Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuwafanya Watoto Waache Kutazama Televisheni

Uchunguzi wa miezi mitano uliohusisha shule 16 za nasari katika jimbo la New York, ulionyesha kwamba kuwapa watoto kazi badala ya kutazama televisheni “kulipunguza muda wanaotazama televisheni kwa saa tatu kwa juma,” linaripoti gazeti The New York Times. Watoto walitiwa moyo kusoma na kufanya kazi kama vile kutengeneza mikeka ya kuwekwa mezani na ishara zinazosema “Usitazame Televisheni” ambazo zingebandikwa kwenye televisheni zote zilizo nyumbani. Watoto wenyewe walidokeza mambo mengine ambayo wangeweza kufanya wakati ambapo hawatazami televisheni au video. Wazazi walitiwa moyo wawasomee watoto wao hadithi kila siku na kuzima televisheni wakati wa chakula. Mara mbili katika kipindi cha uchunguzi huo, familia hazikuwasha televisheni kwa juma moja. Mtafiti mkuu, Dakt. Barbara Dennison alisema kwamba wazazi hawapaswi kuhisi kuwa watoto hawawezi kuacha zoea la kutazama televisheni, huku akiongeza kwamba “kwa kushangaza, watoto huwa tayari kukubali kufanya mambo mengine.”

Tumbaku Hudhuru Mwili Wote

Gazeti New Scientist linaripoti kwamba, “wavutaji sigara wanahatarisha sehemu nyingine za mwili mbali na mapafu na mishipa yao: tishu zote hudhuriwa.” Ripoti moja iliyochapishwa na Ofisa Mkuu wa Afya wa Marekani Richard H. Carmona inaorodhesha magonjwa yanayohusianishwa na tumbaku, kutia ndani nimonia, lukemia, mtoto wa jicho, ugonjwa wa fizi, kansa ya figo, ya mlango wa tumbo la uzazi, ya tumbo, na ya kongosho. Carmona anasema hivi: “Kwa miaka mingi tumejua kwamba ni hatari kuvuta sigara, lakini ripoti hii inaonyesha kwamba ni hatari zaidi kuliko tulivyojua. Sumu za moshi wa sigara husambaa kila mahali ambapo damu huzunguka.” Carmona anaongeza hivi kuhusu wale wanaofikiri kwamba wanaweza kuepuka madhara kwa kutumia sigara zenye kiasi kidogo cha lami na nikotini: “Hakuna sigara isiyo na madhara.” Alisema kwamba kwa kawaida watu wanaovuta sigara hufa miaka 13 au 14 mapema kuliko wale wasiovuta. Carmona alisema hivi kama ilivyoripotiwa katika gazeti The New York Times: “Uvutaji sigara husababisha magonjwa katika karibu kila kiungo cha mwili wakati wowote maishani.”

Kufua Silaha Ziwe Vitu vya Kuchezea

Kampeni iliyoanzishwa nchini Brazili ilikusudiwa kupunguza silaha ambazo raia walikuwa nazo. Watu waliosalimisha silaha zao walilipwa kati ya dola 30 hadi 100. Kama ilivyoripotiwa katika gazeti Folha Online, zaidi ya silaha 200,000 zilikusanywa nchini humo kuanzia Julai hadi Desemba 2004. Silaha zilizokusanywa katika jimbo la São Paulo zilipondwa, zikafinyangwa, na kuyeyushwa, kisha zikageuzwa kuwa vitu vya kuchezea ambavyo viliwekwa katika bustani ya jiji. Sasa bustani hiyo ina pembea na kifaa cha kutelezea, ambavyo vimetengenezwa kutokana na silaha hizo. Waziri wa Masuala ya Haki Márcio Thomaz Bastos alishtumu zoea la watu kuuana kwa sababu ya mambo madogo, na akaongeza: “Mojawapo ya kusudi kuu la kampeni hii ya kutwaa silaha kutoka kwa watu ni kuanzisha sera ya amani miongoni mwa watu.”

