Kutumia Kileo Vibaya—Msiba kwa Jamii
Kutumia Kileo Vibaya—Msiba kwa Jamii
KUNYWA kileo hutokeza mambo mawili yanayotofautiana: furaha na huzuni. Biblia inasema kwamba kunywa kileo kwa kiasi kunaweza kuufurahisha moyo wa mwanadamu. (Zaburi 104:15) Hata hivyo, Biblia pia huonya kwamba kutumia kileo vibaya kunaweza kudhuru au hata kuua, kama tu kuumwa na nyoka mwenye sumu. (Methali 23:31, 32) Na tuchunguze kindani madhara makubwa yanayosababishwa na kutumia kileo vibaya.
“Jumamosi, dereva mmoja aliyekuwa amelewa alimgonga mama mmoja mwenye umri wa miaka 25 na mwana wake mwenye umri wa miaka miwili. . . . Mwanamke huyo kijana aliyekuwa na mimba ya miezi sita, alikufa Jumapili. Mwana wake ambaye alipata majeraha ya kichwa yuko katika hali mahututi,” likaripoti gazeti Le Monde. Kwa kusikitisha, visa kama hivyo hutokea mara nyingi. Labda unamjua mtu fulani aliyehusika katika aksidenti iliyosababishwa na mtu fulani aliyetumia kileo vibaya. Kila mwaka, maelfu ya watu huuawa au kujeruhiwa katika aksidenti za barabarani zinazosababishwa na madereva ambao wamelewa.
Idadi ya Vifo
Ulimwenguni pote, madhara yanayotokana na kutumia kileo vibaya ni makubwa sana. Nchini Ufaransa, kutumia kileo vibaya ndicho kisababishi cha tatu kikubwa cha vifo baada ya kansa na magonjwa ya moyo, kwani kila mwaka, husababisha vifo vya watu 50,000 hivi kwa njia ya moja kwa moja au isiyo ya moja kwa moja. Kulingana na ripoti moja iliyotolewa na Wizara ya Afya ya Ufaransa, “idadi hiyo ni sawa na idadi ya watu ambao wangekufa ikiwa ndege mbili au tatu kubwa zingeanguka kila juma.”
Watu wengi ambao hufa kutokana na kileo ni vijana. Kulingana na ripoti ya Shirika la Afya Ulimwenguni iliyochapishwa mnamo 2001, kileo ndicho husababisha vifo vingi zaidi vya wanaume walio na umri wa kati ya miaka 15 na 29 barani Ulaya. Inatabiriwa kwamba katika nchi fulani za Ulaya Mashariki, hivi karibuni kijana 1 kati ya 3 atakufa kwa sababu ya kutumia kileo vibaya.
Jeuri na Kutendewa Vibaya Kingono
Kileo husababisha jeuri. Kunywa kunaweza kumfanya mtu ashindwe kujizuia na kunaweza kumfanya aelewe vibaya matendo ya wengine na hivyo iwe rahisi zaidi kutenda kijeuri.
Kileo huchangia sana katika jeuri ya nyumbani na kutendewa vibaya kingono. Uchunguzi uliofanyiwa mahabusu nchini Ufaransa ulionyesha kwamba kileo kilihusika katika visa asilimia 75 vya kulalwa kinguvu na kutendewa vibaya kingono. Gazeti Polityka linasema kwamba uchunguzi unaonyesha kuwa nchini Poland, asilimia 75 ya wanawake ambao waume zao ni waraibu wa kileo wametendewa kijeuri. Kulingana na uchunguzi mmoja, inakadiriwa kwamba “kutumia kileo kunahusianishwa na kuongezeka maradufu kwa hatari ya kuuawa kwa watu wa umri wote na kwamba [hata] watu wasiotumia kileo wanaoishi pamoja na wale wanaokitumia walikabili hatari kubwa zaidi ya
kuuawa.”—American Medical Association, Council on Scientific Affairs.Hasara kwa Jamii
Jamii hupata hasara kubwa sana wakati gharama za matibabu, bima na hasara ambazo kampuni hupata kwa sababu ya aksidenti, ugonjwa, au kifo cha mapema zinapojumlishwa. Inasemekana kwamba kutumia kileo vibaya kunagharimu raia milioni nne wa Ireland angalau dola bilioni moja kwa mwaka. Kitabu fulani kilichonukuliwa katika gazeti The Irish Times kilisema kwamba gharama hiyo ni sawa na “gharama ya kujenga hospitali mpya, uwanja wa michezo na kununulia kila Waziri ndege kila mwaka.” Mnamo 1998, gazeti Mainichi Daily News liliripoti kwamba gharama ya kiuchumi inayotokana na kunywa sana nchini Japani ilikuwa “zaidi ya yeni trilioni 6 [dola bilioni 55] kwa mwaka.” Ripoti moja ya Bunge la Marekani ilisema: “Inakadiriwa kwamba gharama ya kiuchumi iliyosababishwa na kutumia kileo vibaya ilikuwa dola bilioni 184.6 mwaka wa 1998 pekee, au dola 638 hivi kwa kila mwanamume, mwanamke, na mtoto aliyekuwa akiishi Marekani mwaka huo.” Namna gani madhara ya kihisia yaliyopata familia zilizovunjika au kupatwa na msiba na kukatizwa kwa elimu au kazi?
Ni rahisi kuona madhara ambayo jamii hupata kwa sababu ya matumizi mabaya ya kileo. Je, mazoea yako ya kunywa kileo yanahatarisha afya yako na ya wengine? Swali hilo litajibiwa katika makala inayofuata.