Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kilitoka Kwenye Anga za Juu

Kilitoka Kwenye Anga za Juu

Kilitoka Kwenye Anga za Juu

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI TANZANIA

JE, UMEWAHI kuona mstari mwangavu wa nuru katika anga lenye nyota nyingi? Labda ulidhani hiyo ni nyota inayoruka. Kwa kweli, mistari hiyo ya nuru inaitwa kwa usahihi zaidi vimondo.

Vimondo vingi vinavyoingia katika anga ya dunia huungua kabisa kabla ya kufika duniani. Hata hivyo, nyakati nyingine vipande hivyo vya mawe au chuma hustahimili joto hilo jingi na kufika duniani. Vipande vingi huwa vidogo, lakini vingine vina uzito wa tani nyingi. Inakadiriwa kwamba kimondo kimoja huko Namibia, Afrika kina uzito wa tani 60 hivi.

Na tutembelee kimondo kimoja huko Mbozi, Tanzania, kinachosemekana kuwa cha nane kwa ukubwa duniani. Kimondo hicho kiko kwenye mlima Marengi katika wilaya ya Mbozi huko kusini mwa Tanzania, karibu na mpaka wake na Malawi na Zambia. Kimondo hicho kina urefu wa meta tatu, upana wa meta moja, na uzito wa tani 16. Asilimia 90 ya kimondo hicho ni chuma, asilimia 9 hivi ni nikeli, na visehemu vyake vidogo vimefanyizwa kwa kobalti, shaba, salfa, na fosforasi.

Hakuna anayejua kimondo hicho kilianguka lini, lakini lazima iwe kilianguka zamani sana kwani hakuna hekaya zozote kukihusu. W. H. Nott, soroveya kutoka Johannesburg, aliandika kwamba aliona kimondo hicho mnamo Oktoba 1930. Tangu wakati huo, mtaro ulichimbwa kukizunguka, na kufanya kionekane kana kwamba kimeinuliwa na kuwekwa juu ya madhabahu ya mawe. Hivyo, kimondo hicho kimebaki mahali kilipoanguka.

Watu fulani wamejaribu kukata sehemu fulani ya kimondo hicho ili kujiwekea kama kumbukumbu, lakini hiyo ni kazi ngumu sana. Mnamo Desemba 1930, Dakt. D. R. Grantham wa Chama cha Jiolojia alipojaribu kukata kisehemu cha karibu sentimeta kumi kwa msumeno, ilimchukua muda wa saa kumi! Kisehemu hicho kinaweza kuonekana katika mkusanyo wa vimondo kwenye Jumba la Makumbusho la Uingereza huko London.

Wageni wanaweza kutembelea kimondo hicho cha Mbozi. Kuna nyumba ndogo ya mapokezi iliyo na benchi kadhaa na meza. Mtunzaji ambaye huishi kwenye nyumba ya udongo iliyo umbali wa meta 50 hivi kutoka kwenye kimondo hicho, anatuomba tuandike majina yetu katika kitabu cha wageni. Tunagundua kwamba wageni wengi kutoka sehemu mbalimbali ulimwenguni wametembelea sehemu hiyo. Tunapitia kijitabu kidogo chenye habari za kimondo hicho, kisha tunapiga picha.

Watoto fulani wanapanda juu ya kimondo hicho na kuwazia kwamba wamebebwa na roketi. Tunapokula mlo karibu na hapo tukifurahia mazingira matulivu, tunastaajabia kitu hicho kisicho cha kawaida kilichosafiri kutoka angani hadi Mbozi.

[Picha katika ukurasa wa 15]

Alama za msumeno kwenye kimondo