Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kutumia Kileo Vibaya—Kunaathiri Afya

Kutumia Kileo Vibaya—Kunaathiri Afya

Kutumia Kileo Vibaya—Kunaathiri Afya

“Santé!” “Salute!” “Za vashe zdorovye!” “Chuc suc khoe!” Iwe ni nchini Ufaransa, Italia, Urusi, au Vietnam, maneno kama hayo, yaani, “Afya njema kwako!” husikika kabla marafiki hawajaanza kunywa kileo pamoja. Hata hivyo, mamilioni ya watu ulimwenguni wanakufa kwa sababu ya kunywa.

KUTUMIA kileo vibaya ni tatizo zito ambalo linahusisha matumizi hatari, matumizi yenye kudhuru, na uraibu. Matumizi hatari, kama yanavyofafanuliwa na Shirika la Afya Ulimwenguni, ni “mazoea ya kutumia kileo ambayo huongoza kwenye madhara” ya kimwili, kiakili, au ya kijamii. Yanatia ndani kunywa kupita kiwango kinachopendekezwa na wizara ya afya au kilichowekwa na sheria. Matumizi yenye kudhuru, ambayo pia yanaitwa matumizi mabaya, yanatia ndani kunywa ambako tayari kumetokeza madhara ya kimwili au ya kiakili lakini bado mtu hajawa mraibu. Uraibu, umefafanuliwa kuwa “kushindwa kujizuia kunywa kileo.” Mraibu wa kileo hutamani sana kileo, huendelea kunywa licha ya kupatwa na matatizo mbalimbali yanayosababishwa na kileo, naye hupatwa na athari asipokunywa.

Haidhuru umri wako, jinsia, au taifa, unaweza kupatwa na hatari za kunywa. Kwani kileo huathirije mwili? Kunywa kupita kiasi kunawezaje kudhuru afya yako? Na ni kiasi gani cha kileo ambacho huonwa kuwa kisichoweza kudhuru?

Ni Hatari kwa Akili

Ethanoli, ambayo ni kemikali inayopatikana katika vileo vingi, ni sumu ambayo inaweza kudhuru au kuharibu mfumo wa neva. Kwa kweli, mtu aliyelewa ana sumu fulani mwilini. Kiasi kikubwa cha ethanoli humfanya mtu apoteze fahamu kwa muda mrefu na kufa. Kwa mfano, wanafunzi huko Japani hufa kila mwaka kwa sababu ya zoea la ikkinomi, yaani, kubugia kileo harakaharaka. Mwili unaweza kubadili ethanoli kuwa kemikali isiyoweza kudhuru, lakini hauwezi kufanya hivyo haraka. Mtu anapokunywa kileo haraka zaidi kuliko mwili unavyoweza kukibadili, ethanoli huongezeka mwilini na kuanza kuvuruga utendaji wa ubongo. Katika njia gani?

Uwezo wa kusema, kuona, viungo kufanya kazi kwa upatano, kufikiri, na tabia unahusiana na utendaji wa kemikali wenye kutatanisha katika chembe za neva za ubongo, au chembe kuu. Ethanoli hubadili utendaji huo, kwa kuzuia au kuongeza kazi ya chembe fulani ambazo hupitisha habari kutoka chembe moja ya neva hadi nyingine. Kwa kufanya hivyo, kupitishwa kwa habari katika ubongo huvurugwa na kuzuia ubongo usifanye kazi kwa njia ya kawaida. Hiyo ndiyo sababu mtu anapokunywa sana, yeye huzungumza kwa njia isiyoeleweka, haoni vizuri, hutembea akiyumba-yumba, naye hushindwa kujizuia kufanya mambo fulani. Mambo hayo yote ni dalili za kawaida za ulevi.

Kileo kinapotumiwa kwa muda mrefu, kemikali za ubongo hubadilika ili kukabiliana na sumu ya ethanoli na kuwezesha chembe za neva kufanya kazi kwa njia ya kawaida. Jambo hilo humfanya mtu asidhurike, hilo linamaanisha kwamba kiwango kilekile cha kileo kinakuwa na athari ndogo kuliko awali. Uraibu hutukia ubongo unapozoea kileo sana hivi kwamba hauwezi kufanya kazi vizuri bila kileo. Mwili hutamani kileo ili kudumisha usawaziko wa kemikali. Mtu asipokunywa, kemikali za ubongo wake huvurugika kabisa naye hupatwa na athari kama vile wasiwasi, kutetemeka, au hata kifafa.

