Njoo tukavune Uyoga!
Njoo tukavune Uyoga!
Na mwandishi wa Amkeni! katika Jamhuri ya Cheki
HUENDA umefurahia kuila mara nyingi sana, labda kwenye piza au katika saladi, supu, au mchuzi. Au labda umevutiwa na umbo lake la ajabu, ambalo huwavutia wasanii wengi wanaochora picha za watoto. Lakini je, umewahi kujiuliza uyoga ni nini hasa? Ni nini hufanya ikue? Ni nani huvuna uyoga, nao hufanyaje hivyo? Hebu tuchunguze.
Kwa kawaida, ni rahisi kutambua uyoga. Haina majani, maua, au rangi ya kijani-kibichi. Kwa hiyo, mara nyingi uyoga huonekana waziwazi katika mazingira ya kijani-kibichi. Aina nyingi za uyoga huwa na kofia kubwa juu ya shina. Lakini uyoga huwa na maumbo na rangi mbalimbali. Hata kuna aina fulani za uyoga ambazo hung’aa gizani. Uyoga ni kuvu ya aina fulani. Lakini kuna aina nyingi za kuvu ambazo si uyoga zinazosemekana kuwa ni za jamii ya uyoga. Kwa mfano, kuna kuvu wanaofanana na matumbawe. Jamii nyingine ambazo hukua kwenye miti hufanana na rafu ndogo za vitabu.
Uyoga Ni Nini?
Kwa muda mrefu, wanasayansi waliamini kwamba uyoga ni mmea wa pekee na wa ajabu. Siku hizi, wanabiolojia wengi husema kwamba uyoga ni kuvu ya hali ya juu. Wao husema kwamba uyoga ni vijiumbe vinavyojitegemea, kwani umbo lake, ukuzi, na njia ya kupata chakula ni za ajabu. Aina nyingi za uyoga zinaweza kuliwa, na nyingine hata ni dawa. Hata hivyo, nyingine hulevya au ni sumu. Jina la kisayansi la uyoga ni Mycota au Mycetes.
Uyoga Hustaajabisha
Uyoga huzaanaje? Jambo hilo liliwatatanisha wanasayansi kwa muda mrefu. Leo, inajulikana kwamba uyoga uliokomaa hutoa mbegu ndogo sana ambazo husambazwa na upepo. Zinapokuwa udongoni mbegu hizo hujibadili kuwa wavu mzito wa nyuzi nyembamba zinazoitwa mycelium. Sehemu ya juu ya uyoga huota kutokana na wavu huo. Hiyo ndiyo sehemu ambayo huonekana na kuvunwa.
Ili iendelee kuwa hai, uyoga huhitaji aina nyingi za mbolea. Kwa hiyo, uyoga hukua katika maeneo ya asili kama vile msituni, bustanini, na kwenye nyasi. Uyoga hula miti yenye ugonjwa au iliyokufa, na hivyo kutimiza fungu muhimu katika kusafisha misitu. Kwa kula mabaki ya mimea, majani, na vijiti, uyoga hutokeza mbolea ya asili na hivyo kuboresha udongo. Aina fulani za uyoga hushirikiana na miti yenye afya; wavu uliotokezwa na mbegu zake hufyonza maji na madini kwenye udongo na kueneza kiasi fulani kwenye mmea. Mmea nao hulipa kwa kulisha uyoga.
Uyoga huhitaji pia unyevu na joto. Hiyo ndiyo sababu uyoga hutokea kwa wingi baada ya mvua ya kiangazi. Chini ya hali nzuri aina fulani za uyoga hukomaa kabisa kwa usiku mmoja. Jamii moja ya uyoga inahitaji siku 10 au 14 tu kuwa na kofia yenye kipenyo cha sentimeta 50. Jamii nyingine huishi kwa muda mrefu ajabu. Wavu ambao hutokeza uyoga unaweza kudumu kwa karne nyingi. Kulingana na habari fulani, kuvu ambazo hutokeza kuvumwani zinaweza kuishi kwa miaka 600 hivi.
Jambo moja lenye kupendeza kuhusu jamii fulani za uyoga, kwa mfano truflle, ni harufu yake kali. Hiyo ndiyo sababu mbwa wanaweza kunusa harufu yake umbali wa meta sita hivi, ingawa aina hiyo ya uyoga hukua chini ya ardhi. *
Uyoga Huvunwa na Nani?
