Ugumu wa Kulisha Majiji
Ugumu wa Kulisha Majiji
“Kulisha majiji ya ulimwengu chakula cha kutosha kunazidi kuwa kazi ngumu inayohusisha ushirikiano wa watu wanaozalisha chakula, wasafirishaji, wenye masoko ya vyakula, na wauzaji wengi wa rejareja.”—JACQUES DIOUF, MKURUGENZI MKUU WA SHIRIKA LA CHAKULA NA KILIMO LA UMOJA WA MATAIFA (FAO).
WATAALAMU wa ugawaji wa chakula wanasema kwamba huenda kuwaandalia wakazi wote wa mijini chakula chenye lishe ambacho kinaweza kupatikana kwa urahisi wakati wote kukawa “tatizo kubwa zaidi linalowakumba wanadamu” katika karne ya 21.
Kwa sasa, chakula kilicho ulimwenguni kinaweza kutosheleza mahitaji ya kila mtu duniani ikiwa kitagawanywa kulingana na uhitaji. Lakini ukweli wa mambo ni kwamba watu wapatao milioni 840 hawapati chakula cha kutosha kila siku. Wengi wao wanaishi mijini. Fikiria pande mbalimbali za tatizo hilo.
Majiji Makubwa Yanayohitaji Chakula Kingi
Majiji yanapozidi kuwa makubwa, mashamba yaliyo karibu ambayo wakati mmoja yalitumiwa kwa ukulima hutumiwa kwa ujenzi wa nyumba, viwanda, na barabara. Hivyo, mashamba yanayolisha majiji yanazidi kuwa mbali na majiji hayo. Mara nyingi, kiasi kidogo cha chakula hukuzwa mijini au hata hakikuzwi, nayo nyama hutoka sehemu za mbali za mashambani. Katika nchi nyingi zinazositawi, barabara za kusafirishia chakula kutoka mashambani hadi mijini ni mbovu. Hilo linamaanisha kwamba itachukua muda mrefu zaidi kusafirisha chakula, chakula kingi kitaharibika, na mwishowe wanunuzi,
ambao wengi wao ni maskini watakinunua kwa bei ya juu.Tayari majiji fulani katika nchi zinazositawi ni makubwa na yanatarajiwa kuwa makubwa hata zaidi. Kufikia mwaka wa 2015, jiji la Mumbai (ambalo zamani liliitwa Bombay) linatarajiwa kuwa na wakazi milioni 22.6, Delhi milioni 20.9, Mexico City milioni 20.6, na São Paulo milioni 20. Inakadiriwa kwamba jiji lenye watu milioni kumi, kama vile Manila au Rio de Janeiro linahitaji kuleta tani 6,000 za chakula kila siku.
Hiyo si kazi rahisi, na inazidi kuwa ngumu, hasa katika maeneo yaliyo na ongezeko kubwa la watu. Kwa mfano, jiji la Lahore, Pakistan, lina idadi kubwa ya watu wanaozaliwa (asilimia 2.8) na pia watu wengi sana wanahamia huko kutoka mashambani. Katika nchi nyingi zinazositawi, mamilioni ya watu wanahamia majiji ambayo tayari yamesongamana ili kutafuta maisha mazuri, kazi, bidhaa, na huduma bora. Kwa sababu ya watu kuhamia jiji la Dhaka, Bangladesh, idadi ya watu katika jiji hilo inatazamiwa kuongezeka kwa milioni moja au zaidi kila mwaka katika miaka ya karibuni. Kulingana na makadirio, idadi kubwa ya watu nchini China ambao sasa huishi mashambani, watahamia mijini kufikia mwaka wa 2025. Kufikia wakati huohuo, inatarajiwa kwamba watu milioni 600 watakuwa wakiishi katika majiji ya India.
