Kunywa Chai Kama Wachina
Kunywa Chai Kama Wachina
UNGEPENDA chai ya aina gani? Mahali nilipolelewa, huko Uingereza, iliandaliwa kwa maziwa na nyakati nyingine sukari na ilikuwa chai nzito yenye harufu nzuri. Tulikuwa tukimwambia mama kwa mzaha kwamba chai yake ilikuwa nzito sana hivi kwamba kijiko kingeweza kuelea! Majani-chai meusi aliyotumia yaliitwa chai ya India, kwani yalitoka India au Sri Lanka. Pia nyumbani kwetu kulikuwa pia na kopo la majani-chai kutoka China, ambayo pia yalikuwa meusi lakini yenye ladha na harufu tofauti. Mimi sikupenda chai hata kidogo, hata ingawa kwa kawaida mama alitia kiasi kidogo ndani ya maziwa yangu.
Baadaye maishani, nilianza kunywa chai ya aina tofauti kabisa. Rafiki yangu mmoja Mjapani alinialika ninywe chai. Aliniandalia chai yenye rangi hafifu ya kijani-kibichi katika vikombe vidogo visivyo na vishikio, lakini haikuwa na ladha kama ile ya chai ninayojua. Nilipenda chai hiyo aliyotuandalia! Hata hivyo, rafiki yangu mwingine alimshangaza mkaribishaji wetu alipoomba chai yake iongezwe maziwa na sukari! Mkaribishaji wetu alimwambia kwamba chai ya Wajapani hainywewi hivyo. Baadaye, nilipokuwa nikiishi Japani, nilifurahi kuona kwamba sikuzote Wajapani waliwaandalia wageni na marafiki chai.
Baadaye, nilihamia Taiwan. Nilijiuliza ikiwa chai ambayo mama alikuwa akitayarisha ndiyo chai ambayo Wachina wengi waliokuwa wakiishi huko walikunywa. Nilifurahi kuona kwamba watu nchini Taiwan walikunywa chai ya kijani-kibichi hata ingawa ladha yake ni tofauti kidogo na ile ya Japani. Kisha kuna chai ya oolong,
pia yenye ladha tofauti kabisa, na inayopendwa sana. Labda ungependa kujua jinsi ambavyo aina hizi tatu za chai zilizo tofauti kabisa hutengenezwa na kwa nini zina ladha tofauti sana.Chai Ilitoka Wapi?
Chai ambayo huitwa Camellia sinensis, hukua porini nchini China na Japani, na miti yake hukua kufikia kimo cha meta tisa hivi. Mmea maridadi wenye majani ya rangi ya kijani-kibichi yanayong’aa na maua ya waridi, meupe au mekundu unaoitwa camellia (Camellia japonicus) ni wa jamii ileile ya chai. Kwa kweli, Wachina huuita mmea huo cha hua, yaani, “ua la chai.”
Lakini chai tunayojua hutoka wapi? Kulingana na The Encyclopedia Americana, chai inatajwa kwa mara ya kwanza katika kitabu kinachoeleza kuhusu maisha ya ofisa mmoja Mchina aliyekufa mwaka wa 273 W.K., ingawa inadhaniwa kwamba chai ndio mmea uliotajwa katika kitabu kilichohaririwa na Confucius, aliyeishi yapata mwaka wa 551 K.W.K. hadi 479 K.W.K. Chai ilitajwa mara ya kwanza katika Kiingereza na R. Wickham, mwakilishi wa Kampuni ya East India ya Uingereza, mwaka wa 1615. Katikati ya karne ya 18, Thomas Garway, mmiliki wa mkahawa mmoja huko London ambao baadaye uliitwa Garraway, alinunua chai nyingi.
Chai hukuzwa katika sehemu nyingi ulimwenguni. Waholanzi walipeleka chai huko Java, katika mwaka wa 1826, nao Waingereza wanaojulikana kuwa wapenzi wa chai, wakaipeleka huko India yapata mwaka wa 1836. Kisha katika miaka ya 1870, chai ilikuzwa badala ya kahawa baada ya miti ya kahawa ya Sri Lanka kuharibiwa na kuvu.
