Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Juhudi za Msanii za Kutafuta Furaha Katika“Paradiso”

Juhudi za Msanii za Kutafuta Furaha Katika“Paradiso”

Juhudi za Msanii za Kutafuta Furaha Katika“Paradiso”

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI TAHITI

TANGU mwanadamu wa kwanza Adamu, apoteze Paradiso, wazao wake wamekuwa wakiitafuta. Jitihada hiyo ya kutafuta Paradiso imewachochea wasanii wengi waitafute kwa bidii kupitia michoro yao. Mmoja wao alikuwa Paul Gauguin, msanii maarufu wa karne ya 19.

Yapata miaka miwili iliyopita, mamia ya wageni kutia ndani wasanii chipukizi, walisafiri kwa meli mbili kufika kwenye kisiwa kidogo cha Hiva Oa, ambacho ni mojawapo ya Visiwa vya Marquesas huko Polinesia ya Ufaransa. Gauguin alikufa kwenye kisiwa hicho mwaka wa 1903. Wakati wa kuadhimisha miaka mia moja ya kifo chake, wageni wengi ambao hupendezwa sana na kazi yake walivutiwa na kuzinduliwa kwa kituo cha utamaduni kilichoitwa kwa jina lake.

Paradiso Iko Wapi?

Lakini kwa nini karne moja mapema Gauguin aliamua kutoroka Ulaya na kuishi kwenye kisiwa hicho chenye amani cha Pasifiki Kusini? Baada ya kuishi maisha magumu akiwa msanii maskini huko Ulaya, mwishowe Gauguin alidharau ustaarabu wa Ulaya. Aliona utamaduni pamoja na ustaarabu wa Ulaya kuwa wenye ubaguzi. Gauguin alifikia mkataa huo baada ya kutembelea Tahiti kwa mara ya kwanza na kukaa huko kwa miaka miwili hivi. Baada ya kurudi Ulaya, aliamua hivi: “Hakuna kitu kitakachonizuia kurudi kuishi huko, nami sitarudi Ulaya kamwe. Kwa kweli, tunaishi maisha yasiyo na kusudi hapa Ulaya!” Alipinga waziwazi maadili ya nchi za Magharibi na kama tu watu wengi walioishi barani humo wakati huo, Gauguin alitamani sana kuishi katika paradiso fulani iliyopotea zamani ambako hangepatwa na madhara yanayotokana na ustaarabu. Gauguin alitumaini kutimiza tamaa yake ya paradiso katika bustani yenye kupendeza huko Pasifiki ambako kungekuwa na jua na amani. Alitamani sana kuhamia mahali pazuri kama hapo, mahali palipofaa hasa kuchorwa.

Kama watu wengine walioishi wakati wake, Gauguin alifikiri kwamba inafaa kuishi mbali na ustaarabu na kwa kupatana na mazingira ya asili kwa sababu maisha hayo ni rahisi. Kwa kuwa Wapolinesia waliishi kwa njia hiyo, watu fulani walifikiri kwamba wao hufanya mema tu. Maisha yao rahisi na upole wao ulionekana kuwa unawakilisha ulimwengu mkamilifu. Gauguin alikuwa akitafuta furaha ya aina hiyo. Hata hivyo, kwa kusikitisha, bado alikuwa akitafuta majibu kuhusu jinsi uhai ulivyoanza, wakati ujao wa wanadamu, suluhisho la kukata tamaa na hofu ya kifo.

Gauguin alipata chanzo cha kumchochea akiwa katika Bahari za Kusini. Mazingira hayo yalimchochea aanze tena kuchora. Alipenda hasa kuwachora watu wa eneo hilo wenye urembo wa asili. Nyuso alizochora zilionyesha utulivu, ujasiri, na uradhi. Kupitia picha zake, Gauguin alitaka kuonyesha mandhari ya ulimwengu wa kuwaziwa wenye amani chini ya jua la tropiki.