Kwa sababu ya watu kuhamia mijini, mpangilio wa kugawanya chakula katika sehemu nyingi za ulimwengu unabadilika. Kwa mfano, katika Afrika Magharibi, asilimia 14 ya watu waliishi mijini katika mwaka wa 1960. Kufikia mwaka
wa 1997, asilimia 40 ya watu waliishi mijini, na inaaminika kwamba kufikia 2020, idadi hiyo itaongezeka kufikia asilimia 63. Katika pembe ya Afrika, idadi ya watu wanaoishi mijini inatarajiwa kuongezeka maradufu katika miaka kumi ijayo. Na inatabiriwa kwamba hivi karibuni, asilimia 90 ya ongezeko la idadi ya watu katika nchi zinazositawi litakuwa katika miji na majiji.Kuongeza kiasi cha chakula kinachopelekwa mijini ili kuwalisha watu hao wote ni kazi ngumu. Inahitaji jitihada ya pamoja ya maelfu ya wakulima, wapakiaji, wasafirishaji, wafanyabiashara, watu wengine wanaoshughulika na chakula, na pia maelfu ya magari. Hata hivyo, katika sehemu fulani, uhitaji unaoongezeka wa chakula mijini unazidi uwezo wa maeneo yanayotoa vyakula. Isitoshe, katika majiji mengi ya nchi zinazositawi, huduma kama vile usafirishaji na majengo ya kuhifadhia vyakula, masoko, na machinjioni tayari zimeshindwa kutosheleza uhitaji uliopo.
Kuenea kwa Umaskini
Inakuwa vigumu hata zaidi kulisha watu wanaozidi kuongezeka katika maeneo yenye umaskini mwingi. Katika majiji mengi makubwa ya nchi zinazositawi, kama vile Dhaka, Freetown, Guatemala City, Lagos, na La Paz, tayari asilimia 50 au zaidi ya wakazi wake wanakabiliana na umaskini.
Wachunguzi wanapozungumza kuhusu kulisha watu hao, wao hutofautisha kati ya kuwepo kwa chakula na uwezekano wa kukipata kwa bei nafuu. Huenda chakula kikapatikana sokoni, lakini maskini wanaoishi mijini hawawezi kufaidika ikiwa kinauzwa kwa bei ya juu sana. Imeonekana kwamba mapato ya wakazi fulani wa mijini yanapoongezeka, uhitaji na matumizi yao ya chakula cha aina mbalimbali huongezeka. Kwa upande mwingine, ni vigumu kwa maskini wanaoishi mjini kununua chakula cha kutosha ili kutosheleza mahitaji na mapendezi yao. Huenda familia hizo maskini zikatumia kati ya asilimia 60 na 80 ya mapato yao kununua chakula.
Huenda gharama zikapungua ikiwa chakula kingenunuliwa kwa wingi; hata hivyo, hilo haliwezekani ikiwa watu hawana pesa za kutosha. Familia nyingi hata haziwezi kupata chakula zinachohitaji, na hivyo hupatwa na utapiamlo. Kwa mfano, inasemekana kwamba utapiamlo ni “tatizo kubwa na lililoenea sana” katika majiji yaliyo kusini mwa jangwa la Sahara.
Watu walio hasa katika hatari ya kukosa chakula cha kutosha ni wale waliohamia majijini kutoka mashambani hivi karibuni na hawajazoea maisha ya mjini, yaani, mama wasio na wenzi, wale walioajiriwa na serikali hivi karibuni ambao mishahara yao huchelewa kwa kuwa serikali haina pesa za kutosha, walemavu, wazee, na wagonjwa. Mara nyingi, watu hao huishi maeneo yaliyo mbali na jiji katika mabanda au nyumba duni ambazo hazina umeme, maji ya mabomba, na mfumo wa kuondoa maji machafu. Mamilioni ya watu ambao hujikakamua kupata riziki chini ya hali kama hizo wanaweza kuathiriwa kwa urahisi na matatizo ya kusafirisha na kugawa chakula. Mara nyingi watu hao huishi mbali na masoko na wanalazimika kununua chakula kibovu kwa bei ya juu. Kwa kweli, hali yao inasikitisha.
Hali Zisizo Salama na Zinazotisha Afya
Katika sehemu nyingi ni jambo la kawaida kwa watu kuhamia mijini bila mpango na kwa njia isiyo halali. Kwa sababu hiyo kunakuwa na mazingira yasiyo safi yenye uhalifu mwingi. Kichapo cha shirika la FAO, Feeding the Cities, kinasema hivi: “Mara nyingi wasimamizi wa jiji katika nchi zinazositawi hujikuta wakifanya kazi nyingi sana ili kukabiliana na kuongezeka haraka kwa watu katika mazingira ambayo yanapaswa tu kukaliwa na watu wachache.”