Mbali na kubadili kemikali za ubongo, kutumia kileo vibaya kunaweza kufanya chembe zidhoofike na kuharibika, na hivyo kubadili muundo wa ubongo. Ingawa mtu anaweza kupona kwa kiasi fulani akiacha kutumia kileo, inaonekana madhara fulani ni ya kudumu, na hivyo kumbukumbu na utendaji mwingine wa akili huathiriwa. Madhara ya ubongo hayatokani tu na kutumia kileo kwa muda mrefu. Utafiti unaonyesha kwamba hata kutumia kileo vibaya kwa muda mfupi kunaweza kusababisha madhara.

Ugonjwa wa Ini na Kansa

Ini hufanya kazi muhimu ya kuyeyusha chakula, kuzuia maambukizo, kudhibiti mzunguko wa damu, na kuondoa vitu vyenye sumu mwilini, kutia ndani kileo. Kutumia kileo kwa muda mrefu huharibu ini katika hatua tatu. Katika hatua ya kwanza, kuvunjwa-vunjwa kwa ethanoli hufanya mafuta yasimeng’enywe haraka, na hivyo kuyafanya yarundamane kwenye ini. Baada ya muda, ini huvimba au mtu hupatwa na mchochota wa ini. Ingawa kileo kinaweza kumfanya mtu apatwe na mchochota wa ini, inaonekana kwamba pia kinaweza kupunguza uwezo wa mwili wa kupigana na virusi vya mchochota wa ini aina ya B na C. * Uvimbe huo usipotibiwa, chembe hupasuka na kufa. Madhara hayo huongezeka kwani inaonekana kwamba kileo huchochea utendaji wa asili wa chembe kujiharibu.

Hatua ya mwisho ni kunyauka kwa ini. Kadiri ini linavyoendelea kuvimba na chembe zake kuharibika, ndivyo kunavyokuwa na madhara yasiyoweza kurekebika. Mwishowe, ini huwa gumu badala ya kuwa laini kama sponji. Hatimaye, tishu zilizoathiriwa huzuia damu isizunguke kwa ukawaida na kufanya ini liache kufanya kazi na kusababisha kifo.

Kileo huathiri ini pia katika njia nyingine isiyoonekana waziwazi, yaani, ini hushindwa kujikinga na athari za vitu vinavyosababisha kansa. Mbali na kuchochea ukuzi wa kansa ya ini, kileo huongeza sana hatari ya kupata kansa ya kinywa, koromeo, zoloto, na umio. Isitoshe, kileo hufanya tezi za mate zilizo mdomoni ziweze kupenywa kwa urahisi zaidi na kemikali zilizo katika tumbaku zinazoweza kusababisha kansa, na hivyo kuwahatarisha wavutaji sigara zaidi. Wanawake ambao hunywa kileo kila siku wanakabili hatari kubwa zaidi ya kupatwa na kansa ya matiti. Kulingana na uchunguzi mmoja, hatari ya kupata kansa ya matiti ilikuwa kubwa kwa asilimia 69 kati ya watu wanaokunywa kileo kuliko wale wasiokunywa.

Watoto Wenye Sumu

Mojawapo ya matokeo yenye kuhuzunisha ni athari za kileo kwa watoto walio tumboni. Gazeti International Herald Tribune linaripoti hivi: “Kileo huathiri kijusi vibaya zaidi kuliko dawa nyingine yoyote ya kulevya.” Mwanamke mjamzito anapokunywa, mtoto wake anayekua tumboni hunywa pia, na sumu ya kileo hudhuru kijusi hata katika kipindi hiki cha ukuzi. Kileo husababisha madhara ya kudumu kwenye mfumo mkuu wa neva wa kijusi. Chembe za neva hazijitengenezi ifaavyo. Chembe huuawa, nazo nyingine hutokea mahali pasipofaa.

Kwa sababu ya hilo, madhara ya kileo kwa kijusi ndio kisababishi kikuu cha watoto kuzaliwa wakiwa na akili punguani. Watoto wenye madhara hayo hupatwa na matatizo kama vile, kuwa na uwezo mdogo wa kufikiri, matatizo ya lugha, kukua polepole kwa akili, tabia zisizofaa au kasoro, ukuzi wa polepole, utendaji unaopita kiasi, na kasoro za kusikia na kuona. Pia watoto wengi wenye ugonjwa huo huzaliwa na kasoro za uso.

