Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Mto Thames—Urithi wa Pekee wa Uingereza

Mto Thames—Urithi wa Pekee wa Uingereza

Mto Thames—Urithi wa Pekee wa Uingereza

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI UINGEREZA

Mto Thames, ambao unajulikana na watu nchini Uingereza kama Baba Mzee Thames, huanzia kwenye vijito vinne katika Milima maridadi ya Cotswold kusini ya kati ya Uingereza. Unapojipinda-pinda kilometa 350 kuelekea mashariki, unaungana na mito mingine hadi unapomwaga maji yake katika Bahari ya Kaskazini kupitia mlango wa bahari wenye upana wa kilometa 29 hivi. Jinsi ambavyo mto huo mfupi uliathiri historia ya Uingereza ni hadithi yenye kuvutia.

KAISARI YULIO aliongoza uvamizi wa kwanza wa Roma dhidi ya Uingereza katika mwaka wa 55 K.W.K. Aliporudi mwaka uliofuata, alizuiwa na mto aliouita Tamesis, yaani, Thames. Maliki Mroma Claudius ndiye aliyeshinda Uingereza miaka 90 baadaye.

Wakati huo vinamasi vilienea pande zote za ukingo wa Mto Thames, lakini mahali ambapo mkondo hubadilika kilometa 50 hivi kutoka kwenye mlango wake wa bahari, jeshi la Roma lilijenga daraja la mbao baadaye. Hapo kwenye ukingo wa kaskazini wa mto walijenga bandari waliyoita Londinium. *

Kwa karne nne zilizofuata, Waroma walipanua biashara na sehemu nyingine za Ulaya na kuingiza bidhaa zenye thamani kutoka Mediterania, kutia ndani mbao kutoka Lebanoni. Pia walitumia Mto Thames kusafirisha bidhaa hadi London kutoka sehemu za ndani, hivi kwamba jiji hilo na mtandao wake wa barabara kuu likawa kituo muhimu cha kibiashara.

Uvutano wa William Mshindi

Baada ya kuanguka kwa Milki ya Roma, vikosi vya Roma viliondoka Uingereza mnamo 410 W.K. Kwa hiyo biashara katika Mto Thames ikapungua kwa sababu jiji la London liliachwa. Wajerumani waliovamia Uingereza waliwatawaza wafalme wao huko Kingston hadi karne ya 11 wakati ambapo William Mshindi alipovamia kutoka Normandy. Kingston kilikuwa kijiji kidogo kilometa 19 kutoka London upande wa juu wa Mto Thames, ambapo mto huo ungeweza kuvukwa kwa urahisi. Baada ya William Mshindi kutawazwa huko Westminster mnamo 1066, alijenga Mnara wa London ndani ya kuta za jiji la Waroma ili kutawala na kupanua jamii ya wafanyabiashara na vilevile kudhibiti yeyote aliyetaka kuingia bandarini. Biashara ilipamba moto tena, na idadi ya watu huko London ilikua kufikia watu 30,000 hivi.

Pia William Mshindi alijenga ngome juu ya mwamba wa chokaa uliojitokeza kilometa 35 hivi magharibi ya London, katika mji ambao leo unaitwa Windsor. Ilijengwa mahali palipokuwa na makao ya kifalme ya Wajerumani na kutoka hapo mtu anaweza kuona mandhari yenye kupendeza ya Mto Thames. Kasri ya Windsor imekarabatiwa mara nyingi, nayo ni mojawapo ya sehemu ambazo watalii hupenda kutembelea nchini Uingereza.

Mnamo 1209, daraja la mawe kuvuka Mto Thames huko London lilikamilishwa baada ya miaka 30. Hilo ndilo lilikuwa daraja la kwanza la mawe huko Ulaya. Daraja hilo la ajabu, ambalo lilikuwa na maduka, nyumba, na vilevile kanisa, lilikuwa na madaraja mawili yanayoweza kuinuliwa na mnara katika eneo la Southwark, upande wake wa kusini, kwa ajili ya ulinzi.