Kukuza Chai Nchini Taiwan
Ingawa kisiwa cha Taiwan si kikubwa, sasa kimekuwa kikikuza chai kwa wingi. Eneo la milimani karibu na Nant’ou ni maarufu hasa, kwani maeneo ya mlimani hutokeza chai bora. Tunakualika ujiunge nasi tunapotembelea mojawapo ya maeneo haya maridadi yenye miti ya kijani-kibichi yanayokuza chai.
Tunatembelea Shirika la Wakulima huko LuGu (Bonde la Mbawala), ambako kuna jumba la makumbusho la chai. Tunashangaa kujua kwamba majani-chai ya oolong na ya kijani-kibichi hukunjwa kabla ya kukaushwa. Zamani yalikunjwa kwa kufunga chai ndani ya mfuko na kuubingirisha kwa miguu. Bila shaka, siku hizi kuna mashini ya kufanya kazi hiyo. Sasa tunaweza kuelewa sababu inayofanya kiasi kidogo cha majani-chai ya China yajikunjue na kujaa katika birika yanapomwagiwa maji moto. Tunashangaa kujua kwamba chai nzuri ni ghali sana. Tunaandaliwa chai tamu ya oolong ambayo gramu 600 huuzwa kwa dola 45 hivi. Chai ya bei ghali zaidi inaweza kuuzwa kwa dola 57, au gramu 600 za chai inayoshinda tuzo katika maonyesho inaweza kuuzwa kwa dola zipatazo 1,400.
Aina Mbalimbali za Chai
Bado watu wengi wa nchi za Magharibi hupenda chai nyeusi. Wanywaji chai katika nchi za Mashariki huiita chai nyekundu kwa sababu ya rangi yake. Chai hii hutengenezwa kwa kuacha majani yachache kabisa baada ya kunyauka, kukunjwa, na kukaushwa.
Ili kutokeza chai ya oolong inayopendwa sana, kwa kawaida majani-chai huchumwa na kuwekwa katika vikapu vikubwa vyenye kina kifupi na kuachwa yachache. Yanapochacha kwa kiwango kinachotakiwa, majani hukaushwa ndani ya vikaango vyenye joto la nyuzi 120 Selsiasi hivi. Hatua hiyo hukomesha uchachishaji. Chai hiyo yenye ladha tamu haiongezwi sukari, maziwa, au ndimu.
Chai ya kijani-kibichi huchachishwa kwa muda mfupi zaidi. Nchini Japani, India, na Sri Lanka, majani husafishwa kwa mvuke ili kuzuia yasichache sana, nao Wachina
hutumia joto kufanya hivyo. Chai ya kijani-kibichi haiongezwi sukari, maziwa, au ndimu.Jinsi Ambavyo Wachina Hunywa Chai
Tumealikwa tunywe chai na familia ya Tsai. Meza yao ni kisiki kikubwa ambacho kimepakwa vanishi hadi kikang’aa kabisa. Mbele ya Tsai Sheng Hsien, ambaye ni mkaribishaji wetu, kuna sinia lenye jiko la stima na birika. Tunashangaa kwamba birika hilo lina kimo cha sentimeta saba hivi, na kuna aina mbili za vikombe vidogo. Tunajiuliza ni kwa nini iko hivyo, na punde si punde tunapata jibu. Maji moto yanamwagwa juu ya birika na vikombe hivyo vidogo na kutiririka kupitia mashimo yaliyo kwenye sinia hiyo. Majani-chai ya kutosha kujaa sehemu ya chini ya birika yanawekwa ndani ya birika hilo, halafu maji moto sana yanamwagwa kwenye majani hayo. Kisha maji hayo yanamwagwa. Mkaribishaji wetu anatuambia kwamba kusudi la hatua hii ni kusafisha majani-chai ili yatoe ladha yake!
