Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Nyumba Zenye “Makoti ya Manyoya”

Nyumba Zenye “Makoti ya Manyoya”

Nyumba Zenye “Makoti ya Manyoya”

Na mwandishi wa Amkeni! nchini Ukrainia

MADUKA, nyumba, na ofisi kotekote Ukrainia zimepambwa kwa kitu fulani kinachoitwa shuba, yaani, “makoti ya manyoya.” Shuba ni chokaa iliyochanganywa na simiti na mchanga ambayo hupakwa kwenye nyumba na kufanya zifanane na koti lenye manyoya ya kondoo. Matajiri wanaoishi kwenye majumba ya kifahari na pia wakulima wa hali ya chini huvutiwa na uzuri wa shuba nao hutumia pesa nyingi kupamba nyumba zao kwa “makoti [hayo] ya manyoya.”

Kwa kawaida, mtu anaweza kujifunza mbinu za kupaka chokaa hiyo kwa muda wa miaka miwili hivi. Vifaa vya kupaka chokaa hiyo ni vichache na sahili. Vinatia ndani ndoo ya kubebea simiti, ufagio mfupi, na fimbo ya mbao au ya chuma. Hata hivyo, ufundi wa kupaka shuba si rahisi hata kidogo.

Shuba inahusisha mambo mengi zaidi kuliko kupaka nyumba chokaa. Inatia ndani kiasi cha chokaa kitakachotumiwa, rangi, na maumbo na michoro mbalimbali. Msanii anaweza tu kujifunza ustadi wa kupaka nyumba shuba ikiwa anaweza kutambua maumbo yatakayofaa jengo fulani.

Maumbo mbalimbali yatakayotumiwa yanaweza kuchorwa ukutani kabla ya kupaka simiti. Ili kufanya maumbo hayo yaonekane, yanaweza kupakwa simiti ya rangi iliyokolea na rangi hafifu. Baada ya shuba kukauka, ukuta hunyunyiziwa rangi ili kuufanya uwe maridadi.

Akiwa ameshika ufagio wake kwa mkono mmoja, msanii anautumbukiza kwenye simiti, kisha anaupigisha kwenye fimbo yake ambayo ameshikilia katika mkono ule mwingine. Simiti inapeperushwa hadi ukutani. Msanii anayefanya kazi kwa mwendo wa kadiri anaweza kupaka shuba kwenye ukuta wenye ukubwa wa kati ya meta 20 hadi 25 za mraba kwa siku.

Ingawa kupaka shuba ukutani ni kazi nyingi sana, ni rahisi kudumisha nyumba zilizopakwa shuba. Mwenye nyumba anahitaji tu kuondoa vumbi mara moja kwa mwaka kwa kumwagia ukuta maji kisha kupaka shuba kwenye sehemu ambazo zimeparara. Kufuata hatua hizo kutahakikisha kwamba shuba itadumu kwa muda mrefu. Kwa kweli, nyumba nyingi bado huonekana kuwa mpya kabisa miaka 20 baadaye kwa sababu ya kupakwa shuba.

Msanii mmoja amefaulu kutumia ustadi wake katika nchi nyingine. Alipomtembelea rafiki yake huko Balingen, Ujerumani, aliombwa apake nyumba ya rafiki yake shuba. Ingawa shuba hutumiwa kwa ukawaida nchini Ukrainia, ilionwa kuwa kitu kipya katika mji huo.

Msanii huyo alipokuwa akipaka shuba, majirani wote walivutiwa na kazi hiyo. Mwanakandarasi mmoja alitazama kwa mshangao jinsi ambavyo vifaa sahili vingeweza kutokeza umaridadi huo. Madereva walipokuwa wakipita mahali hapo, walitoa vichwa vyao nje ili kutazama kilichokuwa kikiendelea, naye mwandishi fulani wa habari wa gazeti la huko alipiga picha. Kazi hiyo ilipokamilika, nyumba hiyo ilishinda tuzo kutoka kwa jiji hilo.

Je, shuba itafaa katika ujirani wako? Labda “koti [jipya] la manyoya” nyumbani kwako litafanya nyumba na ujirani wako uvutie.

[Picha katika ukurasa wa 23]

Nyumba iliyopakwa shuba ambayo ilishinda tuzo huko Balingen, Ujerumani

[Picha katika ukurasa wa 23]

Vifaa vya msanii wa shuba vinatia ndani ufagio mfupi na fimbo ya mbao

[Picha katika ukurasa wa 23]

Kupaka nyumba shuba kunahitaji ustadi mwingi