Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Vijana na Simu za Mkononi

“Vijana Waingereza huona ni vigumu kupanga maisha yao wasipokuwa na simu zao za mkononi,” linaripoti gazeti la London, Daily Telegraph. Watafiti walichukua simu za vijana walio na umri wa kati ya miaka 15 hadi 24 kwa majuma mawili. “Hilo lilikuwa jambo geni kwa vijana hao,” ripoti hiyo ilisema. “Vijana walilazimika kufanya mambo ambayo hawajazoea: kama vile kuzungumza na wazazi wao, kuwatembelea rafiki zao nyumbani na kukutana na wazazi wa rafiki zao.” Profesa Michael Hulme wa Chuo Kikuu cha Lancaster, Uingereza, anasema kwamba vijana hutumia simu za mkononi kama “njia ya kujipa ujasiri na kusitawisha utu wao.” Gazeti hilo linaripoti kwamba kijana mmoja alijihisi kuwa “amechokozeka na kufadhaika” kwa sababu hakuwa na simu yake, naye kijana mwingine alihisi kuwa ametengwa na “alilazimika kupanga kimbele kukutana na watu nyakati hususa,” badala ya “kuzungumza na rafiki [zake] wakati wowote alipotaka.”

Je, Wajerumani Wanahifadhi Maji Kupita Kiasi?

Gazeti Frankfurter Allgemeine Sonntagszeitung linasema kwamba kuna matatizo katika mifumo ya maji safi na ya kuondoa maji machafu nchini Ujerumani kwa sababu watu hawatumii maji mengi. Zamani, ilifikiriwa kwamba watu wangetumia maji mengi, kwa hiyo mifumo hiyo ya kupitisha maji ilijengwa ili kukabiliana na hali hiyo. Wakati huohuo, watu walitiwa moyo wahifadhi maji kama hatua ya kuhifadhi mazingira na maliasili, kwa hiyo matumizi ya maji yamepungua. Tatizo sasa ni kwamba “katika sehemu nyingi, maji ya kunywa hutulia miferejini,” anasema Ulrich Oemichen, wa Shirikisho la Maji na Gesi la Ujerumani. “Maji yakitulia kwa muda ndani ya mifereji, mifereji hiyo huwa na kutu na maji hayo hufyonza metali.” Pia, kusipokuwa na maji ya kutosha katika mabomba ya kutoa uchafu, takataka ngumu hukusanyika na kuanza kuoza. Suluhisho pekee ni kutumia maji safi ya kunywa kusafisha mifereji na mabomba hayo.

Kujifungua kwa Kupasuliwa na Mizio

“Huenda watoto wanaozaliwa kupitia upasuaji wakapatwa na hatari ambazo hatukuwa tumefikiria hapo awali,” anasema Sibylle Koletzko, wa Chuo Kikuu cha Ludwig Maximilian, huko Munich, Ujerumani. “Singependekeza mbinu hiyo kwa sababu nyingi zisizo za kitiba.” Watafiti wanasema kwamba huenda ikawa kuzaliwa kwa njia hiyo kunachangia ongezeko la ugonjwa wa pumu na mizio. Uchunguzi uliofanyiwa vitoto 865 vilivyopewa maziwa ya mama peke yake katika miezi minne ya kwanza ulionyesha kwamba vitoto vilivyozaliwa kupitia upasuaji vilikuwa na matatizo mengi zaidi ya kumeng’enya chakula na uwezekano mkubwa wa kupata mizio inayosababishwa na chakula. Kulingana na gazeti New Scientist, “huenda ikawa hivyo kwa sababu vitoto vinavyozaliwa kupitia upasuaji havipati nafasi ya kumeza bakteria nzuri vinapozaliwa; kuwa na bakteria nyingi kwenye matumbo husaidia sana katika ukuzi wa mfumo wa kinga.”

“Pambo Bora Zaidi la Nyumbani”

Gazeti, The Sunday Telegraph la London linasema: “Watalii na wafanyabiashara kutoka nchi za Magharibi ambao hununua kiharamu ngozi za simbamarara wamechangia kuuawa kwa wanyama hao wanaokabili hatari kubwa zaidi ulimwenguni ya kutoweka.” Idadi ya simbamarara walio mwituni imepungua kutoka 100,000 hivi karne moja iliyopita kufikia chini ya 5,000 leo. Wengi wa wanyama hao hupatikana nchini India, nao wengine katika nchi za Asia Kusini na pia Mashariki ya Mbali. Shirika la kutoa misaada la London, linaloitwa Taasisi ya Uchunguzi wa Mazingira linaripoti kwamba wanunuzi huona ngozi za mnyama huyo “kuwa pambo bora zaidi la nyumbani, lakini wanahatarisha sana simbamarara. . . . Wanyama hao wanakabili hatari kubwa sana ya kutoweka hivi kwamba kila mnyama aliyepo anahitajiwa ili jamii hiyo iendelee kuwa hai.” Kati ya mwaka wa 1994 na 2003, ngozi 684 za simbamarara zilikamatwa, lakini inadhaniwa kwamba idadi hiyo ni sehemu ndogo sana ya ngozi zinazouzwa kwa magendo.

