Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Mtilili—Wanasarakasi wa Angani Wenye Rangi Nyingi

Mtilili—Wanasarakasi wa Angani Wenye Rangi Nyingi

Mtilili—Wanasarakasi wa Angani Wenye Rangi Nyingi

Na mwandishi wa Amkeni! nchini Hispania

WAZIA kikundi cha ndege ambao wana manyoya yenye karibu rangi zote za upinde wa mvua. Wanaweza kuruka vizuri zaidi kuliko baadhi ya wadudu wanaoruka kwa kasi zaidi. Na baadhi yao ni kati ya jamii chache za ndege ambao huishi katika vikundi vya familia ambazo husaidiana kulea makinda. Tabia hizo tatu ni baadhi tu ya tabia nyingi zenye kuvutia za mtilili.

Hata hivyo, watu wanaopenda kutazama ndege huvutiwa mara moja na rangi yao yenye kupendeza. Ndege wengi wanaokula wadudu wana manyoya ya rangi hafifu zisizovutia. Lakini mtilili wana rangi ambazo ndege wengine hawana, nao huruka kwa njia ya ajabu ambayo huwastaajabisha watu wanaopenda kutazama ndege. Wana manyoya ya rangi nyangavu ya kijani-kibichi, buluu, nyekundu, na manjano. Jamii nyingine za mtilili, kama vile polohoyo, wana rangi hizo zote na nyingine nyingi! Na hivyo kwa kufaa, mtilili fulani anayepatikana huko Australia huitwa mtilili mwenye rangi za upinde wa mvua.

Mtilili wanaishi katika sehemu nyingi za Afrika, Asia, Australia, na Ulaya kusini. Kwa kuwa si rahisi kufuga ndege hao, mtu anaweza tu kuwaona porini. Kichapo Wildwatch kilicho katika Intaneti kinasema hivi: “Inavutia sana kutazama ndege hao wajasiri na wenye nguvu. Kwa kuwa wengi wao ni watulivu hata wanapomwona mwanadamu, ni rahisi kuwapiga picha.”

Uwezo wa Kuruka Usio na Kifani

Mtilili wana uwezo wa kukamata wadudu wanaporuka. Na kwa kuwa wanapenda kula wadudu wakubwa wanaoruka kwa kasi, kama vile nyuki, nyigu, na mavu, lazima mtilili waruke kwa kasi na wawe wenye kunyumbulika. Pia wanahitaji kuwa na uwezo mzuri wa kuona. Polohoyo anaweza kumwona nyuki au nyigu akiwa umbali wa meta mia moja. *

Ili kuwakamata wadudu, mtilili fulani huwarukia kutoka juu. Au mara nyingi, wao hutua kwenye tawi linaloonekana wazi na kurukia mdudu anayepita. Aina nyingine za mtilili hutumia mbinu nyingine ngumu zaidi. Kwanza wanaruka chini sana nyuma ya mdudu huyo mahali ambapo mdudu huyo hawaoni. Kisha wanaongeza mwendo, wanainua kichwa chao, na kumkamata mdudu kutoka hewani kwa kutumia midomo yao mirefu.

Aina fulani za mtilili wanaopatikana Afrika husaidiwa na wengine kupata chakula. Huenda wakafuatana na wanyama wakubwa, ndege wengine, au hata magari ambayo hufichua wadudu wanaoweza kukamata. Mtilili mwenye ujasiri anayeitwa kondekonde anaweza hata kupanda mgongoni mwa mbuni, mbuzi, au hata punda-milia anapokimbia. Wanyama hao humpa mtilili mahali pazuri pa kutua na pia hufichua nzige au panzi ambao mtilili hula. Mioto ya msituni pia huvutia kondekonde wengi sana ambao hula panzi wanaojaribu kutoroka mioto hiyo. *

Kuota Jua, Kuchana Manyoya, na Kujisafisha

Ili ndege aweze kuruka kwa kasi, lazima manyoya yake yawe katika hali nzuri kabisa, na mtilili ana mbinu nyingi za kuondoa wadudu na kujisafisha. Hiyo ni kazi muhimu. Mtilili anaweza kutumia saa mbili hivi kila siku akifanya hivyo.

Mtilili huota jua asubuhi na wakati huo yeye huchana manyoya yake kwa mdomo. Inaonekana kuwa joto la jua hufanya wadudu walio kwenye manyoya wajitokeze na hivyo kufanya iwe rahisi kuwaondoa. Jamii fulani za mtilili hupenda kuota jua pamoja ambapo mtilili kadhaa husimama kwa njia ileile. Wanapoelekeza migongo yao kwenye jua na kupanua mabawa yao, wao huonekana kama watalii wanaoota jua ufuoni.

Wao huoga mara chache sana kwa kujitumbukiza haraka kwenye maji wanaporuka. Katika maeneo makame, mtilili huoga kwenye vumbi. Baadaye, ndege hao hutumia wakati wao wakichana manyoya yao kwa mdomo na kujikuna. Kazi hiyo ya kila siku ndiyo njia pekee ya kuwaondoa wadudu ambao husumbua sana wanyama wanaoishi ndani ya mashimo kama mtilili.

