Ni Nini Husababisha Ukosefu wa Makao?
Ni Nini Husababisha Ukosefu wa Makao?
“ULIMWENGUNI pote, kuna zaidi ya watu milioni 100 wasio na makao,” linaripoti shirika la Umoja wa Mataifa. Ikiwa idadi hiyo ni sahihi, basi mtu 1 kati ya watu 60 hivi hana makao yanayofaa! Hata hivyo, bado ni vigumu kutambua tatizo hilo limeenea kadiri gani. Kwa nini?
Ukosefu wa makao hufafanuliwa kwa njia tofauti-tofauti katika sehemu mbalimbali za ulimwengu. Mbinu na malengo ya wale ambao huchunguza tatizo hilo huathiri jinsi wanavyolifafanua. Na ufafanuzi wao huathiri takwimu wanazochapisha. Kwa hiyo ni vigumu, au huenda isiwezekane kupata picha kamili ya tatizo hilo.
Kitabu Strategies to Combat Homelessness, kilichochapishwa na Kituo cha Umoja wa Mataifa Kinachoshughulikia Makao, kinafafanua ukosefu wa makao kuwa hali ya “kutokuwa na makao ya kiwango kinachofaa. Hilo linatia ndani kuishi katika hali zinazoonwa kuwa za kiwango cha chini” zikilinganishwa na zile za watu wanaoishi mahali hapo. Huenda watu wasio na makao wakaishi barabarani au kwenye nyumba zilizobomoka au zilizoachwa, huku wengine wakiishi katika makao yanayojengwa na mashirika ya kutoa misaada. Na hata wengine huishi kwa muda mfupi na marafiki. Vyovyote vile, ripoti hiyo inasema: “Kusema kwamba mtu hana makao kunaonyesha kwamba yuko katika hali ambayo ni ‘lazima jambo fulani lifanywe’ ili kumsaidia.”
Inakadiriwa kwamba huko Poland, nchi iliyo na watu milioni 40 hivi, kuna watu wapatao 300,000 wasio na makao. Kwa kweli hakuna anayejua idadi kamili ya watu wasio na makao, kwa kuwa hawajaandikishwa katika eneo lolote hususa na mara kwa mara wao huhamahama. Watu fulani hukadiria kwamba idadi yao hususa inakaribia nusu milioni!
Kwa kuwa tatizo la ukosefu wa makao limeenea sana, huenda ikawa unamjua mtu fulani asiye na makao. Matatizo yanayowakumba watu wasio na makao hutokeza maswali kadhaa. Watu hao walipataje kuwa bila makao yanayofaa? Wao hujiruzuku jinsi gani? Ni nani huwasaidia? Na watu
wasio na makao wana tumaini gani la wakati ujao?Kukosa Makao Mara kwa Mara
Sabrina * ni mama asiye na mwenzi anayeishi katika eneo lenye umaskini huko Harlem, New York City. Aliacha shule alipokuwa katika kidato cha pili. Sabrina anaishi pamoja na watoto wake watatu katika makao ya manispaa kwa ajili ya watu wasio na makao daima. Anaishi katika nyumba yenye chumba kimoja cha kulala pamoja na wavulana wake watatu wenye umri wa miezi kumi, miaka mitatu, na miaka kumi. Jiji hilo huandaa makao kwa ajili ya watu wasio na mahali pazuri pa kuishi.
Sabrina alihama nyumba ya mama yake miaka kumi iliyopita. Tangu wakati huo, ameishi na rafiki yake wa kiume, marafiki wengine na watu wa ukoo, na hali yake ilipozidi kuwa ngumu, aliamua kuishi katika makao ya manispaa. Sabrina anasema: “Mara kwa mara nimefanya kazi, mara nyingi nimesuka watu nywele, lakini kwa muda mrefu nimekuwa nikitegemea msaada wa serikali.”
Kama ilivyosimuliwa katika gazeti Parents, jambo linalotatanisha ni kwamba matatizo ya Sabrina yalianza alipopata kazi nzuri ya kutunza vyumba katika hoteli fulani. Alipokuwa akifanya kazi huko, mshahara aliopata ulifanya asistahili kupata msaada wa serikali lakini pesa hizo hazikutosha kugharimia mahitaji yake, kutia ndani nyumba, chakula, mavazi, usafiri, na mahitaji ya mtoto. Hivyo, ilikuwa vigumu kwake kulipa kodi ya nyumba na mwenye nyumba alijaribu kumfukuza. Mwishowe, Sabrina aliacha kazi yake na akaamua kwenda kuishi katika makao ya muda ya manispaa hadi alipopata makao ya kudumu ya manispaa anapoishi sasa.
