Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuvu—Faida na Madhara Yake

Kuvu—Faida na Madhara Yake

Kuvu—Faida na Madhara Yake

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI SWEDEN

Kuvu fulani huokoa uhai; nyingine huua. Nyingine hufanya jibini na divai ziwe na ladha nzuri; nyingine hutia chakula sumu. Nyingine hukua kwenye magogo; nyingine hukua kwenye bafu na vitabu. Kwa kweli, kuvu ziko kila mahali na huenda ikawa unaposoma sentensi hii chembe zake zinaingia puani mwako.

IKIWA huamini kwamba kuvu ziko kila mahali, acha tu kipande cha mkate mahali fulani, hata ndani ya friji. Baada ya muda mfupi, utaona kitu chenye manyoya kikikua. Kitu hicho ni kuvu!

Kuvu Ni Nini?

Kuvu hutoka katika jamii kubwa kwani kuna zaidi ya aina 100,000 za kuvu, kutia ndani ukungu, uyoga, na hamira. Ni aina 100 hivi tu za kuvu zinazojulikana kuwa hutokeza magonjwa kwa wanadamu na wanyama. Nyingine nyingi huchangia sehemu muhimu katika kutokeza chakula, yaani, hufanya takataka zioze na hivyo kufanyiza upya vitu muhimu ambavyo vinaweza kutumiwa na mimea. Hata kuvu nyingine hushirikiana na mimea, na kuisaidia kufyonza virutubishi kutoka udongoni. Na nyingine ni vimelea.

Maisha ya kuvu huanza kama chembe ndogo inayobebwa na hewa. Chembe hiyo ikitua mahali penye chakula, halijoto, na unyevu unaofaa, itakua na kutokeza chembe zinazofanana na nyuzi ambazo zinaitwa hyphae. Nyuzi hizo zinapoungana, zinafanyiza kitu chenye manyoya kinachoitwa mycelium, ambacho ndicho kuvu inayoonekana. Pia kuvu inaweza kufanana na uchafu au doa, kama wakati inapokua katikati ya vigae vya bafu.

Kuvu huzaana kwa njia isiyo na kifani. Kuvu inayoitwa Rhizopus stolonifer, ambayo kwa kawaida hukua juu ya mkate, huwa na madoa madogo meusi ambayo ndiyo chembe, au sporangia. Doa moja tu lina zaidi ya chembe 50,000 na kila moja inaweza kutokeza mamia ya mamilioni ya chembe mpya kwa siku chache tu! Na chini ya hali zinazofaa, kuvu zinaweza kukua vizuri juu ya kitabu, kiatu, au ukuta wa nyumba kama tu zinavyoweza kukua juu ya gogo msituni.

Kuvu “hulaje”? Tofauti na wanyama na wanadamu, ambao hula chakula chao kisha hukimeng’enya na kukiyeyusha, mara nyingi kuvu hufanya kinyume cha hilo. Kuvu zinaposhindwa kula molekuli za vitu vilivyooza kwa sababu ya ukubwa wake, zinatokeza vimeng’enyaji ambavyo huvunja-vunja molekuli hizo kisha kuzila. Pia kwa kuwa kuvu haziwezi kwenda kutafuta chakula, hizo huishi ndani ya chakula chao.

Kuvu zinaweza kutokeza vitu vyenye sumu vinavyoitwa mycotoxins, ambavyo vinaweza kudhuru sana wanadamu na wanyama. Mtu anaweza kuathiriwa na kuvu kupitia kupumua, kuila, au inapogusa ngozi. Hata hivyo, kuvu hazitokezi madhara sikuzote, zina manufaa pia.

Manufaa ya Kuvu

Mnamo mwaka wa 1928, mwanasayansi Alexander Fleming aligundua bila kutazamia jinsi kuvu ya kijani ilivyo na uwezo wa kuua vijidudu. Baadaye kuvu hiyo iliyoitwa Penicillium notatum, iliua bakteria lakini haikudhuru wanadamu na wanyama. Ugunduzi huo ulichangia kutokezwa kwa penisilini, ambayo imeitwa “dawa ambayo imeokoa maisha ya watu wengi zaidi katika tiba ya sasa.” Kwa sababu ya kazi yao, Fleming na watafiti wenzake Howard Florey na Ernst Chain walipewa Tuzo la Nobeli la tiba mnamo 1945. Tangu wakati huo, kuvu imetumiwa kutokeza dawa nyingine kutia ndani dawa za kutibu kuganda kwa damu, kipandauso, na ugonjwa wa Parkinson.

