Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuweka Akiba ya Wakati Badala ya Pesa

Benki mpya zimezuka nchini Hispania. Mashirika kadhaa ya kujitolea nchini humo yameanzisha “benki za kuhifadhi wakati” ambazo hutolea watu huduma mbalimbali. “‘Benki ya Wakati’ ndiyo benki ya kwanza isiyotumia pesa,” adai Elvira Méndez, mkurugenzi wa shirika la Hispania linaloitwa Afya na Familia. Benki hizo huwa na orodha ya wananchi wanaojitolea kufanya kazi mbalimbali kama vile kutunza wazee, kulea watoto, kupika, kuosha, au kufundisha. Malipo ni saa, na kazi zote hulipwa kwa kiwango kilekile. Kwa mfano, kufundisha sayansi kwa saa moja ni sawa na kusuka nywele au kukaa na watoto kwa saa moja. Mtu anayefaidika na huduma hizo hulipa kwa kufanya kazi nyinginezo, na wakati anaotumia huongezwa kwenye akiba yake. Hivyo, benki hizo za kuhifadhi wakati hujaribu kupanga na kutia moyo watu wahudumiane kama majirani walivyohudumiana zamani.

Upachishaji Wanyama Vipenzi

Wanyama vipenzi wa kufugwa nyumbani sasa wanapachishwa kupatana na maagizo ya wateja. Gazeti The New York Times laripoti kwamba kisa cha kwanza nchini Marekani ni kile cha mwanamke wa jimbo la Texas aliyeagiza paka. Baada ya kufiwa na Nicky, paka wake aliyekuwa ameishi naye kwa miaka 17, mwanamke huyo aliagiza apachishiwe paka mwingine kutokana na chembe za urithi za Nicky, zilizokuwa zimehifadhiwa kabla ya kifo chake. Ilimgharimu dola 50,000 za Marekani. Yasemekana kwamba paka huyo, anayeitwa Nicky Mdogo, anafanana kabisa na yule paka wa awali, hata katika tabia. Gazeti hilo lasema kwamba kampuni hiyo iliyompachisha Nicky Mdogo inapanga kupachisha mbwa kwa kuwa inatazamia kwamba mbwa wengi zaidi watanunuliwa. David Magnus, mkurugenzi msaidizi wa Kituo cha Maadili ya Tiba ya Viumbe katika Chuo Kikuu cha Stanford huko California, ambaye pia hupinga mazoea hayo, alisema hivi: “Ni jambo lenye kusumbua kiadili na lisilofaa kwa kiasi fulani. Kwa kuwa kwa dola 50,000, angeweza kutunza paka wengi wasio na makao.”

Mbwa Wenye Uwezo wa Kutambua Kifafa

Gazeti moja la Hispania, Diario Médico, laripoti kwamba mbwa fulani wa kufugwa ambao wamekaa nyumbani kwa zaidi ya mwaka mmoja wanaweza kutangulia kuona katika watoto wanaoishi nao ishara za kwamba wanaelekea kuangushwa na kifafa. Watafiti walikata kauli hiyo baada ya kuchunguza familia 45. Wazazi kadhaa walio na watoto wenye kifafa waligundua kwamba kabla ya mtoto kuanza kuanguka, mbwa wao angeanza kutenda “kwa njia isiyo ya kawaida.” Mbwa huyo angemlazimisha mtoto huyo aketi chini au angemwegemea mtoto huyo ili akianguka, asianguke kwa kishindo.

Nchi ya Bhutan Yapiga Marufuku Mauzo ya Tumbaku

Milki ya Bhutan, iliyo katika milima ya Himalaya kati ya India na China, imepiga marufuku biashara zote za vitu vinavyotengenezwa kutokana na tumbaku. Marufuku hiyo haiwaathiri wajumbe wa kigeni, watalii, wala wale wanaofanya kazi katika mashirika yasiyo ya serikali. Inaaminika kwamba Bhutan ndiyo nchi ya kwanza ulimwenguni kuchukua hatua hiyo. Kuvuta sigara hadharani pia hakuruhusiwi. Shirika la habari la BBC lasema kwamba “hatua hizo ni sehemu ya jitihada za serikali za kuifanya Bhutan iwe taifa la watu wasiovuta sigara.”

