Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Michael Agricola—“Mwanamume Aliyetokeza Mwanzo Mpya”

Michael Agricola—“Mwanamume Aliyetokeza Mwanzo Mpya”

Michael Agricola—“Mwanamume Aliyetokeza Mwanzo Mpya”

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI FINLAND

“Hakuna kitabu kingine ambacho kimekuwa na uvutano mkubwa kwa utamaduni, maadili, na mawazo ya Wafini kama Biblia.”—“Biblia 350—The Finnish Bible and Culture.”

JE, BIBLIA imetafsiriwa katika lugha yako ya kienyeji? Kuna uwezekano mkubwa kwamba imetafsiriwa. Biblia nzima au sehemu yake, inapatikana katika lugha zaidi ya 2,000. Na jambo hilo halikutukia tu bila mpango. Katika historia yote, wanaume na wanawake wengi wamejitahidi sana kutafsiri Biblia katika lugha za kienyeji hata chini ya matatizo makubwa. Michael Agricola alikuwa mmoja wa watafsiri hao.

Agricola alikuwa msomi aliyechukua jukumu la kutafsiri Biblia katika Kifini. Maandishi yake yalisaidia kuanzisha utamaduni mpya wa Wafini. Si ajabu kwamba anaitwa Mwanamume Aliyetokeza Mwanzo Mpya!

Agricola alizaliwa yapata mwaka wa 1510 katika kijiji cha Torsby kusini mwa Finland. Baba yake alikuwa na shamba, na hilo linatusaidia kuelewa sababu iliyofanya aitwe Agricola, jina linalotokana na neno “mkulima” la Kilatini. Yaelekea Agricola alizungumza Kiswedi na Kifini, kwa kuwa alikulia mahali ambapo lugha hizo mbili zilizungumzwa. Alijifunza Kilatini alipokuwa katika shule ya Kilatini katika mji wa Vyborg. Baadaye alihamia jiji la Turku, ambalo wakati huo lilikuwa kituo cha usimamizi cha Finland, ambako alikuwa katibu wa Martti Skytte, askofu Mkatoliki wa Finland.

Dini na Siasa za Wakati Wake

Wakati wa kipindi hiki cha maisha ya Agricola, kulikuwa na msukosuko huko Skandinavia. Sweden ilikuwa ikijaribu kujiondoa kwenye Muungano wa Kalmar uliofanyizwa na nchi za Skandinavia. Mnamo 1523, Gustav wa Kwanza alitawazwa kuwa mfalme wa Sweden. Jambo hilo lilitokeza mabadiliko makubwa huko Finland, ambayo wakati huo ilikuwa mkoa wa Sweden.

Mfalme huyo mpya alikuwa na nia ya kuimarisha mamlaka yake. Ili kutimiza miradi yake, aliunga mkono yale Marekebisho Makubwa ya Kidini, ambayo wakati huo yalikuwa yakienea kaskazini mwa Ulaya. Kwa kubadili dini ya serikali yake kutoka Katoliki hadi Ulutheri, alikata uhusiano wake na Papa, akapuuza mamlaka ya maaskofu Wakatoliki, na kunyakua mali ya kanisa. Hadi leo, raia wengi wa Sweden na Finland ni Walutheri.

Jambo muhimu ambalo Waprotestanti walijaribu kutimiza lilikuwa kutumia lugha za kienyeji katika ibada kanisani badala ya Kilatini. Kwa hiyo, mnamo 1526 Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo, au “Agano Jipya,” yalichapishwa katika Kiswedi. Hata hivyo, Uprotestanti haukuwa na uvutano mkubwa huko Finland kama ulivyokuwa kwingineko. Wakati huo, hakukuwa na upendezi mkubwa wa kutafsiri Biblia katika Kifini. Kwa nini?

Kazi ‘Ngumu Inayochosha’

Sababu kuu ni kwamba hakukuwa na kitabu chochote kilichokuwa kimechapishwa katika Kifini. Kabla ya miaka ya katikati ya 1500, ni sala chache tu za Kikatoliki zilizokuwa zimeandikwa katika Kifini. Kwa hiyo, ili Maandiko Matakatifu yatafsiriwe katika Kifini, mfumo wa kuandika maneno mengi yaliyokuwa yakitamkwa tu ungehitaji kuvumbuliwa na vilevile maneno mengi mapya kabisa yangehitaji kubuniwa. Yote hayo yangefanywa bila msaada wa vitabu vya lugha. Licha ya magumu hayo, Agricola alianza kutafsiri Biblia!

Mnamo 1536, Skytte, askofu Mkatoliki wa Finland, alimtuma Agricola huko Wittenberg, Ujerumani, aendeleze masomo yake ya theolojia na lugha. Kulingana na maelezo fulani, ilikuwa katika mji huo kwamba Luther alitundika tasnifu zake 95 maarufu kwenye mlango wa Castle Church miaka 20 mapema.

Alipokuwa huko Wittenberg, Agricola hakuponda tu wakati wake akisomea theolojia na lugha. Alianza kazi kubwa ya kutafsiri Biblia katika Kifini. Mnamo 1537, alimwandikia mfalme wa Sweden barua iliyosema hivi: “Maadamu Mungu anaongoza masomo yangu, nitajitahidi, kama nilivyoazimia, kuendelea kutafsiri Agano Jipya katika lugha ya Wafini.” Aliporudi Finland, Agricola aliendelea na kazi yake ya kutafsiri, wakati huohuo akiwa mkuu wa shule.

Kutafsiri Biblia kulikuwa kazi ngumu kwa Agricola kama ilivyokuwa kwa watafsiri wengine wa Biblia wa mapema. Hata Luther alikuwa amelalamika: “Ni jambo gumu na linalochosha kuwalazimisha waandishi Waebrania wazungumze Kijerumani”! Ni kweli kwamba Agricola angeweza kutumia tafsiri za wengine, lakini tatizo kuu lilikuwa Kifini. Kwa kweli, lugha hiyo haikuwa imewahi kuandikwa kamwe!

