Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kutembea Kusiko kwa Kawaida!

Kutembea Kusiko kwa Kawaida!

Kutembea Kusiko kwa Kawaida!

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI FINLAND

Je, umewahi kusikia kuhusu kutembea kwa vyuma? Nchini Finland, kutembea kwa aina hiyo kumekuwa mojawapo ya njia maarufu zaidi za kufanya mazoezi. Vyuma kama vile vya watu wanaoteleza kwenye barafu hutumiwa. Kulianzaje, na kuna faida gani?

UNAPOMWONA mtu akitembea kwa vyuma, unaweza kufikiri ni mwana-michezo wa masafa marefu wa kuteleza kwenye barafu asiyekuwa na vifaa vya kuteleza. Kwa kweli, watu wanaoteleza kwenye barafu ndio walioanzisha njia hiyo ya kutembea kwa vyuma walipoanza kuboresha mazoezi yao wakati wa kiangazi kwa kutumia vyuma vya kuteleza kwenye barafu. Katika miaka ya 1980, kutembea kwa kutumia vyuma vya aina hiyo kulianza kutumiwa na wana-michezo wengine kama mbinu inayofaa ya kufanya mazoezi. Kufikia mwishoni mwa 1990, watu ambao si wana-michezo walianza pia kutembea kwa kutumia vyuma hivyo. Uchunguzi wa mwaka wa 2004 wa Gallup ulionyesha kwamba watu 760,000 nchini Finland, yaani, asilimia 19 ya idadi ya watu nchini humo, hutembea kwa vyuma angalau mara moja kwa juma. Tuomo Jantunen, mkurugenzi mkuu wa shirika la Suomen Latu ambalo liliidhinisha uchunguzi huo anasema hivi: “Kutembea kwa vyuma kumekuwa mazoezi yanayopendwa sana baada ya mazoezi ya kutembea.” Imethibitika kuwa kutembea kwa vyuma si mtindo wa muda mfupi tu. Katika miaka ya karibuni umeanza kutumiwa katika nchi nyingine pia.

Watu wengi wanafahamu manufaa ya kutembea, lakini kutembea kwa vyuma kuna faida gani? “Faida moja kubwa ni kwamba kutembea kwa vyuma hufanyiza mazoezi sehemu ya juu ya mwili, kutia ndani misuli ya mikono, mgongo, na tumbo,” anasema Jarmo Ahonen, daktari wa kunyoosha viungo ambaye pia ni mtaalamu wa kutembea kwa vyuma. Anaongeza hivi: “Mazoezi hayo pia husaidia kutuliza misuli iliyochoka ya shingo na ya mabega, jambo ambalo huwapata watu wanaofanya kazi ofisini.”

Kutembea huku hufanyiza misuli mingi zaidi mazoezi kuliko kutembea kwa kawaida, na hivyo humfanya mtu atumie kalori nyingi. Kutumia vyuma humwezesha mtu atembee kwa kasi zaidi na kuongeza mpigo wa moyo. Lakini si hayo tu. Watu wanaotetea mazoezi hayo wanadai kwamba vyuma hivyo vinapotumiwa vizuri, vinaweza kumsaidia mtu atembee wima. Ahonen anadai hivi: “Kutembea kwa vyuma hupunguza mkazo kwenye viungo, kwani uzito wa mwili huelekezwa kwenye vyuma hivyo.” Mtu mmoja ambaye hutembea kwa njia hiyo anaeleza kwamba vyuma hivyo humsaidia kudumisha usawaziko anapotembea mahali panapoteleza. Kwa sababu hiyo, wazee wameanza kutumia mbinu hiyo wakati wa majira ya baridi kali, kwa kuwa ardhi huwa imefunikwa kwa barafu au theluji.

[Sanduku katika ukurasa wa 20]

Kujifunza Kutembea kwa Vyuma

Si lazima mtu anunue vifaa vya bei ghali ili atembee kwa vyuma. Unahitaji tu viatu vizuri na vyuma vilivyoundwa kwa njia nzuri vilivyo na urefu unaofaa. Unapotembea mahali pagumu, tumia vidhibiti vya mpira kufunika ncha kali za vyuma hivyo. Si vigumu kujifunza kutembea kwa vyuma. Hata hivyo, ikiwa hujawahi kutembea kwa kutumia vyuma, huenda ikafaa kumwomba mashauri mtu mwenye uzoefu.