Jinsi Biashara ya Almasi ya Kisasa Ilivyoanza
Jinsi Biashara ya Almasi ya Kisasa Ilivyoanza
NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI AFRIKA KUSINI
ILITUKIA mnamo Januari 1871. Adrian van Wyk, mkulima aliyependa kusoma Biblia, aliishi pamoja na familia yake katika eneo fulani kavu la Afrika Kusini linaloitwa Griqualand West. Lakini utulivu aliofurahia ulivurugwa wakati watu wengi walipoingia katika shamba lake na kuanza kupiga kambi hapo. Alipowatazama akiwa ameketi kwenye veranda yake, Van Wyk hangeweza kuamini alichokuwa akiona!
Katika muda wa siku chache, shamba lake lilikuwa limejaa maelfu ya wanaume. Hata baadhi yao walikuwa mbele ya nyumba yake wakichora mipaka bila ruhusa yake na hata bila kumsalimu! Ni nini kilichokuwa kimetukia? Msisimuko wote huo ulikuwa wa nini? Harakati mpya ya kutafuta almasi ilikuwa imeanza habari zilipoenea kwamba kulikuwa na almasi nyingi kwenye shamba la Van Wyk.
Ni Nini Kilichochea Harakati ya Kutafuta Almasi?
Miaka 12 mapema, almasi yenye uzito wa karati tano ilikuwa imepatikana karibu na Mto Vaal, kilometa 70 hivi kaskazini ya shamba la Van Wyk. Mtu aliyepata almasi hiyo alimuuzia kasisi aliyesimamia sosaiti ya Berlin Mission Society kwa dola tisa. Hakuna rekodi nyingine ambayo imepatikana kuhusu ugunduzi wa almasi hiyo ya kwanza. Lakini habari kuihusu zilipoenea, watu walianza kufanya uchunguzi.
Simulizi letu linaendelea miaka tisa baadaye katika shamba la Schalk van Niekerk lililokuwa kando ya Mto Orange, kilometa chache kusini mwa mahali ulipoungana na Mto Vaal. Familia ya Jacobs ilikuwa na nyumba kwenye shamba la Van Niekerk. Watoto wa familia hiyo walifurahia kucheza mchezo waliouita mawe matano. Kati ya mawe hayo kulikuwa na moja lililong’aa ambalo kaka yao Erasmus alikuwa amepata.
Siku moja, mapema mwaka wa 1867, Van Niekerk alitembelea familia ya Jacobs. Bi. Jacobs alijua kwamba alipendezwa na mawe yenye thamani kwa hiyo alimwambia kuhusu jiwe linalong’aa ambalo watoto wake walichezea. Alisema: “Usiku, jiwe hilo humetameta kwenye mwangaza wa mshumaa.” Baada ya kulichunguza, Van Niekerk alipata wazo lenye kusisimua. Alisema hivi kwa msisimko: “Nadhani hii ni almasi!” Alikumbuka kwamba alikuwa amesoma kuhusu jinsi unavyoweza kujua kama jiwe ni almasi. Kwa hiyo, alikwaruza jiwe hilo juu ya dirisha lililokuwa upande wa nyuma wa nyumba hiyo ndogo. Alishangaa kuona jinsi kioo hicho kilivyokatwa na akaomba radhi kwa kukiharibu. * Bi. Jacobs alimpa Van Niekerk jiwe hilo, na akakataa malipo yoyote.