Katika sehemu nyingi za Afrika, mara nyingi masoko huanzishwa bila mpango. Wafanyabiashara huanza kuuza bidhaa zao mahali popote zinapohitajiwa. Kwa hiyo, masoko hayo hukosa huduma za lazima.
Huko Colombo, Sri Lanka, masoko ya rejareja na ya jumla yako mahali pasipofaa na husongamana sana watu. Madereva wa malori hulalamika kwamba inawachukua muda mrefu kufika kwenye soko kuu. Hakuna mahali pa kuegesha malori, kupakia na kupakua bidhaa.
Kwingineko, masoko hayatunzwi na kusimamiwa ifaavyo. Uchafu kutokana na takataka zilizorundamana kwa wingi huwa tisho kwa afya. Meya wa jiji moja huko Asia Kusini alisema kwamba “takataka hizo huchangia kuzorota kwa afya.”
Uzito wa matatizo yanayohusiana na masuala ya usafi na ya kimazingira unaonyeshwa na matokeo ya uchunguzi uliofanyiwa bidhaa zinazotokana na wanyama zilizouzwa katika jiji moja huko Kusini-mashariki ya Asia. Katika jiji hilo, ni jambo la kawaida kwa nyama “kuwekwa chini mahali ambapo hupata vumbi na maji machafu.” Bakteria ya salmonella ilipatikana katika asilimia 40 ya nyama ya nguruwe iliyochunguzwa na asilimia 60 ya nyama ya ng’ombe, huku asilimia 100 ya nyama ya ng’ombe ilikuwa na bakteria ya E. coli. Pia nyama hiyo ilikuwa na sumu inayotokana na metali nzito kama vile risasi na zebaki.
Kwa sababu mfumo wa kusafirisha na kugawa chakula hautegemeki na hautoshelezi mahitaji yao, wakazi wengi wa jijini, kama huko Kano, Nigeria hujaribu kukuza chakula katika sehemu yoyote ya ardhi ambayo haitumiwi. Hata hivyo, wengi wao hawana vibali vya kumiliki ardhi hiyo. Hivyo wanaweza kufukuzwa na mimea waliyokuza kuharibiwa.
Olivio Argenti, mtaalamu wa kuchunguza ikiwa kuna chakula cha kutosha mijini wa shirika la FAO alieleza yale aliyoona alipotembelea sehemu moja ya jiji huko Mexico ambako watu walikuza chakula karibu na mto ambao humwagwa maji machafu kutoka kwa kijiji kilicho karibu. Wakulima wa huko walimwagilia mboga zao maji hayo na kutumia udongo kutoka kwenye mto huo kutayarisha mashamba yao. “Niliwauliza wenye mamlaka ikiwa walifahamu hatari iliyopo,” anaandika Argenti, “nao walisema kwamba hawangeweza kufanya lolote kwa sababu hawakuwa na fedha au ufundi uliohitajika.” Matatizo kama hayo yanaonekana katika maeneo mengi ya nchi zinazositawi.
Majiji Yanajitahidi Kukabiliana na Hali
Inaonekana kwamba matatizo ambayo yanakabili majiji yanayozidi kusongamana watu ni mengi mno. Mashirika ya kimataifa, wapangaji wa miji, na wasimamizi wanajitahidi kufanya yote wanayoweza ili kuyatatua. Mbinu zao zinatia ndani kuwachochea watu katika maeneo ya mashambani wakuze chakula kingi na kufanya kipatikane kwa urahisi, na pia kujenga barabara mpya, masoko, na machinjioni. Wanaona uhitaji wa kuwatia moyo watu watumie pesa
zao kujenga majengo ya kuhifadhi vyakula, wafanye iwe rahisi kwa wakulima, wafanyabiashara, na wasafirishaji kupata mikopo, na kuhakikisha kwamba sheria zinazofaa kuhusu uuzaji na usafi zinafuatwa. Hata hivyo, wachunguzi wanasema kwamba licha ya jitihada ambazo zimefanywa, wasimamizi wengi wa majiji hawatambui wala kushughulikia inavyofaa masuala yanayohusika. Hata wanapofanya hivyo, hakuna pesa za kutosha kushughulikia matatizo hayo.Matatizo mazito yanayoyakabili majiji hasa katika nchi zinazositawi, yamefanya maonyo yatolewe kwa hima. Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti kuhusu Chakula, huko Washington, D.C., inaonya kwamba, “tusipochukua hatua sasa, idadi ya watu mijini itaendelea kuongezeka, na matatizo hayo [njaa, utapiamlo, na umaskini] yataongezeka pia.” Janice Perlman, rais wa Mradi wa Majiji Makubwa Sana, ambalo ni shirikisho la kimataifa la mashirika yaliyojitoa kutatua matatizo ya majiji, alisema hivi kuhusu wakati ujao wa majiji katika nchi maskini: “Hakujawahi kuwa na mbinu yoyote ya kuwalisha, kuwapa makao, kuwaajiri au kuwasafirisha watu wengi sana wanaoishi katika eneo dogo sana chini ya hali ngumu za kifedha na za mazingira. Majiji hayawezi tena kuwaandalia wakazi wake mahitaji yao.”
