Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Mambo Tunayojua Sasa Kuhusu Homa

Mambo Tunayojua Sasa Kuhusu Homa

Mambo Tunayojua Sasa Kuhusu Homa

NI MWAKA wa 1997. Mwanasayansi ameketi katika kijiji kidogo cha Waeskimo cha Brevig kwenye nyika yenye barafu ya Peninsula ya Seward huko Alaska. Mbele yake kuna mwili wa mwanamke kijana ambaye mwanasayansi huyo na Waeskimo wanne walifukua kutoka kwenye barafu. Alikufa kwa homa mwaka wa 1918 na mwili wake ulioganda umekuwa mahali hapo tangu wakati huo.

Kuna manufaa gani ya kuchunguza mwili wake sasa? Wanasayansi wanatumaini kwamba kitu kilichosababisha homa hiyo kingali mapafuni mwake na kwamba kwa kutumia mbinu ya hali ya juu ya kuchunguza chembe za urithi wataweza kukitenga, kukichunguza, na kukitambulisha. Kwa nini ujuzi huo utakuwa wenye manufaa? Ili kujibu swali hilo, tunahitaji kuelewa vizuri zaidi jinsi ambavyo virusi hufanya kazi na ni nini hufanya viwe hatari sana.

Virusi Vinavyoweza Kuwa Hatari

Leo tunajua kwamba homa husababishwa na virusi na kwamba inaweza kuenezwa kutoka mtu mmoja hadi mwingine kwa kukohoa, kupiga chafya, na kuzungumza. Homa iko kila mahali ulimwenguni hata katika nchi za Tropiki, ambako inaweza kutokea mwaka mzima. Katika nchi zilizo kaskazini mwa ikweta, msimu wa homa huanza Novemba hadi Machi; na katika nchi zilizo kusini mwa ikweta, msimu huo huanza Aprili hadi Septemba.

Virusi aina ya A vinavyosababisha homa ambavyo ndivyo hatari zaidi, ni vidogo vinapolinganishwa na virusi vingi. Kwa kawaida vina umbo la mviringo na vina vitu fulani vilivyochomoza. Virusi hivyo vinaposhambulia chembe ya mwanadamu, huzaana haraka sana hivi kwamba kwa muda wa saa kumi hivi, kati ya “nakala” mpya 100,000 na milioni moja za virusi vya homa hulipuka kutoka kwenye chembe hiyo.

Jambo linaloogopesha kuhusu virusi hivyo ni kwamba vinaweza kubadilika haraka. Kwa kuwa virusi hivyo huzaana haraka sana (haraka zaidi kuliko virusi vya HIV), “nakala” zake nyingi hazifanani kabisa. Nyingine ni tofauti sana hivi kwamba hazitambuliwi na mfumo wa kinga. Kwa sababu hiyo, kila mwaka sisi hushambuliwa na virusi tofauti vya homa vyenye antijeni tofauti na hilo hufanya iwe vigumu kwa mfumo wetu wa kinga kuvitambua na kuvishambulia. Ikiwa antijeni hizo zitabadilika mara nyingi, mfumo wetu wa kinga hautakuwa na uwezo wa kujikinga na kuna hatari ya homa hiyo kuenea ulimwenguni pote.

Isitoshe, wanyama pia huambukizwa virusi vya homa na jambo hilo hutokeza tatizo kwa wanadamu. Inaaminika kwamba nguruwe huwa na virusi ambavyo huambukizwa ndege kama vile kuku na mabata. Lakini anaweza pia kuwa na virusi vingine vinavyoambukizwa wanadamu.

Kwa hiyo, nguruwe akiambukizwa aina mbili za virusi, yaani virusi vinavyoambukizwa wanyama na vile vinavyoambukizwa wanadamu, chembe za urithi za virusi hivyo zinaweza kuchanganyika. Hilo linaweza kutokeza virusi vipya vya homa visivyo na kinga. Watu fulani hufikiri kwamba wakulima ambao hufuga kuku na nguruwe, kama huko barani Asia, wanaweza kuambukizwa virusi vipya vya homa.

Kwa Nini Homa Hiyo Ilienea Sana?

Swali ni, Ni nini kilichosababisha virusi vya homa ya 1918-1919 vigeuke na kuwa virusi vilivyosababisha nimonia iliyoua vijana wengi sana? Ingawa virusi hivyo havipo tena, kwa muda mrefu wanasayansi wamehisi kwamba ikiwa wangeweza kupata virusi hivyo vikiwa vimegandishwa, wangeweza kutenganisha RNA zake zikiwa nzima na kugundua kilichofanya ziwe hatari hivyo. Kwa kweli, kwa kiwango fulani wamefaulu kufanya hivyo.

Mwili ulioganda ambao ulipatikana huko Alaska, uliotajwa mwanzoni mwa makala hii, umesaidia kikundi cha wanasayansi kutambua na kuona muungano wa chembe za urithi za virusi vilivyosababisha homa ya 1918-1919. Hata hivyo, bado wanasayansi hawajagundua ni nini kilichofanya homa hiyo iue watu wengi sana. Inaonekana kwamba virusi hivyo vinafanana na virusi vya homa ambavyo huambukiza nguruwe na ndege.