Mfalme John wa Uingereza (1167-1216) alitia muhuri hati yake maarufu ya Magna Carta mnamo 1215 huko Runnymede, kwenye Mto Thames karibu na Windsor. Kupitia tendo hilo alilazimishwa kuhakikisha uhuru wa raia wa Uingereza na pia uhuru wa jiji la London na uhuru wa kibiashara katika bandari za jiji hilo na kwa wafanyabiashara.

Mto Thames Waleta Fanaka

Katika karne zilizofuata, biashara ilitia fora kwenye Mto Thames. Muda ulipopita, kuongezeka kwa biashara kulifanya vifaa vya mto huo vitumiwe kupindukia. Miaka 200 iliyopita, meli 600 tu ndizo zingeweza kutoshea kwenye bandari za Mto Thames, lakini nyakati nyingine meli 1,775 zilikuwa zikisubiri bandarini kupakuliwa bidhaa zilizobebwa. Kwa sababu ya msongamano huo, wizi ulianza kuwa tatizo kubwa. Wezi waling’oa nanga za meli na kuzitoa bandarini usiku ili kuzipora, na kulikuwa na mashua ndogo zilizosafirisha bidhaa zilizoibwa. Ili kukabiliana na tatizo hilo, London ilitokeza kikosi cha polisi wa mtoni cha kwanza ulimwenguni. Bado kikosi hicho kinafanya kazi.

Hata hivyo, mengi zaidi yalihitaji kufanywa ili kupunguza msongamano katika bandari hiyo. Kwa hiyo, katika karne ya 19, Bunge la Uingereza lilikubali kujenga mfumo mkubwa zaidi ulimwenguni wa maegesho ya meli. Mfumo huo ungechimbwa kwenye maeneo ambapo ardhi inakaribiana na usawa wa maji pande zote za mto huo. Maegesho ya Surrey Commercial, London, na West and East India yalikamilishwa kwanza mapema katika miaka ya 1800. Yalifuatiwa na Egesho la Royal Victoria mnamo 1855 na Egesho la Royal Albert mnamo 1880.

Wahandisi wawili, Marc I. na mwanawe Isambard K. Brunel, waliunganisha kingo mbili za Mto Thames mnamo 1840 kwa kujenga njia ya chini ya ardhi inayopita chini ya maji, ambayo ndiyo ya kwanza kujengwa ulimwenguni. Ina urefu wa meta 459 na bado ni sehemu ya mtandao wa reli zinazotumiwa huko London. Mnamo 1894, daraja linaloitwa Tower Bridge ambalo huwavutia watalii wengi lilikamilika. Hilo ni daraja lenye sehemu mbili ambazo hujiinua na kutokeza nafasi yenye ukubwa wa meta 76 ili kuruhusu meli kubwa ziweze kupita kati ya minara yake miwili. Ukipanda ngazi 300 hivi, utatokea kwenye kijia cha juu kinachounganisha daraja hilo na kuona mandhari za ajabu za mto huo.

Kufika karne ya 20, mfumo wa maegesho ya London ulikuwa na uwezo wa kutosheleza idadi inayozidi kuongezeka ya meli kubwa zinazoleta bidhaa za kuuzwa jijini. Kufikia wakati egesho la mwisho la meli lilipojengwa mnamo 1921 ambalo lilipewa jina la Mfalme George wa Tano, London lilikuwa na “mfumo mkubwa zaidi ulimwenguni wa bandari na wenye utajiri zaidi.”

Mto Wenye Makasri, Wafalme, na Maonyesho

Wakati wa kusitawi kwa London, barabara zake zilikuwa katika hali mbaya, bila lami, na mara nyingi hazingeweza kupitika wakati wa majira ya baridi kali. Kwa hiyo, njia bora na ya haraka zaidi ya kusafiri ilikuwa Mto Thames, ambao ulikuja kuwa na shughuli nyingi kadiri miaka ilivyopita. Maneno maarufu “Makasia!” yalitoka kwa mabaharia wa Mto Thames waliposongamana kwenye ngazi ukingoni mwa mto huo. Walisema maneno hayo wakitafuta wateja wa kuwavusha mto huo au kuwapeleka juu au chini au kuingia kwenye vijito vya mto huo kama vile mito Fleet na Walbrook, ambayo imefunikwa chini ya barabara za London zinazoitwa majina yao.