Kiwewe Utotoni Chahusianishwa na Ugonjwa wa Moyo

Matatizo ya kimwili na kiakili yanayomkumba mtu utotoni huongeza uwezekano wa kuwa na ugonjwa wa moyo baadaye maishani. Kauli hiyo ilifikiwa na watafiti huko Atlanta, Georgia, na San Diego, California, Marekani, ambao walichunguza rekodi za watu wazima 17,337. Gazeti Science News laeleza kwamba waliochunguzwa walikadiriwa kulingana na “ni nani kati yao, ambao walipokuwa watoto, walijionea jeuri nyumbani, walitendwa vibaya kiakili au kimwili au kupuuzwa, au ambao waliishi na mtu aliyefungwa gerezani, aliyetumia dawa za kulevya au vileo, au aliyekuwa na ugonjwa wa akili.” Ilionekana kwamba kadiri walivyojionea mambo yenye kutia kiwewe mapema maishani mwao, “ndivyo kulivyokuwa na uwezekano mkubwa zaidi wa kuugua ugonjwa wa moyo” wakiwa watu wazima.

Damu Yenye Viini Nchini Japani

Wizara ya afya ya Japani imechukua hatua isiyo ya kawaida kwa kutaja “majina ya hospitali 6,916 na wafanyabiashara 17 ambao inaaminika kwamba walikuwa na akiba ya bidhaa ya damu iliyokuwa na viini vya mchochota wa ini aina ya C,” lasema gazeti The Japan Times. Kigandishaji hicho kilisababisha “mojawapo ya misiba mikubwa zaidi nchini Japani tangu vita vilipomalizika.” Kulingana na gazeti hilo, kati ya mwaka wa 1980 na 2001, watu wapatao 290,000 walitibiwa kwa kutumia kigandishaji hicho. Inakadiriwa kwamba 10,000 kati yao waliambukizwa. Wengi wao walikuwa wanawake wajawazito waliotibiwa kwa kigandishaji hicho ili kuzuia kuvuja damu wakati wa kujifungua. Wizara hiyo ilitoa tangazo hilo kufuatia maandamano ya manusura, waliotaka kuujulisha umma kuhusu tatizo hilo na kumchochea yeyote ambaye huenda alitibiwa kwa kigandishaji hicho akapimwe kuona iwapo ameambukizwa ugonjwa huo. Mtu anaweza kufa kutokana na ugonjwa huo asipotibiwa.

Kutoweka kwa Vyura

Kulingana na gazeti New Scientist, mamilioni ya vyura wanakufa na hakuna anayejua ni kwa nini. Wamo hatarini zaidi mwa kutoweka kuliko hata ndege na mamalia wengine. Jamii zipatazo 5,743 za mamalia zimo hatarini. Hayo ni baadhi ya mambo yaliyogunduliwa kufuatia uchunguzi uliofanywa ulimwenguni pote kuhusu wanyama wanaoishi nchi kavu na majini. Gazeti hilo laripoti kwamba “wanasayansi wamekuwa wakihangaikia afya ya wanyama wanaoishi nchi kavu na majini tangu 1989, walipochunguza na kulinganisha habari walizokuwa nazo kwenye Kongamano la kwanza la Kimataifa la Hepatolojia waligundua kwamba jamii nyingi ulimwengu pote zilikuwa zikididimia na kutoweka ghafula na kwa njia isiyoeleweka.” Jamii tisa za wanyama wanaoishi nchi kavu na majini zimetoweka tangu 1980, na jamii nyingine 113 zilizokuwako wakati huo “hazipatikani tena.” James Hanken, mwanazuolojia katika Chuo Kikuu cha Harvard asema: “Hatujui kinachosababisha kutoweka kwao.”

Tatizo la Kutoaminika

Ulimwenguni pote, wanasiasa na viongozi wa kibiashara hawaaminiki, laripoti gazeti la Paris International Herald Tribune. Kulingana na kura ya maoni iliyofanywa katika nchi 60, watu wengi waliamini kwamba viongozi wa kisiasa “si waaminifu,” wana “mamlaka nyingi,” “mara nyingi hutumiwa vibaya na wengine,” na “hujiendesha kinyume na maadili.” Barani Afrika, Asia Magharibi, na Amerika ya Latini, zaidi ya asilimia 80 ya watu waliotoa maoni yao walishuku uaminifu wa wanasiasa. Viongozi wa kibiashara ni afadhali kidogo—ni asilimia 40 hivi tu ya watu waliotoa maoni wanaohisi kwamba viongozi wa biashara si waaminifu na wanajiendesha kinyume na maadili. Kuhusu usalama ulimwenguni, asilimia 55 ya watu walio Ulaya Magharibi walikuwa na mashaka kuhusu wakati ujao. Nchini Misri, asilimia 70 ya watu hawakuwa na “tumaini lolote la wakati ujao.” Wengi kati ya wale waliokuwa na matumaini mengi walitoka katika nchi nyingine za Afrika, ambapo asilimia 50 ya watu waliotoa maoni yao walihisi kwamba hali itakuwa nzuri zaidi.