Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Panya Waokoa Uhai

Gazeti la Afrika Kusini, The Citizen, linaripoti kwamba vifaa vya kutambua vyuma ambavyo vimetumiwa kwa muda mrefu kutambua mabomu yaliyotegwa ardhini, “hufanya kazi polepole na huchosha kwa kuwa hivyo hunasa kila kipande cha chuma kisha chuma hicho huchunguzwa. Sasa panya mkubwa wa Gambia mwenye vifuko ameanza kutumiwa kutafuta na kuondoa zaidi ya mabomu milioni 100 yaliyotegwa ardhini katika nchi 60 hivi, ambayo huua au kuwajeruhi watu 50 hivi kila siku.” Panya huyo mkubwa anatumiwa pamoja na vifaa vya kutambua vyuma na mbwa kutafuta mabomu ya aina hiyo ambayo bado yanapatikana Msumbiji muda mrefu baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe kukoma mwaka wa 1992. Gazeti hilo linasema: “Mabomu yaliyotegwa ardhini ni mabaki hatari ya vita hivyo ambayo huwalemaza na kuwaua raia wa Msumbiji hadi leo, kutia ndani watoto wa mashambani ambao walizaliwa muda mrefu baada ya vita hivyo kukoma.” Panya huyo mkubwa wa Gambia ambaye ana vifuko vikubwa mdomoni vya kubebea chakula, hupatikana katika sehemu nyingi za Afrika, anaweza kufugwa kwa urahisi, na anaweza kuwa mnyama kipenzi.

Kupanda au Kuteremka?

Je, kuna tofauti yoyote kwa afya mtu anapofanya mazoezi kwa kutembea akipanda au kuteremka mteremko mkali? Watafiti wanasema kwamba kunaweza kuwa na tofauti. Uchunguzi ulifanywa kwenye mlima mmoja wa Alps ambako kwa miezi miwili wajitoleaji 45 walipanda mlima wenye mwinuko wa digrii 30 na kuteremka kwa gari linaloning’inia kwa nyaya. Kisha, kwa miezi miwili mingine walipanda kwa gari hilo na kuteremka kwa miguu. Ingawa kupanda na kuteremka kulipunguza kolesteroli hatari, uchunguzi huo ulidokeza kwamba “kupanda mlima kulisaidia sana kupunguza kiwango cha mafuta yanayoitwa triglycerides, hali kuteremka kulipunguza kiasi cha sukari kwenye damu na kuboresha uwezo wa kumeng’enya sukari mwilini,” linasema jarida Tufts University Health & Nutrition Letter. Hivyo, huenda mazoezi ya kuteremka mlima yakawasaidia watu walio na ugonjwa wa kisukari na ni mazoezi rahisi kwa wale wanaoanza tu kufanya mazoezi. Wakazi wa mjini wanaweza kufanya mazoezi hayo kwa kupanda lifti katika jengo refu kisha kuteremka kwa ngazi au kushuka gari juu mlimani kisha kuteremka kwa miguu. Hata hivyo, uwe mwangalifu kwani mazoezi ya kuteremka mlima hufanyiza magoti kazi nyingi.

Sakafu ya Bahari Imejaa Viumbe

Mradi wa kimataifa unaoitwa Hesabu ya Viumbe vya Majini, unafanya uchunguzi mkubwa wa bahari, kutia ndani sakafu ya bahari. Gazeti la Hispania El País linaeleza kwamba kufikia sasa, “watu wanajua tu viumbe wa baharini walio katika sehemu ya juu ya bahari, kufikia kina cha meta 200.” Kwa kuwa sakafu za bahari nyingi huwa na kina cha kati ya kilometa 5 hadi 11, asilimia 95 ya sakafu ya bahari haijachunguzwa bado. Ili kutimiza sehemu ngumu ya uchunguzi huo, wanabiolojia watatumia vifaa vya hali ya juu ili kupata na kupiga picha jamii mbalimbali za viumbe katika mazingira yao ya asili, kwa kuwa tabia ya viumbe wengine hubadilika sana wanapopelekwa kwenye sehemu ya juu ya bahari. Kikundi kimoja cha wanabiolojia 50 wanatazamia kupata mamilioni ya jamii mpya za viumbe katika vilindi vya bahari. Pedro Martínez Arbizu, msimamizi wa mradi huo anasema kwamba walipata jamii 500 katika eneo la kilometa moja ya mraba katika sakafu ya bahari karibu na pwani ya Angola, Afrika. Msimamizi huyo anasema kwamba kati ya jamii hizo, “asilimia 90 hazijulikani na wanasayansi na lazima zifafanuliwe na kupewa majina.”