Kuvu imetumiwa pia kuongeza ladha ya chakula. Kwa mfano, fikiria jibini. Je, unajua kwamba aina zifuatazo za jibini Brie, Camembert, Danish blue, Gorgonzola, Roquefort na Stilton zina ladha za pekee kwa sababu ya kuvu ya Penicillium? Vilevile, salami, mchuzi wa soya, na pombe hutengenezwa kwa kutumia aina fulani za kuvu.

Ndivyo ilivyo na divai. Zabibu fulani zinapovunwa wakati unaofaa zikiwa na kiasi cha kutosha cha kuvu kwenye kila kichala, zinaweza kutumiwa kutokeza divai bora sana. Kuvu inayoitwa Botrytis cinerea, huongeza kiasi cha sukari kwenye zabibu na kuboresha ladha yake. Divai inapohifadhiwa, kuvu inayoitwa Cladosporium cellare huboresha ladha yake zaidi inapokomaa. Msemo wa wakulima wa zabibu wa Hungary unasema: ‘Kuvu nzuri hutokeza divai bora.’

Madhara ya Kuvu

Kwa muda mrefu kumekuwepo na kuvu fulani zinazoweza kudhuru. Katika karne ya sita K.W.K., Waashuru walitumia aina ya kuvu inayoitwa Claviceps purpurea kutia sumu visima vya maadui wao. Wakati huo kuvu ilikuwa silaha ya kibiolojia. Katika Zama za Kati, kuvu hiyo, ambayo nyakati nyingine hukua kwenye rai, ilifanya watu wengi washikwe na kifafa, wapatwe na mwasho mkali, kidonda chenye kuoza, na kuona maono. Ugonjwa ambao sasa unaitwa ergotism uliitwa moto wa Mtakatifu Anthony kwa sababu wagonjwa wengi waliotazamia kuponywa kimuujiza, walienda kwenye madhabahu ya Mtakatifu Anthony huko Ufaransa.

Kuvu hutokeza kemikali yenye nguvu zaidi inayosababisha kansa ambayo inaitwa aflatoxin. Katika nchi moja ya Asia, watu 20,000 hufa kila mwaka kutokana na kemikali hiyo. Kemikali hiyo hatari imetumiwa kutengeneza silaha za kisasa za kibiolojia.

Hata hivyo, katika maisha ya kawaida, dalili za kuathiriwa na kuvu za kawaida huwa kero tu bali si tisho kubwa kwa afya. “Kuvu nyingi hazidhuru hata ukizinusa,” linasema jarida UC Berkeley Wellness Letter. Kwa kawaida, watu ambao huathiriwa vibaya wanatia ndani wale walio na matatizo ya mapafu, kama vile ugonjwa wa pumu; watu wenye mizio, wanaoathiriwa na kemikali, au walio na mfumo hafifu wa kinga; na watu wanaofanya kazi shambani ambako huenda kukawa na kuvu nyingi. Huenda pia watoto na wazee wakaathiriwa na kuvu.

Kulingana na Idara ya Huduma za Afya ya California nchini Marekani, kuvu zinaweza kutokeza dalili zifuatazo: ‘Matatizo ya kupumua, kama vile kukoroma, kupumua kwa shida, kupumua haraka-haraka; kuziba kwa pua; kuwashwa na macho (macho kutoa machozi au kuwa mekundu); kikohozi kikali; kuwashwa na pua au koo; vipele au kuwashwa na ngozi.’

Kuvu na Majengo

Katika maeneo fulani ni jambo la kawaida kusikia kwamba shule zimefungwa au watu wamelazimika kuhama nyumba au ofisi zao ili kuvu ziondolewe. Mapema mwaka wa 2002, ilibidi Jumba jipya la Makumbusho la Sanaa ya Kisasa huko Stockholm, Sweden, lifungwe kwa sababu ya kuvu. Gharama za kuondoa kuvu zilikuwa dola milioni tano hivi! Kwa nini tatizo hilo limekuwa la kawaida siku hizi?