Sabrina anasema: “Maisha yamekuwa magumu kwa watoto wangu. Tayari mwana wangu mkubwa amekuwa katika shule tatu tofauti. Anapaswa kuwa katika darasa la tano lakini amerudia darasa moja . . . Tumelazimika kuhama mara nyingi sana.” Sabrina anasubiri kupewa nyumba ya serikali.
Huenda watu ambao hawana mahali popote pa kwenda wakaona hali ya Sabrina kuwa afadhali. Hata hivyo, si watu wote hufurahia kuishi katika makao ya manispaa. Kulingana na Tume ya Poland ya Kusaidia Jamii, wengine “wanaogopa nidhamu na sheria za makao ya manispaa” nao hukataa msaada unaotolewa. Kwa mfano, wale wanaoishi katika makao hayo wanatazamiwa kufanya kazi na kujiepusha na kileo na dawa za kulevya. Si kila mtu anayetaka kutii sheria hizo. Kwa hiyo, ikitegemea majira, watu wasio na makao wanaweza kupatikana wakiwa wamelala katika vituo vya gari-moshi, chini ya ngazi, kwenye ghala zilizo chini ya ardhi, na pia kwenye benchi za bustani,
chini ya madaraja, na kwenye maeneo ya viwandani. Hali kama hizo ziko ulimwenguni pote.Kitabu kimoja kinachozungumzia suala la ukosefu wa makao kinataja mambo mengi yanayochangia tatizo hilo nchini Poland. Yanatia ndani kupoteza kazi, kuwa na madeni, na matatizo ya familia. Kuna ukosefu wa makao kwa wazee, walemavu, na watu walioambukizwa virusi vya UKIMWI. Watu wengi wasio na makao wana matatizo ya akili na ya kimwili au uraibu, hasa wa kileo. Wanawake wengi wamekuwa bila makao baada ya kuwaacha au kuwatoroka waume zao, kufukuzwa nyumbani kwao, au kwa sababu ya ukahaba. Inaonekana kwamba kila mtu asiye na makao amekuwa na maisha yenye kusikitisha.
Watu Walioathiriwa na Hali
Stanisława Golinowska, ambaye ni mtaalamu wa mambo ya kiuchumi na kijamii, anasema: “Hapa [Poland] hakuna mtu ambaye amekosa makao kwa kupenda. . . . Badala yake, hali hiyo imesababishwa na kukosa mafanikio maishani, ambako kumewafanya watu wavurugike akili na kukata tamaa ya kuishi.” Inaonekana kwamba watu ambao kwa sababu fulani hawawezi kutatua matatizo yao hujikuta bila makao. Kwa mfano, wengine wameachiliwa kutoka gerezani na kupata nyumba zao zimeporwa. Wengine wamefukuzwa. Wengi wamepoteza makao kwa sababu ya misiba ya asili. *
Uchunguzi mmoja ulionyesha kwamba karibu nusu ya watu wasio na makao nchini Poland wakati mmoja walikuwa na familia na waliishi na wenzi wao, ingawa mara nyingi familia hizo zilikuwa na matatizo. Wengi wao walifukuzwa kutoka nyumbani au walilazimika kuhama kwa sababu ya hali ngumu sana. Ni asilimia 14 pekee walioamua kuondoka.