Hata hivyo, kuna sababu nzuri za kuamini kwamba matatizo ya kusafirisha na kugawanya chakula yatatatuliwa hivi karibuni.
[Sanduku katika ukurasa wa 5]
MAJIJI YANAKUA
▪ Inatarajiwa kwamba katika miaka 30 ijayo, ongezeko la watu ulimwenguni pote litakuwa hasa katika majiji.
▪ Inatarajiwa kwamba kufikia mwaka wa 2007, zaidi ya nusu ya watu ulimwenguni wataishi katika sehemu za mijini.
▪ Inakadiriwa kwamba idadi ya watu wanaoishi majijini ulimwenguni itaongezeka kwa wastani wa asilimia 1.8 kwa mwaka; ongezeko hilo likiendelea kwa kiwango hicho, idadi ya watu mijini itaongezeka maradufu katika miaka 38.
▪ Idadi ya majiji yenye watu milioni tano au zaidi inatarajiwa kuongezeka kutoka 46 mwaka 2003, hadi 61 mwaka wa 2015.
[Hisani]
Chanzo: World Urbanization Prospects—The 2003 Revision, Idara ya Umoja wa Mataifa ya Masuala ya Uchumi na Jamii, Kitengo cha Idadi ya Watu
[Sanduku katika ukurasa wa 6]
BAADHI YA VISABABISHI NA ATHARI ZA KUTOTEGEMEKA KWA UGAWANYAJI WA CHAKULA
▪ “Kotekote ulimwenguni inajulikana wazi kwamba kuongezeka kwa ghafula kwa bei ya chakula husababisha misukosuko ya kisiasa na ya jamii katika sehemu za mijini.”—Jacques Diouf, mkurugenzi mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa.
▪ Katika mwaka wa 1999, vimbunga Georges na Mitch vilitokea katika eneo la Karibea na Amerika ya Kati na kusababisha uharibifu mkubwa, vikakatiza shughuli za kawaida, na kusababisha ukosefu wa chakula.
▪ Maandamano ya kupinga kuongezeka kwa bei ya mafuta huko Ekuado mnamo 1999 na huko Uingereza mnamo 2000 yalisababisha mvurugo mkubwa katika usafirishaji na ugawanyaji wa chakula.
▪ Ukosefu wa chakula ni baadhi ya madhara ambayo husababishwa na vita.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 7]
MTU MMOJA KATI YA MAMILIONI
CONSUELO na watoto wake 13 huishi katika kijiji cha maskwota (kilichoonyeshwa juu) kwenye vitongoji vya Lima, Peru. Watoto wake watatu wanaugua kifua kikuu. Anasema: “Tulikuwa tukiishi milimani, lakini usiku mmoja mamia ya wanakijiji wenzetu walihamia jijini. Tuliwazia, ‘huko Lima watoto wetu watapata elimu na kuvaa viatu. Wataishi maisha bora.’” Kwa hiyo wanakijiji walifuma mikeka ya nyasi, na usiku mmoja wote wakahamia jijini na kujenga nyumba za mikeka. Asubuhi, kulikuwa na maskwota wengi sana hivi kwamba wenye mamlaka hawangeweza kuwafukuza.
