Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

▪ Ikitegemea uamuzi wa mlipa kodi, serikali ya Hispania hutoa asilimia 0.5 ya kodi hizo kwa mashirika ya kutoa msaada au mashirika ya kanisa Katoliki. Ingawa karibu asilimia 80 ya Wahispania hudai kuwa Wakatoliki, ni asilimia 20 tu wanaokubali kutoa kodi hiyo kwa mashirika ya kanisa Katoliki.—EL PAÍS, HISPANIA.

▪ Kulingana na chati iliyotolewa na Taasisi ya Takwimu za Bima, “Mwanamume anayevuta sigara akiwa na umri wa miaka 30 hupunguza muda wake wa kuishi kwa miaka 5 1⁄2, na mwanamke kwa miaka 6 1⁄2.” Hata hivyo, mtu anapoacha kuvuta sigara akiwa na umri wa miaka 30 anapunguza hatari nyingi za kufa kutokana na magonjwa yanayosababishwa na tumbaku.—THE TIMES, UINGEREZA.

▪ Katika mwaka wa 2004, kiasi cha mafuta yaliyotumiwa ulimwenguni kiliongezeka kwa asilimia 3.4 na kufikia lita bilioni 13.1 kwa siku. Marekani na China zilitumia karibu nusu ya kiasi hicho na sasa Marekani hutumia lita bilioni 3.2 na China lita bilioni 1.0 kwa siku.—VITAL SIGNS 2005, TAASISI YA WORLDWATCH.

“Mheshimu Sana Mama Yako”

Wachanganuzi wa masuala ya kazi wamekadiria kwamba ikiwa mama Mkanada anayekaa nyumbani wakati wote ambaye ana watoto wawili wanaoenda shule angelipwa kwa kazi yote ambayo yeye hufanya, mshahara wake wa mwaka mzima kutia ndani saa za ziada ungekuwa dola 130,000 (za Marekani). Kiasi hicho kinategemea mshahara wa sasa wa wastani wa wale wanaofanya kazi “saa 100 kwa juma, yaani siku sita zenye saa 15 na siku moja yenye saa 10,” linasema gazeti Vancouver Sun. Kazi ambazo mama anayekaa nyumbani hufanya zinatia ndani kutunza watoto, kufundisha, kuendesha gari, kutunza nyumba, kupika, kuwatunza wagonjwa, na kurekebisha vitu. Gazeti hilo linatoa shauri hili: “Mheshimu sana mama yako. Huenda halipwi mshahara wa kutosha kwa kazi anayofanya.”

Vijana Wanajichagulia Maadili

Vijana wengi Wafini “wanajichagulia maadili yao wenyewe,” linasema jarida la Chuo Kikuu cha Jyväskylä huko Finland. Jarida hilo linaendelea kusema kwamba kwa kawaida leo “watu huchagua mambo ambayo wataamini kutoka vyanzo mbalimbali, ni kana kwamba wako dukani.” Nyakati nyingine maadili ambayo wao huchagua hupingana. Kwa mfano, vijana wanaamini kwamba ni muhimu kugawa mali na utajiri kwa usawa; wakati huohuo, “wameanza kuamini kwamba ni sawa kushindana kishupavu na kwa ukatili.”

Hatari ya Kutiwa Protini Zenye Kasoro

Katika taarifa iliyotolewa hivi karibuni katika vyombo vya habari, Shirika la Afya la Kukagua Usalama wa Bidhaa za Tiba la Ufaransa lilisema kwamba hatari za kupitishwa kwa protini zenye kasoro kwa kutiwa damu mshipani imeongezeka sana. Inasemekana kwamba protini hizo zenye kasoro ndizo husababisha aina ya ugonjwa wa Creutzfeldt-Jakob (vCJD) katika wanadamu. Ugonjwa huo hatari unaodhoofisha chembe za neva na ambao hauna tiba, unawakumba wanadamu nao unafanana na kichaa cha ng’ombe. Taarifa hiyo ilitolewa baada ya kugunduliwa kwa visa viwili vya ugonjwa huo nchini Uingereza ambao huenda ulipitishwa kwa kutiwa damu mshipani. Hakuna njia inayotegemeka ya kugundua ugonjwa huo kabla ya dalili zake kuonekana waziwazi.

Wanataka Sana Kuwa Wembamba

Gazeti The Sydney Morning Herald linasema kwamba uchunguzi umeonyesha kwamba “wasichana, kutia ndani wale wenye umri wa miaka mitano, hawapendezwi na miili yao na wangetamani kuwa wembamba.” Ripoti hiyo inataja uchunguzi uliotia ndani wasichana Waaustralia wenye umri wa miaka mitano hadi minane. Karibu nusu ya wasichana hao walitaka kuwa na mwili mwembamba zaidi, huku idadi sawa na hiyo wakisema kwamba “wangepunguza kiasi cha chakula wanachokula ikiwa wangekuwa wanene.” Mtafiti mmoja alipendekeza kwamba maoni yasiyofaa kuhusu mwili unaofaa “yanaweza kuwafanya wasijiheshimu, washuke moyo na baadaye wapate matatizo ya kula.”