Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Usingizi Hutusaidia Kutatua Matatizo

Gazeti The Times la London linasema: “Watu wengi wamegundua kwamba tatizo ambalo halikutatuliwa kabla ya kulala hutatuliwa kwa urahisi asubuhi kana kwamba ubongo umekuwa ukitatua tatizo hilo usiku kucha.” Wanasayansi nchini Ujerumani wanasema kwamba sasa wamepata uthibitisho wa jambo hilo na wamechapisha ugunduzi wao katika jarida Nature. Walifundisha wajitoleaji 66 kanuni mbili za kufanya hesabu fulani lakini hawakuwaonyesha kanuni ya tatu ambayo ilikuwa njia ya mkato ya kupata jibu sahihi. Baadhi ya wajitoleaji hao waliruhusiwa kulala huku wengine wakikesha usiku au mchana. Likiandika kuhusu matokeo ya uchunguzi huo, gazeti The Daily Telegraph la London linaripoti kwamba, “usingizi ulifanya maajabu. Kulikuwa na uwezekano maradufu [kwa wale waliolala] kujua kanuni ya tatu kuliko wale waliokaa macho.” Ili kuhakikisha kwamba matokeo hayo hayakuwa tu kwa sababu kikundi kilicholala kilikuwa kimepumzika, wanasayansi hao walifanya jaribio la pili. Vikundi hivyo viwili vilipewa hesabu asubuhi baada ya kulala au usiku baada ya kukaa macho mchana wote. Wakati huu hakukuwa na tofauti katika matokeo ya vikundi hivyo, kuonyesha kwamba “matokeo hayo hayatokani na kuwa na ubongo uliopumzika bali yanatokana na ubongo kujipanga vizuri mtu anapokuwa amelala,” linasema gazeti The Times. Dakt. Ullrich Wagner, ambaye ni mtafiti, alikata kauli hivi: “Kwa hiyo, usingizi ni njia ya kuboresha kujifunza.”

Ununuzi wa Bidhaa na Watoto

Juliet Schor, mwanasosholojia wa chuo fulani cha Boston ambaye huchunguza jinsi ununuzi wa bidhaa unavyowaathiri watoto, anasema kwamba leo watoto na vijana Wamarekani “hufikiria sana kuhusu bidhaa zenye majina maarufu, hununua bidhaa zaidi, na ndicho kizazi chenye mwelekeo wa kufuatilia vitu vya kimwili zaidi katika historia.” Kulingana na gazeti la Kanada Globe and Mail, mtu aliye na mwelekeo wa kununua sana vitu ni yule ambaye “huhangaikia sana sura na nguo, hupendezwa sana na watu mashuhuri na mali, hutumia wakati mwingi zaidi kutazama televisheni na kwenye Intaneti na kucheza michezo ya kompyuta.” Profesa Schor aligundua kwamba watoto ambao hufikiria sana kuhusu vitu wanavyotaka kununua walitamani sana kuwa matajiri. “Pia walijichambua zaidi na hawakuwa na furaha walipolinganisha maisha yao na maisha ya watu walioona katika televisheni na katika matangazo ya biashara.” Kwa upande mwingine, watoto ambao hawakufuatilia vitu vya kimwili walijiheshimu zaidi, walikuwa na uhusiano mzuri na wazazi wao, hawakushuka moyo na kuwa na wasiwasi sana, na walikuwa na matatizo machache ya akili, linaripoti gazeti Globe.

Wacheza Kamari Wajipiga Marufuku

Gazeti la kila siku la Ufaransa Le Figaro linasema kwamba “inakadiriwa kuwa nchini Ufaransa, watu kati ya 300,000 na 500,000 ni waraibu wa kucheza kamari.” Hata hivyo, wachezaji kamari wengi wametambua tatizo hilo na umuhimu wa kuacha zoea hilo. Gazeti hilo linasema kwamba watu 28,000 nchini humo wamejipiga marufuku kucheza kamari iliyo halali kwa kuwaomba polisi wawazuie kuingia kwenye majumba ya kucheza kamari kwa miaka mitano hivi. Polisi wa Ufaransa wanaripoti kwamba kila mwaka wao hupokea kati ya maombi 2,000 na 3,000 ya aina hiyo na kwamba idadi hiyo imeongezeka mara sita katika miaka kumi. Gazeti Le Figaro linasema kwamba wengi wa wachezaji sugu wangependa uraibu wao uonwe kuwa “tatizo linalotisha afya ya umma kama vile kutumia tumbaku, vileo, na dawa za kulevya.”

