Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Pengo Kati ya Matajiri na Maskini

Pengo Kati ya Matajiri na Maskini

Pengo Kati ya Matajiri na Maskini

BILA kujali neno linalotumiwa kufafanua mataifa mbalimbali, mataifa yaliyoendelea sana na kusitawi kiviwanda na kiuchumi yana kiwango cha juu cha maisha, ilhali mataifa yaliyo na viwanda vichache, ambayo hayajasitawi sana kiuchumi, yana kiwango cha chini cha maisha. Ni kana kwamba mataifa hayo yako katika dunia mbili tofauti.

Bila shaka, hata katika taifa moja, viwango vya maisha vinaweza kutofautiana sana. Fikiria nchi tajiri ambazo zilitajwa katika makala iliyotangulia. Zina matajiri na maskini. Kwa mfano, nchini Marekani, asilimia 30 hivi ya mapato yote ya nchi hiyo hutumiwa na matajiri ambao ni asilimia 10. Wakati huohuo, familia maskini ambazo ni asilimia 20 lazima zijitosheleze kwa asilimia 5 tu ya jumla ya mapato hayo. Huenda ikawa kuna hali kama hiyo katika nchi unamoishi, hasa ikiwa watu wenye mapato ya kadiri ni wachache. Lakini hata serikali za nchi zilizo na watu wengi wenye mapato ya kadiri bado hazijafanikiwa kuziba kabisa pengo la kiuchumi kati ya matajiri na maskini.

Hakuna Jamii Isiyo na Matatizo

Hakuna jamii inayoweza kudai kwamba haina matatizo yoyote. Fikiria magumu yanayowakabili watu wanaoishi katika nchi maskini zaidi. Hawana huduma za afya za kutosha. Katika nchi 9 tajiri zaidi zilizotajwa katika sanduku kwenye ukurasa huu, kuna daktari 1 kwa watu 242 hadi 539, ilhali nchi 18 maskini zaidi zina madaktari wachache sana. Kuna daktari 1 kwa raia 3,707 hadi 49,118. Hivyo, inaeleweka ni kwa sababu gani watu katika nchi tajiri huishi kwa miaka 73 au zaidi, hali wale walio katika nchi maskini zaidi huishi kwa miaka inayopungua 50.

Pia katika nchi maskini, kuna uwezekano mdogo sana wa watu kupata elimu, na kwa sababu hiyo mara nyingi watoto watakuwa maskini vilevile. Ukosefu huo wa elimu unaonyeshwa na idadi ya watu wanaojua kusoma na kuandika. Asilimia 100 ya watu katika nchi 7 kati ya nchi 9 tajiri zaidi wanajua kusoma na kuandika (zile nyingine 2 zina asilimia 96 na 97). Katika nchi 18 maskini zaidi, watu wanaojua kusoma na kuandika ni kati ya asilimia 81 na asilimia 16, huku 10 kati ya nchi hizo zikiwa na chini ya asilimia 50.

Lakini wakazi wa mataifa tajiri pia hukabiliana na magumu fulani. Ingawa huenda watu wanaoishi katika nchi maskini wakakosa chakula cha kutosha, wale wanaoishi katika nchi zenye chakula tele, wanakufa kwa sababu ya matatizo yanayosababishwa na kula kupita kiasi. Kitabu Food Fight kinadai kwamba “kula na kunywa kupita kiasi kumekuwa tatizo kubwa zaidi ulimwenguni kuliko ukosefu wa chakula.” Nalo gazeti The Atlantic Monthly linasema: “Sasa Wamarekani milioni tisa hivi ni ‘wanene kupita kiasi,’ hilo linamaanisha kwamba uzito wao unapita kiasi kwa kilogramu 45 au zaidi, na kila mwaka, matatizo yanayotokana na unene unaopita kiasi husababisha vifo vya mapema vya watu 300,000 katika nchi hii.” Makala hiyohiyo inadokeza kwamba “huenda hivi karibuni unene unaopita kiasi ukawa tatizo kubwa zaidi la afya ulimwenguni kuliko njaa na magonjwa ya kuambukiza.” *

