la wezi na mapinduzi likaogopesha watu, lakini kuna mambo mengine yanayosababisha wasiwasi na hivyo kuzidisha hali ya woga.
Woga Unaosababishwa na Kusumbuliwa Kingono
Kila siku, mamilioni ya wanawake huogopa sana kupigiwa mbinja, kufanyiwa ishara za matusi, na kutazamwa kwa njia ya kimahaba. Gazeti Asia Week linasema: “Uchunguzi unaonyesha kwamba mwanamke mmoja Mjapani kati ya wanne ametendewa vibaya kingono hadharani, huku asilimia 90 ya visa hivyo vikitokea katika magari ya moshi. . . . Asilimia 2 tu ya waathiriwa ndio huchukua hatua wanapotendewa hivyo. Wengi walisema kuwa hawakuchukua hatua yoyote kwa sababu ya kuwaogopa watu waliowatendea vibaya.”
Kusumbuliwa kingono kumeongezeka sana nchini India. Mwandishi mmoja wa habari nchini humo anasema kwamba “kila mara mwanamke anapotoka nje ya nyumba yake yeye huogopa. Kila anapopiga hatua yeye huaibishwa na kutukanwa.” Ripoti moja kutoka jiji fulani la India
ambako wakaaji hujivunia kuwa na barabara salama kwa kadiri inasema: “[Jiji hili] halina tatizo barabarani bali ofisini. . . . Asilimia 35 ya wanawake waliohojiwa walidai kwamba walisumbuliwa kingono kazini. . . . Asilimia 52 ya wanawake walisema kwamba kwa sababu ya kusumbuliwa kingono kazini wao hupendelea kufanya kazi za mishahara midogo . . . mahali ambapo watashughulika [tu] na wanawake.”Woga wa Kulalwa Kinguvu
Kuna jambo ambalo huwaogopesha wanawake zaidi kuliko kupoteza heshima yao. Nyakati nyingine, kusumbuliwa kingono ni kama kutishwa kulalwa kinguvu. Inaeleweka kwa nini wanawake wengi huogopa kulalwa kinguvu kuliko kuuawa. Huenda mwanamke akajipata akiwa peke yake mahali ambapo anaogopa kuwa anaweza kulalwa kinguvu. Huenda akamwona mwanamume asiyemjua au asiyemwamini. Moyo wake unapiga haraka-haraka huku akiwa na wasiwasi anapojaribu kuchanganua hali hiyo. ‘Atafanya nini? Nitakimbia wapi? Je, nipige mayowe?’ Visa kama hivyo vinapotukia mara nyingi, hudhoofisha afya ya mwanamke pole kwa pole. Watu wengi huamua kutoishi mijini au kutotembea mijini kwa sababu ya kuogopa mambo kama hayo.
Kitabu The Female Fear kinasema: “Wanawake wengi wanaoishi mijini hukabiliana na woga, wasiwasi, na kuteseka kila siku. Woga wa kulalwa kinguvu huwafanya wanawake wahisi kwamba wanapaswa kujilinda daima wasishambuliwe, kuwa macho na chonjo, jambo ambalo hufanya mwanamke awe na wasiwasi mtu fulani anapotembea nyuma yake, hasa usiku. Hiyo ni . . . hisia ambayo wanawake huwa nayo daima.”
Wanawake wengi huathiriwa na uhalifu wenye jeuri. Hata hivyo, karibu wanawake wote huathiriwa na woga wa jeuri. Kichapo cha Umoja wa Mataifa, The State of World Population 2000, kinasema: “Ulimwenguni pote, angalau mwanamke mmoja kati ya watatu amewahi kupigwa, kulazimishwa kufanya ngono, au kutendewa vibaya kwa njia nyingine, mara nyingi na mtu anayemjua.” Je, woga huo mwingi umeenea sehemu nyingine? Ni jambo la kawaida kadiri gani kwa watu kuishi kwa woga ndani ya nyumba zao wenyewe?