Baada ya kuishi katika makao ya manispaa kwa muda fulani, wengine huweza kujiruzuku tena na kujipatia makao. Kwa wengine, inakuwa vigumu sana kutatua tatizo hilo. Labda watu hao huwa bila makao daima kwa sababu ya ugonjwa wa akili au wa kimwili, kutumia vibaya kileo au dawa za kulevya, kutokuwa na kichocheo cha kufanya kazi, mazoea mabaya ya kazi, kukosa elimu ya kutosha, au mchanganyiko wa mambo
hayo. Nchini Marekani, asilimia 30 hivi ya watu wasio na makao wameshindwa kujiepusha na kile ambacho shirika moja lisilojipatia faida huita “mfumo wa kutokuwa na makao,” yaani, wakati fulani wanakuwa katika makao ya manispaa, wakati mwingine wako hospitalini, na kwa kusikitisha, nyakati nyingine wanakuwa gerezani. Inasemekana kwamba wale ambao hawawezi kujitoa katika hali hiyo hutumia karibu asilimia 90 ya mapato ya kitaifa yaliyotengwa ili kukabiliana na tatizo la ukosefu wa makao.Msaada kwa Wasio na Makao
Makao fulani ya manispaa hutoa huduma zinazokusudiwa kuwasaidia watu wasio na makao waache kuishi hivyo. Watu hao wanaweza kusaidiwa kupata msaada wa serikali, msaada wa kifedha kutoka kwa mashirika mengine, msaada wa kisheria, kusaidiwa wasitawishe tena uhusiano na familia, au kupewa nafasi za kujifunza ufundi fulani. Makao ya vijana huko London hutoa mashauri kuhusu vyakula, upishi, maisha bora, na jinsi ya kupata kazi. Mashauri hayo yamekusudiwa kufanya watu wajiheshimu zaidi na kuwachochea na kuwasaidia waweze kujitegemea zaidi ili wawe na makao yao wenyewe. Bila shaka, vituo hivyo vinastahili sifa kwa ajili ya maandalizi hayo.
Hata hivyo, si nyakati zote makao ya manispaa huwapa wasio na makao msaada wanaohitaji hasa. Jacek, mmoja wa watu wasio na makao huko Warsaw, anaeleza kwamba maisha katika makao hayo hayamtayarishi mtu kukabiliana na ulimwengu. Anahisi kwamba kwa sababu ya kushirikiana na kuzungumza wao kwa wao tu, watu wanaoishi katika makao hayo huanza “kufikiri kwa njia iliyopotoka.” Anasema, “Makao ambayo hututenga na watu wengine hufanya watu wazima waanze kufikiri kama watoto.” Yeye anaona kwamba ‘akili za wakazi wengi hazifanyi kazi vizuri.’
Uchunguzi mmoja uliofanywa Poland unaonyesha kwamba upweke ndio tatizo baya zaidi kwa watu wasio na makao. Kwa sababu ya matatizo ya kiuchumi na kuonwa kuwa watu wa hali ya chini katika jamii,
watu wasio na makao huwa na mwelekeo wa kujiona kuwa hawafai. Wengine huanza kutumia kileo. Jacek anasema, “Kwa sababu ya kutokuwa na tumaini kwamba hali itabadilika, wengi wetu huanza kukosa uhakika kwamba tunaweza kufanya jambo fulani ili kuboresha hali yetu ngumu.” Wao huaibikia sura yao, umaskini wao na kutoweza kujisaidia, na kwamba hawana makao.Francis Jegede, mtaalamu wa masuala ya ongezeko la watu anasema: “Iwe tunazungumza kuhusu watu wanaoishi kando ya barabara huko Bombay [Mumbai] na Calcutta au watu wachafu wanaolala katika barabara za London, au Watoto wa Mitaani wa Brazili, tatizo la watu wasio na makao ni kubwa mno na lenye kuhuzunisha sana hasa iwapo utakabiliana nalo.” Kisha anaongeza hivi: “Hata iwe tatizo hilo linasababishwa na nini, swali ambalo mtu hujiuliza ni kwamba inakuwaje ulimwengu ulio na utajiri, hekima, na uwezo wa kiteknolojia hauwezi kutatua tatizo la ukosefu wa makao?”
Ni wazi kwamba watu wote wasio na makao wanahitaji msaada, na si msaada wa kimwili tu bali msaada ambao unaweza kuwafariji na kuwatia moyo. Msaada huo unaweza kuwapa watu nguvu za kukabiliana na matatizo mengi yanayosababisha ukosefu wa makao. Lakini watu wasio na makao wanaweza kupata wapi msaada kama huo? Na kuna tumaini gani kwamba tatizo la ukosefu wa makao litakomeshwa?
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 8 Majina fulani katika makala hii yamebadilishwa.
