Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Uvumbuzi Kwenye Ghuba ya Red

Uvumbuzi Kwenye Ghuba ya Red

Uvumbuzi Kwenye Ghuba ya Red

Na mwandishi wa Amkeni! nchini Kanada

“HUO si mwisho wa dunia, lakini unaweza kuona mwisho ukiwa huko,” huenda watu wakasema. Ikiwa umewahi kutembelea Ghuba ya Red, mashariki mwa Kanada, huenda wewe pia ukasema kwamba mahali hapo ni karibu na mwisho wa dunia. Mji huo mdogo uko kwenye pwani maridadi ya Labrador, karibu na Mlango-Bahari wa Kisiwa cha Belle. Ni nini hufanya Ghuba ya Red yenye utulivu na bandari iliyokingwa iwe ya kipekee na yenye kuvutia?

Historia Yake ya Pekee

Mji huo hujaa wageni wakati wa kutazama nyangumi unapofika. Lakini si jambo hilo limekuwa likifanya watu watembelee mji huo. Zaidi ya miaka 400 iliyopita, nyangumi wenye vichwa vikubwa waliwindwa huko kwa sababu ya mafuta yao yenye thamani. Kulingana na kichapo kimoja, “kulipokuwa na uhaba . . . , [mafuta ya nyangumi] yaligharimu dola 10,000 kwa pipa kulingana na pesa za kisasa.” Wavuvi wa nyangumi wa Ghuba ya Biscay, eneo linalopakana na Ufaransa na Hispania walikuwa kati ya Wazungu wa kwanza kutumia maliasili za Kanada. Mafuta ya nyangumi ndiyo hasa yaliyotumiwa kuwasha taa barani Ulaya. Yalitumiwa pia kulainisha mashini, kutengeneza sabuni na vipodozi, na yalitumiwa kutengeneza ngozi, sufu, na rangi. Katika sehemu ya mwisho ya karne ya 16, Ghuba ya Red ndiyo iliyokuwa bandari kubwa zaidi ya kuvua nyangumi ulimwenguni. Hivyo mojawapo ya biashara za kwanza za kuvua nyangumi zilianzishwa nchini Kanada.

Tuna Uthibitisho Gani?

Hati zilizopatikana katika hifadhi ya nyaraka katika Ghuba ya Biscay zilifanya waakiolojia na wanahistoria watembelee Ghuba ya Red. Rekodi hizo zinaonyesha kwamba meli ya Hispania inayoitwa San Juan ilizama huko wakati wa dhoruba mnamo 1565.

Uchimbuzi mbalimbali katika Kisiwa cha Saddle kilichoko karibu na fuo za Ghuba ya Red, ulifukua vitu vilivyotumiwa zamani kuvua nyangumi kama vile kichwa cha chusa chenye vichomeo viwili. Bado wageni wanaweza kuona marundo ya vigae vyekundu vya Wahispania kwenye fuo. Kwa miaka mingi watoto wa eneo hilo walicheza navyo. Mkaazi mmoja alisema hivi: “Tulitumia vigae hivyo vyekundu kama chaki ya kuchora picha na kupaka rangi picha kwenye miamba, bila kujua kwamba tulikuwa tukicheza na vitu muhimu!”

Katika kiangazi cha mwaka wa 1978, waakiolojia wanaochimbua vitu vilivyo majini walipata kipande cha mwaloni meta 30 hivi kutoka kwenye ufuo wa Kisiwa cha Saddle. Uvumbuzi huo ulikuwa muhimu kwani mbao za mwaloni ndizo hasa zilizotumiwa na wajenzi wa meli kutoka Ghuba ya Biscay, nazo hazipatikani katika pwani isiyo na rutuba ya Labrador. Baadaye, waligundua mabaki ambayo waliamini kuwa ni meli ya San Juan, ambayo kwa kushangaza, ilikuwa katika hali nzuri. Maji baridi sana ya Ghuba ya Red yalikuwa yamehifadhi meli hiyo. Ilikuwa meta 10 hivi kwenye sakafu ya bahari ikiwa imefunikwa kwa mchangatope. Inaonekana kwamba baada ya muda mrefu, uzito wa barafu ulipasua meli hiyo katikati na kuilaza kama kitabu kilichofunguliwa. Waakiolojia walisisimuliwa na uvumbuzi huo kwani ilikuwa ndiyo meli ya kwanza ya kibiashara ya karne ya 16 kuvumbuliwa ikiwa nzima huko Amerika, kaskazini ya Florida.

