Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Manufaa za Kucheka

Gazeti la kila juma la Poland Przyjaciółka linaripoti hivi: “Wanasayansi wamekadiria kwamba kucheka kwa furaha kwa nusu dakika ni sawa na kupumzika kabisa kwa dakika 45. Kuangua kicheko kunalingana na kufanya mazoezi ya viungo kwa dakika tatu, hali kutabasamu kwa uchangamfu mara kumi ni sawa na kufanya mazoezi makali kama ya kupiga makasia kwa kutumia mashini kwa dakika kumi.” Manufaa mengine ya kucheka yanatia ndani kuongezeka mara tatu kwa kiasi cha hewa kinachovutwa ndani ya mapafu na vilevile kuboreshwa kwa mzunguko wa damu, umeng’enyaji, kuyeyushwa kwa chakula, utendaji wa ubongo, na kuondolewa kwa vitu vyenye kudhuru. Gazeti hilo linapendekeza kwamba ili uwe mwenye furaha, jambo la kwanza unalopaswa kufanya kila asubuhi ni kutabasamu na kumwonyesha mwenzi wako na watoto wako tabasamu. Linaongeza hivi: “Jifunze kujicheka unapokosea. Jaribu kuona mambo kwa njia nzuri hata wakati hali inapokuwa ngumu.”

Watoto Wanaoota Jua Mchana Hulala Usingizi Mnono Usiku

Uchunguzi uliofanywa hivi karibuni kuhusu mazoea ya kulala ya watoto 56 wenye afya na kuchapishwa katika jarida Journal of Sleep Research, ulionyesha kwamba “watoto waliolala vizuri usiku ni wale ambao walipata mwangaza zaidi mapema alasiri.” Hata hivyo, mwangaza wa asubuhi na jioni hakukutokeza tofauti yoyote katika usingizi. Msimamizi wa uchunguzi huo, Dakt. Yvonne Harrison wa Chuo Kikuu cha John Moores, huko Liverpool, Uingereza, ambaye ni mama, aliamua kuchunguza jinsi nuru huathiri usingizi wa watoto kwa sababu uchunguzi wa hapo awali ulionyesha kwamba wazee hulala vizuri wanapopata mwangaza wa kutosha mchana.

Ugonjwa wa Chagas Unaenea

Ugonjwa wa Chagas hutokana na kimelea kinachopitishwa katika kinyesi cha mdudu anayenyonya damu ambaye huuma karibu na mdomo. Ugonjwa huo hupatikana hasa katika maeneo ya mashambani ya Mexico na Argentina. Gazeti The Herald la Mexico linaripoti kwamba karibu raia milioni moja na nusu wa Mexico wana vimelea hivyo. Hata hivyo, ugonjwa wa Chagas unaenea katika sehemu nyingine za ulimwengu. Njia moja ambayo ugonjwa huo huenezwa ni kupitia kutiwa damu mishipani. Bert Kohlmann, mwanabiolojia wa Mexico anaeleza hivi: “Tayari tumepata ripoti kutoka Australia, Ulaya, Marekani, na Kanada kuhusu damu iliyoambukizwa. Wahamiaji kutoka Amerika ambao kwa kawaida ni wenye afya hutoa damu na hakuna mtu katika sehemu hizo nyingine ambaye hushughulika kuchunguza ikiwa ina ugonjwa wa Chagas.” Shirika la Afya Ulimwenguni linakadiria kwamba huko Amerika Kusini na Kaskazini, watu milioni 16 hadi 18 wameambukizwa ugonjwa huo na watu milioni 100 hivi wanakabili hatari ya kuambukizwa. Kwa sasa, ugonjwa wa Chagas hauna tiba na mara nyingi huua.

Kuchochea Watu Walipe Kodi

Shirika la habari la Reuters liliripoti kwamba ili kuwatia moyo wakazi walipe kodi zao za nyumba na mashamba zenye thamani ya dola milioni 1.15 maofisa wa jiji la Rajahmundry, India, waliahidi kwamba hawatawatoza watu faini na riba. Mbinu hiyo ilipokosa kufaulu, maofisa hao walikodi vikundi 20 vya wapiga ngoma wacheze nje ya nyumba za watu ambao hawakulipa kodi. Wapiga ngoma hao “hutokeza tamasha nje ya nyumba za watu wanaokosa kulipa kodi, wanawavutia kutoka nje na kuwaeleza madeni yao na uhitaji wa kuyalipa haraka iwezekanavyo,” akasema kamishna wa manispaa T.S.R. Anjaneyulu. “Hawaachi kupiga ngoma hadi watu wakubali kumaliza madeni yao.” Mbinu hiyo isiyo ya kawaida ilifaulu. Baada ya wapiga ngoma hao kucheza kwa juma moja tu, jiji hilo lilikuwa limelipwa asilimia 18 ya madeni ya kodi ya mashamba na nyumba.