Furaha ya Kweli

Je, Gauguin alipata furaha huko Tahiti au Hiva Oa, au katika kisiwa kingine chochote? Alilazimika kutambua kwamba hata katika visiwa hivyo vidogo vya tropiki, watu hufa. Hakuna ukamilifu katika ulimwengu huu. Wakati mmoja baada ya kuishi Tahiti kwa miaka michache, aliandika hivi: “Kwa muda fulani sasa nimekuwa na huzuni, na kazi yangu inaathiriwa . . . . Picha zangu hazionyeshi shangwe.” Picha za nchi hizo zenye furaha hazikutimiza matarajio yake. Bado alikuwa na uhitaji wa pesa, lakini pia alikuwa na matatizo ya afya. Hata katika mazingira hayo, bado hakuweza kupata majibu kwa maswali muhimu kuhusu uhai. Alipokuwa akifikiria mambo hayo yenye kutatanisha, aliamua kuchora picha kubwa ambayo ingekuwa picha bora zaidi aliyochora akiwa huko Tahiti. Ilikuwa picha kubwa yenye urefu wa meta 3.75 yenye kichwa D’où venons-nous? Que sommes-nous? Où allons-nous? (Twatoka Wapi? Sisi Ni Nini? Twaelekea Wapi?). Kupitia picha hiyo, alijaribu kueleza jinsi ambavyo hakuelewa ulimwengu na kuwepo kwetu.

Majibu ya maswali kuhusu uhai yaliyo katika picha za Gauguin na wasanii wengine kabla na baada yake yanapatikana katika Biblia, kitabu ambacho Mungu hufunua kusudi lake kwa wanadamu. Inatoa majibu ya kweli na yenye kuridhisha. Yanatoa tumaini hakika kwa wakati ujao. Isitoshe, yanatufundisha kwamba haidhuru tunaishi wapi, iwe ni katika Pasifiki au kwingineko, tunaweza tu kupata furaha ya kweli kwa kuishi kupatana na Muumba wetu, Yehova Mungu. Mashahidi wa Yehova huko Polinesia ya Ufaransa na katika sehemu nyingine za ulimwengu wanafurahi kuwaeleza wengine tumaini hilo zuri la paradiso itakayokuja.

Kumwiga Msanii Mkuu

Wakati wa kuadhimisha miaka mia moja ya Gauguin, kulikuwa na maonyesho ya nakala sahihi za picha zake. Nakala hizo zilichorwa na hasa na wasanii wawili, Claude na Viera Farina. Wameishi huko Hiva Oa kwa muda fulani ili kunakili michoro ya Gauguin, ambayo wameitoa kwa kituo cha utamaduni.

Ili kutokeza na kuonyesha jambo ambalo Gauguin alikuwa akifikiria hasa, wamechunguza kwa uangalifu sana rangi na maumbo kwa kutumia picha kubwa zilizopigwa za michoro ya Gauguin. Wanaeleza kwamba hiyo si kazi rahisi, kwani kutoa nakala za michoro ni kazi ngumu inayochukua muda mrefu na nguvu nyingi. “Msanii mkuu ana uhuru wa kubuni kitu chochote, na hata akichora meza yenye miguu mitano, hakuna anayeweza kumkosoa, badala yake watu watasema kwamba ana kipawa cha hali ya juu. Lakini mtu anayenakili mchoro wa msanii mwingine akisahau tu kuchora jani moja, kazi yake huchambuliwa sana! Hiyo ndiyo sababu kuna wasanii wengi zaidi kuliko watu wanaonakili,” wenzi hao wanasema. Ni nini hufanya mtu awe mnakili stadi? “Lazima awe na ujuzi mwingi kumhusu msanii mkuu na maisha yake kwa sababu anategemea tu picha za michoro ya msanii, na hata kama ana picha hizo, huenda rangi zake zisifanane kabisa na michoro yenyewe. Kwa hiyo, anapaswa kutafuta habari kamili kwenye majumba ya makumbusho.” Leo michoro ya Gauguin huuzwa kwa bei ya juu sana, kwa hiyo, nakala za akina Farina ni zenye thamani katika kituo hicho cha utamaduni.

[Picha katika ukurasa wa 23]

Mchoro wa Paul Gauguin aliouchora mwenyewe

[Picha katika ukurasa wa 23]

“Femmes de Tahiti” au “Sur la plage” (Wanawake wa Tahiti au Kwenye Ufuo)

[Picha katika ukurasa wa 24]

“Femme à la mangue” (Mwanamke Mwenye Embe), nakala ya awali juu, pamoja na nakala iliyochorwa na Claude na Viera Farina, wanaoonekana chini katika studio yao huko Atuona

[Hisani]

Erich Lessing/Art Resource, NY

Copie dʹoeuvre de Gauguin, avec lʹaimable autorisation de Claude et Viera Farina

[Picha katika ukurasa wa 25]

“Les Parau Parau” (Uvumi Mtupu)

[Hisani]

Scala/Art Resource, NY

[Picha katika ukurasa wa 25]

“Quand Te Maries-Tu?” (Utaolewa Lini?)

[Hisani]

Erich Lessing/Art Resource, NY

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 23]

Artwork: Erich Lessing/ Art Resource, NY