Kuogopa Jeuri Nyumbani
Kupiga wake kisiri ili kuwafanya watii ni ukosefu mkubwa wa haki unaotendeka ulimwenguni pote, na hivi karibuni tu ndipo jambo hilo limeonwa kuwa uvunjaji wa sheria katika sehemu nyingi. Huko India, ripoti moja ilidai kwamba “angalau asilimia 45 ya wanawake Wahindi huzabwa makofi, hupigwa mateke au kuchapwa na waume zao.” Kutendewa vibaya na mwenzi ni jambo linalosababisha tatizo baya sana la afya ulimwenguni. Shirika la Upelelezi la Marekani linaripoti kwamba wanawake walio kati ya umri wa miaka 15 na 44 nchini humo hujeruhiwa kupitia jeuri ya nyumbani kuliko jumla ya majeraha wanayopata kutokana na aksidenti za magari, kuvamiwa na majambazi, na kulalwa kinguvu. Kwa hiyo, jeuri ya nyumbani ni hatari zaidi kuliko ugomvi wa kawaida ambao huishia kwa kuchapana makofi. Wanawake wengi huishi kwa woga wa kujeruhiwa au kuuawa wakiwa nyumbani. Uchunguzi wa kitaifa uliofanywa nchini Kanada ulionyesha kwamba wakati mmoja, thuluthi ya wanawake waliojeruhiwa nyumbani waliogopa kwamba wangeuawa. Nchini Marekani, watafiti wawili walikata kauli hivi: “Nyumbani ndipo mahali hatari zaidi kwa wanawake na mara nyingi wao hutendewa kwa ukatili na kuteswa wakiwa huko.”
Kwa nini wanawake wengi hushindwa kuvunja mahusiano hayo hatari? Watu wengi hujiuliza: ‘Kwa nini hawatafuti msaada? Kwa nini wasiondoke?’ Mara nyingi woga ndio huwazuia. Imesemekana kwamba woga ndio hasa huendeleza jeuri ya nyumbani. Kwa kawaida, wanaume ambao huwatendea vibaya wake zao hutumia jeuri kuwadhibiti kisha kuwanyamazisha kwa kuwatisha kwamba watawaua. Hata kama mwanamke anayepigwa atakuwa na ujasiri wa kutafuta msaada, huenda asisaidiwe. Hata watu wanaochukia jeuri za aina nyingine huelekea kupunguza uzito, kupuuza,
au kutetea jeuri inayosababishwa na waume. Pia, huenda mume ambaye humtendea mke wake vibaya, akaonwa na watu wengine kuwa mtu mwenye kupendeza. Mara nyingi, marafiki hawawezi kuamini kwamba yeye humpiga mke wake. Wanawake wengi ambao hutendewa vibaya huhisi kwamba hawana la kufanya ila kuishi kwa woga daima kwa kuwa watu hawawaamini nao hawana mahali pa kutorokea.Nyakati nyingine, wanawake ambao huamua kuondoka hukabili usumbufu mwingine, yaani, kunyemelewa. Uchunguzi wa hivi karibuni uliofanyiwa wanawake zaidi ya elfu moja katika jimbo la Louisiana, huko Amerika Kaskazini ulionyesha kwamba asilimia 15 ya wanawake hao waliripoti kwamba walinyemelewa. Unaweza kuwazia woga waliokuwa nao. Mtu ambaye amekutisha anaendelea kukunyemelea kila mahali unapoenda. Anakupigia simu, anakufuata, anakutazama, na kukungojea. Huenda hata akamuua mnyama wako kipenzi. Ameazimia kukuogopesha!
Huenda hujapatwa na woga wa aina hiyo. Lakini woga huathiri utendaji wako wa kila siku kwa kadiri gani?
Je, Woga Huathiri Utendaji Wako?
Kwa kuwa tunaishi kwa woga, huenda tusitambue jinsi ambavyo woga huathiri maamuzi tunayofanya kila siku. Woga huathiri utendaji wako mara nyingi kadiri gani?
Je, wewe au washiriki wa familia yako huogopa kurudi nyumbani mkiwa peke yenu usiku kwa sababu ya kuogopa jeuri? Je, wewe huogopa kutumia usafiri wa umma? Je, hatari za kusafiri zimefanya uchague kazi utakayofanya? Au je, kuwaogopa wafanyakazi wenzako au watu wengine ambao lazima ushughulike nao kumeathiri uchaguzi wako wa kazi? Je, woga umeathiri uhusiano wako na wengine au tafrija unazofurahia? Labda woga wa kukutana na walevi na watu wenye fujo umekuzuia kwenda kutazama michezo na maonyesho fulani? Je, woga umeathiri mambo unayofanya shuleni? Kwa sababu ya wazazi wengi kuogopa kwamba watoto wao watakuwa wahalifu, wao huchagua shule watakazowapeleka, na woga huo pia hufanya wazazi wengi kwenda kuwachukua watoto wao shuleni kwa gari ingawa wangeweza kutembea au kutumia usafiri wa umma kurudi nyumbani.
Kwa kweli wanadamu wanaishi kwa woga mwingi. Lakini wanadamu wameogopa jeuri kwa muda mrefu. Je, kweli tunaweza kutarajia mabadiliko? Je, kuishi bila woga ni ndoto tu? Au je, kuna sababu nzuri ya kutarajia kwamba wakati ujao watu wataishi bila kuogopa chochote?