Alipoenda tena kwenye jiji la Hopetown lililokuwa karibu, Van Niekerk aliwaonyesha rafiki zake jiwe hilo, lakini hakuna yeyote aliyeweza kuthibitisha kwamba lilikuwa almasi. Jiwe hilo lilipitishwa kutoka kwa mtu mmoja mwenye kutumainika hadi kwa mwingine kisha likatumwa kwa posta na kumfikia Dakt. Atherstone aliyeishi Grahamstown. Aliomba mwalimu mkuu wa shule fulani amsaidie. Kwenye maabara ya shule hiyo, majaribio yalifanywa ili kuchunguza uzito halisi wa jiwe hilo, na alipata kwamba ulikuwa sawa na ule wa almasi. Baadaye, jiwe hilo lilipelekwa kwa muuza-vito ambaye alijaribu bila mafanikio kutia alama jiwe hilo akitumia tupa yake. Watu wengine waliulizwa maoni, na wote wakakubaliana na Van Niekerk kwamba jiwe hilo lilikuwa almasi. Kisha Dakt. Atherstone akathibitisha kupitia barua kwamba jiwe hilo lilikuwa almasi yenye uzito wa karati 21.25. Van Niekerk alilipwa dola 635 kwa ajili ya jiwe hilo, na akamgawia Bi. Jacobs pesa hizo mara moja. Kwa kufaa, jiwe hilo linaitwa Eureka, neno linalomaanisha “shangwe ya kupata kitu.”
Mchungaji na Mkulima Mnyoofu
Simulizi letu linaendelea baada ya miaka miwili kwenye eneo lililokuwa chini ya makutano ya Mito Orange na Vaal. Mchungaji mmoja Mwafrika aliyeitwa Booi alikuwa akichunga kondoo alipoona kitu fulani kikimetameta ardhini.
Aliinama na kuokota jiwe fulani lenye umbo la jozi kisha akalitia mfukoni. Alikuwa amesikia kwamba watu walikuwa wamependezwa na mawe fulani katika eneo hilo, kwa hiyo alipokuwa akitembea akitafuta kazi, kwanza alimwonyesha mkulima jiwe hilo, kisha akamwonyesha mfanyabiashara. Nao wakamwelekeza kwa shamba la Van Niekerk.Hatimaye, Booi alifika kwenye shamba la Van Niekerk na kumwonyesha jiwe hilo. Mara moja, Van Niekerk alitambua kwamba jiwe hilo lilikuwa almasi kubwa na yenye thamani zaidi kuliko ile ambayo Bi. Jacobs alikuwa amempa. Alimuuliza mchungaji huyo angependa kulipwa nini. Booi akajibu hivi kwa heshima: “Bwanangu, unaweza kunipa chochote utakachoona kuwa kinafaa.” Bila kusita, Van Niekerk alimpa karibu kila kitu alichokuwa nacho—kondoo 500 wenye mikia minono, fahali 10, gari la kukokotwa alilotumia kupeleka mboga mjini, na hata farasi wake! Bila shaka, Booi alijiona kuwa tajiri kwa sababu tu ya jiwe linalong’aa lenye umbo la jozi!
Mara moja, Van Niekerk alienda Hopetown kuuza almasi yake. Huko, kikundi cha wafanyabiashara waliopigwa na butwaa walikubali kumlipa dola 20,500 kwa jiwe hilo lenye uzito wa karati 83.5. Hatimaye, liliitwa Nyota ya Afrika Kusini. * Jiwe hilo lililokatwa na kung’arishwa limekuwa sehemu muhimu ya mkufu maridadi ulio katika ukurasa huu. Watu katika nchi nyingine waliposikia habari za almasi hiyo, walianza kuamini kwamba kuna almasi kubwa nchini Afrika Kusini, na maelfu kutoka mbali kama vile Amerika Kaskazini na Kusini, Uingereza, Ulaya, na Australia walimiminika huko wakatafute utajiri.