Vitambulisho Vilivyopandikizwa Mwilini

Jarida Journal of the American Medical Association (JAMA) linaripoti kwamba “Shirika la Usimamizi wa Chakula na Dawa la Marekani limeidhinisha kutumiwa kwa kidude cha elektroni kinachoweza kupandikizwa mwilini” ili kupata habari kuhusu afya ya mgonjwa. Watengenezaji wanapendekeza kwamba kidude hicho kilicho na ukubwa wa punje ya mchele kiingizwe kwenye ngozi ya mgonjwa katika sehemu ya nyuma ya mkono. Kifaa cha kielektroniki cha kusoma maandishi kinapopitishwa mahali penye kidude hicho, wataalamu wanaweza kusoma nambari ya kidude hicho. Kisha nambari hiyo hutumiwa kupata habari zilizohifadhiwa kwenye kompyuta. Jarida JAMA linasema kwamba teknolojia hiyo mpya “inaweza kusaidia kupata haraka habari muhimu za kitiba za wagonjwa waliopoteza fahamu au wasioweza kuzungumza,” na “inaweza kutumiwa kwa ajili ya usalama, shughuli za kifedha, na kama kitambulisho.”

Wakanada Wengi Zaidi Wanaishi Pamoja Bila Kufunga Ndoa

Gazeti, Vancouver Sun linasema kwamba “Wakanada wengi zaidi wanaishi pamoja ili waone kama watafunga ndoa.” Alan Mirabelli, mkurugenzi mkuu wa Taasisi ya Vanier ya Masuala ya Familia huko Ottawa anasema: “Kizazi hiki cha Wakanada walio na umri unaopungua miaka 35 kimeshuhudia idadi kubwa zaidi ya talaka na kutengana kati ya wazazi wao kuliko kizazi kingine. Kwa hiyo wanaogopa kufunga ndoa.” Uchunguzi wa kitaifa uliofanyiwa Wakanada wapatao 2,100 wenye umri wa kati ya miaka 18 hadi 34 ulionyesha kwamba “asilimia 22 . . . wanaishi pamoja bila kufunga ndoa, huku asilimia 27 wamefunga ndoa,” inasema ripoti hiyo. “Uchunguzi wa awali wa Taasisi ya Vanier ulionyesha kwamba katika mwaka wa 1975, asilimia 61 walikuwa wamefunga ndoa, huku asilimia moja tu walikuwa wakiishi pamoja bila kufunga ndoa.”

Mwaka Uliokuwa na Hali Mbaya Sana ya Hewa

Ripoti moja ya Shirika la Habari la Associated Press inasema hivi: “Mwaka wa 2004, ambao ulikuwa na vimbunga vinne vyenye nguvu katika eneo la Karibea na dhoruba kali huko Asia, ndio uliokuwa mwaka wa nne wenye joto zaidi katika historia. Hali hiyo imeendeleza matukio ya tangu mwaka wa 1990 kwani katika kipindi hicho kumekuwa na miaka kumi inayosemekana kuwa yenye joto zaidi.” Pia hasara kubwa zaidi ya kifedha ambayo imewahi kutokezwa na hali ya hewa ilitokea mwaka uliopita. Nchini Marekani na katika Karibea pekee, inakadiriwa kwamba vimbunga vilitokeza hasara ya zaidi ya dola bilioni 43. Dhoruba na joto kali katika maeneo fulani zilitokea huku wakati uleule kukiwa na majira ya baridi kali kwingineko. Kwa mfano, Argentina Kusini, Chile, na Peru, zilikumbwa na baridi kali na theluji katika mwezi wa Juni na Julai. Kulingana na ripoti hiyo, “wanasayansi wanasema kuna uwezekano kwamba kuongezeka kwa muda mrefu kwa halijoto kutaendelea kuathiri hali ya hewa ulimwenguni pote.”