Je, Vitarudi Tena?

Kulingana na wataalamu wengi, swali, si ikiwa virusi hivyo vya homa yenye kuua vitarudi bali ni vitarudi lini na jinsi gani? Kwa kweli, wataalamu fulani wanatarajia kulipuka kwa aina mpya kabisa ya virusi vya homa kila baada ya miaka 11 hivi na homa mbaya sana baada ya kila miaka 30. Kulingana na utabiri huo, huenda tauni nyingine ikatokea hivi karibuni.

Jarida la kitiba Vaccine liliripoti hivi katika mwaka wa 2003: “Miaka 35 imepita tangu kutokea kwa tauni ya homa ulimwenguni, na kipindi kirefu zaidi kuwahi kurekodiwa kati ya tauni moja hadi nyingine ni miaka 39.” Makala hiyo iliendelea kusema: “Virusi hivyo vinaweza kutokea China au katika nchi iliyo karibu nayo na vinaweza kutia ndani antijeni au maambukizo mabaya yanayotokana na virusi vya homa ya wanyama.”

Makala hiyo ya jarida Vaccine ilitabiri hivi kuhusu virusi hivyo: “Vitaenea haraka ulimwenguni pote. Kutakuwa na milipuko kadhaa ya maambukizo. Virusi hivyo vitaenea haraka na kotekote, na watu wa kila umri wataambukizwa, navyo vitavuruga utendaji wa kijamii na kiuchumi katika nchi zote. Watu wengi sana wa karibu kila umri watakufa. Inaelekea kwamba vituo vya afya hata katika nchi zilizoendelea kiuchumi havitaweza kukabiliana ifaavyo na mahitaji ya afya.”

Hali hiyo ni mbaya kadiri gani? John M. Barry, mwandishi wa kitabu The Great Influenza, anatoa maoni haya: “Gaidi mwenye silaha ya nyuklia ni tisho kwa kila mwanasiasa. Tauni mpya ya homa inapaswa kuonwa kuwa tisho kama hilo.”

Kuna Matibabu Gani?

Huenda ukajiuliza, ‘Je, leo kuna matibabu yanayofanya kazi?’ Jibu la swali hilo linahusisha habari nzuri na mbaya. Dawa zinazoua vijasumu zinaweza kupunguza vifo vinavyosababishwa na nimonia inayotokea baada ya mtu kuambukizwa homa mara ya kwanza, na dawa fulani zinaweza kuua aina fulani ya virusi vya homa. Kuna chanjo zinazoweza kusaidia kupigana na virusi vya homa ikiwa aina hususa ya virusi inatambuliwa na ikiwa chanjo yake inaweza kutokezwa kwa wakati unaofaa. Hizo ndizo habari nzuri. Vipi habari mbaya?

Chanjo ya homa, kuanzia chanjo ambayo haikufanikiwa wakati wa mlipuko wa homa ya nguruwe mwaka wa 1976 hadi upungufu wa chanjo wa mwaka wa 2004, imekuwa na sifa mbaya. Hata ingawa sayansi ya tiba imepiga hatua kubwa tangu Vita vya Kwanza vya Ulimwengu, bado madaktari hawajapata tiba ya virusi vyenye nguvu.

Kwa hiyo, swali linalofadhaisha ni: Je, tauni ya mwaka wa 1918-1919 inaweza kutokea tena? Ona maoni yaliyochapishwa na Taasisi ya Kitaifa ya Utafiti wa Kitiba ya London: “Katika njia fulani, hali za leo zinafanana na hali zilizokuwapo mwaka wa 1918: watu wengi sana wanasafiri kutoka nchi moja hadi nyingine kwa sababu ya kuboreshwa kwa njia za usafiri, kuna maeneo mengi yenye vita na matatizo ya utapiamlo na ukosefu wa usafi, idadi ya watu ulimwenguni imeongezeka kufikia bilioni sita na nusu na idadi kubwa ya watu hao wanaishi mijini nayo miji mingi haina mifumo mizuri ya kuondoa maji machafu na takataka.”

Mtaalamu mashuhuri kutoka Marekani anakata kauli hivi: “Kwa ufupi, kila mwaka tunakaribia zaidi tauni nyingine.” Hata hivyo, je, hiyo inamaanisha kwamba hakuna tumaini lolote la wakati ujao? La!

[Picha katika ukurasa wa 8]

Virusi vipya vya homa vinaweza kutokea katika jamii za wafugaji

[Hisani]

BAY ISMOYO/AFP/Getty Images

[Picha katika ukurasa wa 8, 9]

Virusi aina ya A vya homa

[Hisani]

© Science Source/ Photo Researchers, Inc

[Picha katika ukurasa wa 9]

Watafiti wamechunguza virusi vya homa ya 1918-1919

[Hisani]

© TOUHIG SION/CORBIS SYGMA