^ fu. 15 Pia mamilioni ya watu ulimwenguni wamelazimika kukimbia nyumba zao kwa sababu ya misukosuko ya kisiasa au vita. Ikiwa ungependa kusoma kuhusu hali yao, tafadhali ona makala zenye kichwa “Je, Wakimbizi Watapata Makao ya Kudumu?” zilizochapishwa katika toleo la Amkeni! la Januari 22, 2002.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 6]
Matokeo ya Ufukara
Mamia ya maelfu ya watu wanaishi kwenye barabara za majiji ya India. Makadirio ya awali yanaonyesha kwamba watu 250,000 hivi huishi kando ya barabara katika jiji la Mumbai pekee. Makao yao yamejengwa kwa chandarua iliyofungwa kwenye miti na majengo yaliyo karibu. Kwa nini wanaishi hapa badala ya kuishi katika nyumba za bei ya chini karibu na vitongoji vya jiji? Kwa sababu wao ni wafanyabiashara wa rejareja, wachuuzi, waendesha-mikokoteni, au watu wanaookota mikebe na chupa karibu na jiji. Kichapo Strategies to Combat Homelessness kinasema: “Hawana la kufanya. Kwa sababu ya umaskini hawana pesa za kulipa kodi ya nyumba, wana pesa za chakula tu.”
Wanaume, wanawake, na watoto wapatao 2,300 huishi katika Kituo cha Gari-Moshi cha Park, huko Johannesburg, Afrika Kusini. Wao hulala kwenye sehemu iliyoinuka kando ya njia ya reli, wakilalia matambara ya blanketi au katoni. Wengi wao hawana kazi na hawana matumaini ya kupata kazi. Maelfu ya watu wanaishi katika hali kama hizo kotekote jijini. Hawana maji, vyoo, na umeme. Magonjwa huenea sana katika hali kama hizo.
Vikundi hivyo viwili vya watu na wengine kama wao hawana makao kwa sababu ya ufukara.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 7]
Kasoro za Jamii ya Kisasa
Kitabu Strategies to Combat Homelessness, kilichochapishwa na Kituo cha Umoja wa Mataifa Kinachoshughulikia Makao, kinataja kasoro kadhaa za mfumo wa sasa wa kijamii, kisiasa, na kiuchumi katika kuandalia watu wote makao. Baadhi ya kasoro hizo ni:
● “Tatizo kuu kuhusiana na ukosefu wa makao bado ni kwamba serikali zimeshindwa kutoa rasilimali za kutosha kutimiza haki ya kila mtu ya kuwa na makao mazuri.”
● “Kuwepo kwa vizuizi visivyofaa na kutopanga mambo ifaavyo kunaweza . . . kuvuruga mipango ya kuandalia maskini walio wengi makao.”
● “Ukosefu wa makao huonyesha kwamba pesa ambazo serikali hutoa kwa ajili ya makao au kodi hazigawanywi vizuri.”
● “Tatizo la ukosefu wa makao hutokea kwa sababu sera nyingi zimepuuza au hazikuzingatia madhara ya mabadiliko ya kiuchumi, ukosefu wa nyumba za bei nafuu, kuongezeka kwa matumizi mabaya ya dawa za kulevya, na matatizo mengine ya kimwili na kiakili ambayo huwapata wale wanaoweza kuathiriwa kwa urahisi zaidi . . . katika jamii.”
● “Kuna uhitaji mkubwa wa kurekebisha jinsi ya kuwazoeza wataalamu ambao hushughulika na watu dhaifu wanaoweza kuathiriwa kwa urahisi. Badala ya kuwaona watu wasio na makao, hasa watoto wa mitaani, kama mzigo kwa jamii, wanapaswa kuonwa kuwa watu wanaoweza kufaidi jamii.”
[Picha]
Mama anaomba-omba pamoja na binti zake wawili, Mexico
[Hisani]
© Mark Henley/ Panos Pictures
[Picha katika ukurasa wa 6]
Kituo kimoja cha gari-moshi huko Pretoria, Afrika Kusini kiligeuzwa kuwa nyumba za watu wasio na makao
[Hisani]
© Dieter Telemans/Panos Pictures
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 4]
Left: © Gerd Ludwig/Visum/Panos Pictures; inset: © Mikkel Ostergaard/Panos Pictures; right: © Mark Henley/Panos Pictures