Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Mahujaji na Wapuriti Walikuwa Nani?

Mahujaji na Wapuriti Walikuwa Nani?

Mahujaji na Wapuriti Walikuwa Nani?

KWENYE ufuo wa Amerika Kaskazini huko Plymouth, Massachusetts, kuna jiwe kubwa la matale lililochongwa namba 1620 juu yake. Jiwe hilo linaitwa Plymouth Rock, nalo liko karibu na mahali ambapo inaaminika kuwa kikundi cha wasafiri kutoka Ulaya walitua karibu miaka 400 iliyopita. Walikuwa Waingereza waliohamia Marekani na kuanzisha koloni huko Massachusetts na Plymouth.

Watu wengi wanajua hadithi za Mahujaji wakarimu ambao waliwakaribisha Wenyeji wa Asili wa Amerika katika karamu nono za mavuno. Lakini Mahujaji hao walikuwa nani, na kwa nini walihamia Amerika Kaskazini? Ili kupata majibu, na turudi nyuma hadi wakati wa Mfalme Henry wa Nane wa Uingereza.

Msukosuko wa Kidini Huko Uingereza

Karibu miaka 100 kabla ya Mahujaji hao kwenda Marekani, Uingereza ilikuwa nchi ya Kikatoliki na papa alimpa Mfalme Henry wa Nane jina la cheo, Mtetezi wa Imani. Lakini mgawanyiko ulitokea wakati Papa Clement wa Saba alipokataa kuvunja ndoa ya Henry na Catherine wa Aragon, aliyekuwa mke wa kwanza kati ya wake sita wa mfalme.

Henry alipokuwa akijaribu kutatua matatizo yake ya familia, Marekebisho Makubwa ya Kidini yalikuwa yakisababisha msukosuko katika Kanisa Katoliki kwenye sehemu nyingi za Ulaya. Mwanzoni Henry alizuia watu waliochochea Marekebisho ya Kidini wasiingie Uingereza, kwa kuwa hakutaka kupoteza umashuhuri ambao kanisa lilimpa. Lakini baadaye alibadili nia. Kanisa Katoliki lilikataa kuvunja ndoa yake, kwa hiyo Henry akavunja uhusiano wake na kanisa. Mnamo 1534, alikatiza mamlaka ya papa juu ya Makanisa ya Katoliki ya Uingereza na kujitangaza kuwa kichwa cha Kanisa la Anglikana. Punde si punde alianza kufunga makao ya watawa na kuuza majengo yake makubwa. Henry alipokufa mwaka wa 1547, Uingereza ilikuwa imeanza kuwa taifa la Kiprotestanti.

Mwana wa Henry, Edward wa Sita aliendeleza utengano huo. Baada ya kifo cha Edward mnamo 1553, Mary, binti Mkatoliki wa Henry na Catherine wa Aragon, akawa malkia na kisha akajaribu kufanya taifa lote lijitiishe chini ya mamlaka ya papa. Aliwafanya Waprotestanti wengi waende uhamishoni naye aliamuru zaidi ya watu 300 wateketezwe kwenye mti, na hivyo kujipatia jina Mary Mwuaji. Lakini hangeweza kuzuia mabadiliko. Mary alikufa mnamo 1558, na Elizabeth wa Kwanza ambaye alikuwa dada yake wa kambo, akamrithi na kuhakikisha kwamba papa hakuwa na uvutano mkubwa juu maisha ya kidini ya Waingereza.

Hata hivyo, Waprotestanti fulani walihisi kwamba kujitenga tu na Kanisa Katoliki hakukutosha. Walitaka uvutano wote wa Kanisa Katoliki uondolewe. Walitaka kutakasa ibada ya kanisa, kwa hiyo wakaitwa Wapuriti, kutokana na neno la Kiingereza linalomaanisha -liotakata. Wapuriti fulani hawakuona haja ya kuwa na maaskofu na walihisi kwamba kila kutaniko linapaswa kujitegemea bila kuwa chini ya usimamizi wa kanisa kuu. Waliitwa Waliojitenga.