Kwa karne nyingi, watu katika sehemu mbalimbali wamevuna uyoga. Leo, katika sehemu fulani za Ulaya Magharibi na Amerika Kaskazini, uyoga huvunwa hasa na wataalamu ambao huwauzia wafanyabiashara. Tofauti na hilo, kuvuna uyoga ni desturi maarufu
huko Ulaya ya Kati na Mashariki. Watu wanaoishi mjini hupendezwa kuvuna uyoga kama tu wale wa mashambani. Wakazi wengi wa jijini hupenda kutumia miisho-juma wakivuna uyoga msituni. Wao hufanya hivyo ili wapumzishe mwili na akili na pia kuboresha milo yao. Watu huvunaje uyoga?Wavunaji huanza asubuhi na mapema, wakati uyoga bado una unyevu. Wanapotembea polepole msituni, wao hutafuta uyoga katika nyasi, kuvumwani, au miti. Wao huvalia mavazi yanayofaa kazi ya shambani na viatu vigumu, na kubeba koti ambalo wanaweza kutumia iwapo kutanyesha. Wavunaji huheshimu mazingira na hivyo wao hujitahidi wasiyaharibu, au hata wasipige kelele zinazoweza kusumbua wanyama.
Tazama! Mvunaji amepata uyoga. Anainama na bila kuugusa, anachunguza ikiwa unaweza kuliwa. Yeye huvuna uyoga uliokomaa kwani ndio tu anaoweza kuwa na hakika ni wa jamii gani. Baada ya kuhakikisha jamii yake, anauchuma kwa uangalifu akiwa ameshika shina lake, na si sehemu ya juu. Mara moja anaondoa udongo wote na kukata sehemu yoyote iliyoliwa na minyoo au kuharibika. Anafunika sehemu aliyokata kwa kuvumwani au udongo. Anatia uyoga safi ndani ya kikapu chake. Haweki uyoga ndani ya karatasi za plastiki au kontena kwa sababu utaanza kuchacha na kuharibika kabla ya kuufikisha nyumbani.
Pia inafurahisha kuvuna uyoga mkiwa kikundi. Mhudumu mmoja Mkristo anasema hivi: “Kwanza sisi huenda katika huduma tukiwa kikundi, lakini tunapomaliza sisi hupenda kuwa pamoja na kufurahia ushirika mzuri. Nyakati nyingine sisi huelekea kwenye kichaka kilicho karibu na kuvuna uyoga pamoja. Tunapoutafuta, sisi husimuliana mambo tuliyoona katika huduma na kujifurahisha.”
Kutayarisha Uyoga
Uyoga hutumiwa kwa njia mbalimbali katika upishi. Aina fulani ni tamu na zinaweza kuwa sehemu muhimu ya mlo. Kwa mfano, watu wengi hupenda kukaanga sehemu ya juu ya uyoga aina ya portobello kama nyama au kukaanga aina nyingine ya uyoga kwa mboga. Aina fulani za uyoga zenye vikolezo zinaweza kutumiwa kuongeza ladha kwenye milo mbalimbali. Uyoga ukikaushwa vizuri kwa kutumia joto, unaweza kuliwa kama chakula cha kumsaidia mtu kupunguza uzito. Watu hupenda aina fulani za uyoga kwa sababu ya protini, vitamini, na madini yake.
Uyoga huharibika haraka. Kwa hiyo, unahitaji kutayarishwa siku ileile unapovunwa. Kulingana na wataalamu, uyoga unaoweza kuliwa unaweza kuwa sumu ukihifadhiwa vibaya. Ikiwa hutaki kula uyoga mara moja, unaweza kuukausha au kuuchemsha. Hivyo unaweza kutumia uyoga mwaka mzima kukoleza chakula chako. Unaweza kupata habari zaidi katika vitabu vinavyozungumza kuhusu kuvuna uyoga.
Uwe Mwangalifu
Ikiwa hujawahi kuvuna uyoga na ungependa kujaribu, ni muhimu sana kwanza ufanye utafiti kwa makini. Chunguza katika eneo lako ni aina gani za uyoga unaoweza kuliwa na zile zenye sumu. Jifunze jinsi ya kuzitambua. Huenda ukapenda pia kuzungumza na wataalamu fulani. Usivune uyoga kwa sababu tu ni maridadi au unanukia vizuri. Ikiwa huna uhakika uyoga fulani ni wa jamii gani, usiuvune! Uyoga mmoja tu wenye sumu unaweza kuharibu mlo wote, na hata uwe hatari. Ukipatwa na kichefuchefu au uanze kuumwa na kichwa baada ya kula uyoga, mwone daktari mara moja.
Iwe utajaribu kuvuna uyoga au la, unaweza kufurahia umaridadi wake. Huenda kufanya hivyo kukakukumbusha kwamba uumbaji huo muhimu wenye kutatanisha, na kushangaza haukujitokeza wenyewe. Kama tu maajabu mengine ya ulimwengu wa asili, uyoga huonyesha kwamba kuna Muumba mwenye hekima na upendo.—Mwanzo 1:11-13; Zaburi 104:24.
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 11 Mbwa na nguruwe waliozoezwa vizuri hutumiwa kutafuta aina hiyo ya uyoga. Truflle huuzwa kwa bei ghali sana inapolinganishwa na uyoga wa kawaida.
[Picha katika ukurasa wa 26]
Morel
[Picha katika ukurasa wa 26]
Shiitake
[Picha katika ukurasa wa 26]
Portobello
[Picha katika ukurasa wa 26]
Cremini