Isitoshe, watoto ambao mama zao walikunywa hata kiasi kidogo cha kileo walipokuwa wajawazito wanaweza kupatwa na kasoro fulani, kutia ndani tabia zisizo za kawaida na kushindwa kujifunza. Profesa Ann Streissguth wa Chuo Kikuu cha Washington anasema kwamba “si lazima uwe mraibu wa kileo ili umdhuru mtoto wako, unaweza kumdhuru mtoto wako kwa kunywa tu kileo unapokuwa mjamzito.” Ripoti ya Taasisi ya Kitaifa ya Afya na Utafiti wa Dawa ya Ufaransa Alcool—Effets sur la santé inasema: “Kufyonzwa kwa kileo hutokeza madhara katika kipindi chote cha ujauzito, na hakuna kiasi kidogo ambacho kimewahi kuonwa kuwa hakina madhara.” Kwa hiyo, inafaa kwa wanawake wajawazito au wanaopanga kuwa wajawazito wasinywe kileo hata kidogo. *

Kiasi Kisichodhuru

Kuna matatizo mengine ya afya mbali na yale yaliyotajwa. Mnamo 2004, makala moja katika gazeti Nature ilisema kwamba “hata kiasi kidogo cha kileo huzidisha hatari ya kujeruhiwa na huongeza uwezekano wa kupatwa na magonjwa 60 hivi.” Kwa hiyo, ni kiasi gani ambacho hakidhuru? Leo mamilioni ya watu ulimwenguni hunywa kileo mara mojamoja. Ili kuwa na afya bora ni vizuri kuwa na kiasi. Lakini kiasi ni nini? Huenda watu wengi wakaona kwamba kiasi wanachotumia ni cha kadiri, labda wakifikiri kwamba maadamu hawalewi au wao si waraibu, hakuna tatizo. Hata hivyo, mwanamume 1 kati ya 4 barani Ulaya hutumia kiasi cha kileo ambacho huonwa kuwa hatari.

Ripoti mbalimbali hufafanua kunywa kwa kiasi kuwa kunywa gramu 20 za kileo kikali kwa siku, au pombe mbili za kawaida kwa wanaume, na gramu 10, yaani, pombe moja kwa wanawake. Wizara ya afya ya Ufaransa na Uingereza inadokeza “kiwango kinachofaa” kuwa pombe tatu kwa siku kwa wanaume na mbili kwa wanawake. Taasisi ya Marekani Inayoshughulikia Matumizi Mabaya ya Kileo na Uraibu pia inapendekeza “watu wenye umri wa miaka 65 na zaidi wapunguze kileo na kunywa pombe moja kwa siku.” * Hata hivyo, sote huathiriwa na kileo kwa njia tofauti. Watu fulani wanaweza kulemewa na viwango hivyo vidogo. Kwa mfano, Ripoti Maalumu ya 10 ya Bunge la Marekani Kuhusu Kileo na Afya, inasema, “kiasi kinachofaa cha kileo kinaweza kuwadhuru watu wenye wasiwasi na matatizo ya kihisia.” Watu wanapaswa kuzingatia umri, hali ya afya, na maumbile.—Ona sanduku “Kupunguza Hatari.”

Watu ambao hutumia kileo vibaya wanaweza kusaidiwaje? Makala inayofuata itajibu swali hilo.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 11 Kulingana na uchunguzi mmoja uliofanywa nchini Ufaransa, hatari ya kunyauka kwa ini ni maradufu kati ya wagonjwa wenye virusi vya mchochota wa ini aina ya C ambao hunywa sana kuliko ilivyo kati ya wagonjwa wanaokunywa kwa kiasi. Inapendekezwa kwamba watu wenye ugonjwa huo wanywe kileo kidogo sana au wasinywe hata kidogo.

^ fu. 17 Wanawake wanaonyonyesha wanapaswa kuwa waangalifu kwamba baada ya kunywa, kileo huchangamana na maziwa yao. Kwa kweli, mara nyingi kiasi cha kileo katika maziwa ya mama huwa cha juu kuliko katika damu, kwa kuwa tofauti na damu, maziwa yana maji mengi zaidi ambayo hufyonza kileo hicho.

^ fu. 20 Kwa kuwa vipimo vya kileo hutofautiana katika sehemu mbalimbali, kiasi cha kileo ambacho mtu atatumia kinapaswa kupatana na viwango vya nchi anamoishi na mtu anapaswa kufikiria viwango hivyo kabla ya kunywa.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 5]

JE, UNYWE KILEO KABLA YA KUENDESHA GARI?