Wakati wa utawala wa Elizabeth, Wapuriti waliochambua msimamo wa kanisa walijitokeza wazi. Mavazi yasiyo rasmi ambayo makasisi fulani walivalia yalimuudhi malkia. Hivyo, katika mwaka wa 1564 akamwamuru Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana aweke viwango vya mavazi rasmi ambayo makasisi walipaswa kuvalia. Makasisi wa Wapuriti walikataa kutii walipoona kwamba wangekuwa wakivalia tena kama makasisi Wakatoliki. Mabishano zaidi yalitokea kuhusu mfumo wa kale wa kuwaweka maaskofu na maaskofu wakuu. Elizabeth aliendelea kuwaweka maaskofu na kuwataka waendelee kuwa waaminifu kwake akiwa kichwa cha kanisa.

Waliojitenga Wahama

James wa Kwanza alikuwa mfalme baada ya Elizabeth mnamo 1603, naye aliwalazimisha Waliojitenga wajitiishe chini ya mamlaka yake. Mnamo 1608, kutaniko la watu waliojitenga la mji wa Scrooby lilitorokea Uholanzi ambako kulikuwa na uhuru zaidi. Hata hivyo, baada ya muda, watu hao waliojitenga hawakujihisi huru huko kuliko walivyokuwa Uingereza kwa sababu Waholanzi waliruhusu dini nyingine na upotovu wa maadili. Waliamua kuhama Ulaya na kuanza maisha mapya huko Amerika Kaskazini. Kuhamia mbali na nchi yao kwa sababu ya imani yao kulifanya washiriki wa kikundi hicho waitwe Mahujaji.

Mahujaji hao, ambao walitia ndani Wapuriti wengi waliojitenga waliomba ruhusa ya kukaa katika koloni ya Uingereza ya Virginia, nao walianza safari yao kuelekea Amerika Kaskazini mnamo Septemba 1620 kwa meli iliyoitwa Mayflower. Watu wazima na watoto 100 hivi walivuka Bahari ya Atlantiki Kaskazini yenye dhoruba kwa miezi miwili na kufika Cape Cod karibu kilometa 800 hivi kaskazini ya Virginia. Wakiwa huko waliandika Mkataba wa Mayflower, ambao ulikuwa hati iliyoeleza tamaa yao ya kuanzisha jumuiya na kujitiisha chini ya sheria zake. Katika Desemba 21, 1620, walianzisha koloni katika mji wa Plymouth uliokuwa hapo karibu.

Kuanza Maisha Mapya Amerika Kaskazini

Wakimbizi hao walifika Amerika Kaskazini bila kujitayarishia majira ya baridi kali. Baada ya miezi michache nusu ya watu katika kikundi hicho walikufa. Hata hivyo, majira ya kuchipua yalipofika mambo yalitulia. Wale waliobaki walijenga nyumba zilizofaa na kujifunza jinsi ya kupanda chakula cha kienyeji kutoka kwa Wenyeji wa Asili wa Amerika. Kufikia majira ya kupukutika kwa majani ya mwaka wa 1621, Mahujaji hao walikuwa wamefanikiwa sana hivi kwamba walitenga wakati wa kumshukuru Mungu kwa baraka zake. Hapo ndipo Sikukuu ya Kutoa Shukrani ambayo husherehekewa Marekani na katika sehemu nyingine ilianzia. Watu wengi walihamia huko hivi kwamba katika muda unaopungua miaka 15 idadi ya watu huko Plymouth ilizidi 2,000.

Kama tu Wapuriti waliojitenga, Wapuriti fulani huko Uingereza waliamini kwamba “Nchi ya Ahadi” ilikuwa upande mwingine wa Atlantiki. Mnamo 1630, baadhi yao waliwasili mahali fulani kaskazini ya Plymouth na kuanzisha Koloni ya Ghuba ya Massachusetts. Kufikia 1640, karibu Waingereza 20,000 walikuwa wamehamia New England. Baada ya Koloni ya Ghuba ya Massachusetts kutwaa Koloni ya Plymouth mnamo 1691, Mahujaji waliojitenga hawakuwa tena peke yao. Jiji la Boston likawa kituo cha utendaji wa kiroho katika eneo hilo, kwani sasa Wapuriti ndio waliosimamia utendaji wa kidini wa New England. Waliongozaje ibada yao?