Je, Kweli Ilikuwa San Juan?

Wapiga mbizi walichimbua meli hiyo kipande kwa kipande na kuandika kila kipande namba. Baada ya kuichunguza kwa makini, meli hiyo ilirudishwa tena kwenye sakafu ya bahari ili ihifadhiwe. Uchunguzi huo ulionyesha nini? Meli hiyo yenye uzito wa tani 300 hivi iliundwa ili iweze kusafiri baharini, wala si ivutie kwa umaridadi wake. Ilikuwa na miisho ya miraba iliyoiwezesha kubeba kiasi kikubwa cha mizigo ya mafuta ya nyangumi hadi Hispania. Rekodi za awali kuhusu meli ya San Juan iliyozama zinaonyesha kwamba meli hiyo ilikuwa imebeba kiasi kikubwa cha mafuta ya nyangumi. Wanabaharia wake walifaulu kuokoa kiasi kikubwa cha mafuta hayo. Katika sehemu za chini za meli hiyo, wapiga mbizi waligundua mapipa 450 hivi ambayo yaonekana mabaharia walishindwa kuyatoa. Hakuna maiti zozote zilizopatikana kwenye meli hiyo. Hati zilizopatikana kwenye Ghuba ya Biscay hazikutaja kwamba kuna mtu yeyote aliyekufa wakati meli hiyo ilipozama. Mambo hayo yanayopatana yamefanya wachunguzi waamini kwamba meli hiyo ilikuwa San Juan iliyozama. Isitoshe, wapiga mbizi walipokuwa wakichimbua meli hiyo, waligundua mashua moja ya kuvua nyangumi ya wakaaji wa Ghuba ya Biscay iliyoitwa chalupa. Robert Grenier, msimamizi wa akiolojia ya bahari huko Parks, Kanada, anadai kwamba mashua ya chalupa ni “mojawapo ya maendeleo makubwa zaidi katika teknolojia ya meli.”

Nani angefikiri kwamba wakati mmoja Ghuba ya Red ilikuwa kituo muhimu cha uvuvi wa nyangumi? Kwa kweli, mambo yamebadilika. Hata hivyo, bado eneo hilo lina mambo fulani ya kihistoria ambayo yanaweza kuonwa na kila mtu.

[Ramani katika ukurasa wa 14]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Labrador

Ghuba ya Red

Mlango-Bahari wa Kisiwa cha Belle

Kisiwa cha Newfoundland

[Picha katika ukurasa wa 15]

Meli iliyodhaniwa kuwa “San Juan” ikiwa imepunguzwa ukubwa mara kumi

[Hisani]

Parks Canada Agency, Photographer Denis Pagé

[Picha katika ukurasa wa 15]

Kulia kabisa: Mpiga mbizi akichimbua meli hiyo iliyozama

[Hisani]

Bill Curtsinger/National Geographic Images Collection

[Picha katika ukurasa wa 15]

Kulia kabisa: Nyangumi huyu ni mnyama aliye hatarini

[Hisani]

NOAA

[Picha katika ukurasa wa 15]

“Chalupa,” mashua ya wakaaji wa Ghuba ya Biscay iliyogunduliwa katika Ghuba ya Red

[Hisani]

Parks Canada/Shane Kelly/1998

[Picha katika ukurasa wa 15]

Ghuba ya Red

[Hisani]

Photo courtesy of the Viking Trail Tourism Association

[Picha katika ukurasa wa 15]

Vigae vyekundu vya kutengenezea paa husukumwa hadi ufuoni

[Hisani]

Parks Canada/Doug Cook/1997