Ndio Hao!
Ndio Hao!
ILIKUWA jioni-jioni, na kulikuwa na baridi wakati wa majira ya kupukutika kwa majani. Lakini hali hiyo ya utulivu ilivurugwa mara moja na kelele za kundi la bata-bukini. Kwa ghafula, karibu bata-bukini 20 walipita juu ya vichwa vyetu wakiwa wamejipanga kwa herufi ya V huku wakiruka kwa kupiga mabawa yao yenye kuvutia na yenye nguvu. Bata-bukini mmoja alielekea upande wa kushoto na kurudi nyuma ya kikundi. Nilivutiwa sana kutazama jambo hilo hivi kwamba nilianza kujiuliza kwa nini bata-bukini huruka wakiwa wamejipanga kwa herufi ya V, nao wanaenda wapi?
Bata-bukini ni ndege wa majini, ambaye ni wa jamii moja na bata na bata-maji. Kuna jamii 40 hivi za bata-bukini ulimwenguni pote, nao hupatikana hasa huko Asia, Ulaya, na Amerika Kaskazini. Bata-bukini wa Kanada mwenye shingo ndefu nyeusi na doa jeupe kuzunguka koo lake ni mojawapo ya jamii zinazojulikana zaidi. Ndege wa kiume waliokomaa wa jamii nyingine inayoitwa giant Canada geese wanaweza kuwa na uzito wa kilogramu 8 hivi na bawa lao lina upana wa meta 2. Bata-bukini hao huishi huko Alaska na kaskazini mwa Kanada wakati wa kiangazi kisha huhamia upande wa kusini hadi Mexico wakati wa miezi ya baridi kali.
Lazima bata-bukini wahame wakati unaofaa kabisa. Wakihamia kaskazini mapema zaidi, bado maji yatakuwa yameganda na chakula kitakuwa haba. Kwa hiyo, bata-bukini wa Kanada huhamia kaskazini kwa kufuatana na majira. Wanapofika mahali wanapoelekea, bata-bukini hujipanga
wawili-wawili, wa kiume na wa kike, kisha wao hutafuta mahali pa kutaga mayai.Bata-bukini huruka karibu-karibu ili waweze kuonana na kuitikia mara moja ndege aliye mbele anapobadili mwelekeo, mwendo, au arukapo juu zaidi. Isitoshe, wataalamu fulani wanaamini kwamba mkondo wa hewa ambao hutokezwa na ndege walio mbele hupunguza pepo zenye nguvu na hivyo kufanya iwe rahisi zaidi kwa ndege walio nyuma kuruka. Vyovyote vile, inaonekana kwamba kwa kawaida kundi la bata-bukini wanaohama hufanyizwa na familia kadhaa, huku ndege wakubwa wakiongoza.
Mara nyingi, bata-bukini wa Kanada hutumia kiota kilekile mwaka baada ya mwaka. Kwa kawaida, kiota hicho hutengenezwa kwa vitu rahisi, kama vile vijiti, nyasi, na kuvumwani. Bata-bukini huwa na mwenzi mmoja tu maishani. Mwenzi mmoja akifa, yule aliyebaki anaweza kukubali mwenzi mwingine. Hata hivyo, kwa kawaida mwenzi aliyebaki huendelea kuishi peke yake.
Bata-bukini wa kike hutaga kati ya mayai manne na manane, naye huyalalia kwa siku 28 hivi. Wazazi ni walinzi wakali. Wao au makinda yao yanapotishwa, hupigana vikali. Wanaweza kuwapiga wavamizi kwa nguvu sana wakitumia mabawa yao.
Makinda ya bata-bukini huanza kuwasiliana yakiwa bado katika yai. Makinda hayo hutoa sauti nyembamba ya juu (kuonyesha uradhi) na pia sauti za kuonyesha kuna taabu. Wanapowasiliana wao kwa wao na pia na makinda yao bata-bukini wakubwa pia hutoa sauti mbalimbali. Kwa kweli, watafiti wametambua angalau sauti 13 tofauti-tofauti ambazo bata-bukini wa Kanada hutoa.
Kwa kweli, bata-bukini hudhihirisha kwamba wana “hekima ya kisilika.” (Methali 30:24) Bila shaka, Yehova Mungu ndiye anayepaswa kusifiwa kwa kuumba vitu vyote, kutia ndani ndege wa angani.—Zaburi 104:24.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 17]
Je, ulijua?
● Mara tu yanapoanguliwa, makinda ya bata-bukini huondoka kabisa kiotani pamoja na mama na baba yao. Kwa kawaida familia huendelea kuishi pamoja.
● Inasemekana kwamba bata-bukini wa jamii ya bar-headed huruka juu ya Mlima Everest, ambao una kimo cha meta 8,900 hivi.
● Aina fulani za bata-bukini wanaweza kuruka kwa kilometa 1,600 bila kupumzika.
● Bata-bukini wanaporuka karibu-karibu kwa mwendo sawa na yule anayeruka peke yake, wale walio pamoja hupiga-piga mabawa yao mara chache zaidi, na hivyo kupunguza mara ambazo moyo wao hupiga.
[Hisani]
Top left: U.S. Fish & Wildlife Service, Washington, D.C./Duane C. Anderson
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 16]
Flying geese: © Tom Brakefield/CORBIS