Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Uvutano wa Magazeti

Uvutano wa Magazeti

Uvutano wa Magazeti

Vita vya Kwanza vya Ulimwengu vilipokomesha utawala wa kiukoo huko Ujerumani, serikali ya demokrasi ya kijamii ilianza kutawala huko Berlin. Baadaye, Wakomunisti walijaribu kupindua serikali hiyo mpya. Serikali hiyo na Wakomunisti walihisi kwamba kudhibiti vyombo vya habari kungekuwa sawa na kudhibiti watu na maoni yao pia. Hivyo kukatokea mapambano makali ya kudhibiti vyombo vya habari.

KWA karne chache zilizopita, magazeti yameathiri utamaduni, siasa, yamechangia fungu muhimu katika biashara, na kuathiri maisha ya kila siku ya mamilioni ya watu. Yanaathirije maisha yako?

Yaonekana kwamba mnamo 1605, gazeti la kwanza barani Ulaya lilichapishwa nchini Ujerumani. Katika sehemu fulani leo, karibu watu 3 kati ya 4 walio na umri wa zaidi ya miaka 14 husoma gazeti kila siku. Ingawa katika nchi fulani zinazositawi wakazi 1,000 hupata nakala zinazopungua 20 za gazeti la kila siku, Norway ina zaidi ya nakala 600 kwa kila wakazi 1,000. Kwa ujumla, ulimwenguni pote, magazeti yapatayo 38,000 huchapishwa.

Kila mahali, magazeti hujulisha umma habari muhimu. Lakini yanatimiza mengi zaidi. Magazeti hutoa habari ambazo huathiri maoni ya wasomaji wengi. Dieter Offenhäusser, wa Tume ya Ujerumani ya Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) anadai kwamba, “kusoma gazeti kila siku” huathiri “mitazamo, mwenendo, na hata maadili yetu ya msingi.”

Wanahistoria wasema kwamba magazeti yamechochea, yakaunga mkono, na kutetea vita. Wanatoa mfano wa vita vya 1870 hadi 1871 kati ya Ufaransa na Prussia, vita vya 1898 kati ya Amerika na Hispania, na Vita vya Vietnam vya 1955 hadi 1975. Wafanyabiashara, wanasayansi, watumbuizaji mashuhuri, na wanasiasa wengi wameangamia kwa sababu ya kashfa iliyochapishwa katika magazeti. Katika kashfa ya Watergate inayojulikana sana ya miaka ya katikati ya 1970, waandishi wa habari wanaofichua ufisadi wa serikali na mashirika ya umma walifunua mambo ambayo yalimlazimisha rais wa Marekani, Richard M. Nixon kujiuzulu. Naam, magazeti yana uwezo mkubwa wa kuathiri maoni ya watu kwa njia nzuri au mbaya.

Lakini magazeti yalianzaje? Habari tunazosoma katika magazeti yetu ni zenye kutegemeka kadiri gani? Tunapaswa kujihadhari na mambo gani ili tunufaike nayo?

[Picha katika ukurasa wa 3]

Wapiganaji wajificha nyuma ya magazeti huko Berlin baada ya Vita vya Kwanza vya Ulimwengu