Baada ya muda, London lilianza kuonekana kama Venice, likiwa na ngazi katika makasri yake mengi ya kifahari zinazoelekea kwenye mto. Kuishi kwenye kingo za Mto Thames kukawa mtindo wa familia za kifalme, kama inavyothibitishwa na makasri ya Greenwich, Whitehall, na Westminster. Vilevile Hampton Court limekuwa makao ya wafalme na malkia wengi wa Uingereza. Kasri ya Windsor iliyo upande wa juu wa mto huo bado ni makao ya kifalme.

Mnamo 1717, George Frideric Handel alitunga muziki wake “Water Music” (Muziki wa Maji) ili kumpendeza Mfalme George wa Kwanza kwenye karamu ya kifalme iliyofanywa kwenye maji. Gazeti moja la wakati huo liliripoti kwamba mashua kubwa ya mfalme ilifuatwa na “Mashua nyingine nyingi sana, ikawa kana kwamba Mto wote ulifunikwa.” Mashua nyingine iliyokuwa kando ya ile ya mfalme ilibeba wanamuziki 50, ambao walicheza muziki wa Handel mara tatu waliposafiri kilometa nane kuelekea juu kutoka Westminster hadi Chelsea.

Mto Wenye Kuchangamsha na Kustarehesha

Kabla ya Daraja la Westminster kujengwa katika miaka ya 1740, njia pekee ya kuvuka Mto Thames kwa miguu ilikuwa Daraja la London ambalo lilirekebishwa na baadaye jingine likajengwa mahali pake katika miaka ya 1820. Nguzo zilizotegemeza matao 19 ya daraja la awali zilizuia sana utendaji katika mto huo. Kwa sababu hiyo, katika miaka 600 hivi ya kuwapo kwa daraja hilo, Mto Thames umeganda zaidi ya mara nane hivi. Hilo lilipotendeka, masoko makubwa yalisimamishwa kwenye barafu, ambapo michezo mingi ilifanyiwa. Nyama ya fahali ilichomwa na familia za kifalme zilikula huko. Vitabu na vitu vya kuchezea vilivyokuwa na vibandiko “kimenunuliwa kwenye Mto Thames” vilinunuliwa haraka. Magazeti ya habari na hata nakala za Sala ya Bwana zilichapishwa kwenye matbaa zilizosimamishwa kwenye mto huo ulioganda!

Siku hizi, Mashindano ya Mashua kati ya vyuo vikuu vya Oxford na Cambridge, yamekuwa tamasha ya kila mwaka wakati wa majira ya kupukutika kwa majani. Umati mkubwa hujipanga kwenye kingo za Mto Thames katikati ya Putney na Mortlake ili kushangilia wapiga makasia wanane katika kila kikundi wanapopiga makasia umbali wa kilometa saba hivi kwa karibu dakika 20. Mashindano ya kwanza yalifanywa mnamo 1829 sehemu ya juu zaidi ya mto huo huko Henley. Baada ya mkondo kubadilishwa chini zaidi, Henley ilidhamini mashindano yake ya mashua, ambayo ni ya zamani zaidi na yenye fahari zaidi huko Ulaya. Tukio hilo huwavutia wanaume na wanawake walio wapiga makasia bora zaidi ulimwenguni katika mashindano ya umbali wa meta 1,600 hivi. Mashindano hayo ya wakati wa kiangazi huwavutia watu wengi sana.

