Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Jinsi ya Kupambana na Msongamano wa Magari

Jinsi ya Kupambana na Msongamano wa Magari

Jinsi ya Kupambana na Msongamano wa Magari

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI FILIPINO

ONYO: Majiji mengi yamekumbwa na tatizo kubwa. Ijapokuwa linaathiri afya ya mamilioni ya watu, tatizo hilo si ugonjwa wa kuambukiza. Hilo ni tatizo gani? Ni msongamano wa magari!

Watafiti wanasema kwamba kukwama mara kwa mara kwenye msongamano wa magari kunaweza kuathiri afya yako. Uchunguzi wa hivi majuzi unaonyesha kwamba hatari ya kupatwa na mshtuko wa moyo inazidi mtu anapokwama katika msongamano wa magari. Hatari hiyo huwa kubwa katika muda wa saa moja tangu anapokwama. Gazeti The New Zealand Herald linasema kwamba “yaelekea moshi wa magari, mfadhaiko, na kelele, ndiyo mambo ambayo hasa yanazidisha hatari hiyo.”

Sumu Hewani

Karibu magari yote hutoa gesi ya nitrojeni oksidi na chembe fulani zinazosababisha kansa. Magari mengi, hasa yale yanayotumia dizeli, hutoa moshi wenye chembe nyingi ndogondogo. Chembe hizo huathiri sana afya ya watu. Imekadiriwa kwamba kila mwaka watu milioni tatu hivi hufa kwa sababu ya uchafuzi wa hewa unaosababishwa hasa na magari. Ripoti moja inasema kwamba kisa kimoja kati ya visa kumi vya magonjwa ya mfumo wa kupumua ya watoto huko Ulaya husababishwa na chembe ndogondogo zinazochafua hewa. Watoto wengi zaidi hupatwa na magonjwa hayo katika majiji yenye magari mengi.

Fikiria pia jinsi Dunia inavyoathiriwa. Gesi zenye nitrojeni oksidi na salfa dioksidi zinazotoka katika magari husababisha mvua ya asidi. Mvua hiyo huchafua maziwa na mito, nayo huwadhuru wanyama wa majini na mimea mingi. Isitoshe, magari hutoa kiasi kikubwa sana cha kaboni dioksidi. Gesi hiyo ndiyo hasa husababisha ongezeko la joto la dunia ambalo pia hudhuru sayari yetu.

Misiba ya Barabarani Inaongezeka

Idadi ya magari inapoongezeka, watu wengi zaidi hufa katika misiba ya barabarani. Zaidi ya watu milioni moja hufa katika misiba hiyo kila mwaka, na idadi hiyo inaongezeka daima. Katika maeneo fulani misiba hiyo hutokea mara nyingi zaidi. Kwa mfano, wachunguzi wa Tume ya Ulaya wanasema kwamba “watu 690 kwa kila watu milioni moja hufa katika misiba ya barabarani nchini Ugiriki, ikilinganishwa na watu 120 nchini Sweden.”

Jambo lisilopendeza ambalo limezungumziwa sana katika miaka ya majuzi linawahusu madereva wenye hasira. Ni jambo la kawaida kusikia kuwahusu madereva wanaowashambulia wenzao kwa hasira. Kulingana na uchunguzi uliofanywa na shirika la kitaifa la Marekani linaloshughulikia usalama barabarani, madereva husema kwamba jambo linalowafanya wakasirike zaidi ni “ongezeko la idadi ya magari au misongamano.”

Uchumi Unaathiriwa

Misongamano ya magari husababisha hasara za kifedha pia. Uchunguzi mmoja ulionyesha kwamba huko Los Angeles, California, magari hutumia zaidi ya lita bilioni nne za mafuta katika misongamano. Kuna hasara nyingine pia kama vile kupoteza nafasi za kufanya biashara, kuongezeka kwa gharama za matibabu kwa sababu ya uchafuzi, na hasara za misiba ya barabarani.

