Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kila Mtu Anahitaji Makao

Kila Mtu Anahitaji Makao

Kila Mtu Anahitaji Makao

Kila mtu ana haki ya kuishi chini ya hali zinazofaa kutia ndani . . . makao, kwa ajili ya afya na hali yake njema na ile ya familia yake.—Azimio la Watu Wote la Haki za Binadamu, Kifungu cha 25.

VIBARUA wengi wa shambani wanaohama-hama wameanza kuishi katika eneo fulani. Familia nyingi zinaishi katika eneo lililo karibu na mjini kwenye trela zilizoegeshwa zinazoitwa parqueaderos ambazo hukodishwa kwa bei rahisi. Katika eneo hilo, huduma za lazima kama vile mfumo wa kuondoa maji machafu na takataka, na mfumo wa maji safi ni duni sana au hata hazipo. Ripota mmoja alisema kwamba “eneo hilo ni duni sana hivi kwamba [vibarua wa shambani] wangeweza kuishi huko.”

Miaka mitatu iliyopita, wenye mamlaka walipoanza kuwafukuza watu kutoka maeneo fulani kama hayo, familia fulani ziliuza trela zao na kuhamia nyumba ambazo tayari zilikuwa na watu wengi na katika magereji yaliyo katikati mwa mji. Wengine walifunganya tu virago vyao na kwenda kutafuta mahali pa kwenda baada ya mavuno, mahali ambapo wangehisi ni nyumbani.

Je, unawazia kwamba eneo hilo liko Amerika ya Kati au Kusini? Huenda ikawa umekosea. Unaweza kuona eneo hilo lenye trela zilizoegeshwa karibu na mji wa Mecca kusini mwa California, Marekani, umbali wa nusu saa kutoka kwenye jiji lenye utajiri la Palm Springs. Ingawa inasemekana kwamba kwa sasa watu wengi zaidi nchini Marekani wana nyumba zao wenyewe na mapato ya familia za kawaida yalikuwa dola 42,000 hivi mwaka wa 2002, imekadiriwa kwamba zaidi ya familia milioni tano za Wamarekani bado hazina nyumba zinazofaa.

Hali hiyo ni mbaya zaidi katika nchi zinazositawi. Licha ya miradi mingi ya kisiasa, kijamii, na kidini, tatizo la nyumba ulimwenguni pote linazidi kuwa baya.

Tatizo la Ulimwenguni Pote

Inakadiriwa kwamba idadi ya watu wanaoishi katika mitaa ya mabanda ulimwenguni ni zaidi ya bilioni moja. Wataalamu wa Brazili wanaoshughulika na uhamiaji wa watu kutoka mashambani hadi mijini wanahofu kwamba hivi karibuni favelas, yaani, mitaa ya mabanda inayoongezeka daima nchini humo “itakuwa mikubwa na yenye watu wengi zaidi kuliko majiji ambapo mitaa hiyo ilianzia.” Katika majiji fulani huko Nigeria, zaidi ya asilimia 80 ya watu huishi katika mitaa ya mabanda na maeneo ya maskwota. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan, alisema hivi mnamo 2003: “Hatua madhubuti isipochukuliwa, idadi ya watu wanaoishi katika mitaa ya mabanda ulimwenguni pote inakadiriwa kuwa itaongezeka na kufikia bilioni 2 hivi katika miaka 30 ijayo.”

Hata hivyo, takwimu hizo pekee hazionyeshi hata kidogo athari zinazosababishwa na hali duni za maisha kwa wakazi maskini ulimwenguni. Kulingana na Shirika la Umoja wa Mataifa, zaidi ya asilimia 50 ya watu katika nchi zinazositawi hawana mfumo wa kuondoa maji machafu na takataka, asilimia 33 hawana maji safi, asilimia 25 hawana nyumba zinazofaa, na asilimia 20 hawawezi kupata matibabu ya kisasa. Watu wengi katika nchi zilizositawi hata hawawezi kamwe kuruhusu wanyama wao vipenzi waishi katika hali kama hizo.

Haki ya Kila Mtu

Kila mwanadamu ana haki ya kuwa na nyumba inayofaa. Azimio la Watu Wote la Haki za Binadamu, lililopitishwa na Umoja wa Mataifa mwaka wa 1948, lilitangaza kwamba kila mtu ana haki ya kuishi chini ya hali zinazofaa, kutia ndani kuwa na makao yanayofaa. Kwa kweli, kila mtu anahitaji kuwa na nyumba nzuri.

Hivi karibuni, katika mwaka wa 1996, nchi kadhaa ziliidhinisha hati ya UM ambayo baadaye iliitwa Habitat Agenda. Hati hiyo inataja maazimio hususa ya kumwandalia kila mtu makao yanayofaa. Baadaye, katika Januari 1, 2002, UM liliimarisha azimio hilo kwa kufanya hati hiyo kuwa programu rasmi ya UM.

Inashangaza kwamba wakati baadhi ya mataifa tajiri yanapoanza kutoa wito tena wa kujenga makao kwenye mwezi na kupeleleza sayari ya Mihiri, idadi inayoongezeka ya raia wao maskini zaidi hawawezi hata kugharimia mahali pazuri pa kuishi hapa duniani. Tatizo la nyumba linakuathirije? Je, kuna tumaini lolote kwamba siku moja kila mtu atakuwa na nyumba yake nzuri?

[Blabu katika ukurasa wa 4]

Baadhi ya mataifa yanapofikiria kujenga makao kwenye mwezi, raia zao wengi hawana mahali pazuri pa kuishi hapa duniani

[Picha katika ukurasa wa 2, 3]

FAMILIA YA WAKIMBIZI WAASIA.

Katika jiji moja, kuna familia 3,500 zinazoishi katika mahema ya muda, nazo zinahitaji sana maji safi na mfumo wa kuondoa takataka

[Hisani]

© Tim Dirven/Panos Pictures

[Picha katika ukurasa wa 4]

AMERIKA KASKAZINI