Ibada ya Wapuriti

Wapuriti waliohamia Amerika kwanza walijenga mahali pa kukutania kwa mbao, nao walikutana kila Jumapili asubuhi. Hali ndani ya majengo hayo ilikuwa sawa hali ya hewa ilipokuwa nzuri, lakini wakati wa majira ya baridi kali uvumilivu hata wa Wapuriti thabiti zaidi ulijaribiwa. Majengo hayo hayakupashwa joto, na waumini walitetemeka kwa baridi. Mara nyingi makasisi walivalia aina fulani za glavu ili kujikinga na baridi walipotoa ishara.

Imani ya Wapuriti ilitegemea mafundisho ya Mfaransa John Calvin, Mprotestanti aliyeleta marekebisho ya kidini. Walikubali fundisho la kwamba Mungu huwa amempangia mtu mambo mapema. Pia waliamini kwamba Mungu alikuwa ameamua kimbele wanadamu watakaookolewa na wale watakaoadhibiwa milele katika moto wa mateso. Haidhuru watu wangefanya nini, hawangeweza kubadili msimamo wao machoni pa Mungu. Mtu hakujua ikiwa atakapokufa ataishi mbinguni au kuteketea milele katika moto wa mateso.

Baada ya muda, makasisi Wapuriti walianza kufundisha kuhusu toba. Walionya kwamba ingawa Mungu ni mwenye rehema, wote walioasi sheria zake wangeenda moja kwa moja motoni. Makasisi hao walifundisha kwa mkazo kuhusu moto wa mateso ili wafuasi watii sheria. Pindi moja, mhubiri Jonathan Edwards wa karne ya 18 alizungumza kuhusu “Watenda Dhambi Mkononi mwa Mungu Mwenye Hasira.” Ufafanuzi wake wa moto wa mateso ulikuwa wenye kuogopesha sana hivi kwamba makasisi wengine walihitaji kutuliza hisia za kutaniko lililovurugika baada ya kusikia mahubiri hayo.

Wahubiri walioenda kuhubiri Massachusetts walihatarisha maisha yao. Wenye mamlaka walimfukuza mara tatu mhubiri wa dini ya Quaker aliyeitwa Mary Dyer; lakini kila mara alirudi na kuhubiri maoni yake. Walimnyonga huko Boston Juni 1, 1660. Inaonekana kwamba Phillip Ratcliffe alisahau jinsi ambavyo viongozi wa Wapuriti walivyoshughulika na wapinzani kwa ushupavu. Kwa sababu ya hotuba alizotoa za kupinga serikali na kanisa la Salem, walimpiga mijeledi na kumtoza faini. Kisha wakamkata masikio na kumfukuza ili kumfunza adabu. Kwa sababu Wapuriti hawakukubali ushindani wa dini nyingine watu wengi walihama kutoka Massachusetts na kufanya koloni nyingine zikue.

Kiburi Husababisha Jeuri

Wakijiona kuwa “wateule” wa Mungu, wengi wa Wapuriti waliwaona wenyeji wa eneo hilo kuwa watu duni walioishi tu katika ardhi ambayo haikuwa yao. Mtazamo huo ulichochea chuki, na wenyeji fulani wakaanza kuwavamia. Kwa hiyo viongozi wa dini hiyo walibadili sheria kuhusu Sabato ili kuwaruhusu wanaume wabebe bunduki wanapoenda kuabudu. Kisha, mnamo 1675, mambo yakaharibika.

