Kuutazama Ulimwengu
Kuutazama Ulimwengu
Mnyama Anayependwa Zaidi Ulimwenguni
Gazeti The Independent la London linaripoti kwamba “huenda mbwa ndiye rafiki mkubwa zaidi wa binadamu, hata hivyo, simbamarara ndiye mnyama anayependwa zaidi ulimwenguni.” Baada ya mfululizo wa sinema zilizoonyesha wanyama kumi, katika kura iliyopigwa na watu zaidi ya 52,000 kutoka nchi 73, simbamarara alimshinda mbwa kwa kura 17 tu. Nafasi ya tatu ilichukuliwa na pomboo, kisha farasi, simba, nyoka, tembo, sokwe, orangutangu, na nyangumi. Mtaalamu wa kuchunguza tabia za wanyama Dakt. Candy d’Sa alisema kwamba wanadamu “wanaweza kupendezwa na simbamarara, kwa kuwa mnyama huyo ni mkali na mkubwa kwa kuonekana, lakini ana sifa zenye kuvutia na utambuzi. Tofauti naye, mbwa ni mnyama mwaminifu na mwenye heshima naye hufanya watu wawe wenye urafiki zaidi na wawasiliane.” Wahifadhi-mazingira walifurahia ushindi wa simbamarara. Callum Rankine, wa Hazina ya Mazingira Ulimwenguni Pote, alisema hivi: “Ikiwa watu wanampigia kura simbamarara kuwa mnyama wanayempenda zaidi, inamaanisha kwamba wanatambua kuwa yeye ni muhimu, na ninatumaini kwamba watahakikisha anaendelea kuwapo.” Inakadiriwa kwamba kuna simbamarara 5,000 pekee porini.
Bakteria Zilizo Mdomoni na Afya
Gazeti Science linasema: “Mdomo ni sehemu yenye kutatanisha. Kwa miaka zaidi ya 40, wanabiolojia wa kuchunguza kinywa wamekuwa wakichunguza bakteria nyingi zinazoishi kwenye meno, fizi, na ulimi.” Kwa muda fulani wanabiolojia wamefahamu kwamba kwa kawaida bakteria zilizo mdomoni zinaweza kuhama na kusababisha madhara katika sehemu nyingine za mwili. Tayari matatizo ya moyo yamehusianishwa na bakteria za mdomoni, na uchunguzi unaonyesha kwamba bakteria nyingine hufanya watoto wazaliwe kabla ya wakati. Kwa kweli, bakteria mbaya hutokeza madhara moja kwa moja. Zinapoungana na kushinda bakteria nzuri mdomoni, zinasababisha matundu, fizi kuvuja damu, na harufu mbaya. “Watu 3 kati ya 10 walio na umri unaozidi miaka 65 wamepoteza meno yao yote,” inasema ripoti hiyo. “Nchini Marekani, asilimia 50 ya watu wazima wana ugonjwa wa fizi ama meno yao yameoza.” Kwa kuchunguza bakteria hizo, watafiti wanatumaini kwamba watajifunza jinsi ya kutengeneza “dawa za kusafisha mdomo ambazo huua tu bakteria mbaya za mdomoni badala ya kuua bakteria nzuri pamoja na zile mbaya.”
Mazoea ya Kulala
“Kulingana na uchunguzi uliofanywa ulimwenguni pote kuhusu mazoea ya watu ya kulala, watu huko Asia hulala wakiwa wamechelewa sana kuliko watu wa Amerika na wa Ulaya nao huamka mapema zaidi,” linaripoti shirika la habari la Aljazeera. Zaidi ya watu 14,000 katika nchi 28 waliulizwa wakati ambao wao huenda kulala na wakati ambao wao huamka. Nchini Ureno, watu 3 kati ya 4 hulala baada ya saa sita za usiku. Watu wa Asia ndio huamka mapema zaidi, wakiongozwa na watu wa Indonesia “ambao asilimia 91 walisema kwamba wao huwa wameamka kufikia saa 1 asubuhi.” Wajapani ndio hulala saa chache zaidi. Zaidi ya asilimia 40 ya Wajapani hulala kwa muda wa saa sita hivi kila usiku. Waaustralia ndio hulala muda mrefu zaidi. Waaustralia wengi hulala kabla ya saa 4 usiku, lakini karibu mtu 1 kati ya 3 alisema kwamba yeye hulala kwa wastani wa zaidi ya saa 9 kila usiku.
Acha Kuvuta Sigara Sasa!
