Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Barafu Juu ya Ikweta

Barafu Juu ya Ikweta

Barafu Juu ya Ikweta

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI KENYA

JOHANN LUDWIG KRAPF, mmishonari Mjerumani mwenye umri wa miaka 39, alidai kwamba aliona mlima uliokuwa na theluji kwenye kilele katika eneo la ikweta la Afrika, Desemba 3, 1849. Ripoti yake ilidhihakiwa na wanajiografia wa Ulaya. Walisema kwamba alikuwa ameona chaki tu. Krapf ambaye alikuwa zaidi ya kilometa 140 kutoka kwenye mlima huo, alikubali kwamba aliona kilele hicho kwa dakika chache tu kabla ya kufunikwa na wingu.

Krapf hakushangazwa na dhihaka ya wanajiografia hao. Mwaka mmoja mapema ripoti kuhusu kuonekana kwa mlima mrefu zaidi Afrika, uliokuwa kilometa 300 kusini mwa mlima aliouona, ilikuwa imetiliwa shaka pia. Hata hivyo, muda mfupi baadaye, ilithibitishwa kwamba mlima huo upo, yaani, Mlima Kilimanjaro, ulio na urefu wa meta 5,895. Nayo madai ya Krapf yalithibitishwa miaka 34 baadaye, miaka miwili baada ya kifo chake!

Mnamo 1883, Joseph Thomson, mvumbuzi Mskoti alithibitisha kuwepo kwa Mlima Kenya ambao Krapf aliona wenye urefu wa meta 5,199 ambao una theluji na vilele vyake viko kusini tu mwa ikweta. Mlima huo ndio wa pili kwa urefu Afrika. Watu fulani wanafikiri kwamba wakati mmoja Mlima Kenya, ambao sasa ni volkano isiyotenda, ulikuwa na urefu wa zaidi ya meta 6,000. Inasemekana kwamba mmomonyoko uliondoa vumbi na majivu na kuacha wazi vilele viwili vilivyochongoka vyenye urefu wa zaidi ya meta 5,100 na kilele cha tatu chenye urefu wa meta 4,985.

Uliabudiwa na Wenyeji

Muda mrefu kabla ya Wazungu kuja Afrika, watu walioishi katika maeneo ya chini ya Mlima Kenya waliabudu mlima huo. Wengine waliamini kwamba muumba wa ulimwengu aliishi katika kilele kirefu zaidi cha mlima huo na huko ndiko alimuumba mwanadamu. Pia iliaminika kwamba muumba huyo ndiye aliyeleta mvua iliyonyesha kwenye mashamba yenye rutuba yaliyo chini ya mlima huo. Ili kumtuliza, dhabihu za wanyama zilitolewa na zingali zinatolewa na wale wanaoshikilia imani hiyo.

Kwa sababu ya theluji na barafu iliyo katika vilele vyeusi vya Mlima Kenya, wakazi wa mapema waliuita mlima wenye madoadoa na mlima mweupe. Vilele vitatu virefu zaidi vya mlima huo, yaani, Batian, Nelion, na Lenana vilipewa majina ya chifu mashuhuri wa jamii ya wenyeji. Sehemu hiyo ni maridadi zaidi kwa sababu ina maziwa mengi ya mlimani yenye rangi hafifu ya kijani kibichi.

Una Mimea na Wanyama Wengi

Mlima huo una mandhari nyingi zenye kupendeza kwa wale wanaopendezwa na maumbile. Kwa miaka mingi, barafu inayoyeyuka imegeuza eneo hilo kavu lililotokana na lava na kulifanya liwe lenye rutuba na mimea ya kila aina. Kuna misitu mingi kwenye nyanda za chini. Miti hiyo inatia ndani mierezi, miti ya yew, na kafuri, ambayo hupendwa na maseremala. Pia kuna mianzi mirefu ambayo hufanyiza “msitu” wa nyasi unaokua kufikia urefu wa meta zaidi ya sita na kuzuia mimea mingine isikue.

Eneo hilo lina wanyama wengi. Wanyama wakubwa wanatia ndani simba, chui, pundamilia wa Burchell, nyati, mbawala, na kuro. Pia kuna tembo na vifaru katika mlima huo. Wanyama wadogo wanatia ndani tumbili wa Syke, kima wa rangi nyeusi na nyeupe, tumbili, perere, na jamii mbalimbali za wanyama wadogo.

Kuna ndege wengi wa aina mbalimbali katika eneo hilo. Kuna tumbusi mwenye manyoya meupe mgongoni, kozi, tai, matepe, shakivale wa mlimani, na shakivale mweupe. Ndege hao hula wanyama wadogo na nyoka. Ili kuongeza uzuri wa rangi tofauti kwenye misitu ya kijani kibichi, kuna shorobo mwenye rangi nyekundu, kwezi mwenye rangi ya zambarau, na hondohondo mwenye mashavu ya rangi ya fedha, na vilevile kirumbizi. Jamii fulani za chozi wenye manyoya yenye kuvutia huonekana mara nyingi kwenye msitu wa mlima huo.

