Kutenda Kupatana na Dhamiri Njema Humtukuza Mungu
Kutenda Kupatana na Dhamiri Njema Humtukuza Mungu
NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI UKRAINIA
WALIPOKUWA wakirudi nyumbani baada ya kuhudhuria mkutano wa Kikristo, familia ya Chibisov, ambao ni Mashahidi wa Yehova nchini Ukrainia, waliokota kibeti kilichokuwa na vitu vyenye thamani, kutia ndani leseni ya dereva, kadi za mkopo, na fedha taslimu zipatazo dola 500 za Marekani. Katika familia hiyo yenye watu watano, mume tu ndiye aliyekuwa ameajiriwa. Alikuwa akipata mshahara wa dola 70 kwa mwezi. Kwa hiyo, pesa hizo zingaliweza kuwasaidia sana. Walifanyaje?
Mama yao asimulia: “Binti zetu walianza mara moja kujadiliana jinsi ya kukirudisha kibeti hicho kwa mwenyewe, ambaye, kulingana na ile leseni ya dereva, alikuwa mwanamke. Mimi na mume wangu tulifurahi kuona jinsi watoto wetu walivyokuwa wakitumia dhamiri zao zilizozoezwa vizuri. Kesho yake nilimpigia simu mwanamke aliyekuwa amekipoteza kibeti hicho. Akitokwa na machozi kwa furaha, Olha alikuja na kutuambia kwamba yeye na mume wake wana maduka kadhaa madogo mjini kwetu. Pesa zilizokuwa katika kibeti hicho zilikuwa mishahara ya wafanyakazi wao. Isitoshe, mojawapo ya stakabadhi za kifedha zilizokuwa katika kibeti hicho ilikuwa muhimu sana kwa ajili ya rekodi zake za kibiashara.
“Olha alituuliza tulikipata wapi kibeti hicho. Tukamwambia mahali tulipokipata na kumweleza kwamba wakati tulipokipata tulikuwa tukirudi kutoka katika mkutano wa Kikristo. Tulipompa vichapo kadhaa vya Biblia, alivikubali kwa heshima.
“Majuma machache baadaye, Shahidi mwenzetu katika kutaniko letu alituambia kwamba alipokuwa akiwapa wapita-njia vichapo vya Biblia barabarani, mwanamke mmoja alisema kwamba awali hakuwa akiwasikiliza Mashahidi wa Yehova. Hata hivyo, sasa alikuwa tayari si kuwasikiliza tu bali pia kuchukua vichapo. Alisema alibadili nia yake kwa kuwa Mashahidi walikuwa wamemrudishia binti yake kibeti alichokuwa amepoteza.”
[Picha katika ukurasa wa 31]
Familia ya Chibisov