Tangawizi Hupunguza Kichefuchefu

Gazeti Australian linasema: “Tangawizi hutuliza kichefuchefu katika miezi ya kwanza ya ujauzito.” Utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha South Australia, ulionyesha kwamba kutumia gramu moja ya tangawizi kila siku kulipunguza kichefuchefu miongoni mwa wanawake ambao ni wajawazito kwa mara ya kwanza. Tangawizi ni dawa ya kienyeji ya kutibu kichefuchefu katika sehemu nyingi. Hata hivyo, nguvu zake hazikuthibitishwa kisayansi. Uchunguzi huo ulionyesha kwamba tangawizi huwa na matokeo kama ya kiwango cha kila siku cha vitamini B6, ambacho watu hupewa kutibu tatizo hilo.

Kutia Damu Mishipani Huongeza Vifo

Kulingana na uchunguzi uliochapishwa katika jarida JAMA (Journal of the American Medical Association), wagonjwa walio na tatizo baya la moyo ambao walitiwa damu mishipani walikabili hatari kubwa zaidi ya kufa walipolinganishwa na wale ambao hawakutiwa damu mishipani. Ripoti hiyo inasema: “Bado kulikuwa na uwezekano mkubwa wa kufa kwa sababu ya kutiwa damu mishipani hata baada ya kufikiria mambo kama vile umri, jinsia, rangi, na uzito wa mwili wa mgonjwa, na mambo yanayotukia hospitalini kama vile kuvuja damu na kupasuliwa.” Madaktari waliofanya uchunguzi huo walitoa muhtasari huu kuhusu uchunguzi wao: “Tunatoa onyo dhidi ya zoea la kutia watu damu mishipani ili tu kudumisha kiwango cha chembe nyekundu katika damu ya watu walio na tatizo la kuziba kwa mishipa ya moyo.”

Mgawanyiko Kati ya Waanglikana

Hivi karibuni, Philip Jensen, kasisi mkuu wa Anglikana wa Sydney, na ambaye ni mmojawapo wa maaskofu mashuhuri zaidi nchini Australia, alishutumu Askofu Mkuu wa Canterbury kuwa “kahaba wa kidini ambaye anapata mshahara kwa kutumia hila,” linaripoti gazeti la Australia The Age. Jensen alimshutumu kiongozi wa kanisa lake kwa kutopinga sana ngono kati ya watu wa jinsia moja. Gazeti The Age linasema: “Ulimwenguni pote Kanisa la Kianglikana, limegawanyika sana kuhusu suala la ngono za watu wa jinsia moja, na matawi yake mengi Afrika na Asia yamevunja uhusiano wao na kanisa hilo huko Kanada kwa kufunganisha ndoa ya watu wa jinsia moja na pia kuvunja uhusiano wao na kanisa hilo huko Marekani kwa kumtawaza waziwazi askofu basha.”

Watoto Bilioni Moja Wanateseka

Gazeti The New York Times linaripoti kwamba kulingana na Hazina ya Watoto ya Umoja wa Mataifa, zaidi ya nusu ya watoto ulimwenguni, yaani, watoto zaidi ya bilioni moja wanaishi katika umaskini mwingi. Maendeleo mengi yaliyofanywa katika miaka 15 iliyopita yamekatizwa na vita, UKIMWI, na umaskini. Tangu 1990, vita—55 kati yake vikiwa vita vya wenyewe kwa wenyewe—vimewaua watu wapatao milioni 3.6, karibu nusu yao wakiwa watoto. Katika vita vingi, watoto hutekwa na waasi, hulalwa kinguvu, au kutumiwa kuwa askari. Utapiamlo huenea; na mara nyingi hakuna huduma za afya. Idadi ya watoto walioachwa wakiwa mayatima kwa sababu ya UKIMWI ilifikia milioni 15 mwaka wa 2003. Zaidi ya watoto milioni mbili waliajiriwa katika biashara ya ngono. Na ripoti hiyo inasema kwamba ingawa matumizi ya kijeshi ya kila mwake yamefikia dola bilioni 956, ni kati ya dola bilioni 40 au 70 tu ambazo zingehitajiwa kupambana na umaskini.