Dini Nchini Urusi

Zamani, ilifikiriwa kwamba wanawake, wazee, na watu ambao hawakumaliza masomo yao ya sekondari ndio hasa waliojishughulisha na dini zaidi nchini Urusi. Hata hivyo, gazeti la Urusi Rossiyskaya Gazeta linaripoti kwamba takwimu zinaonyesha kuwa idadi ya vijana, wanaume, na watu wenye elimu ya juu wanaojishughulisha na dini inaongezeka. Kati ya mwaka wa 1989 na 1991, ni asilimia 30 tu ya watu waliodai kuwa waumini wa kanisa la Othodoksi. Lakini baada ya 1999, idadi hiyo iliongezeka na kuwa zaidi ya asilimia 50. Hivi karibuni, wanasoshiolojia wa Urusi walipata kwamba asilimia 30 ya Warusi wanaamini kwamba kuna uhai baada ya kifo, asilimia 24 wanaamini kwamba watu huenda mbinguni na motoni, na asilimia 28 huamini katika miujiza ya kidini. Karibu thuluthi moja ya wale waliohojiwa walikubaliana na maneno haya ambayo watu husema: “Ninaamini kwamba Mungu yuko na sina shaka kuhusu hilo.” Wakati huohuo, “asilimia 30 ya Warusi huamini katika unajimu, na asilimia 50 hadi 55 wanaamini katika ndoto za kinabii na ishara za bahati,” inasema ripoti hiyo.

Kanisa la Ugiriki Linaanza Kutumia Kigiriki cha Kisasa

Akiwa na wasiwasi kwamba Wagiriki wengi ambao huenda kanisani hawaelewi maandiko ya Biblia yanayosomwa kanisani katika Kigiriki cha kale, askofu mkuu wa Ugiriki aliagiza makanisa ya Athens yatumie Kigiriki cha kisasa pia. “Agano Jipya limesomwa katika Kigiriki cha awali, yaani ‘Koine’ au lugha ya kawaida, lugha ambayo ilizungumzwa na Wagiriki mwishoni mwa karne ya nne K.W.K. hadi karne ya tano W.K.,” likaeleza gazeti Kathimerini. Lakini askofu mkuu huyo alikuwa na “wasiwasi kwamba hasa vijana hawawezi kuelewa Kigiriki hicho na hawawezi kuelewa mambo yanayosemwa kwenye ibada,” ilisema ripoti hiyo. Katika programu ya majaribio ambayo gazeti Kathimerini liliitaja kuwa “badiliko kubwa sana katika Kanisa ambalo hushikilia sana mapokeo yake,” maandiko ya Biblia yalisomwa kwanza katika Kigiriki cha Koine kisha katika Kigiriki cha kisasa. Hata hivyo, karibu mwaka mmoja baadaye, gazeti hilo liliripoti kwamba kanisa “lilikuwa likitupilia mbali” jitihada hiyo ya “kuwafanya watu waelewe Agano Jipya linaposomwa.”

Vituo vya Kutafuta Marafiki wa Zamani Vinaongeza Idadi ya Talaka

Vituo vya Intaneti vinavyowakutanisha wanashule wa zamani “vinachochea ongezeko la kuvunjika kwa ndoa wakati waume na wake waliochoshwa na wenzi wao wanapowasiliana na wapenzi wao wa zamani,” linaripoti gazeti la Uingereza Guardian Weekly. Akieleza jinsi zoea hilo linavyoathiri idadi ya talaka nchini Uingereza, ambayo katika mwaka wa 2004 ilifikia kiwango cha juu zaidi katika miaka saba, Christine Northam, msemaji wa shirika la Relate linalotoa mashauri ya ndoa alisema hivi: “Watu wengi hukumbuka kwa furaha uhusiano wa kwanza ambao walikuwa nao wakiwa shuleni au chuoni. Ikiwa hawafurahishwi na mwenzi wao, wanaanza kujiuliza hali ingekuwaje iwapo wangeishi na mpenzi wao wa awali.” Sasa ni rahisi zaidi kwa wenzi wa ndoa wasio na furaha “kutafuta mahaba kwenye Intaneti,” linasema gazeti hilo, “badala ya kutatua matatizo ya kihisia ya ndoa yao.”

Ngazi Ni Hatari

Gazeti la Marekani The Week, linasema kwamba kutumia ngazi “husababisha majeraha kila mwaka kuliko aksidenti za magari.” Ripoti hiyo inaongeza hivi: “Kila mwaka Wamarekani 1,091 ambao hutumia ngazi hufa na 769,400 hujeruhiwa.” Ni nini humfanya mtu ajikwae na kuanguka? Kwa kawaida, watu hukosa kukadiria umbali na kukanyaga mahali pasipofaa,” linasema gazeti The Week.