Hivyo, ilikuwa kana kwamba Agricola alikuwa akijenga nyumba bila ramani ya ujenzi, akiwa na vifaa vichache tena duni. Alifanyaje kazi hiyo? Agricola alianza kazi yake kwa kuchagua maneno kadhaa kutoka lahaja za Kifini na kuyaandika jinsi yalivyotamkwa. Yaelekea Agricola ndiye aliyekuwa mtu wa kwanza kubuni maneno haya katika Kifini, “serikali,” “mnafiki,” “hati,” “jeshi,” “kielelezo,” na “mwandishi.” Alibuni nomino ambatani, akafanyiza minyambuliko, na kutohoa maneno kutoka lugha nyingine, hasa Kiswedi. Baadhi ya maneno hayo ni enkeli (malaika), historia (historia), lamppu (taa), marttyyri (mfia-imani), na palmu (mtende).

Wenyeji Wapata Neno la Mungu

Mwishowe, mnamo 1548, sehemu ya kwanza ya tafsiri ya Agricola ilichapishwa, yaani Se Wsi Testamenti (Agano Jipya). Watu fulani wanaamini kwamba tafsiri hiyo ilikuwa imekamilishwa miaka mitano mapema lakini ilichelewa kuchapishwa kwa sababu ya ukosefu wa pesa. Inadhaniwa kwamba Agricola alitumia pesa zake nyingi kugharimia uchapishaji.

Miaka mitatu baadaye Dauidin Psaltari (Zaburi) ilichapishwa, ambayo yaelekea Agricola aliitafsiri kwa msaada wa rafiki zake. Pia alikuwa mstari wa mbele katika kutafsiriwa kwa vitabu fulani vya Musa na vya manabii.

Kwa unyenyekevu, akitambua udhaifu wake, Agricola aliandika hivi waziwazi: “Mkristo na mtu yeyote anayemwogopa Mungu au msomaji yeyote wa Kitabu hiki Kitakatifu, asiudhike iwapo ataona kosa au jambo lisilo la kawaida au lisilopendeza au lililoelezewa kwa njia mpya katika kitabu hiki kilichotafsiriwa na mtu wa kawaida asiye na ujuzi katika kazi hii.” Licha ya kasoro zozote zinazoweza kupatikana katika tafsiri yake, Agricola anapaswa kusifiwa sana kwa sababu ya bidii yake ya kufanya Biblia ipatikane kwa watu wa kawaida.

Urithi Ulioachwa na Agricola

Mapema mnamo 1557, Agricola, ambaye wakati huo alikuwa Mlutheri na vilevile askofu wa Turku, alichaguliwa kuwa kati ya wajumbe waliotumwa Moscow kutatua mizozo ya mpaka kati ya Sweden na Urusi. Safari yao ilifanikiwa. Hata hivyo, yaonekana kwamba magumu aliyopata katika safari yake ya kurudi yalimfanya Agricola awe mgonjwa ghafula. Alikufa akiwa njiani kuelekea nyumbani akiwa na umri wa miaka 47 hivi.

Katika muda mfupi alioishi, Agricola alichapisha vichapo kumi tu vya Kifini vyenye jumla ya kurasa 2,400. Hata hivyo, wengi wanaamini kwamba ‘Mwanamume huyo Aliyetokeza Mwanzo Mpya’ alichochea ukuzi wa utamaduni wa Finland. Tangu wakati huo, Kifini na Wafini wenyewe wamepiga hatua kubwa katika nyanja ya sanaa na sayansi.

Jambo muhimu zaidi ni kwamba Michael Agricola alisaidia kuanzisha jambo muhimu. Alisaidia Wafini waone wazi zaidi nuru ya Neno la Mungu. Shairi la kumkumbuka lililoandikwa katika Kilatini baada ya kifo chake linasema hivi kwa ufupi: “Hakuacha tu urithi wa kawaida bali pia aliacha kazi yake, yaani, alitafsiri vitabu vitakatifu katika Kifini, na kazi hiyo inastahili kusifiwa sana.”

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 23]

Biblia ya Kifini

Biblia ya kwanza nzima ya Kifini, ambayo ilitafsiriwa hasa kwa kutegemea maandishi ya Michael Agricola, ilichapishwa katika mwaka wa 1642. Baada ya muda ikawa Biblia rasmi ya Kanisa la Lutheri la Finland. Kwa miaka kadhaa Biblia hiyo ilifanyiwa masahihisho madogo mara kadhaa lakini haikubadilishwa hadi 1938. Nakala iliyofanyiwa masahihisho ya mwisho ilichapishwa mnamo 1992.

Biblia nyingine kamili katika Kifini ni Biblia Takatifu—Tafsiri ya Ulimwengu Mpya iliyochapishwa na Mashahidi wa Yehova. Ilitolewa mnamo 1995. Miaka 20 mapema, mnamo 1975, tayari Mashahidi walikuwa wametafsiri Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo katika Kifini. Biblia Takatifu—Tafsiri ya Ulimwengu Mpya imefuata kwa ukaribu iwezekanavyo maandishi ya awali. Kufikia sasa, nakala 130,000,000 zimechapishwa.

[Picha katika ukurasa wa 22]

Michael Agricola na Biblia ya kwanza ya Kifini. Postikadi ya mwaka wa 1910

[Hisani]

National Board of Antiquities/Ritva Bäckman

[Picha katika ukurasa wa 23]

“Agano Jipya” iliyotafsiriwa na Agricola

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 21]

National Board of Antiquities