Sabuni Jinsi Ilivyopata Kuwa Muhimu
Sabuni Jinsi Ilivyopata Kuwa Muhimu
NI BIDHAA chache sana zilizo muhimu na ambazo hutumiwa sana kama sabuni. Kuanzia utotoni, sisi hutumia sabuni kila siku. Tangu ilipotengenezwa kwa mara ya kwanza, sabuni imeacha kuwa bidhaa ya matajiri wachache na kuwa bidhaa muhimu inayotumiwa kila siku.
Kwa kweli, mwanakemia mmoja wa karne ya 19 alisema kwamba utajiri na ustaarabu wa taifa huamuliwa na kiasi cha sabuni kinachotumiwa. Leo, sabuni huonwa kuwa muhimu kwa usafi na afya. Bidhaa hiyo muhimu ilianzaje kutumiwa kila siku?
Nyakati za Kale
Kuna uthibitisho mdogo sana kwamba sabuni ilitumiwa kuoga kabla ya Wakati wa Kawaida. Ni kweli kwamba Biblia inasema hivi katika Yeremia 2:22: “Hata ukijiosha kwa magadi na kujichukulia kiasi kikubwa cha sabuni.” Hata hivyo, kuna sababu za kutilia shaka kwamba “sabuni” inayotajwa hapo ni sawa na zile tunazotumia leo, ziwe ni za vipande, unga, au za aina nyingine. Badala ya hivyo, inaonekana kwamba andiko hilo linazungumza kuhusu alkali fulani iliyotumiwa kusafisha ambayo ni tofauti sana na sabuni zinazotumiwa leo.
Wagiriki na baadaye Waroma walitumia mafuta yenye harufu nzuri kuoga. Huenda walijifunza kutengeneza sabuni kutoka kwa Waselti. Katika kitabu chake Natural History, mwandishi Mroma wa karne ya kwanza, Plini Mkubwa anatumia neno la Kiselti saipo, ambalo inasemekana neno la Kiingereza na Kifaransa la sabuni limetokana nalo.
Katika karne zilizofuata, matumizi ya sabuni yalitajwa mara chache ingawa katika Zama za Kati, Italia, Hispania, na Ufaransa zilitengeneza sabuni. Hata hivyo, licha ya jitihada za kutengeneza sabuni kwa wingi, inaonekana kwamba sabuni haikutumiwa sana huko Ulaya. Kwa kweli, kufikia mwaka wa 1672, wakati Mjerumani mmoja alipomtumia mshiriki fulani wa familia ya kifalme zawadi ya sabuni kutoka Italia kama ishara ya kumtakia mema, aliona inafaa kuweka maagizo kuhusu jinsi ya kutumia bidhaa hiyo ya ajabu!
Utengenezaji wa Sabuni Nyakati za Kale
Mojawapo ya maagizo ya kwanza kuhusu utengenezaji wa sabuni yanapatikana katika mkusanyo wa karne ya 12 wa siri za watengenezaji sabuni. Kwa miaka mingi, mbinu ya kutengeneza sabuni haijabadilishwa. Mafuta ya maji-maji na yaliyoganda kutoka vitu mbalimbali yalichemshwa pamoja na magadi soda na kufanyiza sabuni ambayo haikuwa imesafishwa. Hatua hiyo inaitwa usabunishaji.
Inaeleweka kwamba ubora wa sabuni hutegemea vitu vilivyotumiwa. Hapo zamani, majivu ya mbao na mafuta ya wanyama yalitumiwa kutengeneza sabuni, na watu waliohamia huko Marekani zamani walitumia vitu hivyo kutengeneza sabuni
yenye rangi ya kahawia na laini kama jeli waliyotumia kila siku. Shahamu, yaani mafuta ya ng’ombe na kondoo yaliyoyeyushwa ndiyo yaliyotumiwa hasa kutengeneza sabuni na mishumaa wakati huo, kwa hiyo mara nyingi wafanyabiashara walitengeneza na kuuza bidhaa zote mbili. Baada ya kuchemshwa, watengenezaji sabuni waliongeza chumvi na kutia harufu ya mrujuani na kisibiti ili kutokeza sabuni ngumu iliyosafirishwa kwa urahisi.Kwa kawaida, sabuni kutoka kusini mwa Ulaya zilitengenezwa kwa mafuta ya mzeituni. Watengenezaji sabuni wa maeneo yenye baridi waliendelea kutumia shahamu. Wengine hata walitumia mafuta ya samaki. Ingawa sabuni hizo zilifaa kufulia nguo, hazikufaa kwa kuogea! Hata hivyo, mafuta ya maji-maji na yaliyoganda ni sehemu tu ya vitu vinavyotumiwa kutengeneza sabuni.
Sabuni Yatengenezwa Viwandani
Kwa karne nyingi, magadi yaliyohitajiwa ili kutengeneza sabuni yalitokana na majivu ya miti hususa kutia ndani mimea ya baharini. Huko Hispania, mmea unaoitwa saltwort ulichomwa na kutokeza jivu lenye magadi lililoitwa barilla. Jivu hilo lilipochanganywa na mafuta ya mzeituni lilitokeza sabuni bora nyeupe iliyoitwa sabuni ya Castile.
Katika karne ya 18 nchi nyingi zilikuwa na uhitaji mkubwa wa potashi iliyotumiwa kutengeneza sabuni, glasi, na baruti. * Mnamo 1790, Nicolas Leblanc, daktari-mpasuaji na mwanakemia Mfaransa, alibuni mbinu ya kutengeneza magadi kutokana na chumvi ya kawaida. Baadaye, wanakemia walifaulu kutengeneza magadi soda kutokana na maji ya chumvi. Hatua hizo zilichangia kutokea kwa viwanda vya kutengeneza sabuni.