Hasara hizo zote huathiri uchumi wa nchi mbalimbali. Uchunguzi mmoja ulionyesha kwamba wakati na mafuta yanayopotezwa katika misongamano huwagharimu Wamarekani dola bilioni 68 hivi kila mwaka. Gazeti Philippine Star la Mashariki ya Mbali lilisema hivi: “Nchi hii inapoteza mabilioni ya peso kila mwaka kwa sababu ya misongamano ya magari.” Imekadiriwa kwamba barani Ulaya, gharama hiyo ni dola bilioni 207 za Marekani.

Je, Misongamano ya Magari Itazidi?

Licha ya jitihada nyingi za kutatua tatizo la msongamano wa magari, mambo yamezidi kuwa mabaya. Uchunguzi wa kitaifa uliofanywa na Taasisi ya Usafiri ya Texas katika miji 75 huko Marekani, ulionyesha kwamba muda ambao watu walikuwa wakikwama katika misongamano ya magari kabla ya mwaka wa 1982 uliongezeka kutoka saa 16 kwa wastani kila mwaka hadi saa 62 katika mwaka wa 2000. Muda ambao wasafiri wanatarajia kukabili misongamano kila siku uliongezeka kutoka muda wa saa 4.5 hadi saa 7. Uchunguzi huo unaonyesha kwamba “misongamano ya magari iliongezeka daima katika kila eneo ambalo uchunguzi huo ulifanywa. Muda wa misongamano unaongezeka na misongamano inahusisha barabara nyingi na magari mengi kuliko zamani.”

Kuna hali kama hiyo katika nchi nyingine. Watafiti wanaofanya kazi chini ya usimamizi wa Tume ya Ulaya walikata kauli hii: “Tusipobadili kabisa tabia zetu za kusafiri, misongamano ya magari itazuia kabisa usafiri kwenye majiji mbalimbali katika miaka kumi ijayo.”

Nchi za Asia zina matatizo hayohayo. Tokyo huwa na misongamano mingi ya magari, na idadi ya magari inaongezeka katika majiji mengine nchini Japani. Ripoti kama hii katika gazeti Manila Bulletin ni ya kawaida nchini Filipino: “Barabara zimejaa magari, na maelfu ya watu wanaosafiri kwenda na kutoka kazini wanalazimika kungojea usafiri kwa muda mrefu zaidi.”

Ni wazi kwamba kwa sasa hakuna masuluhisho kamili ya tatizo la msongamano wa magari. Anthony Downs, mwandishi wa kitabu Stuck in Traffic—Coping With Peak-Hour Traffic Congestion alikata kauli hii: “Hata serikali zichukue hatua gani ili kusuluhisha tatizo la msongamano, yaelekea tatizo hilo litazidi kuwa baya katika sehemu nyingi za ulimwengu. Kwa hiyo, ushauri wangu ni: Lizoee.”

Unaweza Kufanya Nini?

Unaweza kufanya nini ili kukabiliana na tatizo hilo linalokera? Ikiwa wewe ni kati ya mamilioni ya watu ambao hukwama katika misongamano, kuna mambo unayoweza kufanya ili ulinde afya yako ya mwili na akili.

▪ JITAYARISHE. Wengi hufadhaika hata kabla ya kukwama katika msongamano wa magari. Wao huchelewa kuamka. Wao huoga, huvaa, na kula haraka-haraka. Wana wasiwasi wa kwamba watachelewa kazini. Msongamano huzidisha mfadhaiko wao. Ukiona kwamba utakwama katika msongamano, anza safari mapema. Ukiondoka mapema huenda hata ukatangulia magari mengi. Kitabu Commuting Stress—Causes, Effects, and Methods of Coping kinasema hivi: “Ukitaka kupunguza mfadhaiko unaposafiri kwenda kazini, anza kujitayarisha jioni. Ili kupunguza shughuli za asubuhi, tayarisha mavazi na mikoba jioni, na vilevile chakula cha mchana cha yule anayeenda kazini au cha watoto.” Bila shaka, ni muhimu kupata usingizi wa kutosha. Ili uamke mapema ni lazima ulale mapema.

