Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Jifunze Kuhusu Mmea Unaoitwa Nopal

Jifunze Kuhusu Mmea Unaoitwa Nopal

Jifunze Kuhusu Mmea Unaoitwa Nopal

Na mwandishi wa Amkeni! nchini Mexico

Nopal ni mmea wa dungusi usiovutia ambao kwa karne nyingi umetumiwa sana na Wamexico. Mmea huo unaweza kupatikana katika nchi nyingine za Amerika, kutia ndani maeneo mengine makame ulimwenguni pote, lakini huenda watu wasitambue faida zake mara moja kwa sababu una miiba mingi. Mmea huo unaweza kukua kufikia kimo cha meta tano. Una mashina membamba yenye umbo la yai yaliyojaa miiba, na mmea huo huzaa matunda matamu.

Jiji la Milpa Alta lililo karibu na Mexico City, ni eneo linalofaa kukuza mimea ya nopal, na kwa muda mrefu wakulima huko wamesafirisha mimea hiyo hadi sehemu nyingine za ulimwengu. Kila mwaka, jiji la Milpa Alta huwa na sherehe ya kuonja vyakula mbalimbali ambavyo hutengenezwa kutokana na mmea wa nopal.

Nchini Mexico, mtu anaweza kununua mashina ya nopal sokoni na hata katika maduka makubwa ya kisasa. Hizo huuzwa zikiwa safi na tayari kuliwa.

Kwa kawaida, nopal huwa nzuri zaidi zikiliwa baada tu ya kuchumwa ikiwa bado nyororo. Wamexico huzitayarisha kwa njia mbalimbali na kuiandaa na aina mbalimbali za nyama. Mlo wa kawaida ni mashina ya nopal yaliyochomwa na kuandaliwa na nyama. Nopal iliyokatwakatwa na kukaangwa pamoja na mayai ni kiamsha-kinywa kitamu.

Isitoshe, saladi yenye ladha tamu inaweza kutayarishwa kwa kukatakata vipande vidogo vya mashina ya nopal yaliyochemshwa, kuongeza vipande vya nyanya, vitunguu, na giligilani, na kuvichanganya katika bakuli iliyotiwa siki, chumvi, na mafuta ya zeituni. Ingawa huenda mwanzoni mashina ya nopal yakaonekana kuwa hayana ladha nzuri, kwa sababu ya ngozi yake yenye utelezi, yanapokolezwa kwa michuzi ya Mexico yenye vikolezo vingi, yanakuwa na ladha yenye kupendeza.

Wakulima wenye uzoefu wanaweza kukata na kusafisha mashina ya nopal haraka na kwa ustadi. Ukiamua kujifanyia hivyo, unahitaji kujihadhari na miiba yake mingi. Inapendekezwa uvae glavu za plastiki.

Imegunduliwa kwamba mmea wa nopal unaweza kutibu magonjwa fulani. Taasisi ya Kitaifa ya Lishe nchini Mexico ilieleza manufaa yake ya afya kwa kusema kwamba inaweza kufanya mambo mengi kama vile kupunguza kolesteroli na LDL (kolesteroli inayodhuru). Wengine wamependekeza kwamba itumiwe kudhibiti kisukari. Huenda wanasayansi wakapata manufaa mengine ya afya yanayotokana na mmea wa nopal wanapoendelea kujifunza kuhusu mmea huo.

Lakini, kwa nini usionje mlo wa kienyeji wa Mexico uliotayarishwa kwa mmea wa nopal? Huenda ukagundua kwamba una manufaa mengi zaidi kuliko inavyoonekana.