Ni kweli kwamba raia wa nchi tajiri wana kiwango cha juu cha maisha, lakini wakati huohuo, huenda wakaona mali kuwa muhimu zaidi kuliko kuwa na mahusiano mazuri na wengine, na hivyo kuona kwamba kuwa na mali ni muhimu kuliko kufurahia maisha. Wana mwelekeo wa kumwona mtu kuwa muhimu kwa kutegemea kazi, mshahara, au mali zake, badala ya ujuzi, hekima, uwezo, au sifa zake nzuri.

Ikikazia kwamba maisha rahisi ndiyo huleta furaha, kichwa cha makala moja katika gazeti la kila juma la Ujerumani Focus kiliuliza hivi: “Vipi Kuwa na Mali Chache Zaidi?” Makala hiyo ilisema: “Raia wengi wa nchi za Magharibi hawana furaha zaidi leo kuliko waliyokuwa nayo miaka mingi iliyopita, licha ya kwamba sasa wana mali nyingi zaidi. . . . Yaelekea mtu yeyote anayetamani kupata mali hatakuwa mwenye furaha.”

Kuwa na Usawaziko Kamili

Naam, ukweli ni kwamba, ingawa watu wanaoishi katika nchi tajiri na maskini hukabili hali fulani zinazofaa, wao pia hukabili hali zisizofaa. Ingawa huenda maskini wakaishi maisha yasiyo na anasa, matajiri wanaweza kuishi maisha yenye kutatanisha sana. Ingefaa sana iwapo maskini na matajiri wangejifunza kutoka kwa mmoja na mwenzake. Lakini je, ni jambo linalopatana na akili kufikiri kwamba siku moja kutakuwa na usawaziko kamili kati ya maskini na matajiri?

Kwa maoni ya kibinadamu, huenda ukahisi kwamba ingawa huo ni mradi mzuri, wanadamu hawawezi kuutimiza hata kidogo. Nayo mambo yaliyotukia zamani yanathibitisha ukweli wa jambo hilo. Hata hivyo, hali hiyo inaweza kurekebishwa. Huenda ikawa hujatilia maanani suluhisho bora zaidi la tatizo hilo. Suluhisho hilo ni lipi?

[Maelezo ya Chini]

[Blabu katika ukurasa wa 6]

“Huenda hivi karibuni unene unaopita kiasi ukawa tatizo kubwa zaidi la afya ulimwenguni kuliko njaa na magonjwa ya kuambukiza.”—The Atlantic Monthly

[Grafu katika ukurasa wa 5]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Majina ya nchi Muda Ambao Wanaume Wanaojua

yamepangwa Wanatarajiwa Kusoma na

katika alfabeti Kuishi (Miaka) Kuandika (%)

Nchi Tisa Denmark 74.9 100

Tajiri Iceland 78.4 100

Zaidi Japani 78.4 100

Kanada 76.4 96.6

Luxembourg 74.9 100

Marekani 74.4 95.5

Norway 76.5 100

Ubelgiji 75.1 100

Uswisi 77.7 100

Nchi 18 Benin 50.4 37.5

Maskini Burkina Faso 43 23

Zaidi Burundi 42.5 48.1

Chad 47 53.6

Ethiopia 47.3 38.7

Guinea-bissau 45.1 36.8

Jam. ya Kongo 49 80.7

Madagaska 53.8 80.2

Malawi 37.6 60.3

Mali 44.7 40.3

Msumbiji 38.9 43.8

Niger 42.3 15.7

Nigeria 50.9 64.1

Rwanda 45.3 67

Sierra Leone 40.3 36.3

Tanzania 43.3 75.2

Yemen 59.2 46.4

Zambia 35.3 78

[Hisani]

Source: 2005 Britannica Book of the Year.

[Picha katika ukurasa wa 4]

© Mark Henley/Panos Pictures