Jibu linahusisha sababu mbili kuu: vifaa vya ujenzi na muundo wa jengo. Katika miaka ya hivi karibuni vifaa vya ujenzi vimetia ndani vitu vinavyoweza kushambuliwa na kuvu kwa urahisi. Mfano mmoja ni ukuta uliotengenezwa kwa karatasi zilizounganishwa kwa chokaa. Chokaa huwa na unyevu. Kwa hiyo ukuta huo ukiwa na unyevu kwa muda mrefu, chembe za kuvu zinaweza kukua, na kula karatasi za ukuta huo.

Pia miundo ya ujenzi imebadilika. Kabla ya miaka ya 1970, majengo mengi nchini Marekani na nchi nyingine hayakuzuia baridi na kuhifadhi joto kama ilivyo na majengo ya baadaye. Watu walifanya mabadiliko kwa kujenga nyumba ambazo huhifadhi nishati kwa kupunguza kiasi cha joto linalotoka na vilevile hewa inayoingia. Kwa hiyo maji yanapoingia kwenye kuta, yanadumu kwa muda mrefu, na hivyo kuchochea ukuzi wa kuvu. Je, kuna suluhisho la tatizo hilo?

Njia bora zaidi ya kutatua tatizo hilo, au kupunguza kutokea kwa kuvu, ni kusafisha na kukausha kila kitu na kuhakikisha kwamba hakuna unyevu. Mahali fulani pakianza kuwa na unyevu, pakaushe mara moja na kufanya mabadiliko au marekebisho yanayohitajiwa ili maji yasijikusanye tena. Kwa mfano, safisha paa na michirizi na kuidumisha katika hali nzuri. Na hakikisha kwamba maji hayajikusanyi kwenye msingi kwa kuyaelekeza mbali na msingi. Ikiwa una mfumo wa kuingiza hewa, hakikisha kwamba njia zote za kuingiza hewa ni safi na hazijaziba.

Mtaalamu mmoja anasema kwamba “njia bora ya kudhibiti kuvu ni kudhibiti unyevu.” Hatua hizo rahisi zitakuepusha wewe na familia yako na madhara ya kuvu. Katika njia fulani, kuvu ni kama moto. Inaweza kudhuru, lakini pia inaweza kunufaisha sana. Inategemea hasa jinsi tunavyoitumia na kuidhibiti. Bila shaka, tuna mengi zaidi ya kujifunza kuhusu kuvu. Lakini tunanufaika kwa kujifunza kuhusu uumbaji wa Mungu wenye kushangaza.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 14, 15]

Je, Kuvu Inatajwa Katika Biblia?

Biblia inataja “pigo la ukoma katika nyumba,” yaani, katika jengo lenyewe. (Mambo ya Walawi 14:34-48) Imedokezwa kwamba pigo hilo ambalo pia limeitwa “ukoma hatari,” lilikuwa aina fulani ya ukungu au kuvu, lakini hakuna uhakika kuhusu jambo hilo. Vyovyote vile, Sheria ya Mungu iliwaagiza wenye nyumba waondoe mawe yote yaliyoambukizwa, wakwangue sehemu yote ya ndani ya nyumba, na kutupa uchafu huo wote nje ya jiji katika “mahali pasipo safi.” Ikiwa pigo hilo lingerudi, nyumba yote ingeonwa kuwa si safi, ibomolewe, na vifaa vyote vitupwe. Maagizo hususa ambayo Yehova alitoa yalionyesha kwamba aliwapenda sana watu wake na alijali afya yao ya kimwili.

[Picha katika ukurasa wa 13]

Dawa zilizotengenezwa kutokana na kuvu zimeokoa maisha ya wengi

[Picha katika ukurasa wa 15]

Kuta zilizotengenezwa kwa karatasi na chokaa na plastiki ngumu zinaweza kufungia unyevu, ambao huchochea ukuzi wa kuvu