Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Watunzaji Wenye Mkazo

Kulingana na uchunguzi uliofanywa na shirika la Takwimu la Kanada, “watu watatu kati ya 10 wenye umri wa miaka 45 hadi 64 wanalazimika kumtunza mtu wa jamaa aliyezeeka ambaye anahitaji msaada huku wakiwatunza watoto walio na umri unaopungua miaka 25 na wakati huohuo wakifanya kazi siku nzima,” linasema gazeti National Post la Kanada. Uchunguzi huo ulionyesha kwamba kati ya watu wanaotunza wazee huku wakilea watoto, wanawake ndio hushuka moyo zaidi kuliko wanaume. Wanawake wanaofanya kazi hutumia saa 29 hivi kwa mwezi kuwatunza wazee ikilinganishwa na saa zipatazo 13 kwa mwezi ambazo wanaume hutumia. Pia huenda wanawake wakafanya kazi zaidi za kuwatunza wazee kama vile kuwapikia na kuwaosha. Gazeti Post linasema kwamba zaidi ya nusu ya watu waliohojiwa walihisi kuwa “wangeweza kuwatunza wazee vizuri zaidi iwapo wangepumzika mara kwa mara.”

Upumzike kwa Muda Gani Mchana?

Gazeti la Australia Sydney Morning Herald linasema kwamba “zoea la zamani la kulala kidogo linaweza kuwa na manufaa katika kazi ambayo mtu anafanya.” Hata hivyo, muda ambao mtu anatumia kulala ni muhimu. Baada ya kuwafanyia uchunguzi watu waliolala kwa muda tofauti-tofauti, Profesa Leon Lack wa Chuo Kikuu cha Flinders alisema hivi: “Ilionekana kwamba kulala kwa dakika moja hakutokezi manufaa yoyote. Ilionekana kwamba kulala kwa dakika tano huwanufaisha watu fulani lakini si sana. Hata hivyo, ilionekana kwamba kati ya uchunguzi wote tuliofanya, kulala kwa dakika 10 ndiko kulitokeza manufaa makubwa.” Tofauti na hilo, watu waliolala kwa muda mrefu zaidi hadi dakika 30 walihisi uchovu kwa muda wa saa moja hivi baada ya kuamka.

Aanza Kumwamini Mungu

Profesa wa falsafa kutoka Uingereza, ambaye ametajwa kuwa “mtu mwenye uvutano mkubwa zaidi ulimwenguni anayeamini kwamba hakuna Mungu” sasa anasema kwamba anamwamini. Katika mahojiano yaliyopangwa kuchapishwa katika jarida Philosophia Christi, Dakt. Antony Flew, mwenye umri wa miaka 81 alisema kwamba ‘alilazimika kukubaliana na uthibitisho uliopo.’ Kulingana na Flew, uthibitisho huo unatia ndani ugunduzi wa karibuni katika nyanja mbalimbali za sayansi. Isitoshe, alieleza kwamba “ugunduzi ambao umefanywa kwa zaidi ya miaka hamsini kuhusu DNA umetoa hoja zenye nguvu zinazoweza kutumiwa kutetea kuwapo kwa Mbuni mwenye akili.” Hata “simulizi la Biblia [la Mwanzo sura ya kwanza] linaweza kuwa sahihi kisayansi,” anasema. Kwa hiyo, je, anataka kuwa Mkristo? “Sidhani,” anasema. Hata hivyo, “ikiwa wakati ujao ningetaka kuwa Mkristo, basi nitakuwa Shahidi wa Yehova.”

Fizi Zenye Afya Huboresha Moyo

Kupiga meno mswaki kwa ukawaida ambako huzuia ugonjwa wa fizi kunaweza kupunguza hatari ya kupatwa na kiharusi au ugonjwa wa moyo, linaripoti gazeti Milenio la Mexico City. Watafiti katika Chuo Kikuu cha Minnesota waligundua kwamba watu wenye bakteria nyingi zinazosababisha ugonjwa wa fizi pia walikuwa na mishipa myembamba inayopeleka damu kichwani. Gazeti hilo linasema kwamba huenda hilo linatukia kwa sababu “vijiumbe ambavyo husababisha ugonjwa wa fizi huhama na kusafiri katika damu, na hivyo kuchochea mfumo wa kinga utende na kusababisha uvimbe.” Kulingana na maelezo ya watafiti, uvimbe huo husababisha kuongezeka kwa mafuta katika mishipa mikubwa au huchangia kuganda kwa damu ambako kunaweza kutokeza mshtuko wa moyo. Kwa hiyo, “kutunza afya ya kinywa kunaweza kuboresha sana afya ya moyo,” linasema gazeti Milenio.