Kuna manufaa mengine ya kuamka mapema. Kwa mfano, ukikwama kwa muda mrefu katika msongamano wa magari, misuli yako itakuwa migumu. Ikiwa hali inafaa unaweza kufanya mazoezi asubuhi. Kufanya mazoezi kwa ukawaida kunaweza kuboresha afya yako na kukusaidia kupambana na mfadhaiko unaotokana na kukwama katika msongamano. Ukiamka mapema unaweza pia kula kiamsha kinywa kizuri. Utafadhaika zaidi ukikwama katika msongamano ukiwa na njaa au ikiwa umekula chakula kisichojenga mwili.

Unaweza pia kuepuka mfadhaiko kwa kuhakikisha kwamba gari lako liko katika hali nzuri. Unaweza kufadhaika sana gari likiharibika kwenye msongamano, hasa mvua inaponyesha. Kwa hiyo, hakikisha kwamba breki, magurudumu, kisafisha hewa, kipasha-joto, waipa za kioo cha mbele, na vitu vingine muhimu vinafanya kazi vizuri. Hata hitilafu ndogo inaweza kukufadhaisha sana barabara inapojaa magari. Kila mara, hakikisha kwamba gari lako lina mafuta ya kutosha.

▪ PATA HABARI. Kabla hujaondoka huenda ikafaa kupata habari kuhusu mambo kama vile hali ya hewa, ujenzi wa barabara, vizuizi vya muda barabarani, misiba, na hali nyinginezo. Unaweza kupata habari hizo kwa kusikiliza redio au kusoma magazeti. Ukiwa na ramani, unaweza kupitia barabara nyingine na kuepuka sehemu zenye matatizo.

▪ STAREHE. Hakikisha kwamba kuna hewa ya kutosha, na urekebishe kiti chako ili ustarehe kadiri inavyowezekana. Ukiwa na redio au kifaa cha kuchezea kaseti au CD unaweza kusikiliza muziki unaopenda. Aina fulani za muziki hutuliza na zinaweza kupunguza mfadhaiko. Ukifanya hivyo unaweza pia kuepuka kelele zinazokera za magari mengine. *

▪ USIZUBAE TU. Jambo moja lenye manufaa ambalo unaweza kufanya ukikwama katika msongamano wa magari ni kufikiria mambo yanayofaa. Badala ya kufikiria tu msongamano, fikiria shughuli za siku hiyo. Ukikwama katika msongamano ukiwa peke yako garini, una nafasi nzuri ya kuchanganua mambo muhimu na hata kufanya maamuzi bila kukatizwa.

Ikiwa wewe ni abiria, kutazama magari yaliyo mbele yenu kunaweza kufadhaisha zaidi. Kwa hiyo, panga utumie vizuri muda unaosafiri. Unaweza kubeba kitabu unachopenda au gazeti la kila siku. Unaweza kusoma baadhi ya barua ulizopokea siku iliyotangulia. Watu fulani huandika barua au kufanya kazi kwa kutumia kompyuta ndogo.

▪ TARAJIA MISONGAMANO. Ukiishi katika eneo ambalo huwa na misongamano, tarajia kukwama, na ufanye mipango kupatana na hali. Tatizo la misongamano ya magari litaendelea katika majiji mengi. Kitabu Stuck in Traffic—Coping with Peak-Hour Traffic Congestion kinasema hivi: “Yaelekea tatizo la misongamano ya magari litadumu katika majiji ambayo tayari yana tatizo hilo.” Hivyo, ni afadhali uzoee misongamano ya magari na utumie wakati vizuri iwezekanavyo unapokuwa katika msongamano!

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 25 Wasomaji wengi wa Amkeni! husikiliza kaseti za gazeti la Amkeni! na vilevile za Mnara wa Mlinzi. Magazeti haya yanapatikana katika kaseti, CD, na MP3, katika lugha kadhaa.

[Picha katika ukurasa wa 26]

Epuka msongamano kwa kupanga mambo mapema

[Picha katika ukurasa wa 26]

Kabla hujaanza safari, chagua kaseti au CD inayofaa

[Picha katika ukurasa wa 26]

Ukiwa abiria, jitahidi kutumia vizuri wakati wa kusafiri

[Picha katika ukurasa wa 26]

Usiudhike kwa sababu ya mambo usiyoweza kuyabadili