Harakati Yaanza
Mwanzoni, almasi ilichimbwa kando ya Mito Orange na Vaal. Kisha, mnamo 1870, habari zikaenea kwamba almasi kubwa zilikuwa zikipatikana kwenye mashamba yaliyokuwa kati ya mito hiyo miwili. Kwa hiyo, watu waliokuwa wakichimba almasi kando ya mito
walianza kuelekea mahali ambapo kulikuwa na shamba la Adrian van Wyk. Van Wyk na majirani wake hawakujua kwamba mashamba yao yalikuwa mahali penye volkano isiyotenda. Almasi hizo zilipatikana katika eneo lililoitwa ardhi ya buluu ambapo volkano za zamani zililipukia.Wakati huohuo, vijiji vya mahema vilivyojengwa haraka-haraka vilianza kutokea, na baada ya muda vikaanza kujengwa kwa mabati. Vijiji hivyo vilikuwa duni kwani hakukuwa na maji ya kutosha na huduma za lazima. Watu waliohamia eneo hilo walikabiliana na vumbi nyingi, nzi wengi, majira ya joto kali lililofikia nyuzi 40 Selsiasi na majira ya baridi kali sana. Walivumilia hali zote hizo zisizofaa wakitumaini kwamba watakuwa matajiri.
Ni nini kilichompata Adrian van Wyk baada ya shamba lake kuvamiwa na watu waliokuwa wakichimba almasi? Mwanzoni, aliwaruhusu watu hao wachimbe sehemu fulani tu ya shamba lake kwa gharama ndogo ya kila mwezi. Lakini wachimbaji walipozidi kuvamia shamba lake, hali ilikuwa mbaya sana hivi kwamba Van Wyk hangeweza kuidhibiti. Kampuni moja ya kuchimba madini ilipomwambia ingempa dola 3,630 kwa ajili ya shamba lake, alikubali haraka, akatia sahihi hati zilizohitajika, na kuhamia shamba jingine lenye utulivu.
Karibu na shamba la Van Wyk kulikuwa na shamba jingine la ndugu wawili ambao jina la familia yao lilikuwa De Beer. Jina lao lilitumiwa kuandikisha kampuni ya De Beers Consolidated Mines, ambayo bado ndiyo kampuni kubwa zaidi ya almasi ulimwenguni. Jiji la Kimberley limejengwa mahali mashamba hayo yalipokuwa. Kazi nyingi sana ilifanywa kwenye shamba la akina De Beer hivi kwamba wanaume walichimba shimo pana sana na lenye kina kirefu ambalo liliitwa Big Hole (Shimo Kubwa).
Kabla ya almasi za mapema kugunduliwa nchini Afrika Kusini, mawe hayo ya thamani yalikuwa yakichimbwa nchini India na Brazili. Lakini hayakuwa mengi kutosheleza uhitaji uliokuwapo ulimwenguni. Biashara ya almasi ilianza wakati kiasi kikubwa cha almasi kilipogunduliwa Afrika Kusini.
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 8 Zaidi ya karne moja baadaye, unaweza kuona kioo cha dirisha hilo kilicho na alama ya mkato uliotokezwa na almasi hiyo kwenye Jumba la Makumbusho la Colesberg, Afrika Kusini.
^ fu. 13 Nyakati nyingine, watu hukosea jina la almasi hii na kuiita jina la almasi nyingine inayoitwa Nyota ya Afrika.—Ona sanduku “Mgodi Bora,” kwenye ukurasa wa 16.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 16, 17]
MGODI BORA
Mnamo 1903, mgodi wa almasi ulianza kuchimbwa karibu kilometa 30 mashariki ya Pretoria, Afrika Kusini. Uliitwa kwa kufaa Mgodi Bora. Miaka miwili baadaye, mgodi huo ulipokuwa na kina cha meta 10, mfanyakazi mmoja aliona kitu kinachometameta kwenye ukuta wa mwamba. Meneja wake aliteremka chini kwa uangalifu na kukata kitu hicho kwa kisu chake. Mkononi mwake alishika almasi kubwa zaidi iliyowahi kuchimbwa kwani ilitoshana na ngumi ya mwanamume. Almasi hiyo kubwa yenye uzito wa karati 3,106 ilipewa jina la aliyegundua mgodi huo, Thomas Cullinan. Ilipokatwa, almasi hiyo ilitokeza vito tisa vikubwa na vingine 96 vidogo. Mojawapo ya vito hivyo, ambacho kinaitwa Cullinan ya Kwanza, au Nyota ya Afrika, ndiyo almasi kubwa zaidi duniani iliyokatwa. Almasi hiyo hupamba fimbo ya enzi ya Uingereza, kama inavyoonekana katika picha hapa. Baada ya karne moja, Mgodi Bora bado unaendelea kutokeza almasi kubwa na bora.
