Je, Kweli Kuna Ziwa Lenye Rangi ya Waridi?
Je, Kweli Kuna Ziwa Lenye Rangi ya Waridi?
Na mwandishi wa Amkeni! nchini Senegal
JE, KWELI ziwa linaweza kuwa la rangi ya waridi? Ziwa Retba linaitwa Ziwa la Waridi, na kwa kuwa liko kilometa 30 tu kutoka mahali tunapoishi huko Dakar, Senegal, Afrika Magharibi, tuliamua kulitembelea ili kuona kama kweli lina rangi ya waridi. Tunapofika huko, tunaona maji yanayong’aa na kwa kweli yana rangi ya waridi yenye kupendeza. Yule anayetutembeza anatueleza kwamba mwangaza wa jua huathiri vijiumbe vilivyo majini na hivyo kutokeza rangi hiyo ya pekee. Hata hivyo, kuna mambo mengine yenye kupendeza mbali na rangi ya ziwa hilo.
Ziwa hilo lisilo na kina kirefu lina sakafu ya chumvi. Maji hayo yana chumvi nyingi sana hivi kwamba mtu anaweza kuelea kwa urahisi. Wageni fulani wanachukua fursa hii kuelea kwenye ziwa hilo.
Ni wazi kwamba watu wengi hutegemea Ziwa la Waridi ili kupata riziki (1). Kwenye kingo za ziwa hilo, wafanyakazi wanapakia chumvi kwenye malori. Tunatua kidogo ili kuwatazama wenyeji wakitoa chumvi kwenye ziwa. Tunawaona wanaume wakiwa wamesimama kwenye ziwa wakivunja chumvi kwa sururu huku maji yakiwa yamewafika kifuani. Wanachota chumvi hiyo kwa kutumia sepetu na kuiweka kwenye vikapu kisha wanaipakia mashuani. Mmoja wa wafanyakazi hao anatuambia kwamba inachukua saa tatu kukusanya tani moja ya chumvi. Mashua hizo zimepakiwa chumvi nyingi sana hivi kwamba inakuwa vigumu kuelea (2). Zinapofika ufuoni, wanawake wanapakua chumvi hiyo na kuibeba vichwani wakitumia ndoo (3). Wote wanafanya kazi hiyo kwa upatano.
Safari yetu ilikuwa yenye kufurahisha. Ziwa la Waridi ni mojawapo ya maajabu mengi ambayo hufanya dunia yetu iwe zawadi yenye thamani kutoka kwa Yehova.—Zaburi 115:16.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 18]
Photo by Jacques CLEMENT, Clichy, FRANCE at http://community.webshots.com/user/pfjc