Chokoleti Hudhuru Mbwa

Shirika la Utangazaji la Uingereza linaonya kwamba chokoleti “hufanya mbwa watapike na kuzimia” na hata “inaweza kuua [mbwa] wakila kiasi kikubwa.” Chokoleti ina kemikali inayoitwa theobromine ambayo ni sumu kwa mbwa nayo huathiri moyo, figo, na mfumo wao mkuu wa neva. Ripoti hiyo inasema kwamba “[gramu 200] za chokoleti nyeusi zinaweza kuua mbwa mwenye uzito wa [kilogramu 25], kama vile Labrador wa kike.” Mbwa mdogo anaweza kufa kutokana na gramu 30 tu za chokoleti chungu inayotumiwa kuoka. Hata hivyo, chokoleti iliyotengenezwa hasa kwa ajili ya mbwa na ambayo hununuliwa katika maduka ya wanyama haiwezi kuwadhuru.

Mtu Anapojaribu Kuiba Gari Lako

Gazeti El Universal linaripoti kwamba wizi wa magari umekuwa biashara kubwa huko Mexico City. Kila siku wastani wa magari 80 huibwa na kuuzwa tena. Kulingana na mwendesha-mashtaka mmoja, wezi hao hupendelea kushambulia wanaume wanaosafiri peke yao kwani wao huona kuwa huenda wanawake wakapiga mayowe au wakaambatana na watoto na hivyo kufanya iwe vigumu kuiba gari. Asilimia 85 ya wezi waliokamatwa ni vijana walio na umri wa kati ya miaka 18 hadi 25. Mbinu zinazotumiwa kwa ukawaida hutia ndani kumtisha dereva kwa bunduki anaposimama kwenye taa za barabarani, kugonga gari na hivyo kumfanya dereva atoke, au kumvamia dereva anapofungua mlango wa gereji yake. Gazeti hilo linapendekeza madereva wasishindane na wezi, bali watulie, hasa ikiwa wezi hao wana silaha, na wajaribu kukumbuka habari nyingi wawezavyo kuhusu wezi hao. Ili kurahisisha kazi ya kutafuta gari lililoibwa, watu wanapaswa kujua nambari na rangi ya gari lao na kutoa habari hizo na habari nyingine muhimu kwa polisi mara moja.

Madereva Matineja

Wazazi ambao hutaka kuwazuia matineja wao wasiendeshe gari sasa wanaweza kupata habari zaidi kuhusu manufaa ya kufanya hivyo kwa kutegemea utafiti uliofanywa na Taasisi za Kitaifa za Afya huko Marekani. Uchunguzi huo “unadokeza kwamba sehemu ya ubongo ambayo huzuia tabia zinazoweza kutokeza hatari hukomaa kabisa mtu anapofikia umri wa miaka 25,” linaripoti gazeti la kimataifa The Miami Herald. Hapo awali ilidhaniwa kwamba ubongo hukomaa mtu anapofikia umri wa angalau miaka 18 wakati hisi na uwezo wa kunyumbulika hukomaa kabisa. Hata hivyo, takwimu za Taasisi ya Bima ya Usalama wa Barabarani zinaonyesha kwamba “kuna uwezekano mara nne zaidi wa matineja kuhusika katika aksidenti kuliko madereva wenye umri mkubwa na kuna uwezekano mara tatu zaidi kwa matineja kufa katika mojawapo ya aksidenti hizo.” Jambo hilo linaonyesha kwamba matineja wanaweza kukengeushwa kwa urahisi zaidi nao wana mwelekeo wa kuendesha gari kwa njia hatari.

Onyo Kuhusu Dawa za Kufanya Meno Yawe Meupe

Gazeti Milenio la Mexico City linaripoti kwamba wataalamu wa meno katika Hospitali ya Umma ya Fray Antonio Alcalde huko Guadalajara, Mexico, wanaonya kwamba dawa za kufanya meno yawe meupe zinaweza kudhuru na kusababisha maumivu. Zinaweza “kudhuru sehemu za juu na za ndani” za meno na bado huenda zisifanye meno yawe meupe. Kulingana na wataalamu hao, meno yenye afya yanaweza kuwa ya rangi tofauti-tofauti kuanzia ya machungwa hadi ya kijivu. Mtaalamu Rocío Liliana Hernández anasema kwamba kuwa na meno meupe hakumaanishi kwamba yana afya, ingawa watu wamesadikishwa kwamba meno meupe ndiyo meno “maridadi na yenye afya zaidi.”