“Asilimia 50 hadi asilimia 66 hivi ya wavutaji-sigara sugu hatimaye watakufa kwa sababu ya zoea hilo,” inasema ripoti moja ya jarida la kitiba la Uingereza BMJ. Watafiti waligundua kwamba kuvuta sigara ni hatari sana kuliko walivyofikiri hapo awali na pia zoea hilo lilibatilisha manufaa yoyote ambayo mvutaji-sigara “angepata miaka 50 iliyopita.” Ingawa uchunguzi huo ulionyesha kwamba watu wenye umri wa miaka 70 ambao hawajawahi kuvuta sigara wana uwezekano wa asilimia 33 wa kufikisha umri wa miaka 90, uwezekano huo kwa wavutaji-sigara ulipungua kutoka asilimia 10 hadi 7. “Kwa wastani, wavutaji-sigara hufa miaka 10 hivi mapema kuliko watu wasiovuta sigara,” inasema makala hiyo, na kuacha zoea hilo kunaweza kurefusha maisha ya mtu. Mtu hupata manufaa anapoacha kuvuta sigara mapema zaidi. Iligunduliwa kwamba watu wenye umri wa miaka 50 walipunguza madhara ya kuvuta sigara kwa asilimia 50, na wale walioacha kuvuta sigara wakiwa na umri wa miaka 30 wangeweza kuepuka karibu madhara yote ya kuvuta sigara.
Ukosefu wa Ujuzi wa Biblia
Kura iliyopigwa hivi karibuni huko Uingereza kwenye Intaneti ambayo ilitayarishwa na kampuni ya kusimamia kura ya YouGov “iligundua kwamba zaidi ya asilimia 25 ya wale waliopiga kura hawakujua kwamba Yesu Kristo alizaliwa Bethlehemu,” linasema gazeti la London The Guardian. “Na ni asilimia 75 tu waliojua kwamba Yesu alikuwa Myahudi.” Walipohojiwa kuhusu zile Amri Kumi, karibu nusu ya wale waliofanyiwa uchunguzi huo walihisi kwamba amri ya sita inayosema, “Usiue,” ndiyo inayohusu hasa hali za sasa. Amri iliyoonwa kuwa si muhimu wakati wetu ni ile ya kwanza, ambayo katika Tafsiri ya Ulimwengu Mpya inasema: “Mimi ni Yehova Mungu wako . . . Usiwe na miungu mingine yoyote dhidi ya uso wangu.”—Kutoka 20:2, 3.
Kupungua kwa Rasilimali za Dunia
“Thuluthi mbili za rasilimali za dunia, kama vile nishati, maji na hewa safi zimepungua sana au kuchafuliwa,” linaripoti gazeti Daily News la New York. Uchunguzi mmoja, “uliotayarishwa na wataalamu 1,360 kutoka mataifa 95,” ulitaja madhara ambayo yamesababishwa na wanadamu kwenye mazingira katika miaka 50 iliyopita. “Utendaji wa wanadamu unadhuru sana utendaji wa asili wa Dunia hivi kwamba hatuwezi kuwa na uhakika kwamba mifumo yake ya ikolojia itaweza kutegemeza vizazi vijavyo,” ripoti hiyo ilimalizia kusema. Ikiungwa mkono na UM na Benki ya Dunia, ripoti hiyo ilionya kwamba baada ya muda, mifumo ya asili itaacha kutenda na hivyo kusababisha kuharibiwa kwa misitu, magonjwa, au bahari zisizokuwa na viumbe hai.
Kukumbatia Watoto
“Watoto wanaokumbatiwa hulala kwa muda mrefu zaidi, hupumua vizuri na kuongeza uzito haraka zaidi,” linasema gazeti la Japani Daily Yomiuri. Mbinu hiyo inahusisha akina mama au baba kulala kitandani wakiwa vifua wazi na kuwakumbatia watoto wao kwa saa moja au mbili kila siku. Toyoko Watanabe, mkuu wa idara ya vitoto kwenye Hospitali Kuu ya Bokuto huko Tokyo, alisema: “Mbinu ya wazazi kukumbatia watoto wakiwa kifua wazi ilianza Kolombia kwa sababu ya upungufu wa vifaa vya kupasha vitoto joto. Shirika la Hazina ya Watoto ya Umoja wa Mataifa lilitambua kwamba idadi ya vifo vya vitoto vilivyozaliwa kabla ya wakati ilipungua, navyo vilikaa hospitalini kwa muda mfupi zaidi.” Gazeti hilo linasema kwamba sasa, “mbinu hiyo inatumiwa sana katika nchi zilizositawi kwa ajili ya vitoto vilivyozaliwa kabla ya wakati na vile vilivyozaliwa katika muda wa kawaida.” Kuna manufaa mengi kama vile mzazi kuwa na uhusiano wa karibu na kitoto chake wakati ngozi yake inapogusana na ya kitoto. Isitoshe, mbinu hiyo haigharimu chochote na haihitaji kifaa maalumu.