Sheria za kutoendesha gari baada ya mtu kunywa kileo zimekuwepo tangu magari yalipovumbuliwa. Nchi ya kwanza kutunga sheria hiyo ilikuwa Denmark, mnamo mwaka wa 1903.

Unapokunywa kileo ukiwa na njaa, kiasi cha kileo katika damu yako huongezeka katika muda wa nusu saa hivi baada ya kumeng’enywa. Kinyume na maoni ya wengi, kunywa kahawa, kupunga hewa, na kufanya mazoezi hakutakusaidia ulevuke. Athari za kileo zitaisha mwilini mwako baada tu ya muda kupita. Pia usisahau kwamba kileo ni kileo, yaani, ukinywa glasi moja ya divai, pombe, au kileo kikali, itakuathiri kwa njia ileile. *

Hata kiasi kidogo cha kileo kinaweza kuathiri uwezo wako wa kuendesha gari. Kileo huathiri uwezo wako wa kuona. Ishara za barabarani huonekana kuwa ndogo. Uwezo wako wa kuona vitu vilivyo upande na pia uwezo wa kukadiria umbali na kuona vitu vilivyo mbali hupungua. Uwezo wa ubongo wa kupitisha habari, uwezo wa kuitikia, na uwezo wa viungo kutenda kwa upatano hupungua.

Ukipatwa na aksidenti baada ya kunywa kileo, huenda majeraha yako yakawa mabaya zaidi kuliko kama hungekuwa umelewa. Isitoshe, kunakuwa na uwezekano mdogo wa kuokoka baada ya kufanyiwa upasuaji wa dharura kwa sababu ya athari za kileo kwenye moyo na damu yako. Ripoti ya Taasisi ya Kitaifa ya Afya na Utafiti wa Dawa ya Ufaransa inasema: “Hivyo, tofauti na maoni yanayokubaliwa na wengi, mara nyingi madereva walevi ndio hufa katika vifo vingi vinavyosababishwa na kileo.” Kwa sababu ya hatari hizo, ripoti hiyo inatoa madokezo yafuatayo:

▪ Usinywe kileo na kuendesha gari.

▪ Usikubali kubebwa na dereva ambaye amekunywa kileo.

▪ Usiwaruhusu marafiki au wazazi waendeshe gari wakiwa wamekunywa kileo.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 29 Kwa kawaida, karibu gramu saba za kileo huondolewa mwilini kila baada ya saa moja. Kila nchi ina kiwango chake cha kipimo cha kawaida. Shirika la Afya Ulimwenguni linafafanua kipimo cha kawaida kuwa gramu 10 za ethanoli. Kiasi hicho ni sawa na mililita 250 za bia, mililita 100 za divai, au mililita 30 za kileo kikali.

[Picha]

Vipimo hivi vina karibu kiasi kilekile cha kileo

Chupa moja ya bia (ml 330 yenye asilimia 5 ya kileo)

Kiasi kidogo cha mvinyo (wiski, jini, vodka) (ml 40 yenye asilimia 40 ya kileo)

Glasi ya divai (ml 140 yenye asilimia 12 ya kileo)

Glasi ndogo ya pombe kali (ml 70 yenye asilimia 25 ya kileo)

[Sanduku katika ukurasa wa 6]

JE, WATU HURITHI URAIBU WA KILEO?

Katika jitihada za kutafuta tiba ya uraibu wa kileo, wanasayansi wamejitahidi kuelewa jinsi chembe za urithi zinavyohusika katika kumfanya mtu awe mraibu wa kileo. Tangu wakati huo wanasayansi wamegundua chembe fulani ambazo inaonekana humfanya mtu aathiriwe na kileo. Hata hivyo, kuna mengi zaidi yanayohusika katika uraibu wa kileo mbali na mambo ambayo mtu amerithi. Hata ikiwa baadhi ya watu wana mwelekeo fulani waliorithi, wanaweza kuepuka uraibu. Mazingira yanahusika pia. Malezi yasiyofaa, washiriki wengine wa familia au marika kutumia kileo vibaya, kutoelewana na wengine, matatizo ya kihisia, kushuka moyo, tabia ya ugomvi, kutafuta msisimko, kuwa na uwezo mkubwa wa kudhibiti athari za kileo, au uraibu wa kitu kingine ni mambo yaliyotajwa kuwa yanachangia tatizo hilo. Mambo hayo na mengine hutokeza uraibu.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 6]

