Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Mnamo mwaka wa 2000, watu milioni 8.3 hivi walipatwa na kifua kikuu ulimwenguni pote, na karibu milioni mbili kati yao walikufa. Karibu wote walitoka nchi maskini.—MEDICAL JOURNAL OF AUSTRALIA.

“Leo vijana milioni kumi wana virusi vya UKIMWI, na zaidi ya nusu ya watu milioni 4.9 ambao huambukizwa virusi hivyo kila mwaka ulimwenguni pote wana umri wa kati ya miaka 15 na 24.”HAZINA YA IDADI YA WATU YA UMOJA WA MATAIFA.

Satelaiti zilirekodi safari za alibatrosi kuzunguka dunia. Alibatrosi aliyeruka kuzunguka dunia kwa kasi zaidi alifanya hivyo kwa siku 46 tu.GAZETI SCIENCE, MAREKANI.

“Kila siku, ulimwengu hutumia zaidi ya dola milioni 100 kila saa moja kwa wanajeshi na silaha.”—VITAL SIGNS 2005, TAASISI YA WORLDWATCH.

Jeuri Dhidi ya Makasisi Inaongezeka

Gazeti la London Daily Telegraph la 2005 liliripoti kwamba “kuwa kasisi ni mojawapo ya kazi hatari zaidi nchini [Uingereza].” Uchunguzi uliofanywa na serikali mwaka wa 2001 ulionyesha kwamba karibu asilimia 75 ya makasisi waliohojiwa walikuwa wametendewa vibaya au kushambuliwa miaka miwili iliyopita. Tangu mwaka wa 1996, angalau makasisi saba wameuawa. Katika mji wa Merseyside, “kwa wastani, kila siku mojawapo ya majengo 1,400 ya ibada yaliteketezwa, yakashambuliwa, au kuporwa.”

Unamna-namna wa Ajabu wa Wanyama na Mimea

Licha ya kuharibiwa kwa misitu ya mvua, “kisiwa cha Borneo bado kina unamna-namna mwingi wa ajabu wa wanyama na mimea katika sehemu zake za ndani,” linasema gazeti The New York Times. Kulingana na Hazina ya Wanyama wa Pori Ulimwenguni, kati ya mwaka wa 1994 na 2004, wanabiolojia waligundua aina mpya 361 za mimea na wanyama kwenye kisiwa hicho, ambacho ni sehemu ya Brunei, Indonesia, na Malaysia. Ugunduzi wao ulitia ndani aina mpya 260 za wadudu, mimea 50, samaki 30, vyura wadogo 7, mijusi 6, kaa 5, nyoka 2, na chura mkubwa 1. Hata hivyo, misitu ya mvua iliyo katika sehemu za ndani inakabili tisho la kuongezeka kwa ukataji wa miti unaosababishwa na kutumiwa sana kwa mbao ngumu, mpira, na mawese.

Ushirikina Unaongezeka

“Hata katika enzi hii ya teknolojia na sayansi, bado watu wanavutiwa na ushirikina,” inaripoti Allensbach, taasisi ya Ujerumani ya kura ya maoni. Uchunguzi wa muda mrefu umeonyesha kwamba “bado watu wanaamini ishara za bahati nzuri au mbaya, na zoea hilo linapendwa zaidi leo kuliko ilivyokuwa miaka 25 iliyopita.” Katika miaka ya 1970, asilimia 22 ya watu waliamini kwamba kuona nyota ipitayo kasi angani kungeathiri maisha yao. Sasa asilimia 40 ya watu wanaamini hivyo. Leo ni mtu 1 tu kati ya 3 ambaye hukataa ushirikina wa kila aina. Uchunguzi mwingine uliofanyiwa wanafunzi 1,000 wa chuo kikuu huko Ujerumani ulionyesha kwamba 1 kati ya 3 huamini kwamba hirizi ambazo wao hubeba ndani ya gari au kwenye vishikio vya funguo zitawaletea mema.

Barafu za Antaktika Zinazidi Kuyeyuka

“Katika miaka 50 iliyopita, asilimia 87 ya barafu 244 kwenye peninsula ya Antaktika zimeyeyuka,” na hilo limetukia haraka zaidi kuliko vile wataalamu walivyokuwa wamedhania, linaripoti gazeti Clarin la Buenos Aires. Uchunguzi wa kwanza kamili wa barafu katika eneo hilo pia uligundua kwamba halijoto katika hewa ilikuwa imeongezeka kwa zaidi ya nyuzi 2.5 Selsiasi katika miaka 50 iliyopita. David Vaughan wa Uchunguzi wa Antaktika wa Uingereza anasema kwamba kuyeyuka kwa barafu nyingi kulisababishwa hasa na badiliko la hewa. “Je, wanadamu ndio wamesababisha hali hiyo?” anauliza. “Hatuna uhakika kabisa, lakini tunakaribia sana kupata jibu la swali hilo muhimu.”