Alipoona kwamba watu wake walikuwa wamepoteza ardhi yao, Metacomet, ambaye pia alijulikana kama Mfalme Philip wa kabila la Wampanoag la Wenyeji wa Asili wa Amerika alianza kuvamia vijiji vya Wapuriti, kuteketeza nyumba zao, na kuwachinja wahamiaji. Wapuriti walilipiza kisasi, navyo vita vikaendelea kwa miezi kadhaa. Mnamo Agosti 1676, Wapuriti walimkamata Philip huko Kisiwa cha Rhode. Wakamkata kichwa na kuvuta mwili wake na kuukata vipande vinne. Huo ukawa mwisho wa Vita vya Mfalme Philip na maisha ya uhuru kwa Wenyeji wa Asili wa Amerika huko New England.

Katika karne ya 18, Wapuriti walionyesha bidii yao kwa njia tofauti. Makasisi fulani huko Massachusetts walishutumu utawala wa Uingereza na kuchochea tamaa ya kupata uhuru. Walichanganya siasa na ibada katika mazungumzo yao kuhusu mapinduzi.

Wapuriti walifanya kazi kwa bidii, walikuwa jasiri, na walifuatia dini sana. Bado watu husema kuhusu mtazamo na unyoofu wao. Lakini unyoofu pekee hautoshi kumtakasa mtu kutokana na mafundisho bandia. Yesu aliepuka kuchanganya siasa na dini. (Yohana 6:15; 18:36) Nao ukatili haupatani hata kidogo na ukweli huu muhimu: “Yeye ambaye hapendi hajamjua Mungu, kwa sababu Mungu ni upendo.”—1 Yohana 4:8.

Je, dini yako hufundisha kuhusu moto wa mateso, kupangiwa mambo kimbele, au mafundisho mengine yasiyo ya Biblia? Je, viongozi wa dini yako hujihusisha na kampeni za kisiasa? Kujifunza Neno la Mungu, Biblia kwa unyoofu kutakusaidia kupata “namna ya ibada iliyo safi na isiyotiwa unajisi,” ibada iliyotakata kikweli na yenye kukubalika machoni pa Mungu.—Yakobo 1:27.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 13]

WAPURITI NA MOTO WA MATESO

Mahubiri ya Wapuriti kuhusu moto wa mateso yalipingana na Neno la Mungu. Biblia inafundisha kwamba wafu hawajui jambo lolote, hawawezi kuhisi uchungu au kufurahi. (Mhubiri 9:5, 10) Isitoshe, wazo la kuwatesa watu halijawahi ‘kuingia moyoni’ mwa Mungu wa kweli. (Yeremia 19:5; 1 Yohana 4:8) Yeye huwasihi watu wabadili maisha yao, naye hashughuliki kwa ukatili na wakosaji wasiotubu. (Ezekieli 33:11) Tofauti na ukweli huo wa Maandiko, mara nyingi wahubiri wa dini ya Wapuriti walimfanya Mungu aonekane kuwa mkatili na asiye na fadhili. Pia walifanya watu wasiwe na huruma kwa kuwachochea watumie nguvu kuwanyamazisha wapinzani.

[Picha katika ukurasa wa 10]

Mahujaji wakitua huko Amerika Kaskazini, 1620

[Hisani]

Harper’s Encyclopædia of United States History

[Picha katika ukurasa wa 12]

Kusherehekea Sikukuu ya Kutoa Shukrani kwa mara ya kwanza, 1621

[Picha katika ukurasa wa 12]

Jengo la ibada la Wapuriti huko Massachusetts

[Picha katika ukurasa wa 12]

John Calvin

[Picha katika ukurasa wa 12]

Jonathan Edwards

[Picha katika ukurasa wa 13]

Wenzi wa ndoa Wapuriti wenye silaha wakienda kanisani

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 11]

Library of Congress, Prints & Photographs Division

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 12]

Top left: Snark/Art Resource, NY; top right: Harper’s Encyclopædia of United States History; John Calvin: Portrait in Paul Henry’s Life of Calvin, from the book The History of Protestantism (Vol. II); Jonathan Edwards: Dictionary of American Portraits/Dover

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 13]

Photos: North Wind Picture Archives