Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Delta ya Ulaya Yenye Mandhari Mbalimbali

Delta ya Ulaya Yenye Mandhari Mbalimbali

Delta ya Ulaya Yenye Mandhari Mbalimbali

Na mwandishi wa Amkeni! nchini Rumania

Mto Danube unaanzia huko Black Forest Ujerumani. Ukiwa kijito kinachotiririka kwa kasi, huo husonga kuelekea mashariki kupitia Austria na kwenye mpaka wa Slovakia. Unapokuwa mto mkubwa, huo hutiririka kusini kuelekea Hungary kisha hutiririka kwenye mpaka kati ya Kroatia na nchi ya Serbia na Montenegro. Kisha hutiririka polepole na kupanuka unapojipinda-pinda kwenye mpaka wa Bulgaria kabla ya kugeuka na kuelekea kaskazini kupitia Rumania. Mwishowe unapita kwenye mpaka wa Ukrainia.

Ukiwa umejaa mchanga-tope na maji mengi kutoka vijito 300 hivi, hatimaye mto huo mkubwa hutokeza delta maridadi kwenye ufuo wa Bahari Nyeusi. Karibu na jiji la Tulcea, kusini-mashariki mwa Rumania, mito mitatu inayotokana na Mto Danube, yaani, Kiliya, Sulina, na St. George, hufanyiza mifereji mikuu ambayo huelekeza maji kwenye Bahari Nyeusi.

Mito hiyo mitatu inayotokana na Mto Danube inapopita polepole kwenye delta hiyo, inagawanyika na kutokeza vijito vingi vidogo ambavyo huelekeza maji kwenye vinamasi na maziwa kadhaa. Mchanga kutoka kwenye mto huo pamoja na ule wa baharini huungana na kutokeza vilima vikubwa vya mchanga na visiwa. Vilima fulani vya mchanga kama vile vya Caraorman vina urefu wa meta sita hivi na huonekana kama jangwa.

Hata hivyo, Delta ya Danube si mandhari tu ya mchanga na mchanga-tope unaobadilika-badilika. Delta hiyo ina eneo la kilometa 4,300 hivi za mraba na ndilo eneo kubwa zaidi lenye vinamasi barani Ulaya. Isitoshe, inaelekea kwamba delta hiyo ndiyo eneo kubwa zaidi lenye matete ulimwenguni—lina ukubwa wa kilometa 1,700 hivi za mraba!

Misitu mikubwa yenye miti aina ya mibetula, mialoni, na alder hukua kwenye vilima kadhaa vya mchanga vya delta hiyo. Mimea mingi ambayo hutambaa kama vile mizabibu-mwitu, mwefeu, mtambaa, na mimea mingine hukwamilia miti hiyo ili kupata nuru ya jua. Katika njia fulani, delta hiyo ni kichungi ambacho hutumika kama mfumo mkubwa zaidi wa kuchuja maji huko Ulaya.

Makao Mazuri ya Wanyama

Mamilioni ya ndege wa jamii zaidi ya 300 huja kwenye paradiso hiyo ya ndege. Karibu nusu ya waari weupe walio duniani na zaidi ya asilimia 60 ya aina fulani ya mnandi ulimwenguni hutaga mayai katika Delta ya Danube. Pia, karibu bata-bukini wote wenye manyoya mekundu kifuani ambao wamo katika hatari ya kutoweka, huja hapa wakati wa majira ya baridi kali. Katika mwezi wa Machi, waari hujenga viota vyao na kutaga mayai kwenye visiwa vya matete vinavyoelea vilivyo mbali. Majira ya kupukutika kwa majani yanapoanza, waari huhamia Delta ya Nile, Ugiriki, na pwani za Asia zilizo mbali kama vile India.

Ndege hao hurudi kwenye Delta ya Danube si kwa sababu tu mazingira hayo yanafaa bali pia kwa sababu ya samaki. Kuna zaidi ya jamii 90 za samaki katika mifereji ya delta hiyo. Kwa kweli, nusu ya samaki wote wa maji yasiyo na chumvi wanaoliwa nchini Rumania hutoka katika Delta ya Danube. Kati ya samaki maarufu wa delta hiyo ni sturgeon, ambao huogelea dhidi ya mkondo wa Mto Danube wakati wa majira ya kutaga mayai. Mayai hayo ni chakula kitamu kinachouzwa kwa bei ghali.

Eneo hilo lina sehemu ndogo sana ya nchi kavu—ni asilimia 13 tu ya eneo hilo la delta lililo juu ya maji. Mbwa-mwitu, mbweha, sungura, na muskrati huwinda katika eneo hilo. Wanyama wanaokabili hatari ya kutoweka kama vile fisi-maji na aina fulani ya cheche wa Ulaya ambao wakati mmoja ngozi yao ilipendwa sana na wanawake wa mitindo pia huishi kwenye delta hiyo. Isitoshe, jamii zaidi ya 1,800 za wadudu huvuma na kutambaa katika nchi hiyo nzuri yenye maji.

Hifadhi ya Viumbe Inayopaswa Kulindwa

Katika mwaka wa 1991, Delta ya Danube iliorodheshwa kati ya Maeneo Yanayostahili Kuhifadhiwa Ulimwenguni. Mwaka uliofuata, ilitambuliwa ulimwenguni pote kuwa hifadhi ya viumbe. Hifadhi hiyo husimamiwa na jiji la Tulcea. Uvuvi unadhibitiwa na serikali, ingawa uwindaji haramu bado ni tatizo kubwa.

Hata hivyo, hali ya delta hiyo inategemea majiji na viwanda ambavyo humwaga uchafu kwenye Mto Danube wenye urefu wa kilometa 2,850 unapoelekea baharini. Kwa miaka mingi, mbuga zenye maji zilichuja sehemu ya chini ya Mto Danube kabla maji hayo hayajaingia kwenye delta. Sasa, karibu asilimia 80 ya mbuga hizo zimetoweka.

Leo delta hiyo inapanuka kwa meta 30 hivi kila mwaka kuelekea kwenye Bahari Nyeusi. Kama ambavyo imekuwa ikifanya kwa maelfu ya miaka, Delta ya Danube inaendelea kupanuka na kurekebisha eneo hilo lenye mandhari mbalimbali.

[Ramani katika ukurasa wa 24]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

UKRAINIA

MOLDOVA

RUMANIA

Bucharest

Delta ya Danube

BAHARI NYEUSI

Mto Danube

BULGARIA

[Picha katika ukurasa wa 24]

Eneo la delta, ambalo ni mojawapo ya maeneo makubwa zaidi yenye matete ulimwenguni, lina wanyama wa kila aina

[Picha katika ukurasa wa 24]

Muskrati

[Picha katika ukurasa wa 25]

Karibu nusu ya waari weupe ulimwenguni hutaga mayai hapa

[Picha katika ukurasa wa 26]

Mdiria na zaidi ya jamii 300 za ndege huja kwenye paradiso hii ya ndege

[Picha katika ukurasa wa 26]

Zaidi ya jamii 1,800 za wadudu zinapatikana katika Delta ya Danube

[Picha katika ukurasa wa 25]

All photos: Silviu Matei

[Picha katika ukurasa wa 26]

All photos: Silviu Matei

[Picha katika ukurasa wa 24]

All photos: Silviu Matei