[Picha]
Fimbo ya enzi ya Uingereza
Almasi ya Cullinan kabla ya kukatwa, inayotoshana na ngumi ya mwanamume
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 17]
HABARI KUHUSU ALMASI
◆ Almasi ndicho kitu kigumu zaidi cha asili kinachojulikana na wanadamu.
◆ Kama vile risasi ya penseli au grafati, almasi hutokana na kaboni. Hata hivyo, kwa nini almasi ni ngumu hali grafati ni nyororo? Hizo hutofautiana kwa sababu ya jinsi ambavyo atomu za kaboni zimepangwa.
◆ Almasi hupimwa kwa karati. Karati ina uzito sawa na sehemu moja ya tano ya gramu.
◆ Mara nyingi, ni lazima kuchuja tani 400 hivi za mawe, changarawe, na mchanga ili kupata karati moja ya almasi.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 18]
BIG HOLE (SHIMO KUBWA) HUKO KIMBERLEY
Katika kipindi cha miaka minne kuanzia 1869 hadi 1873, idadi ya watu katika jiji la sasa la Kimberley ilikua kutoka wakulima wachache kufikia watu 50,000 hivi. Wengi wao walitoka sehemu zote za ulimwengu ili kuchimba almasi. Maelfu walitembea kilometa 1,000 kutoka bandari ya Cape Town. Wakitumia sururu na sepetu, walichimba mlima na kuugeuza kuwa shimo kubwa zaidi lililowahi kuchimbwa na wanadamu. Hatimaye, baada ya kumaliza kuchimba, shimo hilo lilikuwa na kina cha meta 240. Shimo hilo liliendelea kuchimbwa chini kwa chini hadi kina cha meta 1,097. Kulingana na kichapo Standard Encyclopaedia of Southern Africa, kufikia mwaka wa 1914, wakati uchimbaji madini ulipokoma, “tani milioni 25 za mchanga” zilikuwa zimechimbuliwa. Kichapo hichohicho kinasema kwamba tani tatu za almasi zenye thamani ya zaidi ya dola 85,000,000 zilipatikana katika mawe na mchanga huo.
[Picha katika ukurasa wa 17]
Dakt. Atherstone
[Picha katika ukurasa wa 17]
Schalk van Niekerk
[Picha katika ukurasa wa 17]
Almasi ya Eureka
[Hisani]
De Beers Consolidated Mines Ltd.
[Picha katika ukurasa wa 18]
Nyota ya Afrika Kusini
[Picha katika ukurasa wa 18, 19]
Big Hole (Shimo Kubwa) mwaka wa 1875. Kamba hizi zilitumiwa na mamia ya watu waliodai kumiliki migodi mbalimbali kuteremsha wafanyakazi kwenye shimo na kuinua mawe yaliyokuwa na almasi
[Picha katika ukurasa wa 19]
Harakati ya kutafuta almasi ilitokeza kambi zilizojengwa haraka-haraka
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 16]
Crown ©/The Royal Collection © 2005, Her Majesty Queen Elizabeth II; Photo: www.comstock.com
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 16]
Photo by Fox Photos/Getty Images
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 17]
Portraits: From the book The Grand Old Days of the Diamond Fields by George Beet
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 18]
Photos: De Beers Consolidated Mines Ltd.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 19]
Photos: De Beers Consolidated Mines Ltd.