UFARANSA:

Uchunguzi mbalimbali unaonyesha kwamba watu milioni tano hivi hutumia kileo vibaya, na kati ya watu milioni mbili na milioni tatu ni waraibu

NIGERIA:

Kulingana na gazeti la Lagos Daily Champion, “zaidi ya Wanigeria milioni 15 ni waraibu wa kileo,” yaani, karibu asilimia 12 ya idadi ya watu nchini humo

URENO:

Nchi hiyo ni mojawapo ya nchi zenye idadi kubwa zaidi ya watu wanaokunywa vileo vikali. Gazeti la Lisbon, Público linaripoti kwamba asilimia 10 ya idadi ya watu hupatwa na “madhara makubwa yanayosababishwa na kileo”

MAREKANI:

Kulingana na Ripoti Maalumu ya 10 ya Bunge la Marekani Kuhusu Kileo na Afya, “inaweza kusemwa kwamba Wamarekani milioni 14 hivi, yaani, asilimia 7.4 ya idadi ya watu, hutumia kileo vibaya au ni waraibu”

[Sanduku katika ukurasa wa 8]

KUPUNGUZA HATARI

Maelezo yafuatayo yanayofafanua jinsi ya kupunguza hatari yalichapishwa na Idara ya Magonjwa ya Akili na Uraibu wa Madawa ya Kulevya ya Shirika la Afya Ulimwenguni. Maelezo hayo ya kupunguza hatari hayamaanishi kwamba mtu hawezi kupatwa na madhara yoyote kwa kutumia kileo. Watu huathiriwa na kileo kwa njia tofauti.

▪ Usinywe zaidi ya vipimo viwili vya kawaida kwa siku *

Usinywe kileo angalau siku mbili kwa juma

Unapokuwa katika hali zifuatazo, hata chupa moja au mbili zinaweza kupita kiasi:

▪ Unapoendesha gari au kutumia mashini

▪ Unapokuwa mjamzito au unaponyonyesha

▪ Unapotumia dawa fulani

▪ Unapokuwa na matatizo fulani ya afya

▪ Ikiwa huwezi kudhibiti kunywa kileo

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 58 Kipimo cha kawaida ni sawa na gramu 10 ya kileo kwa kila glasi moja.

[Hisani]

Chanzo: Brief Intervention for Hazardous and Harmful Drinking

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 9]

JE, KILEO HUNUFAISHA MOYO?

Wanasayansi wanaamini kwamba kemikali zilizo katika divai nyekundu (polyphenols) huzuia kemikali ambayo hufanya mishipa ya damu ijibane.

Isitoshe, inasemekana kwamba kileo kinaweza kuongeza kolesteroli nzuri. Pia kinapunguza vitu ambavyo hufanya damu igande.

Inaonekana kwamba manufaa yoyote ya kileo hupatikana mtu anapokunywa kiasi kidogo siku tofauti-tofauti katika juma badala ya kukibugia jioni moja. Inasemekana kwamba kunywa zaidi ya chupa mbili kwa siku hufanya shinikizo la damu lipande, na kunywa sana huongeza uwezekano wa kupatwa na kiharusi na kunaweza kuufanya moyo uvimbe na upige isivyo kawaida. Madhara hayo ya afya na mengine mengi yanayosababishwa na kunywa kupita kiasi huzidi manufaa yoyote ambayo kileo huletea moyo. Kwa kweli, si vizuri kutumia kitu kupita kiasi.

[Mchoro/Picha katika ukurasa wa 7]

JINSI KILEO KINAVYOWEZA KUKUDHURU

Ubongo

Kufa kwa chembe, kupoteza kumbukumbu, mshuko moyo, tabia ya ugomvi

Kudhurika kwa uwezo wa kuona, kusema, na upatano

Kansa ya koo, kinywa, matiti, ini

Moyo

Misuli kudhoofika, uwezekano wa kupatwa na ugonjwa wa moyo

Ini

hujaa mafuta, huvimba, kisha hunyauka

Hatari nyingine

Kudhoofika kwa mfumo wa kinga, vidonda, kuvimba kwa kongosho

Wanawake wajawazito

Hatari ya kuzaa watoto walemavu au wenye akili punguani

[Picha katika ukurasa wa 8]

“Kileo huathiri kijusi vibaya zaidi kuliko dawa nyingine yoyote ya kulevya”