Watu Wanasahau Yaliyotukia Auschwitz

Zaidi ya watu milioni moja walikufa katika kambi ya kifo yenye sifa mbaya ya Auschwitz huko Poland wakati wa Vita vya Pili vya Ulimwengu. Hata hivyo, kulingana na gazeti The Daily Telegraph la London, “karibu nusu ya idadi ya watu wazima [nchini Uingereza] hawajawahi kusikia kuhusu Auschwitz.” Uchunguzi huo uliofanyiwa watu 4,000 uliidhinishwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza ili kuadhimisha miaka 60 tangu watu walipokombolewa kutoka kambi hiyo ya kifo.

Mwanasesere wa Kufundisha Braille

Shirika la Kitaifa la Hispania la Vipofu (ONCE) limebuni mwanasesere anayeitwa Braillín. Mwanasesere huyo ambaye amebuniwa kuwafundisha watoto Braille, ana vibonyezo sita vikubwa katika sehemu ya mbele ya mwili wake ambavyo vinafanana na nukta sita zinazotumiwa katika Braille. Hata wavulana au wasichana wasio na matatizo ya macho wanaweza kujifunza Braille wanapocheza na Braillín. Wataalamu 30 waliboresha na kujaribu mwanasesere huyo na watoto 50 hivi walisaidia kufanya umbo lake lipendeze zaidi. Shirika la ONCE linakusudia kugawanya wanasesere zaidi ya 1,100 katika shule zake za vipofu. Kulingana na María Costa wa Shirikisho la Utafiti wa Vitu vya Kuchezea, “Braillín ni kifaa kizuri sana cha kufundisha. Isitoshe, hiyo ni njia mpya ya kucheza inayohusisha kujifunza na kucheza.”

Uchafuzi wa Hewa Unaoua

Gazeti la Hispania El País linasema kwamba “kila mwaka, uchafuzi wa hewa husababisha vifo vya watu 310,000 huko Ulaya.” Wataalamu wanahangaishwa hasa na vitu viwili vinavyosababisha uchafuzi huo: gesi zinazoathiri tabaka la ozoni na vitu vilivyo hewani. Vitu hivyo hutokezwa hasa wakati magari, vituo vya nguvu za umeme, na viwanda vinapochoma makaa ya mawe, mafuta, na gesi za asili. Maeneo yaliyoathiriwa zaidi huko Ulaya ni Benelux, likifuatwa na Italia kaskazini na Ulaya Mashariki. Gazeti hilo linaongeza hivi: “Mbali na kudhuru afya ya binadamu, uchafuzi wa hewa huharibu mazingira. Uchafuzi ndio hutokeza asidi katika misitu, maziwa, na mazingira mengine. Ozoni hudhuru mimea nao uchafuzi wa hewa huharibu majengo yaliyo jijini.”

Dayosisi za Katoliki Zimefilisika

Kufikia mwisho wa mwaka wa 2004, dayosisi tatu za Katoliki nchini Marekani zilikuwa zimetangaza kuwa zimefilisika. Zote tatu zililazimika kuchukua hatua hiyo kwa sababu ya kutumia pesa nyingi kugharimia kashfa za ngono zinazohusisha makasisi. Dayosisi kadhaa zimetaja uwezekano wa kutangaza kuwa zimefilisika, lakini dayosisi ya kwanza kufanya hivyo ilikuwa Dayosisi Kuu ya Portland, Oregon, mnamo Julai 2004. Hatua hiyo ilikomesha kesi mbili ambapo wahusika walidai kulipwa jumla ya dola milioni 155 kama malipo ya kutendewa vibaya. Kulingana na National Catholic Reporter, “dayosisi kuu na kampuni za bima tayari zimetumia zaidi ya dola milioni 53 ili kulipa watu zaidi ya 130 waliodai kuwa walitendewa vibaya na makasisi.” Mnamo Septemba 2004, dayosisi ya Tucson, Arizona, ndiyo iliyokuwa dayosisi ya pili kutangaza kuwa imefilisika ili isilipe watu wanaoidai mamilioni ya dola. Dayosisi ya Spokane, Washington, ikawa ya tatu kutangaza hivyo, mnamo Desemba 2004.