Kitabu kimoja kuhusu Uingereza kinasema kwamba Mto Thames “una mandhari nyingi za kuvutia kwa kuwa unapita kwenye maeneo ya Uingereza yenye milima, misitu, mashamba, nyumba za mashambani, vijiji vyenye kuvutia na miji midogo. . . . Katika sehemu nyingi hakuna barabara inayofuata mto huo lakini mara nyingi kuna njia ya mashua ndogo inayovutwa na wanyama. Tokeo ni kwamba ingawa mtu anayesafiri kwa gari anaweza kufurahia mandhari ya mto huo kwenye miji iliyo karibu nao, umaridadi wa Mto Thames unaweza tu kufurahiwa kikamili mtu anaposafiri kwa mashua au kwa miguu.”

Je, unapanga kutembea Uingereza? Basi tenga wakati wa kutembelea Mto Thames na kufurahia historia yake. Tokea chanzo chake katika maeneo maridadi ya mashambani hadi kwenye mlango wa bahari wenye shughuli nyingi, kuna mengi ya kuona, kufanya, na kujifunza! “Baba Mzee Thames” hatakutamausha.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 5 Ingawa jina London linatokana na neno la Kilatini Londinium, maneno yote mawili yanaweza kutolewa katika maneno ya Kiselti llyn na din, ambayo yakiwa pamoja yanamaanisha “mji [au ngome] ulio kwenye ziwa.”

[Sanduku katika ukurasa wa 27]

VITABU NA MTO THAMES

Jerome K. Jerome alieleza vizuri hali yenye kustarehesha ya Mto Thames katika kitabu chake Three Men in a Boat (Wanaume Watatu Katika Mashua). Kinaeleza jinsi ambavyo marafiki watatu waliokuwa likizoni walipiga makasia kuelekea upande wa juu wa mto huo wakiwa na mbwa wao. Walisafiri kutoka Kingston wakipitia Mto Thames hadi Oxford. Kiliandikwa katika mwaka wa 1889 na kutafsiriwa katika lugha nyingi, na bado ni “kitabu maarufu na chenye ucheshi.”

Kitabu kingine cha hadithi The Wind in the Willows (Upepo Kwenye Miti), kinapendwa na watu wazima pamoja na watoto. Kilikamilishwa mnamo 1908 na Kenneth Grahame, ambaye aliishi huko Pangbourne, mji ulio kando ya Mto Thames. Kitabu hicho kina hadithi kuhusu wanyama wanaoishi ndani au karibu na kingo za mto huo.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 27]

MFALME DHIDI YA MTO THAMES

Wakati mmoja, Mfalme James wa Kwanza, aliyetawala mapema katika karne ya 17, aliamuru apewe pauni 20,000 kutoka kwa Shirika la London. Bwana Meya alipokataa, mfalme alimtisha hivi: “Nitakumaliza pamoja na jiji lako milele. Nitaondoa mahakama zangu, makao yangu ya kifalme, na Bunge langu na kuyahamisha hadi Winchester au Oxford, kisha nifanye Westminster liwe jangwa; hebu wazia mambo yatakayokupata wakati huo!” Meya alimjibu hivi: “Hata ukifanya hivyo wafanyabiashara wa London hawataumia sana, kwani mfalme hawezi kuhamisha Mto Thames.”

[Hisani]

From the book Ridpath’s History of the World (Vol. VI)

[Ramani katika ukurasa wa 24]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

UINGEREZA

London

Mto Thames

[Hisani]

Map: Mountain High Maps® Copyright © 1997 Digital Wisdom, Inc.

[Picha katika ukurasa wa 24, 25]

Mnara wenye saa na majengo ya Bunge, huko Westminster, London

[Picha katika ukurasa wa 25]

Daraja la London, lililojengwa kwa mawe, 1756

[Hisani]

From the book Old and New London: A Narrative of Its History, Its People, and Its Places (Vol. II)

[Picha katika ukurasa wa 26]

Mchoro huu wa 1803 unaonyesha mamia ya meli zilizoegeshwa katika bandari ya London

[Hisani]

Corporation of London, London Metropolitan Archive ▶

[Picha katika ukurasa wa 27]

Mchoro unaoonyesha soko juu ya barafu ya Mto Thames mnamo 1683

[Hisani]

From the book Old and New London: A Narrative of Its History, Its People, and Its Places (Vol. III)