Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuteleza Mawimbini kwa Ujasiri kwa Kutumia Matete

Kuteleza Mawimbini kwa Ujasiri kwa Kutumia Matete

Kuteleza Mawimbini kwa Ujasiri kwa Kutumia Matete

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI PERU

Mashindano yasiyo ya kawaida ya kuteleza mawimbini huwavutia watu kwenye ufuo fulani ulio karibu na jiji la Trujillo, Peru. Badala ya kutumia mbao za kawaida za Hawaii kuteleza, washindani hutumia “farasi-maji,” au caballitos del mar. Mashua hizo ndogo zinatengenezwa kwa matita ya matete ya totora, ambayo hukua hapa. Kila mashua inafanana na kayak (mashua ya Waeskimo) lakini sehemu yake ya mbele ni ndefu nayo imejipinda kuelekea juu, na hivyo kuwezesha “farasi-maji” akabiliane na mawimbi makubwa. Huku wakiwa wameinama kwenye sehemu ya juu ya mashua yao kama wapanda-farasi, watelezaji hao hujisukuma mbele kwa kutumia makasia ya mianzi na kupita juu ya mawimbi makubwa. Watazamaji fulani wanasema kwamba watelezaji hao hufanana na wapanda-farasi wanaoruka viunzi. Mashua hizo zisizo za kawaida zilianza kutengenezwa lini?

Kwa sababu jangwa limeenea hadi baharini mahali hapa, kuna miti michache hivyo hakuna mbao za kutosha kutengeneza mashua. Mafundi wa hapa wamejifunza kutoka kwa babu zao jinsi ya kutengeneza “farasi-maji” kwa dakika chache tu. Wao huanza kwa kutengeneza tao lililochongoka la gubeti kwa kufunga matita ya matete pamoja. Ufundi huo humalizika baada ya kujenga tezi fupi lenye chumba kidogo cha kuweka vifaa vya uvuvi na pia mahali pa kuhifadhi samaki. Matete hayo yanafaa katika utengenezaji wa mashua kwa kuwa upande wake wa nje hauwezi kupenya maji nao upande wa ndani ni laini na unaweza kuelea. Hata hivyo, baada ya mwaka mmoja, mashua hiyo huwa imejaa maji na hivyo hutupwa.

Kwa karne nyingi, wavuvi wa hapa wamekabiliana kwa ujasiri na mawimbi yenye nguvu ya Bahari ya Pasifiki kwa kutumia “farasi-maji” hao wa kujitengenezea. Sasa ufundi huo unatokomea. Boti kubwa za kuvulia samaki ambazo hutumia mbinu za kisasa zimevua samaki wengi, na hivyo nyakati nyingine kuwalazimisha wavuvi wa kawaida kusafiri kilometa nyingi kutoka pwani ili kutafuta samaki. Lakini wenyeji wachache wangali wanatumia “farasi-maji” kuvua samaki, hasa nyakati zenye magumu ya kiuchumi ambapo huenda hiyo ikawa njia pekee ya kuruzuku familia zao.

Wakati huohuo, kutumia “farasi-maji” kuteleza mawimbini bado kunawaletea faida mafundi wa kutengeneza mashua, vilevile kunawavutia watalii wanaopendezwa na utamaduni wa zamani na kuleta wateja kwenye hoteli za hapa. Mara nyingi wageni wamesikika wakisema kwamba inavutia sana kutazama mashindano ya mashua za “farasi-maji” kwenye ufuo wa Huanchaco.

[Picha katika ukurasa wa 18]

Chombo cha udongo cha kabla ya enzi ya Wainka chenye picha ya mvuvi akiwa ndani ya mashua ya matete

[Hisani]

Museo Rafael Larco Herrera/Lima, Perú