Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

“Je, Umeona Jiwe la Bolivianita?”

“Je, Umeona Jiwe la Bolivianita?”

Je, Umeona Jiwe la Bolivianita?”

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI BOLIVIA

TULIJIPENYEZA katika chumba kidogo, na hatukutazamia kupata kitu chochote chenye umaridadi wa ajabu. Sonara ambaye ni kijana alitutazama kutoka kwenye benchi yake kuukuu iliyokuwa imejaa vifaa na michoro. Tulimwambia kwamba tunatafuta vito.

Alikuwa mwenye urafiki, na tulipomwambia kwamba tulikuwa tumejaribu kujitengenezea vito, macho yake yaling’aa kwa uchangamfu. Alianza kutueleza kuhusu kazi yake na kutuonyesha baadhi ya vitu alivyotengeneza. Yeye ni sonara stadi. Kisha akatuuliza, “Je, mmeona jiwe la bolivianita?”

Jiwe Lililogunduliwa Hivi Karibuni

Alipoona nyuso zetu zenye mshangao, aliondoa takataka zilizokuwa juu ya benchi yake. Kisha akakunjua kwa uangalifu kitambaa cheusi cha mahameli, na kwa mara ya kwanza tukaona vito vya bolivianite vyenye nyuso mbalimbali ambavyo vilionekana kuwa vya rangi ya zambarau. Lakini tulipoinua kimoja mahali penye nuru na kukitazama, tuliona kikimeta-meta kama dhahabu. Huo ndio uzuri wa pekee wa jiwe la bolivianite, ambalo limefanyizwa kwa mchanganyiko wa amethisti ya zambarau na citrine ya manjano.

Bolivianite (bolivianita, katika Kihispania) ni jina la kibiashara la jiwe la ametrine. Liliuzwa hadharani kwa mara ya kwanza mnamo 1989. Tuliposikia kwamba jiwe hilo la asili hupatikana tu katika nchi tunayoishi ya Bolivia, tulitaka kuona mahali jiwe hilo la bei nafuu lisilopatikana kwa urahisi hutoka.

Safari Isiyo ya Kawaida

Safari ya kutembelea mgodi haikuwa ya kawaida. Huko Puerto Suárez, karibu na mpaka wa Bolivia na Brazili, tulipanda boti dogo yenye injini iliyotusafirisha kilometa 150 kaskazini mwa Mto Paraguai, kupitia Pantanal. Tuliona wanyama mbalimbali—yangeyange na jabiru wakiruka hewani, aligeta waliokuwa majini, na fisi-maji wakicheza ukingoni mwa mto.

Safari yetu ilichukua muda wa saa sita, kisha tukapanda gari linaloendeshwa kwa magurudumu yote manne hadi kwenye mgodi. Watu 120 hivi hufanya kazi katika mgodi huo. Mainjinia wawili walikubali kwa furaha kututembeza. Mgodi huo una ukubwa wa kilometa kumi hivi za mraba na una mashimo mengi, mengine yakiwa ya kina cha karibu meta 60. Mainjinia hao walitueleza kwamba wao hutumia mbinu za kawaida za kuchimba na kulipua mgodi lakini wanapofika katika sehemu zilizo na mawe ya thamani, wao hutoa vito hivyo kwa mkono. Wao hupeleka mawe hayo kwenye kiwanda cha kusafishia ambako asilimia 18 kati yake hutengenezwa kuwa vito. Mengine hutumiwa kutengeneza shanga, mawe ya mviringo, na vioo vyenye pembe tatu. Vipande vingine huchongwa kuwa vinyago, navyo vingine huuzwa jinsi vilivyochimbuliwa kama mapambo.

Pango la Vito

Tulivaa kofia ngumu na glavu kabla ya kuteremka kwenye mgodi. Tukitumia tochi, tuliteremka ngazi sita zilizo ndani ya shimo lenye kina cha meta 20 hivi. Tulipofika mwisho wa shimo hilo lililojipinda, tulipigwa na butwaa. Tulikuwa tukitazama pango lenye urefu wa meta nne, upana wa meta tatu, na kimo cha meta moja lililokuwa na vito vyenye rangi ya zambarau na dhahabu. Mwenye mgodi ananuia kulidumisha jinsi lilivyo likiwa na umaridadi wake wa asili. Hiyo ni mojawapo ya mandhari maridadi zaidi ambayo tumewahi kuona.

Haieleweki kikamili jinsi jiwe moja lilivyoweza kuwa na rangi mbili. Inaonekana kwamba wakati chembechembe za kwazi zilipokuwa zikitengenezwa, badiliko fulani lilitokea katika miamba, halijoto, mnururisho, au kanieneo. Wataalamu wa vito hukata na kung’arisha kwa ustadi mawe hayo ili rangi zote mbili zionekane.

Ilikuwa safari isiyosahaulika. Tunapokumbuka mgodi huo ulio mbali na jitihada inayohitajika kuchimba, kukata, na kung’arisha vito hivyo, tunathamini uzuri wa jiwe la bolivianite hata zaidi.—Zaburi 104:24.

[Picha katika ukurasa wa 16, 17]

Mchimba-mgodi achunguza kito

[Picha katika ukurasa wa 16, 17]

Pango lenye vito

[Picha katika ukurasa wa 16, 17]

Kuchimba vito

[Picha katika ukurasa wa 17]

Kito cha bolivianite chenye nyuso mbalimbali

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 16]

All photos except cavern: Minerales y Metales del Oriente, S.R.L.

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 17]

Gems: Minerales y Metales del Oriente, S.R.L.