Nyumba ya Consuelo ina sakafu ya udongo na kuna shimo kubwa kwenye paa. “Ninafuga kuku hawa ili niwauzie matajiri,” anasema akizungumza kuhusu kuku wanaokimbia-kimbia nyumbani kwake. “Nilitaka pesa za kumnunulia binti yangu viatu. Lakini sasa lazima nitumie pesa hizo kulipia gharama za hospitali na dawa.”
Consuelo hana chakula kingine nyumbani mwake ila tu vitunguu vichache. Ni vigumu sana kupata kazi, naye hana hata pesa za kutosha kununua maji kwa ukawaida. Nyumba yake mbovu haina maji ya bomba wala choo. Anaeleza hivi: “Sisi hutumia ndoo hii kama choo. Kisha usiku mimi huwatuma watoto waende kumwaga uchafu huo mahali fulani. Hatuna lingine la kufanya.”
Consuelo hapati msaada wowote kutoka kwa mume wake ambaye yeye humwona mara chache sana. Ana umri wa miaka 30 na kitu tu lakini anaonekana mzee zaidi. Mwandishi aliyemhoji anasema hivi: “Uso wake umefura kidogo na macho yake madogo hayana hisia yoyote. Yanaonyesha kwamba hana tumaini lolote.”
[Hisani]
Chanzo: Jarida In Context
AP Photo/Silvia Izquierdo
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 9]
“JE, NIHAMIE JIJINI?”
MTU yeyote anayetaka kuhamia jijini anapaswa kufikiria mambo fulani. Kichapo cha Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, Feeding the Cities kinasema: “Mojawapo ya mambo makuu ambayo huwavutia watu ni matarajio ya kuboresha maisha yao wanapoyalinganisha na maisha ya sehemu za mashambani.” Hata hivyo, “maisha yao hayataboreka mara moja. Huenda yakaboreka baada ya kizazi kimoja au zaidi.”
Ukweli wa mambo ni kwamba watu wengi ambao huhamia jijini kutoka mashambani hujikuta bila makao, kazi, na wakiwa maskini zaidi kuliko walivyokuwa, huku wakiishi katika mazingira wasiyofahamu. Kwa hiyo, ikiwa unafikiria kuhamia jijini, je, una hakika kwamba kufanya hivyo kutakuwezesha kuruzuku familia yako? Ni vigumu kupata kazi jijini, na hata ukipata, kwa kawaida mshahara ni mdogo. Je, mkazo wa kufanya kazi kwa saa nyingi ili tu kujiruzuku utafanya wewe na familia yako mpuuze utendaji ambao ni muhimu zaidi kwenu?—Mathayo 28:19, 20; Waebrania 10:24, 25.
Wazazi fulani wameamua kuhamia jijini na kuacha familia zao mashambani. Je, hilo ni jambo la hekima? Wazazi Wakristo wana wajibu wa kuandalia familia zao mahitaji ya kimwili, lakini kutengana hivyo kutaathirije familia kihisia na kiroho? (1 Timotheo 5:8) Je, akina baba wataendelea kuwalea watoto wao kwa njia inayofaa “katika nidhamu na mwongozo wa akilini wa Yehova?” (Waefeso 6:4) Je, kutengana kwa mume na mke kunaweza kuwafanya wakabili vishawishi vya maadili?—1 Wakorintho 7:5.
Bila shaka, uamuzi wa kuhama ni jambo la kibinafsi. Kabla ya kufanya uamuzi huo, Wakristo wanapaswa kuzingatia mambo yote yanayohusika na kusali ili kupata mwongozo wa Yehova.—Luka 14:28.
[Picha katika ukurasa wa 8]
Majiji yanakabiliana na mazingira machafu na msongamano
India
Niger
Mexico
Bangladesh
[Picha katika ukurasa wa 8]
Katika familia nyingi maskini zinazoishi mijini, lazima watoto pia wafanye kazi
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 8]
India: © Mark Henley/Panos Pictures; Niger: © Olivio Argenti; Mexico: © Aubrey Wade/Panos Pictures; Bangladesh: © Heldur Netocny/ Panos Pictures; bottom photo: © Jean-Leo Dugast/Panos Pictures