Sasa maji moto zaidi yanamwagwa ndani ya birika, na baada ya mkaribishaji wetu kuacha chai ikolee kwa dakika moja hivi, anajaza chai yote kwenye jagi ndogo. Akitumia jagi hiyo anajaza chai moto sana kwenye vikombe vya “harufu” ambavyo ni virefu na vyenye kipenyo cha sentimeta mbili na nusu. Anamwaga chai hiyo kwenye vikombe vya kunywea kwa kuinamisha vikombe vya harufu juu ya vikombe hivyo na kuvifunika. Kisha anatualika tuchukue vikombe vitupu vya harufu na kuvinusa! Tunamwambia kwamba vikombe hivyo vinanukia vizuri sana.
Tunashika kwa uangalifu sehemu ya juu ya vikombe moto hivyo visivyo na vishikio. Tunaonja chai hiyo, “Ni tamu sana!” Sasa tumeelewa kwamba Wachina hawapendi tu ladha ya chai bali pia harufu yake. Tunapomaliza kunywa chai hiyo, vikombe hivyo vinajazwa tena na tena. Ladha yake inapungua kidogo baada ya kikombe cha sita au cha saba, na mkaribishaji wetu anatupa majani hayo. Anatuuliza, “Je, mngependa kunywa chai ya aina nyingine?” Kwa kuwa tuko karibu kwenda kulala, tunakataa kwa heshima. Kwa kuwa chai ina kafeini, inaweza kuchangamsha mwili na huenda ikawa vigumu sana kulala baada ya kunywa vikombe kadhaa vya chai hiyo bora sana ya oolong.
Mkahawa wa Chai
Hatujawahi kutembelea mkahawa wa chai, hivyo tunaamua kutembelea mkahawa mmoja. Mikahawa fulani ina bustani maridadi ambazo wateja hufurahia wanapokunywa chai. Mikahawa mingine iko milimani, na mandhari nzuri hufanya mtu afurahie hata zaidi kunywa chai.
Tunaamua kwenda kwenye mojawapo ya milima inayozunguka Taipei na kunywa chai katika mkahawa wenye kuvutia ulio na mazingira yanayofanana sana na ya China. Orofa ya pili ina vijito vya maji vyenye samaki wengi wanaoitwa goldfish na inatubidi tukanyage mawe machache yaliyo ndani ya vijito hivyo ili tuingie ndani ya chumba kidogo ambako tutakunywa chai yetu. Tunaweza kunywa chai pamoja na keki tamu zilizopikwa kwa maharagwe (maharagwe mekundu au meupe yaliyopondwa pamoja na sukari), mbegu za tikiti-maji, tofu iliyokaushwa (maziwa ya maharagwe), keki za mchele, au matunda yaliyokaushwa au yaliyotiwa siki na chumvi. Tunaamua kula mbegu za tikiti-maji, embe lililokaushwa, na plamu zilizochachishwa kwa majani-chai. Utamu wa vyakula hivyo unapatana na ladha ya chai. Tunapotiliwa chai, tunawazia jinsi Wachina wa kale walivyokunywa chai.
Manufaa ya Kunywa Chai
Kulingana na Wachina wengi, chakula humeng’enywa haraka zaidi mtu anapokunywa chai. Inadaiwa kwamba kwa kiwango fulani jambo hilo husaidia mtu asiongeze uzito. Ikiwa ni kweli, basi chai ina manufaa kwelikweli! Hivi karibuni, watafiti wamedai pia kwamba chai ya kijani-kibichi inaweza kupunguza hatari za kupatwa na kansa. Manufaa nyingine ya kunywa chai ya oolong na ya kijani-kibichi ni kwamba aina hizo humwacha mnywaji akiwa na ladha tamu na yenye kupendeza kinywani.
Kwa hiyo, tunakuuliza tena, “Ungependa chai ya aina gani?” Kwa kuwa sasa umejifunza mengi kuhusu chai, huenda jibu lisiwe rahisi sana. Mbona usijaribu kunywa chai iliyo tofauti na kugundua jinsi ya kunywa chai kama Wachina!—Tumetumiwa makala hii.
[Picha katika ukurasa wa 21]
Chai ya oolong
[Picha katika ukurasa wa 21]
Wanawake wakichuma majani-chai
[Hisani]
Taiwan Tourism Bureau