Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Jicama—Chakula Chenye Afya cha Wamexico

Jicama—Chakula Chenye Afya cha Wamexico

Jicama—Chakula Chenye Afya cha Wamexico

Na mwandishi wa Amkeni! nchini Mexico

Majani na maganda mabivu ya jicama, mmea wa jamii ya kunde unaotambaa si matamu. Hiyo si hoja kwa kuwa hayaliwi. Sehemu yake tamu iko chini ya ardhi, kwenye mizizi yake.

Wamexico wamekuwa wakila jicama tangu zamani. Jina lake, linalotokana na lugha ya Nahuatl linamaanisha “kinachoonjwa.” Na unaweza kudondokwa na mate uonapo tu picha ya chakula kinachopendwa cha Mexico kilichotayarishwa kwa vipande vilivyokatwa-katwa vya jicama mbichi ambavyo vimekolezwa maji ya ndimu, chumvi, na pilipili.

Jicama ina ladha gani? Watu fulani wanasema kwamba ina ladha kama ya tofaa na pia ya chestinati. Mmea wa jicama ambao ulianza kukuzwa Mexico na Amerika ya Kati, sasa unakuzwa katika nchi za mbali kama vile Ufilipino, China, na Nigeria. Leo unakuzwa katika nchi nyingi, ambako unatayarishwa katika njia mbalimbali kama vile, kukaangwa, kuhifadhiwa katika siki na chumvi, kutumiwa katika saladi, na kuchemshwa katika supu.

Katika mapishi ya nchi za Mashariki, jicama hutumiwa badala ya chestinati. Mboga hizi zinathaminiwa kwa sababu hata baada ya kupikwa huendelea kuwa kavu. Ndivyo ilivyo hasa kuhusiana na jicama ya maziwa, ambayo hutokeza umajimaji wa maziwa, tofauti na jicama ya maji. Kwa kupendeza, mimea yote miwili inaweza kukua kutokana na mbegu ileile.

Jicama ni chakula kinachofaa. Kinajenga mwili, kinaburudisha, kina umajimaji, ni rahisi kumeng’enya, na hakina kalori nyingi. Uchunguzi uliofanywa na taasisi ya chakula ulionyesha kwamba ingawa gramu 100 za viazi vya chipsi vina kalori 540, kiasi hichohicho cha jicama kina kalori 40 tu! Pia jicama inafaa kwa sababu ina kalisi, fosforasi, na vitamini C.

Kama ilivyotajwa, sehemu nyingine za mmea wa jicama isipokuwa mizizi yake haziliwi, lakini hiyo haimaanishi kwamba hazifai. Mbegu zilizo kwenye ganda zina vitu kadhaa ambavyo vinaweza kutumiwa kutengeneza dawa ya kuua wadudu. Zinapopondwa, mbegu zake zinaweza kutumiwa kutengeneza dawa ya kuua wadudu na pia hizo hutumiwa kutengeneza dawa fulani za ngozi. Kwa upande mwingine, matawi yake yana nyuzinyuzi ngumu zinazoweza kutumiwa kutengeneza nyavu za kuvua samaki.

Mizizi ya jicama ina ukubwa mbalimbali, kuna ile yenye uzani unaopungua gramu 300, kisha kuna ile yenye uzani wa kilogramu moja. Inaweza kukaa ndani ya friji kwa muda wa majuma matatu hivi bila kuharibika. Ili kutumia jicama, unahitaji tu kuiosha, kuiminya, na isipokuwa iwe changa sana, ondoa ganda lake la juu lenye nyuzinyuzi.

Kwa hiyo ikiwa kuna jicama mahali unapoishi, kwa nini usijaribu kuipika? Huenda ikaboresha afya yako!