Unapofika meta 3,000 juu ya usawa wa bahari, msitu unafikia mwisho na unaona mbuga isiyo na kikomo. Hapo pana nyasi zinazokua kilimani ambazo hufunika ardhi kama mkeka. Mmea mwingine wa kipekee ni ule unaoitwa cabbage groundsel ambao huchanua maua mara moja baada ya miaka 20. Pia kuna mmea unaoitwa tree groundsel wenye majani mapana kwenye sehemu ya juu ya shina na mmea unaoitwa lobelias ambao hukua kufikia meta zaidi ya sita. Mimea hiyo pamoja na mmea-pori mkubwa hutokeza mandhari nzuri ya milimani katika eneo hilo kubwa.

Ni wanyama wachache sana wanaoishi katika sehemu hizo za mlimani na wengi wao huishi huko kwa kipindi fulani tu cha mwaka. Wanyama pekee wanaoishi huko daima ni pimbi. Wao huishi meta 4,300 hivi, eneo lililo juu zaidi kuliko wanyama wengine wanaoishi katika mlima huo. Miili yao huwawezesha kuishi katikati ya miamba katika sehemu hizo zilizo juu. Wao hula hasa mimea. Kwa kuwa ni wenye urafiki na hawawaogopi watu, wanyama hao wanaotoshana na sungura huiba vyakula kutoka kwa wapanda-milima waliochoka na wasiokuwa chonjo!

Kwenye Vilele Maridadi

Vilele maridadi vya mlima huo ni tofauti kabisa na sehemu zake za chini. Vilele vya Batian (meta 5,199) na Nelion (meta 11 chini yake) vinafanana na pembe mbili kubwa. Vilele hivyo vina mawe meusi makubwa ya volkano ambayo huonekana kana kwamba yanaelea juu ya mawingu. Chini ya vilele hivyo, kuna barafu 11 ambazo hazijayeyushwa na jua la ikweta, ambalo liliyeyusha barafu 7 baada ya muda kupita. Sasa barafu kubwa zaidi ni nusu ya jinsi ilivyokuwa miaka 100 iliyopita. Baadhi ya barafu hizo huonekana kutoka mji mkuu wa Kenya, Nairobi, ulio umbali wa kilometa 130.

Mlima huo unaoonekana kutoka mbali umewavutia wapanda-milima kutoka sehemu zote ulimwenguni. Halford Mackinder ndiye aliyekuwa mzungu wa kwanza kufika kwenye kilele cha Batian, Septemba 13, 1899. Ingechukua miaka 30 kabla ya mtu mwingine kuripotiwa kuwa amefika kwenye kilele hicho. Watu fulani wamekufa wakijaribu kupanda hadi kwenye kilele cha mlima huo. Kufikia mwaka wa 1987, zaidi ya watu 60 walikuwa wamekufa.

Wapanda-milima wamepatwa na magonjwa mbalimbali ya mlimani. Kwa kweli, inasemekana kwamba mlima huo umechangia nusu ya visa vyote ulimwenguni vya ugonjwa wa mapafu kujaa maji. Kitabu On God’s Mountain—The Story of Mount Kenya kinasema: “Wale ambao hawapatwi na ugonjwa huo [ugonjwa wa mlimani], huchoshwa sana na kutembea na kupanda hivi kwamba wao hukokota tu miguu yao. Kando yao kuna mteremko mkali wenye urefu wa mamia kadhaa ya meta. Kichwa huuma sana. Mtu huhisi kichefuchefu, ana malengelenge miguuni nayo macho hutoa machozi.”

Ingawa huenda vilele vya Mlima Kenya vimechakaa kwa sababu ya hali ya hewa na barafu zake kupungua, bado mlima huo ni maridadi na ni wenye fahari. Ingawa mlima huo umechongoka, bado umaridadi wake unamsifu kimyakimya Muumba wake, Yehova Mungu.—Zaburi 148:9, 13.

[Ramani katika ukurasa wa 16]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Ikweta

Mlima Kenya

[Picha katika ukurasa wa 16]

Mojawapo ya maziwa mengi ya mlimani

[Picha katika ukurasa wa 17]

Vilele vitatu virefu zaidi vya Mlima Kenya

[Picha katika ukurasa wa 18]

Wapanda-milima kutoka ulimwenguni pote huvutiwa na vilele hivi virefu

[Picha katika ukurasa wa 18]

Kuna ndege wengi kama chozi huyu mwenye kifua chekundu

[Picha katika ukurasa wa 18]

Pimbi huishi meta 4,300 juu ya usawa wa bahari

[Picha katika ukurasa wa 18]

Kwenye nyanda za chini kuna miti, kutia ndani miti ya yew

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 16]

Page 16: Pictures Courtesy of Camerapix Ltd.

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 17]

Picture Courtesy of Camerapix Ltd.

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 18]

All inset photos except climber: Pictures Courtesy of Camerapix Ltd.; background: Duncan Willetts, Camerapix