Kushirikiana na Wengine

Jamii nyingi za mtilili hupenda kushirikiana. Jamii kadhaa hutaga mayai wakiwa katika vikundi vikubwa, na huenda hata vikundi fulani vikawa na ndege wapatao 25,000. Mara nyingi wao hufanya hivyo katika maeneo yenye mchanga kando ya mto ambapo ndege hao wanaweza kuchimba mashimo kwa urahisi. Kutaga mayai wakiwa katika vikundi vikubwa huwapa ulinzi mwingi zaidi kutoka kwa wavamizi, na kushirikiana kwao kwa ukaribu huwasaidia wapate sehemu yenye chakula kingi haraka. Hata wanapotafuta chakula, mtilili hao wenye ushirikiano huwasiliana kwa vilio vyao vya juu.

Katika jamii fulani za mtilili kama vile jamii ya kinepa-mkubwa, washiriki wa familia hushirikiana kuwalea makinda. * Kwa kawaida, wasaidizi huwa makinda ya ndege wazazi, na ushirikiano wao hufanya idadi kubwa ya vifaranga kukua vizuri. Kitabu Kingfishers, Bee-Eaters and Rollers kinaeleza hivi: “Wasaidizi hufanya kazi zote ambazo mzazi angefanya: wao husaidia kuchimba kiota, kulalia mayai na, jambo muhimu zaidi, kulisha makinda.”

Familia za mtilili hupenda sana kutua mahali pamoja katika vikundi. Kila ndege hutua karibu sana na mwenzake hivi kwamba mtu anaweza kufikiri wameamua kukaribiana ili wapigwe picha. Nyakati nyingine ndege kadhaa watakaribiana kwenye tawi moja. Bila shaka zoea hilo huwasaidia kudumisha joto mwilini kunapokuwa na baridi usiku.

Ndege Maridadi Wenye Udhaifu Mmoja

Hivi karibuni, mtilili wameanza kula nzige sana, hasa huko Afrika Magharibi, ambako kuna nzige wengi waharibifu na wanaohama-hama. Hata mtilili anayeitwa kondekonde amebadili wakati wake wa kutaga mayai na kuhama ili afaidike na chakula hicho kingi. Sasa yeye hufuata nzige wanaohama-hama wanaporuka kando ya Mto Niger.

Hata hivyo, mtilili ana udhaifu mmoja. Yeye hupenda sana kula nyuki. Hivyo, bila shaka wafugaji nyuki hawawapendi. Kwa upande mwingine, wao hunufaisha kwa kula nyigu na mavu ambao hula nyuki, na wakati wa majira ya kupukutika kwa majani, wao hula nyuki wazee ambao huenda wakaleta ugonjwa kwenye mzinga. Kitabu Handbook of the Birds of the World kinasema:

“Leo watazamaji wengi wa ndege huvutiwa na mtilili kwa sababu ya manyoya yake mbalimbali yenye rangi maridadi.” Maeneo fulani ambayo ndege hao hutagia mayai yamekuwa sehemu za pekee zinazotembelewa na watalii wanaokuja Afrika.

Kwa hiyo, ikiwa unaishi katika maeneo ambayo hutembelewa mara nyingi na mtilili, mbona usitenge wakati wa kutazama mandhari ya pekee inayotokezwa na wanasarakasi hao wa angani wenye rangi nyingi?

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 7 Wanapokamata wadudu wenye miiba kama vile nyuki au nyigu, mtilili huhakikisha kwamba wameondoa sumu yao kabla ya kuwameza. Kwa kawaida, wao hutua kwenye tawi na kusugua tumbo la mdudu kwenye tawi hilo ili kuondoa sumu. Wao hata hufunga macho ili yasiingiwe hata na tone moja la sumu.

^ fu. 9 Kwa sababu ya zoea hilo, jina la kienyeji la kondekonde huko Afrika Magharibi humaanisha “binamu ya moto.”

^ fu. 16 Kikundi kimoja cha kinepa-mkubwa wapatao 400 nchini Kenya walikuwa na ukoo wenye familia 60. Watafiti wanaeleza maisha ya kijamii ya ndege hao kuwa yenye kutatanisha zaidi hata ingawa jamii hiyo ya ndege ndiyo ambayo imechunguzwa zaidi kuliko jamii nyingine yoyote ya ndege.

[Picha katika ukurasa wa 23]

Kinepa-mdogo, Afrika Mashariki

[Picha katika ukurasa wa 23]

Mtilili mwenye rangi za upinde wa mvua, Australia

[Picha katika ukurasa wa 23]

Mtilili anayeitwa Somali, Kenya

[Picha katika ukurasa wa 23]

Kinepa-mkubwa, Afrika

[Picha katika ukurasa wa 24]

Polohoyo, Hispania

Mtilili wakichumbiana, wa kiume akimpa wa kike “crane fly”

[Picha katika ukurasa wa 24]

Mtilili, Israeli

[Picha katika ukurasa wa 24]

Kondekonde, Botswana

[Picha katika ukurasa wa 25]

Kondekonde, Botswana

[Hisani]

©kevinschafer.com

[Picha katika ukurasa wa 25]

Kondekonde, Singapore