Sabuni Yapata Umaarufu
Mwisho wa karne ya 19 ulikuwa wakati wa mabadiliko makubwa yaliyotia ndani jitihada za kuelimisha watu kuhusu afya na usafi. Hata hivyo, sabuni iliyotumiwa wakati huo ilikuwa ya rangi ya kahawia na isiyopendeza, nayo ilikuwa na mabaki ya magadi yaliyowasha ngozi. Bado ilitengenezwa kwa mikono, kwa kuchemshwa ndani ya mapipa. Mwenye duka alipata sabuni hiyo ikiwa vipande vikubwa visivyokuwa na jina la mtengenezaji, kisha akaikata vipande-vipande na kuuzia umma kulingana na uzito.
Sabuni fulani zilikuwa na povu jingi lakini zilitokeza matone ya mafuta yaliyofanya vidole viwe na mafuta na baada ya muda sabuni hizo zilioza. Kwa kuzingatia mahitaji ya watu, watengenezaji walianza kutia ndani vitu kama citronella iliyokuwa na harufu kama ya ndimu ili kuondoa harufu mbaya.
Maendeleo zaidi yangefanywa. Sabuni zenye kupendeza zilizotengenezwa kwa mafuta ya mboga zilianza kuwa maarufu. Mabadiliko makubwa yaliyofanywa katika usafiri yalifanya iwe rahisi zaidi kwa watengenezaji sabuni kupata vitu vingi
bora vya kutengeneza sabuni. Michikichi ilikuzwa huko Afrika Magharibi, na umaji-maji fulani wenye rangi nyangavu na wenye mafuta uliotolewa katika tunda lake ulitumiwa kutengeneza sabuni na vipodozi. Mbata, yaani, nazi iliyokaushwa ambayo hutokeza mafuta ya nazi, ilitoka katika visiwa vya Pasifiki. Vitu hivyo vilivyotoka mbali viliboresha sabuni.Watengenezaji walielewa tamaa ya watu ya kuwa safi. Ilibidi wanunuzi wasadikishwe kwamba sabuni ni bidhaa ya lazima. Watangazaji walihusianisha matokeo ya bidhaa zao na asali, nuru ya jua, na theluji. Wengine walichora upya picha maarufu na kufanya matangazo yao na sabuni zionekane kuwa nzuri zaidi na za kisasa. Kufikia mwanzo wa karne ya ishirini sabuni ilikuwa ikiuzwa ulimwenguni pote. Ilichochea kuwepo kwa matangazo mengi ya biashara. Mnamo 1894, matangazo ya kuchochea watu wanunue sabuni yaliwekwa kwenye stempu nchini New Zealand. Sasa sabuni ikaanza kuwa maarufu.
Jinsi Inavyotengenezwa Leo
Zamani, bidhaa zilizotengeneza sabuni zilichemshwa katika vyungu vikubwa. Mtu mwenye ustadi alitumia mwiko kukoroga mchanganyiko huo. Ikitegemea jinsi mchanganyiko huo ulivyoteleza kutoka kwenye mwiko, angeweza kujua ikiwa alihitaji kuongeza vitu fulani kwenye mchanganyiko huo.
Leo utengenezaji wa sabuni unahusisha hatua tatu. Hatua ya kwanza ni usabunishaji ambao unatia ndani kuchanganya mafuta mbalimbali na magadi ili kutokeza mchanganyiko mzito wa sabuni na gliseroli ambao asilimia 30 ni maji. Nyakati nyingine, mchanganyiko huo huchemshwa katika pipa, lakini watengenezaji wengi wa sabuni leo hutumia kompyuta katika hatua hiyo. Hatua ya pili ni kukausha kwa kutumia joto na hewa ili kutokeza vidonge vidogo vya sabuni vilivyo na asilimia 12 hivi ya maji. Katika hatua ya tatu na ya mwisho vidonge hivyo hutiwa marashi, rangi, na vitu vingine ambavyo hufanya sabuni iwe ya kipekee na yenye harufu nzuri. Vipande vya sabuni hutiwa ndani ya kisindilio na kufanyizwa katika maumbo mbalimbali. Siku hizi watumiaji wa sabuni hutaka ziwe na harufu ya matunda na mimea ili kufanya sabuni ionekane kuwa na vitu vya “asili,” na iburudishe zaidi!
Ingawa maendeleo makubwa yamefanywa ili kuelewa vitu ambavyo hufanyiza sabuni, nao utengenezaji wa sabuni umefanyiwa mabadiliko, bado sabuni ya kawaida inapendwa. Watu wengi watakubali kwamba sabuni inahitajika ili kuwa safi na wenye afya. Lakini bado inashangaza kwamba katika ulimwengu ambao uchafu wa kiadili na wa kiroho umeenea, ni rahisi kudumisha usafi wa kimwili kuliko wakati mwingine wowote. Hata hivyo, usafi wa nje huwa muhimu zaidi unapodhihirisha usafi wa mtu wa ndani.
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 14 Potashi ni mabaki ya magadi yaliyochemshwa na kukaushwa kabisa. Poda laini nyeupe hutokea potashi inapookwa hadi uchafu wote kuondolewa.
[Picha katika ukurasa wa 12]
Utengenezaji wa sabuni nyakati za mapema huko Amerika Kaskazini
[Picha katika ukurasa wa 13]
“Povu” lililochorwa na Bwana John E. Millais, iliyotumiwa kutangaza sabuni
[Picha katika ukurasa wa 13]
Kuchemsha vitu vinavyotumiwa kutengeneza sabuni katika pipa
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 13]
Top: Victoria & Albert Museum, London/Art Resource, NY; bottom: © Jeff Greenberg/Index Stock Imagery