Watawa wa Kike Wamepungua

Mnamo 2004, gazeti Clarín la Buenos Aires liliripoti hivi: “Nchini Argentina wanawake wanaotaka kuwa watawa wanazidi kupungua.” Liliongeza hivi: “Katika miaka minne iliyopita idadi ya watawa wa kike imepungua kwa asilimia 5.5, kutoka 9,113 katika mwaka wa 2000 hadi 8,612 mwaka huu. Upungufu huo ni mkubwa hata zaidi, karibu asilimia 36, unapolinganishwa na mwaka wa 1960 ambapo kulikuwa na watawa wa kike 13,423.” Kati ya sababu zilizochangia upungufu huo ni “maoni yasiyofaa ambayo watu huwa nayo kuhusu miito ya kidini” na “kuogopa kujitoa muda wote wa maisha yao” ili kufanya kazi ya kidini. Idadi ya makasisi ilipungua katika kipindi hichohicho. Gazeti Clarín lilisema kwamba, “wengi wanahisi kuwa idadi hiyo itazidi kupungua katika miaka ijayo, na wote wanakubali kuwa jambo hilo linatukia ulimwenguni pote.”

Kuwatunza Wazee Kwenye Meli

Gharama za kuwatunza wazee zimeongezeka sana hivi kwamba watu fulani wanasema kuwa ni afadhali wazee waishi katika meli kuliko katika vituo vya kuwatunzia wazee. Kulingana na ripoti katika jarida Journal of the American Geriatrics Society, “meli za kuwatunzia wazee ni sawa na vituo vingine unapolinganisha huduma zinazotolewa, gharama za kila mwezi na mambo mengine mengi.” Kwa kweli, meli nyingi hutoa huduma ambazo hazipatikani katika vituo vya kuwatunzia wazee. Huenda huduma hizo zikatia ndani daktari anayepatikana wakati wote, kuwapeleka wazee mahali pa kula, na kusafisha vyumba na nguo zao. Manufaa nyingine zinatia ndani msisimko wa kusafiri na nafasi ya kukutana na watu. Pia, ripoti hiyo inasema kwamba “wageni wengi zaidi wangependa ‘kwenda kumtembelea nyanya yao’ ikiwa anaishi kwenye meli.”

Hofu za Ghafula

Gazeti Vancouver Sun linasema hivi: “Hofu za ghafula zinaweza kumpata mtu wakati wowote, hata zinaweza kumfanya mtu aamke usiku akiwa na maumivu ya kifua, ashindwe kupumua, woga mwingi, kusakamwa, kutokwa na jasho, na kutaka kutoroka.” Ripoti ya hivi karibuni iliyokusanywa baada ya kuwahoji watu 36,894 inaonyesha kwamba tatizo hilo hupata asilimia 3.7, au watu milioni moja hivi wa Kanada wenye umri wa miaka 15 au zaidi. Wanawake wengi zaidi (asilimia 4.6) waliripoti kupatwa na hofu za ghafula kuliko wanaume (asilimia 2.8). Gazeti hilo linasema kwamba watu walio na tatizo hilo “wana uwezekano maradufu wa kutumia kileo ili kukabiliana na tatizo hilo na kuna uwezekano mara tatu wa kuvuta sigara wanapolinganishwa na watu wasio na tatizo hilo.” Jambo linalotia moyo ni kwamba karibu asilimia 70 ya watu wenye tatizo hilo humwona daktari. Ripoti hiyo inasema kwamba, Dakt. Jacques Bradwejn, mwenyekiti wa idara ya kuwachunguza watu wenye matatizo ya akili katika Chuo Kikuu cha Ottawa, anaamini kwamba ingawa huenda mtu akarithi tatizo hilo, “linaweza kusababishwa pia na mambo yanayoleta mkazo maishani.”

Kashfa Kubwa Zaidi ya Chakula

Gazeti la Italia Corriere della Sera linaripoti kwamba kulingana na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, karibu watoto milioni tano hufa njaa kila mwaka. Ripoti ya shirika hilo inaonyesha kwamba ulimwenguni pote watu milioni 852 hawana chakula cha kutosha, yaani, milioni 815 katika nchi maskini, milioni 28 katika nchi zinazositawi, na milioni 9 katika nchi zilizositawi. Ripoti hiyo inataja azimio lililotiwa sahihi na wawakilishi kutoka mataifa 110 waliohudhuria Mkutano wa 2004 wa Viongozi wa Ulimwengu Kuhusu Njaa uliofanywa katika makao makuu ya UM, huko New York. Ripoti hiyo ilisema hivi kwa sehemu: “Kashfa kuu zaidi si kwamba kuna njaa lakini kwamba njaa inaendelea kuwako hata ingawa tuna uwezo wa kuimaliza.”